MKOPO WA BENKI AU TAASISI ZA FEDHA: SOMA HAPA NA HUTAKAA UWALAUMU TENA! | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MKOPO WA BENKI AU TAASISI ZA FEDHA: SOMA HAPA NA HUTAKAA UWALAUMU TENA!

Mabenki na taasisi mbalimbali za fedha zinazotoa mikopo Tanzania, zimekuwa zikitolewa lawama na malalamiko lukuki kutoka kwa wateja wao pasipo wateja hao kufahamu vyema jinsi sheria na kanuni mbalimbali za nchi zilizoziweka benki na taasisi hizo zinavyofanya kazi. Ingawa kweli yapo baadhi ya malalamiko na lawama zinazotolewa kwa haki kabisa na wakopaji kama vile mambo ya rushwa, huduma mbaya nk. Na wala hapa sina nia ya kutetea upande wowote bali kuelezea hali halisi  jinsi ilivyo.

Malalamiko ya walio wengi hujikita zaidi kwenye masharti wanayokumbana nayo pindi wanapoamua kwenda kuomba mikopo, iwe ni mikopo ya biashara zao, kuendeleza ujenzi wa nyumba/makazi, kulipia masomo/chuo au shule, kununulia vifaa kama magari, mitambo nk.

SOMA: Kuendesha biashara na mtaji kidogo ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.

Mabenki na taasisi nyingine zote za fedha zipo kwenye biashara kama yalivyokuwa makampuni mengine yeyote yale ya kibiashara au watu binafsi, wanafanya biashara ya kukopesha fedha na malengo yao ya msingi kabisa ni kutengeneza faida kwa kutoza gharama(riba) kwenye zile huduma wanazozitoa kwa wateja wao. Hakuna kampuni au mfanyabiashara anayekubali kupata hasara wala kuingia kwenye makubaliano ya biashara yenye mashaka yasiyokuwa na uhakika wa kurudisha mtaji uliowekezwa na faida.

Baadhi tu ya malaamiko na lawama hizo wanazotupiwa taasisi za mikopo zikiwemo benki, ni kama hizi zifuatazo;

·       Benki siyo rafiki wa watu wadogo(masikini)

·       Benki na taasisi za fedha zina masharti magumu

·       Benki zina riba kubwa

·       Maafisa mikopo wengi huwabana sana wateja kwa masharti magumu siyo kwa maslahi ya benki au taasisi, bali kwa maslahi yao binafsi hasa ya kutengeneza mazingira ya kupatiwa rushwa.

·       Baadhi ya taasisi na mabenki hupendelea mteja aje akwame marejesho mwishoni karibu na kumaliza mkopo kusudi wao waje wauze dhamana zake, na hasa kama ikiwa dhamana zenyewe ni nyumba, kiwanja au gari. Wanunuzi huwa wao wao wenyewe maafisa au huwatuma watu wao kinyemela kwa kupanga nao dili.

·       Taasisi na mabenki mengi wana tabia ya kutokuweka bayana gharama mbalimbali na faini za mikopo kabla, na mteja huja kubaini wakati tayari amekwisha tia saini fomu za mkopo.

·       Taasisi na mabenki mengine huwahadaa wateja (Mithili ya mchinjaji anavyomrushia kuku mahindi au mtama kusudi tu apate kuingia ndani na kumbe lengo lake siyo kumlisha bali amkamate na kumchinja kama kitoweo) kwa ahadi tamutamu kupitia matangazo ya biashara na ukishachukua mkopo tu ndipo utakapojua ubaya au uzuri wao.

Kwanini basi wateja hutoa malalamiko hayo yote kwa mabenki na taasisi za mikopo?
Ni hulka ya binadamu tuseme karibu wote, kwamba hatupendi kulipa deni. Mtu angependelea baada ya kukopa basi arejeshe baada ya muda atakaotaka yeye mwenyewe, na hata kama ikiwezekana basi asilipe deni hilo kabisa. Kulipa deni mara nyingi huleta maumivu fulani kwa yule anayelipa deni, ingawa ni wajibu wake na haki kufanya hivyo.

SOMA NA HII: Je, Mtanzania unakopesheka na taasisi za fedha na benki?

Kutokana na sababu hiyo, Serikali na mamlaka za nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, zimeweka sheria na taratibu kuwa mabenki na taasisi za fedha kote nchini kufuata taratibu maalumu ili kuhakikisha kwamba mitaji yao ambazo ni fedha na amana za watu walizohifadhi katika mabenki na taasisi hizo hazipotei kirahisi na zinazunguka kwa ajili ya watu wengine nao waje wakope hapo baadaye ikiwa ni pamoja na taasisi na mabenki hayo kujiendesha, kulipa wafanyakazi wake pamoja na kulipa kodi na gharama mbalimabali za uendeshaji biashara.

