Mmiliki biashara ya bucha la kuuza nyama na samaki agundua siri ya kupata wateja wengi wa kipato cha chini | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Mmiliki biashara ya bucha la kuuza nyama na samaki agundua siri ya kupata wateja wengi wa kipato cha chini


Biashara ya bucha la kuuza nyama au samaki kama zilivyokuwa biashara nyingine za rejareja siri yake kubwa ya mafanikio ni eneo utakalofungua biashara yako. Eneo zuri la biashara ya bucha unayoweza kupata wateja wengi wa kutosha ni maeneo yale yaliyokuwa na mzunguko wa watu wengi ama yaliyozungukwa na makaazi mengi ya watu. Bucha za kisasa nyingi utakuta zimewekwa maeneo wanakopita watu wengi kama stendi za magari na sokoni.

Kigezo kingine kinachoweza kuamua bucha lako lipate wateja wengi ni kipato cha wateja walioko katika eneo utakalochagua kufungua bucha. Kuna wateja wa aina tatu kulingana na kipato, wapo wateja wa kipato cha juu, kipato cha kati na wale wa kipato cha chini. Kwa mfano eneo linapokuwa na wakaazi wengi wa kipato cha juu, biashara ya bucha inalipa sana kwani wateja watakuwa wengi tofauti na eneo lenye watu wa vipato vya chini.


Si kama watu wa vipato vya chini hawapendi kula nyama na samaki hapana, bali uwezo wao wa kununua bidhaa hizo ni mdogo jambo linalowafanya wengi kununua mara chache sana kwa mwezi. Unaweza ukakuta mtu anapitisha hata miezi miwili bila kugusa kabisa nyama. Sanasana utakuta akinunua dagaa na samaki mara chachechache.

Ni katika mtaa mmoja maeneo ya Mbezi ya Kimara, eneo ambalo wakazi wake wengi  ni watu wa kipato cha chini na cha kati mjasiriamali mmoja mmiliki wa bucha la nyama ajulikanae kwa jina la Mushi amebuni mbinu mpya ya kuongeza mauzo kutoka kwa wateja wa kipato cha chini, mbinu hiyo hapo kabla hakuna mtu mwingine aliyekuwa amewahi kuitumia katika kitongoji hicho.


Kabla ya ujio wa mjasiriamali huyu mbunifu, wafanyabiashara wengine wa mabucha ya nyama na samaki katika eneo  hili waliwahi kufungua mabucha lakini wengi “walichemka” kutokana na wateja kuwa wachache mno. Mpaka anakuja palikuwa na bucha moja tu eneo hilo na wateja wake wengi walikuwa ni watu wachache sana wa vipato vya kati wanaoishi eneo lile. Hapakuwa na butcher la nyama wala bucha la saki lolote lililokuwa likiwalenga wateja wa kipato cha chini.

MBINU YENYEWE ALIYOKUJA NAYO HUYU JAMAA NI HII HAPA.
Nilipofanya naye mazungumzo ya kirafiki, Bwana Mushi alianza kunieleza hivi;
Kabla sijafungua bucha katika eneo hili wala kununua vifaa vya bucha kitu cha kwanza nilifanya utafiti kujua kama kuna wateja wa kutosha kuniwezesha niweze kupata faida. Katika utafiti huo niligundua kwamba watu wengi hasa wale wenye vipato vidogo wanapenda sana kula nyama na samaki kama vitoweo lakini kikwazo kikubwa kinakuwa ni uwezo wa kununua, wanaishia tu kununua dagaa mchele wa buku, dagaa wa kigoma na wale wa mwanza, maharage na mbogamboga za majani kama vile mchicha, spinachi, matembele, majani ya maboga, majani ya kunde, matembele, kabichi nk.


Ukichunguza vitoweo vyote hivyo nilivyovitaja bei zake hazizidi shilingi elfu moja(1000) kwa mlo mmoja lakini ili mtu aweze kupata nyama kiwango cha chini kabisa anachoweza kununua ni robo kilo ¼ na atalazimika kulipa shilingi elfu moja na mia tano(1500), tena mwenye duka naye akigundua tu hana washindani wengi hupandisha na kuuza nyama robo kilo kwa shilingi elfu mbili( 2000), hii sasa inakuwa ni kama kuwakomesha wateja ili wakome kununua roborobo, wanunue kuanzia nusu kilo, kilo moja na kuendelea.

Baada ya kubaini hali hii, niligundua fursa kubwa ya soko la nyama ya ng’ombe na samaki wa mwanza kama vile sangara na sato kwa watu wa hali za chini ambao vipato vyao si vya uhakika sana. Nilifikiri kwamba kama nitaanzisha biashara ya bucha la kuuza nyama ya ng’ombe, nyama ya kuku na samaki kisha nikaweka bei ya kawaida lakini nianze kupima kiasi kidogo kadiri iwezekanavyo basi ningeweza kuwanasa wateja wengi sana wa kipato cha chini na wale wa kati pia.


Mwanzoni nilipanga kuuza kuanzia robo kilo kwa bei ileile ya kawaida nisiwakomoe wateja kwa kuwauzia elfu mbili bali kama kilo moja ya nyama ni shilingi elfu 6 basi robo kilo niuze shilingi elfu moja na mia tano(1500). Na samaki hivyohivyo, kama kilo moja ya sato ni shilingi labda elfu tisa(9) basi robo kilo ya samaki hao niuze shilingi elfu mbili na mia mbili na hamsini(2250) tu pasipo kumbugudhi mteja kuhusiana na chenchi wala nini.

