MTAJI WA KUANZISHA BIASHARA YA VOCHA ZA SIMU JUMLA, MILIONI MBILI 2 INATOSHA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MTAJI WA KUANZISHA BIASHARA YA VOCHA ZA SIMU JUMLA, MILIONI MBILI 2 INATOSHA?

LAINI ZA MITANDAO MBALIMBALI, TIGO, VODACOM, AIRTEL, HALOTEL, SMART NA TTCL
Leo hii kwenye kipengele cha ongea na mshauri wako kuna msomaji wetu mmoja kutoka Dar es salaam, yeye anataka kujua ikiwa kama anaweza akaanzisha biashara ya kuuza vocha za simu za jumla kwa mtaji wa shilingi million mbili. Swali lake alilotuma  ni hili hapa chini’
                                                                            
Ndugu mshauri naomba ushauri wako, mimi naishi maeneo ya uwanja wa ndege jijini Dar es salaam nimepata sehemu(fremu ya duka) maeneo ya stendi ya njia panda ya kuelekea segerea na ninao mtaji wa shilingi milioni mbili, kwa mtaji huo je, naweza nikafungua biashara ya kuuza vocha za simu za mkononi? Au mshauri ningeomba kama haiwezekani basi unishauri biashara za kufanya nyingine ninazoweza kuanza kwa mtaji huo,
Majibu ya swali hilo ni haya yafuatayo.
Kulingana na swali uliloniuliza, kwanza mimi nitalijibu kwa mtazamo wa namna ya kuanzisha biashara kwa ujumla pasipo kujali kama ni biashara ya kuuza vocha za simu jumla au ni biashara nyingine yeyote ile na kisha ndipo tutakapokuja kwenye biashara yenyewe ya vocha za simu.

SOMA: Natengeneza sabuni, shampoo, batiki na unga wa lishe lakini sioni unafuu wowote kimaisha, naomba ushauri.

Unapotaka kuanzisha biashara yeyote ile kuna hatua mtu unazotakiwa uzipitie na wakati mwingine hatua hizo wala siyo lazima uwe umezisomea ila unajikuta tu wewe mwenyewe umezifanya kama ni mdadisi. Moja ya hatua hizo ni kufanya utafiti wa biashara ile unayokusudia kuianzisha. Utafiti wa biashara au utafiti wa masoko unakuwezesha kufahamu kwa kina mambo mbalimbali yanayohusiana na biashara husika ambayo ndiyo yanayohitajika kuja kutekelezwa ndipo biashara yenyewe iweze kupata mafanikio.

Utafiti au upembuzi wa biashara unakuwezesha kutambua vikwazo au matatizo kama vile ya mtaji yanayoweza kuja kujitokeza baadae hivyo kuchukua tahadhari ya kuyapunguza mapema kuliko kuja kuyashitukiza ghafla na kuanza kuhangaika huku na kule pasipokujua ufanye nini.

Moja ya majukumu hayo kwenye utafiti ni kujua ikiwa biashara tarajiwa itahitaji mtaji kiasi gani ili kuweza kuanza. Mahitaji ya kuanzisha biashara ni rahisi kujua kwani baada ya kupita katika maduka kadhaa yanayosambaza bidhaa au kile wewe utakachouza na kuuliza bei zao, bila shaka kwa haraka haraka utafahamu bei ya malighafi au bidhaa utakazouza utaweza kuzipata kwa gharama kiasi gani na utakapokwenda kuuza utapata faida ghafi kiasi gani.

SOMA: Biashara ya vocha za simu, je ulikuwa unalijua hili?

Huishii hapo tu, bali utauliza kila kitu kingingine kinachohusiana na biashara hiyo ikiwa utakipata kwa gharama kiasi gani, vitu kwa mfano eneo la kufanyia biashara husika, vifaa na vyombo utakavyotumia wakati ukifanya biashara, Gharama mbalimbali wakati wa kusajili biashara, vitu kama umeme, maji, simu nk. kama biashara yenyewe itavihitaji, pamoja hata na gharama za kumuajiri mtu kwenye hiyo biashara ikiwa labda utalazimika kwenda kumtafuta kutoka vituo vya ajira.

Baada ya kumaliza kazi hiyo ya utafiti sasa chukua kalamu yako na karatasi na kisha uchore jedwali kama hili lifuatala

JEDWALI LA MAHITAJI YA KUANZISHA BIASHARA.

MAHITAJI MBALIMBALI YA KUANZA BIASHARA
Tsh.
1. Kusajili biashara

2. Leseni

3. Kodi ya chumba/eneo la biashara

4. Maboresho ya eneo/chumba

5. Mtaji wa kununulia bidhaa/malighafi

Jumla ya mahitaji yote ya kuanzia
Y











Kisha utajaza kila hitaji kiasi cha fedha unazokadiria kutegemeana na mtaji wako uliokuwa nao. Utakuwa umeshafahamu kwani katika utafiti wako ni lazima uulize watu mbalimbali wanaouza bidhaa au huduma kama za kwako kwamba unaweza ukaanza na bidhaa kiasi gani halafu bidhaa hizo utazidisha mara bei ya kununulia uliyokwisha ifahamu pia baada ya kutafiti kwa wauzaji au wasambazaji wakubwa wa bidhaa hiyo kwa jumla.

