PESA NI KILA KITU: USHINDANI KATIKA BIASHARA HAULIPI TENA UMEPITWA NA WAKATI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

PESA NI KILA KITU: USHINDANI KATIKA BIASHARA HAULIPI TENA UMEPITWA NA WAKATI

MAPAMBANO NA WASHINDANI KIBIASHARA
Katika historia nzima ya mwanadamu tokea kuumbwa kwa Adamu na Hawa pamekuwepo na ushindani karibu katika kila nyanja ya kimaisha, biashara ikiwemo. Ushindani huu tangu zama hizo umekuwa ukijulikana kama mpambano wa kujinusuru ambapo mwenye nguvu ndiye huibuka mshindi(Struggle for the survival in which the fittest win). Historia inatuambia kuwa watu walipambana wakigombea ardhi, rasilimali, njia kuu za kiuchumi, wanawake,nk. na mara nyingi mshindi alipatikana baada ya mpambano mkali uliosababisha umwagikaji wa damu, mauaji, udanganyifu na matumizi makubwa ya nguvu.

SOMA: Mshindani wako kibiashara anapoanza kukuhujumu badala ya kushindana kihalali ufanyeje?

Lakini Ulimwengu wa leo uliostaarabika katika karne ya 21, ushindani wa namna hiyo umeshapitwa na wakati kitambo haupo tena. Ikiwa kweli mtu umedhamiria kutengeneza pesa nzuri, unapaswa kusahau kuhusiana na kupambana na washindani wako kwa “mapanga”. Mshindani wako mkubwa leo, kesho anaweza akaja kugeuka kuwa mshirika wako mkubwa wa kibiashara mnayegawana faida na ambaye bila ya yeye kuwepo basi na biashara yako haiwezi pia kushamiri. Kwa hiyo ikiwa unapambana na wapinzani wako inamaana kwamba wewe bado unaishi katika nyakati fulani hivi kwenye karne ya 18 au ya 19.

Teknolojia ya kisasa inamruhusu mtu yeyote yule kufanya maajabu, inamwezesha kuzalisha bidhaa ama huduma za kipekee kwa namna ambayo itazifanya ziwe za aina yake na zisizoweza kamwe kuigizwa kirahisi na mtu mwingine. Siku hizi badala ya mtu kupoteza nguvu zako nyingi katika shughuli za uzalishaji na za mauzo, nguvu hizo unapaswa uzielekeze zaidi katia kufikiria na kubuni ni kitu gani mteja anachohitaji, na atakubali kutoa fedha yake shilingi ngapi kukilipia. Unatakiwa pia ufikirie wewe ni nani, unafanya nini na ni kwa jinsi gani unavyoweza kutengeneza fedha zaidi.

SOMA: Njia mpya za kufanya mambo, Dunia, biashara, ajira, vinabadilika kwa kasi ya ajabu!

Sahau kabisa kuhusiana na mapambano na washindani wako kwasababu kama utajiingiza katika mpambano inamaana kwamba unajiingiza katika jambo lisilokuwa na faida wala halitakuingizia pesa. Sisemi uache kabisa kuwafahamu washindani wako au kuwapuuzia hapana, wafahamu kama kawaida ni nini udhaifu wao na nguvu zao ni zipi lakini acha kupambana nao, majirani kuchuniana bila sababu, hata hamsalimiani na mpaka wakati mwingine mnaendeana kwa waganga matapeli wanatafuna pesa zenu bure, ukiuliza kisa, eti unaambiwa ni ushindani wa kibiashara. Tazama zaidi wateja wako wanahitaji nini.

Mfano mzuri nitakaokupa hapa ni hii mitandao ya kijamii. Ilivyo ni kwamba haiwezekani kabisa mmoja, mfano facebook kumtoa nje ya ulingo wa soko mwenzake kama ilivyokuwa kwa biashara nyingine za kawaida. Kinachofanyika ni kwa kila mmoja anayo fursa sawa na mwenzake ya kujitanua kwa kuvutia na kushawishi wateja wengi zaidi watarajiwa.