Nilipofungua bucha langu nilianza na mzani wa mawe huu wa kawaida wenye jiwe la kuanzia robo kilo mpaka kilo 5, lakini pamoja na mbinu hiyo niliyoazimia kuitumia bado sikuona wateja wengi wakija kununua nyama na samaki kama nilivyokuwa nikifikiria. Nilijitahidi kubandika tangazo ukutani(TUNAPIMA NYAMA KUANZIA ROBO KILO KWA SHILINGI 1500) ;lakini wapi, wateja wala hawakuongezeka kama nilivyodhania.


Mwishoni katika pitapita yangu mjini siku moja nikaingia duka moja Kariakoo linalouza vifaa mbalimbali ikiwemo mizani kwa ajili ya kupimia vitu mbalimbali. Niligundua kuna mzani mmoja wa kichina wenye uwezo wa kupima kiasi chochote kile cha bidhaa bila kutumia mawe ya kawaida, ni mzani wa kielektroniki na unasoma mahali kama vile unavyosoma saa au mashine zinazotumika shelli za mafuta ya magari. Unaweza kupima kitu kuanzia uzito wa chini kabisa kuliko hata robo kilo na cha kushangaza zaidi ni kwamba mzani huo una mahali unapoandika bei moja kwa moja kulingana na utakavyo useti.

Kama umeseti kilo moja ya nyama kuwa ni shilingi elfu 6 basi kiasi chochote kile cha nyama utakachoweka kwenye bakuli la mzani, mzani utakuandikia ni gramu ngapi na kiasi cha fedha kinachoendana na gramu hizo moja kwa moja (automatically) wala hupati shida ya kuanza kukokotoa mwenyewe tena kwa mashine ya hesabu. Hata uweke gramu moja ya nyama itakuonyesha bei yake ni shilingi ngapi.


Kwa mtindo huo mteja wa nyama au samaki hata akitaka nyama ya shilingi mia tano anaweza kupata bila kumpunja wala wewe muuzaji kupunjika kwani mzani unapima na kutoa bei sawasawa kulingana na kiasi kile ulichoweka pale kwenye bakuli.

Baada ya wateja wengi kugundua vile, nilianza kuona wateja wengi wakimiminika kuja wakitaka kupimiwa nyama na samaki za shilingi elfu moja(1000), wengine hata huja na pesa kiasi chini ya hapo na mimi wala sikatai nawapimia kwani nafahamu sipotezi kitu chochote na mwisho wa siku nyama na samaki vikiisha hesabu zangu hubakia vilevile sahihi sawasawa tu kama ningeuza kwa kupima kilo mojamoja.

Siku hizi buchani kwangu nyama na samaki wabichi hazikai tena muda mrefu nikileta leo kesho nimemaliza na wateja wangu wengi ni akina mama wa familia za kipato cha chini na kidogo wale wa kipato cha wastani. Badala ya kwenda sasa kununua dagaa za shilingi elfu mojamoja au samaki wa kukaanga wanakuja nawapimia nyama ya shilingi elfu moja. Wapo wengine husema niwapimie ya elfu mbili, 1500 au kiasi chochote kile kulingana na hela aliyokuwa nayo mteja.

Mzani huu umewapa wateja uhuru mkubwa wa kuchagua wanunue nyama na samaki kiasi gani bila vikwazo vyovyote vile visivyo na msingi. Unajua wateja wana kawaida moja ya kupenda kuwa huru wanapofanya manunuzi yao ya aina yeyote ile pasipo kubanwabanwa. Mfanyabiashara ukigundua hili na kuwapa wateja uhuru huo utashangaa vile watakavyokuwa marafiki zako.” Alimaliza Bwana Mushi maelezo yake.

.............................................

Ndugu msomaji wa makala hizi napenda kukujulisha pia kwamba kila siku tunakuwa na masomo yahusuyo fedha katika group la MICHANGANUO-ONLINE ambalo kiingilio chake ni shilingi elfu 10. 

Unakuwa mwanachama wa kudumu na pia mbali na masomo hayo ya kila siku na semina za mara kwa mara za kuandika michanganuo ya biashara mbalimbali zenye fursa,  tunakutumia masomo yote na semina zilizopita, vitabu na michanganuo kama ilivyorodheshwa hapo chini. 

Somo la leo usiku tarehe 22/9/2018 linasema hivi;

"HUWEZI KUAMINI KAMA SIRI YA KUPATA UTAJIRI NI KITU KIDOGO NAMNA HIII !"

Malipo ni kupitia namba hizi, 0765553030  au  0712202244 na baada tu ya kulipia tuma ujumbe kwa wasap 0765553030 usemao "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO" na tutakuunganisha muda huohuo pamoja na kukutumia vitu mbalimbali vifuatavyo; 

Ukihitaji vitabu vya ujasiriamali na biashara katika lugha ya kiswahili pia tembelea hapa,  >> SMART BOOKS TZ


0 Response to "Mmiliki biashara ya bucha la kuuza nyama na samaki agundua siri ya kupata wateja wengi wa kipato cha chini"

Post a Comment