Kwa suala lako itakubidi hata uende mpaka kwa watoa huduma wa makampuni ya simu za mkononi kama vile Vodacom, Tigo, Airtel, Zantel, Smart, Halotel, TTCL NK. kwenye vituo vyao kama vile kule mlimani city na kuwauliza wale maafisa masoko namna unavyoweza kupata vocha kwa ajili ya kwenda kuuza jumla na bei ya kuuziwa kwa wewe mtu unayekwenda kuuza jumla.

Ukisha maliza zoezi hilo hapo kwenye hilo jedwali la mahitaji ya fedha za kuanzishia biashara sasa jumla ya kiasi hicho cha fedha “Y” ndiyo mtaji utakaotosha kuanzisha mradi au kampuni yako ndogo.

Kumbuka kwamba idadi ya mahitaji hayo itategemea ukubwa wa biashara au kampuni unayotaka kuianzisha yakwangu hapo ni mfano tu, wewe kama mjasiriamali ni lazima ujiongeze kujua jinsi ya kufanya biashara uliyochagua kuifanya, kuwa mbunifu, siyo lazima biashara yako ihusishe ununuzi wa bidhaa au malighafi, pengine wewe utaanzisha biashara ya kutoa huduma, itakubidi pale badala ya kuorodhesha bidhaa au malighafi basi utaorodhesha posho za siku za wafanyakazi watakaotoa huduma ukiwemo wewe mwenyewe kama utahusika pamoja na gharama labda za steshenari nk.

Inawezekana pia labda wewe biashara yako ni ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha bidhaa, kwenye mahitaji yako ni lazima uhakikishe vitu muhimu vya kuanzisha kiwanda kama mashine, ujuzi na malighafi unavitaja na gharama zake zote.
Baada ya majibu hayo ya jumla hebu sasa tuje kwenye swali lako la msingi,

NATAKA KUFUNGUA DUKA LA KUUZA KADI ZA SIMU ZA KIGANJANI KWA BEI YA JUMLA KWA MTAJI WA SHILINGI 2,000,000/= (MILIONI 2), JE MTAJI HUO UTATOSHA?

Ndugu msomaji wangu kulingana na majibu ya jumla niliyokupa hapo juu, nadhani utakuwa umekwisha pata mwangaza kuhusiana na swali lako hili. Lakini pia sijafahamu ikiwa hiyo fremu ya duka au eneo unalosema umepata njia panda ya Segerea kama umeshalilipia kodi ya pango au umepewa na mhisani au ndiyo unategemea mtaji huo huo uliokuwa nao wa shilingi milioni mbili ndio utakaotumia hapo kiasi kulipia pango.


SOMA: Kuanzisha biashara ningali bado chuoni nasoma je, inawezekana?


Hata hivyo, vyovyote vile iwavyo, ni lazima ufanye zoezi kama nililoonyesha hapo juu na kama ukigundua kiasi cha fedha ulichokuwa nacho kitabakia kidogo sana kiasi cha kushindwa kununua mzigo au vocha idadi watu waliokushauri kuanza nazo, basi nakushauri biashara hiyo hebu iache kwanza na utafute biashara nyingine itakayoendana na mtaji uliokuwa nao. Ikiwa inatosha basi ruksa endelea.

Ikiwa itatosha na una moyo wa kutosha wa kuifanya biashara ya kuuza vocha za jumla basi ni vizuri hapo hakuna kitu kingine tena kitakachoweza kukuzuiak kuanzisha biashara uliyoichagua . Mtaji wa kutosha ni kigezo nyeti sana kwenye kufanikiwa au kufeli kwa biashara mpya inayoanza.

………………………………………………………………..

Mpenzi msomaji wa Jifunzeujasiriamali, kama unapenda kelewa maswala mbalimbali yahusuyo ujasiriamali na biashara kwa kina kabisa kama vile,

·       Namna ya kuanzisha biashara au kampuni
·       Kufanya utafiti wa biashara yeyote ile
·       Kuandika au kuandaa kichwani mpango wa biashara
·       Kusoma michanganuo halisi na iliyokamilika ya biashara mbalimbali zinazolipa hapa Tanzania
·       Kujua ikiwa biashara unayotaka kuanzisha italipa au kutengeneza hasara badala ya faida
·       Kutafuta soko la bidhaa/huduma zako
·       Utunzaji wa mahesabu na kumbukumbu za biashara yako
·       Namna ya kufanya mauzo kitaalamu
·       Jinsi ya kumhudumia mteja arudi tena na tena kwenye biashara yako.
·       Mbinu za kusimamia biashara kitaalamu
·       Matumizi ya teknolojia na mawasiliano katika kuboresha biashara.
·       Mbinu zinazotumiwa na matajiri wkubwa kutajirika na kuendelea kubakia kileleni muda wote.nk.

Yajue mambo hayo yote ndani ya KITABU CHA MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALIkwa bei ya shilingi elfu 10 tu kama ni softcopy na shilingi elfu 20 tu ikiwa utahitaji hardcopy. Kwa mawasiliano piga simu, 0712 202244  au 0765 553030

Ukinunua kitabu hiki unapata ofa ya kujiunga bure na blogu hii hapa ya SEMINA YA MICHANGANUO YA BIASHARA




Picha ni kwa hisani ya Swahiba Media.



0 Response to "MTAJI WA KUANZISHA BIASHARA YA VOCHA ZA SIMU JUMLA, MILIONI MBILI 2 INATOSHA?"

Post a Comment