SOMA: Kubuni kitu kizuri ni hatari, watu ni lazima wakopi na kupesti, ufanye nini ili kuzuia hili?

Hebu watazame Facebook, Twitter, Whatsapp, Instagram na wengineo, kila mmoja ana uwanja wake wa kujidai na hakuna hata mmoja utamsikia akitoa malalamiko kwamba eti kuna mwenzake anamzibia rizki au kumuibia wateja wake. Ukishindwa kuvutia wateja ukatoka nje ya soko, hayo ni matatizo yako mwenyewe huna wa kumlaumu, utakaa benchi ukiwaacha wenzako wakiendelea kupeta ulingoni.

Katika Dunia ya utandawazi hakuna “wanaoshindwa” kwasababu zipo rasilimali za kutosha kwa kila mtu, tatizo moja tu lipo kwenye jinsi ya kuzitumia rasilimali hizo kwa ufanisi. Tumezungukwa na Ulimwengu uliojaa fursa zisizokuwa na mipaka, sasa ni kwanini upoteze nguvu zako bure ukipambana na washindani wako?

Tazama Mataifa makubwa ya Magharibi na hata yale ya Mashariki kama vile Uchina, zamani ili taifa limshinde adui yake  ilikuwa ni lazima kwanza kulipua madaraja, kuharibu barabara, viwanda na miundombinu mingine ya kimkakati, kisha majeshi huingia na baada ya kuteka nchi yote sasa yanaanza tena kuijenga upya kama Tanzania ilivyofanya kule Uganda enzi za Mwalimu Nyerere au Marekani kule Afghanistan na Iraq.

SOMA: Kila mtu anastahili kupewa tena nafasi ya kurekebisha maisha yake upya, Barrack Obama. 

Leo hii Mataifa yamebadilika, hutoa pesa kama misaada/mikopo na rasilimali nyingine nyingi kama teknolojia kwa Mataifa masikini, na nchi hizo maskini kwa kukubali kwao misaada hiyo zinakuwa zimejitia kitanzi shingoni zenyewe kwani hatimaye hujikuta zimekuwa tegemezi kila kitu kwa Mataifa hayo tajiri kwa kuendelea kubakia kuwa chini yao daima baada ya kushindwa kulipa mikopo hiyo.

Na watu wa nchi masikini tulivyokuwa wajinga, utakuta baadhi yetu tukichukua pesa zilezile walizotupatia kwa njia za kifisadi na kwenda tena kuwekeza katika mabenki yao kinyemela au kununulia vitegauchumi katika majiji yao makubwa mfano huko London, New York, Paris, Monaco na kwingineko.

SOMA: Mwaka 2019 hebu ishi kama Mbayuwayu.

Hivyo badala ya kufikiria mapambano hebu kuwa kama Nchi tajiri, fikiria faida utakayoipata kwa kujenga ushirikiano wa kimkakati. Mara utakapoanza kufikiria kuhusu faida na wateja wako, biashara yako itaanza kubadilika, mauzo mapya yataibuka na utaona waliokuwa washindani wako wakubwa wakigeuka kuwa kikundi kimoja na wewe cha kutengeneza faida.

Hakuna haja ya kuogopa mabadiliko na kushikilia  tu njia zilezile za kizamani za kufanya mambo sawa na mtu anayeng’ang’ania kuishi kwenye pagala linalokaribia kubomoka ili-hali anao uwezo wa kuishi kwemye nyumba bora, imara na mpya ya kisasa.


…………………………………………..


TAARIFA IFUATAYO NDUGU MSOMAJI WANGU SI MUHIMU SANA KAMA HAUHIFADHI DATA NYINGI KATIKA SIMU & COMPYUTA YAKO, INGAWA UNAWEZA KUIPITIA KIDOGO KAMA MUDA UNARUHUSU.

