RAIS OBAMA: KILA MTU ANATAKIWA APEWE NAFASI YA KUREKEBISHA MAISHA YAKE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

RAIS OBAMA: KILA MTU ANATAKIWA APEWE NAFASI YA KUREKEBISHA MAISHA YAKE


Ikiwa leo ndiyo siku ya mwisho ya Rais Barack Obama kuwa madarakani, Obama atakabidhi madaraka rasmi kwa raisi mpya wa Marekani bwana Donald Trump majira ya saa sita mchana saa za huko Marekani au saa 2 usiku saa za Afrika Mashariki. Katika siku yake ya mwisho akiwa ofisini hapo jana tarehe 19 January 2017 Rais Obama alitoa msamaha kwa wafungwa wapatao 330 huku akitoa kauli hii nzito na yenye maana kubwa, “KILA MTU ANASTAHILI KUPEWA NAFASI YA KUREKEBISHA MAISHA YAKE KWA MARA NYINGINE TENA” 

Kauli hii aliyoitoa Rais Obama kwa kweli ina maana kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Ijapokuwa sikubaliani na Obama katika mambo kadhaa kama pia nisivyokubaliana baadhi ya mambo na Raisi mteule Donald Trump, ukweli utabakia palepale kwamba hakuna binadamu aliyekamilika.

Rais Barack Obama bila shaka angetamani na yeye kupewa tena muda mwingine ili kurekebisha baadhi ya vitu alivyovifanya vibaya lakini ndiyo hivyo tena katiba ya Taifa hilo kubwa Duniani haiwezi kumruhusu labda ingelikuwa Gambia kwa Yahya Jammey na Adam Barrow. Mimi kwa mtazamo wangu Rais Obama na wasaidizi wake kama kina Hillary Clinton na Joe Biden ndiyo watu wa kulaumiwa  kwa matatizo ya kusambaratika nchi za Kiarabu kama Syria, Libya, Misri na hata kuanzishwa kwa vikundi vya kigaidi kama IS na Al nusra front kutokana na sera zao bovu za kutaka kulazimisha demokrasia ya nchi za Magharibi katika Mataifa ambayo yana taratibu, mila na desturi zao wenyewe. 

SOMA: Kati ya Obama na Putin ni nani anayeisaidia IS?

Obama alikuwa haambiliki  linapokuja suala la demokrasia ya Kimagharibi, alikuwa radhi hata kuwasaidia magaidi kuliko kukaa meza moja na kusikilizana na watu anaodai ni madikteta kama kina Bashar Al Assad, Muamar Gadafi, Mugabe na Putin wa Urusi.

Pamoja na baadhi ya hayo mambo aliyoboronga hata hivyo Rais Obama atakumbukwa pia kwa mambo mengine mengi mazuri aliyosimamia yakiwamo kutetea haki za binadamu japo hili mimi naona amelifanya kinadharia zaidi kwani huwezi ukasema unaheshimu haki za binadamu wachache tu na huku ukiwaacha maelfu wakiuwawa na kutimuliwa makwao kama wanyama kwa kisingizio eti cha kutokushirikiana na madikteta.

Assad ni mtu mmoja tu iweje amnyime Obama usingizi kiasi cha kuwaacha maelfu ya Wasyria wakiangamia? Mbona Urusi wameweza kubadilisha hali ijapokuwa kwa shida huku wakiwa hawapewi sapoti yeyote na Marekani na washirika wake?. Obama alipaswa kukaa meza moja pamoja na Putin na Assad kwa maslahi ya Wasyria na wala siyo kukaa tu kimya na kulalamika kuwa, Assad ni lazima aondoke. Libya ndiyo hivyohivyo walishirikiana na washirika wake hatimaye wakamng’oa na kumuua Gadafi na mpaka leo Libya si mahali salama tena kama zamani.

SOMA: Ugaidi ni matokeo ya kimbelembele cha Marekani na Uingereza kueneza demokrasia duniani.

Hii ni sababu kubwa iliyochangia Wamarekani wenyewe kuamua kukiadhibu chama cha Obama cha Democrat kwa kukinyima ushindi kilichotegemea Bibi Hillary Clinton kuwa mwanamke wa kwanza Marekani kuwa Rais, wakampa ushindi mtu aliyeonekana kuwa na kauli zenye utata lakini aliyekuwa na msimamo usioyumba juu ya kuifanya Marekani kuwa Taifa kubwa kwa mara nyingine tena.

