Utajiri ni wenye aibu na woga, umasikini ni shupavu katili na hauhitaji mipango | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Utajiri ni wenye aibu na woga, umasikini ni shupavu katili na hauhitaji mipango


FIKIRI UTAJIRIKE THINK & GROW RICH SURA YA 10 SEHEMU YA 4
Soma, fikiri na tafakari kadiri utakavyokuwa ukisoma. Mara moja somo zima litajifunua na utaliaona kwa mapana. Sasa utaona undani wa sura mojamoja.

Pesa zina aibu na ni zenye hila, ni lazima zibembelezwe na kupatikana kwa njia ambazo siyo tofauti na zile zinazotumika na mpenzi aliyedhamiria kumtafuta mwenza. Na kwa kadiri vinavyofanana, nguvu inayotumika katika kubembeleza(kutongoza) pesa haina tofauti kubwa na ile inayotumika katika kumtongoza mpenzi. Nguvu hiyo  inapotumika vizuri katika kutafuta pesa, ni lazima ichanganywe na Imani. Ni lazima ichanganywe na Shauku. Ni lazima ichanganywe na Msimamo. Ni lazima itumiwe katika mpango, na mpango huo ni lazima uwekwe kwenye vitendo.

Pesa zinapokuja kwa kiasi kikubwa zinazojulikana kama ‘Pesa nyingi’ hutiririka kwa yule anayezikusanya kwa urahisi kama vile maji yatiririkavyo chini ya mlima. Upo mfereji mkubwa wa nguvu isiyoonekana ambao unaweza kulinganishwa na mto, isipokuwa kwamba unatiririka kuelekea pande mbili. Upande mmoja hubeba wale wote wanaoingia katika upande huo wa mfereji kwenda mbele na juu kuelekea utajiri na upande mwingine hutiririka upande mkabala ukibeba wale wote walio na bahati mbaya kuingia humo(na hawawezi kujinasua wenyewe kutoka humo) kuelekea chini katika taabu na umasikini.

Kila mtu aliyejikusanyia utajiri mkubwa anatambua uwepo wa mfereji huu wa maisha. Ndani una mchakato wa mtu kufikiri. Mihemko chanya ya fikra hutengeneza upande wa mfereji ule unaompeleka mtu kwenye utajiri. Mihemko hasi hutengeneza upande ule unaompeleka mtu chini kwenye umasikini.

Hili hubeba wazo lenye umuhimu mkubwa kwa mtu anayefuatilia kitabu hiki kwa lengo la kujipatia utajiri. Ikiwa kama upo katika upande wa mfereji wa nguvu unaolekea kwenye umasikini, hii inaweza kuwa kama makasia ambayo unaweza ukaitumia kujisogeza mbele mwenyewe kuingia ndani upande mwingine wa mfereji. Inaweza kukusaidia tu ikiwa utaiweka katika matumizi na kuitumia. Kuisoma tu peke yake na kujadili aidha kwa njia moja au nyingine haitakunufaisha kwa njia yeyote ile.

Baadhi ya watu hupitia uzoefu wa kupokezana kati ya upande chanya na upande hasi wa mfereji, wakati mmoja kuwa katika upande chanya na wakati mwingine upande hasi. Anguko kubwa la soko la hisa Marekani(The wall street crash ’29) lilifyagia mamilioni ya watu kutoka upande chanya kwenda upande hasi wa mfereji. Mamilioni hao walipambana –baadhi yao katika hali ya kukata tamaa na woga-kurudi tena katika upande chanya wa mfereji. Kitabu hiki kiliandikwa mahsusi kwa ajili ya hao mamilioni.

Umasikini na utajiri mara nyingi hubadilisha nafasi. Umasikini unaweza na kwa ujumla unaweza kwa hiyari kuchukua nafasi ya utajiri. Utajiri unapochukua nafasi ya umasikini, mabadiliko kwa kawaida huletwa kupitia mipango iliyopangwa vizuri na kutekelezwa kwa uangalifu. Umasikini hauhitaji mipango. Hauhitaji mtu kuuongoza kwasababu ni shupavu na katili. Utajiri ni wenye aibu na woga. Ni lazima ‘uuvute’

Mtu yeyote anaweza akatamani utajiri, na watu wengi hufanya hivyo, lakini ni wachache tu wanafahamu kwamba mpango kamili pamoja na Shauku kali kwa ajili ya kupata utajiri ndiyo njia pekee za uhakika za kuupata.

...............................................................

Tumefika mwisho wa Sura hii ya 10 wiki ijayo tutaanza Sura mpya ya 11, "MAAJABU YA KUBADILI FIKRA ZA KIMAPENZI"

Usikose Semina ya kuandika mpango wa biashara ya mgahawa wa chakula siku ya Jumamosi tarehe 3 Novemba 2018 itakayofanyika kupitia watsap, kujiunga lipia kiingilio sh. elfu 10 kupitia namba za simu, 0712202244  au  0765553030.


 FUNGUA SURA NA KURASA NYINGINE ZOTE ZILIZOKWISHAWEKWA HAPA
 


0 Response to "Utajiri ni wenye aibu na woga, umasikini ni shupavu katili na hauhitaji mipango"

Post a Comment