Mbinu za kufanikiwa kufikia malengo katika uwekezaji wowote utakaofanya. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Mbinu za kufanikiwa kufikia malengo katika uwekezaji wowote utakaofanya.


MAFANIKIO KATIKA UWEKEZAJI
Mjasiriamali kujijengea vitegauchumi tofautitofauti ndio njia bora zaidi ya kujihakikishia mzunguko chanya wa fedha muda wote. Hata hivyo mtu kujijengea vitegauchumi hivyo siyo jambo linaloweza kufanywa kwa siku moja au mbili hasa kwa wale wajasiriamali vijana au wanaoanza na ambao hawaelewi waanzie wapi. Mjasiriamali yeyote yule mdogo au mkubwa huna budi kuzijua mbinu za kufikia malengo yako kifedha katika maisha.

Kabla mtu yeyote hajaanza kujikusanyia utajiri kwa njia ya uwekezaji vitegauchumi anapaswa kwanza afahamu tofauti iliyokuwepo kati ya rasilimali(asseti) na Madeni(liabilities). Watu wengi hutumia pesa zao kwa vitu wanavyodhania kuwa ni rasilimali/mali na kwamba vinaweza hatimaye kuwafanya wawe matajiri lakini kumbe vitu hivyo huzidi kuwadidimiza kwenye lindi la umasikini kwa kuwabebesha mzigo mzito wa gharama na madeni. Watu hawa huishia kukata tamaa kabisa ya kufanikiwa maishani.


Nitatolea mfano mmoja, mtu anaweza akaamini kwamba kwa kujenga nyumba basi atakuwa ameshawekeza kitegauchumi au rasilimali  itakayomhakikishia mzunguko chanya wa fedha hapo baadae lakini ukweli ni kwamba kujenga nyumba itategemea ikiwa nyumba hiyo umejenga kwa malengo gani. Nyumba unayojenga itakuwa rasilimali(asseti) endapo tu itakuwa na uwezo wa kukuzalishia pesa badala ya kukumalizia pesa.

Nyumba unayoilipia kodi ya majengo na gharama nyinginezo kama za ukarabati, umeme na maji pasipo kukuingizia hata senti tano hiyo siyo asseti bali ni deni(liability).

Ikiwa utajenga nyumba na kisha ukaweka wapangaji watakaokuwa wakikulipa kodi kila mwisho wa mwezi basi nyumba hiyo unaweza ukaiita rasilimali(asseti). Hali ni hivyohivyo ilivyo kwa yule anayenunua kitu kama gari. Gari lina gharama kama vile, gharama za bima, gharama za mafuta na hata matengenezo inapotokea limeharibika. Ikiwa basi gari hilo haliingizi fedha yeyote, hiyo siyo rasilimali bali ni deni kwani linakufanya utoe fedha ulizokuwa nazo badala ya kukuingizia pesa. Tena mbaya zaidi ni kwamba kitu kama gari lina tabia ya kupoteza thamani yake kidogokidogo kadiri muda nao unavyosonga mbele.


Unapofahamu kitu hiki mapema, ndipo unapoweza kuwa makini na katika nafasi nzuri zaidi ya kukwepa kuwekeza mtaji/pesa zako zote kwenye vitu vinavyoweza kukugharimu zaidi siku za baadae. Utatambua ni kwanini unatakiwa kujijengea rasilimali za kweli katika uwekezaji wako wa kifedha na jinsi ya kutimiza malengo yako ya kujiongezea utajiri na mali zaidi.

Faida za Mjasiriamali kujijengea Rasilimali. 
1.Rasilimali hukuongezea fedha zaidi.
Kitu chochote kile utakachokinunua na kikakuzalishia faida(kuongeza mzunguko wako wa fedha) kitu hicho ni rasilimali. Rasilimali inaweza ikawa ni hisa, hati za dhamana(bond), mashine, ardhi ama hata biashara yeyote ile yenye uwezo wa kuzalisha faida inaweza kuwa rasilimali. Lakini ikiwa biashara inakuongezea gharama na mzigo wa madeni hiyo haiwezi tena kuwa ni rasilimali bali ni deni.


Njia rahisi zaidi ya kutajirika duniani ni kuhakikisha unatumia fedha zako kununulia rasilimali. Hata rasilimali watu kwa mfano, usikubali kukaa na mfanyakazi yeyote yule asiyeongeza chochote katika kuhakikisha mafanikio makubwa kwenye biashara yako.