Ndugu msomaji, ingawa binadamu hatuna uwezo asilimia 100% wa kutabiri ni nini kinaweza kutupata au kutokea siku zijazo hiyo haiwezi kutufanya tuache moja kwa moja kupanga na kubashiri mambo yajayo. Nasema hivi kutokana na mkasa uliotupata blogu hii siku chache zilizopita yapata kama wiki 2 hivi wa kupotelewa na vitenndeakazi vyetu, simu na kompyuta. Kwa kweli vifaa hivyo vilikuwa ndio kila kitu katika shughuli hizi za kublogu na kupotea kwake lilikuwa ni mtihani mkubwa mno kwetu. Nakumbuka siku chache kabla ya tukio lile nilikuwa nimeahidi hapa mambo mengi ikiwemo semina ya mahesabu ya michanganuo na ujio mpya baada ya likizo yangu ya mwezi Januari lakini haikuweza tena kuwa hivyo.

Namshukuru Mungu ingawa vifaa(Hardware) vilipotea lakini taarifa(software) nyingi muhimu zilikuwa salama kwani hapo kabla nilikuwa nikifanya back up kwenye Google drive(Manually), na nyingine nilikuwa nazo katika flash ingawa pia kuna baadhi ya vitu vingine vilipotea kabisa na itanichukua muda kuvipata tena upya, kitu kimoja nilichopoteza kabisa ni pamoja na kazi nilizokuwa nimezianza hivi karibuni pamoja na meseji au historia nzima katika mtandao wa WASAP.

Hata hivyo majina ya wadau wote whatsape yalirudi kama yalivyokuwa, na hili ni kosa moja kubwa nililofanya, kumbe kuna option katika whatsap unaweza ‘kubackup’ kila kitu kwenye google drive automatically simu ikija kupotea au kuharibika kila kitu kinarudi upya kwenye simu mpya utakayotumia. Unaingia ktk settings, kisha Chat,  kisha Chat backup.

Changamoto nyingine niliyokutana nayo katika tukio hili ni katika kufuatilia urudishaji wa line na kufunga simu iliyoibiwa. Kwenye kurudisha line hamna utata wowote ila kufunga simu mwizi asiweze kuitumia. Wahudumu wa mtandao wa simu waliniambia kinachohitajika ni ripoti ya polisi, kitambulisho, Risiti ya kununulia simu au IMEI namba za simu iliyopotea. Nilikamilisha vyote lakini mhudumu akadai ile karatasi ya polisi simu haijaorodheshwa, nikarudi tena polisi. wahusika wakaniambia nikafungue kesi ya kuibiwa simu counter kwani, wao wanahusika na line tu.

Nilifanya hivyo nikapangiwa mpelelezi nikajua ataniandikia tu ripoti nirudi zangu ofisi za simu lakini mpelelezi alikomaa na kudai yeye kazi yake ni kupeleleza kesi tu na wala siyo kuandika ripoti.”Hawa wafanyakazi wa makampuni ya simu wanajifanya kutufundisha kazi sisi polisi, kila mtu ni mtaalamu katika eneo lake la kazi, na sisi pia ni wataalamu hapa ofisini kwetu, waambie wasitufundishe kazi hapa na hata wewe kama una utaalamu wako ni hukohuko, unauacha pale mlangoni unapoingia hapa” Aling’aka kwa ukali yule askari wa kike akionekana kukerwa sana na mimi kuomba ripoti ya kupotea simu baada ya kupewa ya line tayari.