Hapo Wamarekani walithibitisha kwamba Binadamu anachohitaji zaidi ni usalama wake na hali bora ya kiuchumi kwanza kabla hata ya uhuru na demokrasia. Ukiwa na hali mbaya kiuchumi hata huo uhuru wenyewe hauna maana sana kwako, kwanza ndiyo utazidi kuwa mtumwa kwa wale wenye uwezo. Trump hataki Wamarekani waje kuwasujudia Wachina, ni lazima ahakikishe Marekani inaendelea kushika usukani wa kiuchumi duniani na ndipo mambo mengine yatawezekana.

Kauli ya Obama kwamba kila mtu anatakiwa kupewa nafasi ya kurekebisha tena maisha yake ninaifananisha na ile ya Donald Trump ya Marekani kujirudishia tena ukuu wake, 'make America Great again.' Ni kama vile anakubaliana na Trump kuwa Marekani inastahili kupewa nafasi ya kujirudishia tena ukuu wake unaokaribia kupotea.

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa maisha yetu ya kawaida hata sisi  huku. Inawezekana maisha yako imefikia mahali mambo yamekuwa magumu sana hayaendi kiasi ambacho watu waliokuzunguka kama ndugu, jamaa na marafiki wanakucheka na kukukatia tamaa kabisa wakifikiri kwamba wewe siyo mtu wa kuinuka tena na wala haiwezekani kabisa wewe kuja kuwa bora tena. Lakini kauli hii ya Rais wa Marekani anayeondoka madarakani  kuwa KILA MTU ANASTAHILI KUPEWA TENA NAFASI YA KUREKEBISHA MAISHA YAKE ni ujumbe tosha kwao kwamba inawezekana mtu kujirekebisha.

SOMA: Maziwa na Asali vya Gadafi na Sadam Hussein vipo wapi tena?

Mtu anaweza kurekebisha tena maisha yake ikiwa ataamua kujikagua na kujua ni wapi alipojikwaa, lakini mara nyingi ili mtu aweze kurekebisha maisha yake yaliyokwisha haribika anahitaji kupewa nafasi kama Obama anavyosisitiza, na nafasi hiyo ipo katika mifumo mingi. Kwa mfano wafungwa kama hao Obama aliowaachia huru wasingeliweza kubadilisha maisha yao tena kamwe ikiwa kusingelitokea msamaha wa rais.

Vivyo hivyo mtu aliyechoshwa sana na umasikini anahitaji angalao kupigwa jeki kimtaji kwa namna fulani ili aweze kuinuka tena. Anahitaji kitu kama mkopo au hata ruzuku ili aweze kukuza biashara ambayo ndiyo suluhisho pekee la umasikini. Anaweza pia kupewa kazi ambayo ataitumia kama nyenzo ya kupatia mtaji wa kuanzishia shughuli ya kiuchumi. Lakini bila ya kupata kianzio chochote kama mtaji itamuwia vigumu sana kubadilisha maisha yake na ataendelea kuonekana katika jamii kama mtu asiyekuwa na maana yeyote au omba omba. 

Unaweza ukamcheka mtu aliyefulia kimaisha lakini siyo sahihi, mtie moyo na kujaribu kumpa mbinu za kuondokana na hali aliyokuwa nayo. Siyo lazima umpe pesa, hata kumtia moyo tu inatosha badala ya kuanza kumnyooshea kidole na kusema, “kachezea maisha yule, mwache akome”

....................................................................................................

VITABU HIVI VYOTE, vinapatikana na unaweza kuagiza popote pale ulipo ukiwa Dar au Mikoani. Wasiliana nasi kwa simu 0712202244 au 0765553030. Hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa zaidi ya kumiliki biashara au kuwa na kazi inayolipa vizuri. Lakini kwa bahati mbaya kazi nyingi malipo huwa kidogo yasiyotosheleza mahitaji yote. Suluhisho lake ni kuijua Mifereji 7 ya Pesa ili hata kama una kazi basi ujue ni kwa namna gani utaongeza kipato chako.   



0 Response to "RAIS OBAMA: KILA MTU ANATAKIWA APEWE NAFASI YA KUREKEBISHA MAISHA YAKE"

Post a Comment