Kabla hujanunua kitu chochote hebu jiulize kwanza mwenyewe ikiwa kama kweli kitu hicho kina uwezekano wa kuzalisha kipato au kuchukua pesa kutoka mfukoni mwako. Lengo lako linapaswa kuwa ni kujilimbikizia rasilimali zinazoweza kukutengenezea fedha za ziada kuliko kukukaushia fedha kupitia gharama itakazokupa. Ikiwa utakuwa na uwezo wa kutengeneza kipato cha ziada kila mwezi ni vizuri zaidi kwani mzunguko wako wa fedha utakuwa chanya. Hii ni mbinu ya kufanikiwa katika biashara au uwekezaji wowote ule.

2.Rasilimali huongezeka haraka zaidi unapojiwekea misingi imara ya utunzaji wa pesa.
Kwa wale wanaofanikiwa kujijengea rasilimali za uhakika, utakuta pia kabla ya hapo walianza kwanza kujijengea misingi  madhubuti ya kifedha. Wana nidhamu ya hali ya juu kwenye pesa, ni wavumilivu katika kujiwekea akiba na wanafahamu vyema jinsi ya kujiwekea malengo  yanayoweza kutimizika kama vile kujiwekea akiba ya kutosha kabla ya kuamua kuwekeza katika miradi na vitegauchumi.


Siyo rahisi kuishi maisha pasipo kupitia matukio yasiyotarajiwa kama vile majanga mbalimbali ya asili mfano mafuriko nk. Ni hivyohivyo na kwa upande wa biashara au uwekezaji rasilimali, kuna vipindi mambo huweza kuwa magumu  na biashara kushuka lakini kitu kikubwa cha kujiuliza, ni lini  na ni kwa kiasi gani hali hiyo itaweza kukugharimu. Hapa unatakiwa kuweka mipango ya kifedha(makisio) pamoja na kuweka akiba ya pesa. Hii itakupunguzia sana hatari ya kuingia madeni yasiyokuwa ya lazima hata kama majanga na vikwazo vitajitokeza.

3.Rasilimali nyingi hukupa uhuru tofauti unaoutaka.
Kumiliki rasilimali zinazoweza kubadilishwa kuwa pesa taslimu haraka kama vile hisa au vito vya thamani kunakupa uhuru mkubwa pale utakapohitaji fedha haraka kwani hautapoteza muda mwingi kutafuta mteja. Lakini kwa rasilimali mfano wa nyumba au ardhi, hizi ingawa zinaweza zikachukua muda mrefu kuuzika lakini pia siyo mbaya kwani zinaweza kukupa uhuru mwingine wa kifedha ambao utahitaji kuwa na subira kidogo.

Kwahiyo basi ikiwa una uwezo wa kumiliki rasilimali tofauti tofauti na zitakazokupa uhuru tofauti pia unaweza kuamua kuziuza muda wowote ule rasilimali hizo ikiwa utaona kama zitakupa faida nzuri na kuamua kununua nyingine ukitaka.

HITIMISHO.
Ili kuweza kuwa mwekezaji uliyebobea, jielimishe vizuri mambo mbalimbali kuhusiana na uwekezaji  kusudi uweze kuwa na mikakati sahihi iakayokuwezesha kufanya maamuzi mazuri pale soko litakaposhuka au kupanda na mwisho utajikuta ukifanikiwa katika kila uwekezaji utakaoamua kuufanya.
…………………………………

Ndugu msomaji wa makala hii,

Makala zinazohusiana na fedha na mzunguko wa fedha katika biashara zetu nazitoa pia kila siku katika group la wasap la michanganuo-online. Ikiwa unapenda kujifunza zaidi karibu uje ujiunge kwa mchango kidogo wa sh. Elfu 10. Unapata pia masomo yote yaliyopita katika group hilo, semina, vitabu na michanganuo kamili bunifu ya biashara tuliyowahi kuandika.

Somo la leo Septemba 21 2018 ni hili hapa chini; 

"KWANINI WANAOSEMA NIKISHINDA MILIONI 100 BAHATI NA SIBU NITAFANYA HIKI NITAFANYA KILE NI WAONGO?" 

Namba zetu ni:
0712202244 wasap: 0765553030
Asante sana
Peter A. Tarimo

0 Response to "Mbinu za kufanikiwa kufikia malengo katika uwekezaji wowote utakaofanya."

Post a Comment