Nilijaribu kumwelewesha yule askari kuwa mimi shida yangu haikuwa kuipata simu bali karatasi ya polisi tu ili nikaifunge simu yangu isiendelee kutumiwa na mwizi aliyeiiba, akakataa kata kata na kudai ni lazima nifuate taratibu za kipolisi. Baada ya kulumbana  sana alinipa kijana askari mwingine mvulana nifuatane naye kwenye stationary moja ili wakanichapie maelezo fulani aliyodai ni kwa ajili ya kutuma Tume ya mawasiliano kusudi hatua za awali za upelelezi wa simu ilipo zianze. Kutoka nje ya jengo la polisi yule askari akadai steshenari ipo mbali tunatakiwa tupande bajaji, nikamwambia hamna shida nitalipa bajaji, tukaenda. Tulifika mlango wa steshenaru yenyewe ulikuwa umefungwa akachukua simu akijaribu kumpigia mhusika lakini sijui alimjibu nini, akaniambia turudi tena kule polisi.

Kuona ile mizunguko na gharama zimeshaanza, nikajisemea moyoni, “kwani simu yenyewe ni shilingi ngapi, nia yangu kwanza ilikuwa kumkomesha tu yule mwizi tukose wote ili siku nyingine hata akiokota smartphone ya mtu aone ni bora kumpigia mwenyewe waelewane ampoze ili amrudishie simu yake”. Nilimshukuru yule askari na kumwambia ni heri yule mwizi aendelee tu kuitumia ile simu kuliko usumbufu na urasimu ule nilioanza kuuona pale, tukaagana akarudi ofisini kwa bosi wake na jalada langu na mimi nikaondoka zangu mpaka kule kwa wahudumu wa mtandao wa simu. Niliwaeleza kuwa nimefungua tu kesi lakini hawajanipa karatasi yeyote ya maelezo lakini nao wakawa wagumu kunielewa. Waliniambia wataomba simu ifungwe lakini ni 50 kwa 50 ifungwe au isifungwe kwani sijakamilisha vigezo vyote. Niliwaachia vielelezo nikaondoka zangu

Kweli nilipokuja kusearch mtandaoni, IMEI za ile simu mpaka leo hii zipo active bado yule mwizi anadunda nayo kama kawaida simu haijazimwa wala nini, roho iliniuma lakini nifanyeje. Serikali ilitakiwa kuweka utaratibu unaoeleweka na uliokuwa wazi kuwa mtu akipoteza simu yake, iwe kama vile ilivyo kwa line, kusiwe na longolongo au urasimu mkubwa kiasi hicho wa kufungiwa simu. Vinginevyo wezi na vibaka wataendelea kuiba simu za watu bila woga kwani wanafahamu si rahisi mtu kuifunga simu pindi inapokuwa imeibiwa. Kama IMEI namba ninazo hadi risiti ya kununulia simu, na polisi nimetoa ripoti, kwenye mtandao simu inaonekana line zilikuwa za kwangu tatizo lipo wapi simu hiyo kufungwa?

Ikiwa unafanya biashara za mtandaoni kwa kutumia vifaa kama vile, kompyuta, simu nk. Bima kubwa zaidi unayoweza kuiwekea biashara yako ni kufanya BACKUP ya taarifa zako muhimu kila mara. Unaweza kutumia medium(vyombo) mbalimbali kama vile flash, cd, DVD, External hard disc, Google drive ama cloud storage nyingine yeyote ile nk. Si lazma uwe unafanya biashara za mtandaoni, hata taarifa zako tu mwenyewe binafsi zinapopotea zinaweza kukuumiza kichwa mno hata kushinda simu yenyewe au kompyuta.

Mwisho niwashukuru tena sana wadau wote mliotufariji na kutupa pole nyingi katika kipindi hicho kigumu hasa kupitia email na group la wasap, na mimi kwa niaba ya timu nzima ya Blog hii nasema ASANTENI SANA!

Peter Augustino.


*Yale Masomo ya kila siku katika Group la Michanganuo-online yameanza tena, na leo hii tutakuwa na somo lisemalo hivi,

 “UKWELI ULIOFICHWA JUU YA PESA: WATU HAWATAFUTI KAZI BALI HUTAFUTA PESA”

0 Response to "PESA NI KILA KITU: USHINDANI KATIKA BIASHARA HAULIPI TENA UMEPITWA NA WAKATI"

Post a Comment