KITU KIMOJA (1) MUHIMU KULIKO VYOTE MJASIRIAMALI ANACHOPASWA KUFANYA MAISHANI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KITU KIMOJA (1) MUHIMU KULIKO VYOTE MJASIRIAMALI ANACHOPASWA KUFANYA MAISHANI

toa msaada
Mjasiriamali unaweza usiamini au kukubaliana na ukweli huu, lakini ukweli utabakia kuwa ukweli daima. Mara nyingi wajasiriamali wengi wanapofanikiwa kuvuka vikwazo vya kuanza biashara au kwa kimombo huita ‘startups’ wengi hujisahau na kuona wameweza kufika pale walipo wenyewe kwa kutumia nguvu, maarifa na ujanja wao bila msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote yule.

Ukweli ni kwamba kwa namna moja au nyingine wajasiriamali waliofanikiwa kama hao kuna nyakati fulani walipata misaada ya aina mbalimbali kutoka kwa jamii inayowazunguka wakiwemo ndugu jamaa na marafiki. Misaada ninayoizungumzia hapa siyo lazima iwe ni pesa, mtaji au rasilimali bali hata ile kuungwa mkono tu kwa dhati peke yake nayo ni msaada, kutiwa moyo nk. Unapokuwa katika hatua za mwanzo za biashara yako kitendo cha wale wanaokuzunguka mfano hata wanafamilia kukupa utulivu wa nafsi na kukuacha ufanye shughuli zako vizuri nao ni msaada.


Ili ufanikiwe kibiashara utahitaji watu kukuunga mkono, na kitendo hata kile cha wateja kununua kutoka biashara yako nacho kinahesabika kama msaada, hebu fikiria kama kila mtu angeghairi kununua kutoka kwako ungelijisikiaje. Wakati mjasiriamali unapohangaika kabla hujatoka utakutana na watu wengi wanaokupa ushauri mbalimbali mfano ni jinsi gani unaweza kupata mtaji zaidi, mbinu mbalimbali za kupata soko, kupata msaidizi nk. Vyote hivyo unavipata au kuvifahamu kupitia watu wengine waliokuwa na mapenzi mema kwako.

Wakati mwingine unaweza ukawa umenunua mizigo mahali fulani na huwezi ukaibeba peke yako, ingawa utatoa pesa kidogo kwa ajili ya vijana au watu watakaokusaidia kuibeba lakini wakati mwingine pesa unayowalipa ni kama kifuta jasho tu, ungewalipa inavyostahili pengine mzigo wenyewe usingepata faida, hivyo hapo unaweza ukahesabu umepata msaada.


Kwa kweli mpaka pale mtu anafikia hatua ya kupata mali au kutajirika anakuwa amepitia uungwaji mkono kutoka kwa watu wengi ingawa pia kunakuwa na watu wengine wachache ambao wanakuwa hawampi ushirikiano wowote na wangetamani aanguke ili wamcheke. Lakini kwa kuwa wanaomtakia mema ni wengi kushinda wasiomtakia mema basi  ndiyo hukuta mtu anafanikiwa.

Ni kitu gani hicho kimoja basi  Mjasiriamali unachotakiwa kukifanya zaidi kushinda vitu vingine vyote?

Mjasiriamali unapaswa kila ufanyacho na wewe ufanye kwa mtindo uleule unaofanyiwa na waliokuwa wengi, KUWASAIDIA WENGINE. Msaada haimaanishi pesa tu au kupoteza muda wako bure kuwasaidia kazi watu wengine, msaada hapa unamaanisha kwamba; kusaidia kwa kadiri ya uwezo uliokuwa nao. Misaada mingine  si lazima iwe ni vitu vya kushikika, ushauri mzuri, elimu na hata kumtakia mtu mema tu navyo ni msaada mkubwa sana. Unapoonyesha matendo chanya kwa wengine unaasaidia kushinda hata umewapa pesa.


Utakuta mtu anaangamia au ‘kutumbukia katika shimo’, badala ya kusaidia asiendelee kutumbukia wewe unamwacha, na kusema “mwache azame kwanza kajitakia mwenyewe” huo siyo msaada, mwonyshe njia japo kidogo. Kama mjasiriamali msaada wako mkubwa kabisa unatakiwa kuutoa kwa wateja wako. Wateja wako wanatakiwa wahisi kile unachowauzia kina msaada mkubwa kwao.

Mjasiriamali pia usiwe mchoyo kuwaelekeza na wale wanaotaka kuwa wajasiriamali kama wewe, kumbuka na wewe kuna wakati ulikuwa hivyohivyo ukashikwa mkono kwa namna moja au nyingine na watu wengine na ndiyo maana leo hii upo pale ulipo, hukufika hapo peke yako.

Rudisha sehemu ya kile ulichokipata kwa jamii unapofikia hatu ya juu kabisa. Katika mlolongo huohuo wa kuhakikisha mjasiriamali unakuwa ni mtu wa kuwasaidia watu wengine, kuna mahali unafika sasa inakuwa huna budi kuiambia ile jamii iliyokufikisha pale ulipo asante, hapa ndiyo utakuta matajiri, viongozi na watu wengine waliopata nafasi kimaishai wakitoa misaada mbalimbali kwa jamii kama ujenzi wa mashule, mahospityali nk.


Wanafahamu kwamba utajiri waliokuwa nao waliwezeshwa na jamii nzima inayowazunguka na mtazamo huu mtu anaanza kuwa nao kabla hata hajafanikiwa kwa kuanza kujijengea mtazamo chanya kwa kila analolifanya kwa watu wengine waliomzunguka. Na mtazamo chanya ni msaada kwa watu wengine. Hakuna kitu kitakachokufanya ujisikie amani moyoni mwako na nafsi yako kuridhika kama kutoa msaada kwa wengine.

.......................................................................................................

Ndugu msomaji wa makala hii, ukipenda vitabvu vyetu vya ujasiriamali, biashara na maendeleo binafsi usisite kutembelea, SMART BOOKS TANZANIA



0 Response to "KITU KIMOJA (1) MUHIMU KULIKO VYOTE MJASIRIAMALI ANACHOPASWA KUFANYA MAISHANI"

Post a Comment