UZURI WA BIASHARA YA UWAKALA WA TIGO PESA, M-PESA, AIRTEL MONEY NA EZY PESA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UZURI WA BIASHARA YA UWAKALA WA TIGO PESA, M-PESA, AIRTEL MONEY NA EZY PESA

Uwakala wa makampuni ya simu za mkononi, kufanya miamala ya kutuma na kupokea pesa hapa nchini Tanzania ni biashara inayokua kwa kasi  kubwa na haijaanza siku nyingi. Ni kama miaka mitano hivi  hapa na 7 kwa wenzetu Wakenya ambako ndiko huduma hii ilikozaliwa na baadae kusambaa katika mataifa ya Tanzania, Msumbiji, Lethoso, Misri, Afrika ya Kusini, Afghanistan na  Ulaya Mashariki.


Huduma hii ikiwa imeasisiwa na Vodacom chini ya Safaricom na baadae makampuni mengine nayo kuanzisha , huduma zinazotolewa ni kama vile, kuweka na kutoa pesa, kutuma pesa kwa watumiaji wengine wa mtandao na kwa wale wasiotumia mtandao, kulipia bili mbalimbali kama maji, umeme nk. Kununua muda wa maongezi na kuhamisha fedha  kwenda akaunti za mabenki au kinyume chake.


Kabla ya huduma hii kubuniwa, watumiaji wa simu za mkononi walipata shida sana wakifikiria njia rahisi ambayo wangeweza kuitumia  katika kuwatumia wapendwa wao pesa, wengi waliamua kutuma muda wa maongezi, na kisha anayetumiwa hulazimika kwenda kuuza muda huo wa maongezi kwa watu wengine kama njia ya kupata  kiasi cha fedha kilichotumwa. Ilikuwa ni njia ngumu na iliyogharimu muda. Wataalamu wa Vodaphone  baada ya kubaini tatizo hilo hapo mnamo mwaka 2007 wakaanzisha utafiti uliosababisha hatimae M- PESA kuzaliwa.

Tuachane sasa na historia hiyo ya m-pesa tuje moja kwa moja kwenye mada yetu, miaka kabla ya 2012, jiji la Dar es salaam lilisheheni vibanda vya kupigisha na kuchaji simu za mkononi, ambavyo wajasiriamali wengi wadogowadogo walijiajiri kupitia hivyo. Lakini ujio wa huduma za kipesa kupitia simu za mkononi umebadilisha kabisa sura ile na sasa katika kila kona ya jiji utaona vibanda lakini vingi vikiwa vinatoa huduma za pesa za makampuni mbalimbali yakiwamo Tigo, Vodacom, Airtel, Zantel, Smart na TTCL.


Biashara hii ya kuwa wakala wa makampuni hayo ya simu katika kufanya miamala ya pesa kwa wateja  mwanzoni ilionekana  kama vile siyo ‘dili’ nikiwa na maana kwamba haikuwa inalipa vizuri, hata ulikuwa ukienda katika makampuni ya simu kuomba laini kwa ajili ya uwakala ulikuwa unapewa chapchap. Muda unavyozidi kusonga mbele sasa hivi, hata mtu ukihitaji line kwa haraka, labda upitie kwa mtu aliyekwisha ipata vinginevyo ni lazima ufanye ufuatiliaji  kwa subira ndipo uweze kuipata.

Watu kuna kitu walichogundua katika biashara hii. Mara zote mjasiriamali aliyekuwa makini hupendelea urahisi katika kufanya biashara, simaanishi urahi wa bei,  la, bali ni urahisi katika uendeshaji usiokuwa na ‘longolongo’ nyingi kwa mfano, biashara hii hata kama unamuachia majukumu msaidizi ama mfanyakazi, huumii sana kichwa kwani  hesabu zake zinajulikana na isitoshe, miamala yote hurekodiwa kiteknolojia na kampuni husika ambapo huwa rahisi mwisho wa mwezi au kipindi cha biashara kuja kupewa kamisheni ya miamala iliyofanyika. Hakuibii mtu hapa.

Uzuri mwingine wa biashara hii ya uwakala wa makampuni ya simu ni kwamba, jioni baada ya kufunga kazi mjasiriamali unafahamu mara moja faida uliyopata katika siku husika kulingana na idadi ya watu na kiasi cha miamala waliyofanya. Husumbuani na mteja kwenye bei kwani bei zinakuwa zimeshapangwa tayari na makampuni, na hamna shida ya wateja kwani mahitaji ya huduma za kipesa ni mengi na mawakala bado ni wachache nchini.

Kuna vikwazo pia katika biashara hii, na kubwa likiwa ni suala zima la usalama. Ili kuanzisha biashara hii mahali fulani yafaa kwanza suala la usalama wa pesa na wewe utakayekaa hapo  litiliwe kipaumbele cha kwanza kabisa. Ikiwa ni duka au kibanda basi ni sharti uhakikishe, unajengea  ‘gril’kuzunguka dirisha na milango ili kuhakikisha  hapawi kivutio kwa wezi na majambazi wenye silaha.
........................................................................................................

Ndugu msomaji, kampuni yako ya Self Help Books publishers ltd inatangaza rasmi kwamba vile vitabu vilivyokuwa vimekwisha sasa zimeshachapwa nakala nyingine na vinapatikana ukiwa sehemu yeyote nchini, na wale waliokuwa wametoa oda zao pia zipo tayari. Ukihitaji kitabu chochote kile tuwasiliane kwa namba zilizoko katika blogu hii au 0712 202244 au 0765 553030

3 Responses to "UZURI WA BIASHARA YA UWAKALA WA TIGO PESA, M-PESA, AIRTEL MONEY NA EZY PESA"

  1. Asante kwa ushauri.... Me nipo chuo nataman kufanya Sana hii biashara ya Pesa za kimtandao Lakin Sina Elimu Sana na hii biashara.... Naomba msaada wa kiushaur

    ReplyDelete