Hitaji muhimu zaidi (mashart) Maafisa Mikopo wa Benki, Saccos na taasisi nyingine za mikopo wanayotaka mkopaji atimize kwanza kabla hajapewa mkopo wa biashara.

Dhana iliyojengeka miongoni mwa wakopaji wengi ni kwamba hitaji kubwa na la msingi kushinda yote benki au taasisi wanalohitaji toka kwako ni DHAMANA YA MKOPO, lakini ukweli wenyewe ni kuwa wala Dhamana ya mkopo siyo kitu cha kwanza wanachokiangalia, kuna vigezo vingine muhimu zaidi wanavyotaka wavijue ndipo waweze kutambua ikiwa unazo sifa zinazostahili kupewa mkopo. Vigezo hivyo ni hivi hapa chini;

1. Kipato chako.
Wanahitaji kujua unapata shilingi ngapi kwa siku, wiki, mwezi au mwaka na chanzo/vyanzo vya kipato hicho ni kitu gani. Je ni biashara au ajira?. Mathalani ni biashara, watataka kujua ikiwa biashara hiyo ni yakwako, halali, imesajiliwa kisheria na ni endelevu. Ndiyo maana watakutaka uwaonyeshe hati mbalimbali mbali zinazoweza kuthibitisha mambo hayo kama vile leseni ya biashara, namba ya mlipa kodi TIN nk.

2. Mwenendo na historia yako ya ulipaji madeni siku za nyuma.
Wanataka wafahamu ikiwa una rekodi nzuri ya ulipaji madeni, siyo kwa taasisi husika tu bali na kwa taasisi nyinginezo au mabenki uliyowahi kukopa. Kwa mfano serikali ya Tanzania chini ya Benki kuu BOT imeanzisha wakala(taasisi maalumu) ambayo kazi yake ni kufuatilia na kutunza kumbukumbu zote za wakopaji kutoka taasisi na mabenki yote nchini zikiwemo hata mamlaka za umeme na maji kama Tanesco na Dawasco. Benki au taasisi zinapotaka kutoa mkopo kwa mteja huwasiliana na mamlaka hiyo kupata taarifa za mteja husika ikiwa alishawahi kusumbua sehemu nyingine au la. Taarifa zako zikisoma una alama nzuri basi inakuwa rahisi kukukopesha.

Ufanyeje ili kutokuwekewa alama mbaya kwenye taasisi hiyo inayotunza historia ya wakopaji mikopo na madeni?
Lipa madeni yako yote kwa wakati, Usikope kutoka taasisi au mabenki mengi tofauti kwa wakati mmoja hasa ikiwa wewe bado ni mkopaji mdogo. Kufanya hivyo mara nyingi kutawafanya maafisa wa benki kukutilia mashaka na hata wengine tu kutokana na udhaifu wa kibinadamu wanakuwa na wivu, ni kwa nini ukakope kwa washindani wao, hivyo hutafuta njia ya kukukomesha na ikitokea tu umefanya kosa hata kama ni dogo la bahati mbaya basi watakuripoti kwenye taasisi hiyo kusudi wakukomoe.

Upo ushahidi wa watu waliofanyiwa hivyo hapahapa Tanzania na kwa kuwa wakopaji wengi uelewa wao juu ya taasisi hiyo bado hawajawa nao basi wengi wataumizwa bila kujua.

SOMA: Unaogelea ndani ya maji baridi huku ungali unakufa kwa kiu.

Kwa nchi za wenzetu zilizoendelea jambo hili lipo wazi sana na huwezi ukasingiziwa alama mbaya uwongo kwani unapewa fursa ya kujua maafisa wa benki wanachokuripoti na kama watakuhujumu kwa kukutolea taarifa za uwongo ili kukukomoa, unakuwa na uwezo wa kukata rufaa kwenye hiyo taasisi. Kosa kwa mfano la kuchelewesha marejesho siku moja au mbili sidhani kama linaweza kukufanya uwekewe alama mbaya za kukufanya usindwe kwenda kukopa mahali pengine.

3. Tabia yako ya uwekaji akiba.
Watapenda kufahamu kama unatabia ya kuweka akiba, na ndiyo maana mabenki au taasisi nyingi humtaka mkopaji kabla ya kupewa mkopo kwanza awe ameshafungua akaunti katika benki au taasisi husika angalao miezi sita au mwaka kabla, ili kuona mwenendo wake wa kujiwekea akiba ikiwa ni pamoja na kufahamu mzunguko wake wa pesa katika biashara au mshahara upoje. Ikiwa mzunguko huo wa fedha ni mzuri (chanya)  basi uwezekano wa kupata mkopo unakuwa mkuwa zaidi.

4. Deni ulilokuwa nalo.
Kama ilivyo kwa historia ya ulipaji madeni ya nyuma, pia wanaangalia ni deni kiasi gani ulilokuwa nalo kwa wakati huo. Inawezekana umechukua mkopo mahali pengine na bado haujamalizia. Inakubidi taarifa hizo uwape mapema na hata ikiwezekana uonyeshe ni kwa jinsi gani mkopo unauomba dhamana zake hazitaingiliana na mikopo mingine uliyokuwa nayo kusudi kuwashawishi kuwa utakapokuja kushindwa kulipa mkopo hawatapata shida ya kuuza dhamana ulizoziweka.

Kinyume na hapo ukiwaficha kuwa huna deni mahali pengine wakaja kugundua kwa njia zao wenyewe ikiwemo ile taasisi ya kuweka kumbukumbu za wadaiwa basi utachukuliwa kama mtu usiyekuwa na sifa za kupewa mkopo.

5. Dhamana ya mkopo.
Na mwisho kabisa ndiyo wanaangalia ikiwa unayo dhamana itakayotumika kulinda mkopo ikiwa utafika mahali mkopo ukakushinda kulipa. Mara nyingi dhamana huwa ni mali ulizokuwa nazo hasa zisizohamishika kama vile nyumba, kiwanja au shamba, lakini pia dhamana yaweza kuwa ni vyombo vyako vya ndani, gari, mashine, fedha ulizoweka katika akaunti ya kudumu ya benki, pia unaweza ukadhaminiwa na mtu mwingine aliye na mali au anayefanya kazi sehemu inayotambulika.

HITIMISHO.
Kabla ya kutoa malalamiko kwa taasisi za mikopo na mabenki, wakopaji inatupasa kwanza kufahamu kuwa, mkopo/mikopo siyo ruzuku wala zawadi, bali sheria za nchi zinatutaka turejeshe mikopo tunayokopa iwe ni ya benki, saccos, ama taasisi nyingine yeyote ile ya pesa.

Ndiyo maana unaposhindwa kulipa mkopo uliokopa maafisa wa benki au taasisi husika huwa na mamlaka kisheria ya kuja kukufilisi kwa kuuza mali zako ulizoziweka kama dhamana iwe ni nyumba, gari, kiwanja , shamba, vyombo vya ndani au mali nyingine yeyote ile unayomiliki na kisha mkopaji kuanza kulalamika na kuyaona mabenki au taasisi za mikopo ni wabaya wasiokuwa na huruma.

SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara unayoipenda.

Kwa upande wa mabenki nayo na taasisi za kifedha, wajitahidi kuwaelimisha wateja wao maswala mbalimbali, wasifikirie kuwa wateja wa kawaida wanaelewa kila kitu, wengine hawana uelewa kiasi hicho. Wasisubirie tu kuja kuwakomoa siku za kuomba mikopo. Vile vile maafisa mikopo wengine kusema ukweli ni kero kubwa hasa linapokuja suala la “kitu kidogo” ni bora kabisa mabenki na taasisi zote wakasisitiza kwa dhati kubainisha gharama zote zinazotakiwa kwa jumla ndipo mtu apewe mkopo na kuwe na uwezekano wa mteja kuonana na meneja iwapo ataona afisa mkopo anamuwekea vizingiti visivyokuwa na umuhimu.

Inafika mahali mtu ukichukua mkopo wa mwanzo usipompa afisa chochote baada ya kuondoka pale dirisha la benki, basi ujue kabisa na huo ndio utakaokuwa mkopo wako wa mwisho katika benki au taasisi hiyo. Atakujengea vigingi vya ajabu na longolongo kibao mpaka uonekane wewe hufai kabisa kukopeshwa tena.

…………………………………………………………………..

Msaada zaidi kwa Mkopaji.
Ili uweze kupata mkopo kwa urahisi zaidi kutoka taasisi za fedha na benki kuna vitu unavyopaswa kuzingatia navyo ni kama hivi hapa chini;

Kabla haujakwenda kukutana na afisa mkopo wa benki au taasisi unayotaka kukopa, kwanza kaa chini utafakari na kupanga mambo mbalimbali ambayo unajua ni lazima watu wa benki au taasisi watakwenda kukuuliza. Usifike pale ukaanza tena kubabaika. Njia rahisi itakayokuwezesha kupanga kila jambo kuhusiana na biashara yako na ukapata kila jibu la swali unaloweza ukaulizwa na afisa wa benki ni kupitia utafiti au mchanganuo wa biashara ambao siyo lazima umtafute mtaalamu aliyebobea kukufanyia, labda kama ni biashara kubwa kubwa za mamilioni ya pesa. Kwa biashara zile ndogo tu za kawaida au za kati wewe binafsi unaweza ukafanya utafiti na kuchanganua biashara yako kwa mahitaji ya kuiendesha kwa ufanisi zaidi na hata kujibu baadhi ya maswali utakayoulizwa na wadau kama benki au wabia.

Kuchanganua biashara pia itakuwezesha kupata jibu la swali muhimu sana kwako wewe binafsi la ni kiasi gani cha mkopo utakachohitaji katika kuuongezea nguvu mtaji wako. Jibu hili litakuwezesha kukwepa kuomba mkopo mkubwa kupita mahitaji yako au mdogo kushinda mahitaji, jambo linaloweza kukusababishia matatizo hapo baadaye.

Unaweza wewe mwenyewe hata pasipo kuandika kwenye karatasi kufanya utafiti wa biashara yako na kutengeneza kichwani mpango/mchanganuo ambao utakupa majibu mengi yatakayosaidia hata katika uendeshaji wa biashara husika.

Biashara yeyote ile ina vipengele ambavyo ni lazima vipitiwe wakati wa mwenendo mzima wa kuiendesha, vitu kama vile, una malengo yapi na biashara hiyo, umiliki wa biashara upoje, mtaji wa biashara ni kiasi gani na utaupata vipi, ni watu gani watakaohusika katika biashara hiyo, matarajio ya mauzo yapoje, utauza bidhaa/huduma shilingi ngapi, utazalisha au kununua bidhaa kiasi gani, wateja wako watarajiwa ni kina nani, utajitangaza vipi kuwafikia wateja watarajiwa, faida yako baada ya wiki, mwezi na mwaka unakadiria inaweza kuwa kiasi gani nk.

Ni mambo ya msingi kabisa mfanyabiashara na mjasiriamali yeyote hujiuliza hata ikiwa hataki kuandika kitu kinachoitwa mpango rasmi wa biashara, na vitu vyote hivyo hupatikana baada ya mtu kufanya utafiti na utafiti haimaanishi ule wa kitaalamu la hasha, hata kwa mtu mwenyewe kuzunguka na kuchunguza mtaani, tayari huo ni utafiti.

Kitabu cha Michanganuo ya biashara na Ujasiriamali kimeelezea vizuri sana mada hizi mbili za “Kufanya utafiti wa biashara na masoko” pamoja na Namna ya kutayarisha mpango au mchanganuo wa biashara” katika viwango vyote, yaani kwa mtu anayependa kuandika mchanganuo rasmi au hata yule mtu wa kawaida kabisa anayependa tu kufahamu vitu hivyo kwa ajili ya uendeshaji mzuri wa biashara yake ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa vipengele mbali mbali kama hivyo ambavyo watu wa mikopo wanaweza wakakuuliza unapotaka kwenda kuomba mkopo benki au taasisi yeyote ile.

Kitabu hiki mbali na kuwa na kozi hizo za Utafiti na namna ya kuandaa Michanganuo ya biashara, Michanganuo yenyewe halisi unayoweza kuitumia kama kielelezo au mifano unapojifunza, vile vile kina masomo mengine karibu yote ya ujasiriamali kuanzia, Ujasiriamali wenyewe na jinsi ya kuanzisha biashara, Uendeshaji wa biashara: namna ya kutafuta masoko, mifumo mbalimbali ya biashara, utunzaji na uwekaji wa kumbukumbu za biashara yeyote ile, namna ya kutangaza bidhaa au huduma zako, jinsi ya kusimamia vizuri biashara yako, mbinu bora za kufanya mauzo na njia mbalimbali halali watu wanazotumia kutajirika haraka.

Bei ya kitabu hiki kikiwa katika mfumo wa kielektroniki kwa njia ya E-mail ni shilingi elfu kumi, 10,000/=

Kitabu cha kawaida cha karatasi bei yake ni Shilingi elfu ishirini, 20,000/=

Wasiliana na sisi kwa namba, 0712 202244

Au pia unaweza ukatembelea >>SMARTBOOKSTZ kwa maelezo zaidi.

Tunapatikana pia kwenye;0 Response to "MKOPO WA BENKI AU TAASISI ZA FEDHA: SOMA HAPA NA HUTAKAA UWALAUMU TENA!"

Post a Comment