WAFANYAKAZI KWENYE KAZI ZA AJIRA WENGI HAWANA FURAHA, UPO UKWELI WOWOTE AU NI UZUSHI MTUPU? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WAFANYAKAZI KWENYE KAZI ZA AJIRA WENGI HAWANA FURAHA, UPO UKWELI WOWOTE AU NI UZUSHI MTUPU?


WAAJIRIWA WENYE FURAHA KAZINI
Ni jambo la kushangaza sana ukisoma au kuelezwa ripoti ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu zinazohusiana na suala zima la furaha ya waajiriwa katika kazi mbalimbali. Mambo yaliyokuwa gumzo na yanayoonekana kubishaniwa zaidi miongoni mwa waajiriwa wenyewe na hata wale waliokuwa nje ya ajira kwa ujumla ni ikiwa, ufanisi wa kazi kwa mwajiriwa aliye na furaha kazini ni mkubwa kushinda ufanisi wa mwajiriwa yule asiyekuwa na furaha kazini.

Jambo hili kuhusiana na furaha kazini limezua sintofahamu kubwa hadi kusababisha wataalamu mbalimbali waliobobea katika fani zao kuamua kulifanyia tafiti zilizopelekea kuibuka matokeo hayo ya kustaajabisha. Nitakueleza matokeo hayo ya kushangaza taratibu kadiri utakavyoisoma makala hii, hivyo tafadhali ‘stay tunned’ hakikisha tunakwenda pamoma mpaka mwisho wa makala.

Tukiachana kwanza na huo utafiti kwa muda, tuendelee kwanza na mada yetu hii ya ikiwa kama kuna ukweli wowote kwamba walio katika ajira wengi hawana furaha……

Furaha ni kitu nyeti sana maishani, maono na malengo ya karibu kila mwanadamu, vyote dhumuni lake kubwa ni kuwa na furaha maishani au akhera, hivyo furaha ijapokuwa utaona  katika somo hili tutaegemea zaidi furaha kwa waajiriwa wawapo makazini lakini vilevile somo lina manufaafa makubwa hata kwa wajasiriamali kwani uwe umeajiriwa, umeajiri au umejiajiri mwenyewe, wote wanahitaji furaha, wanachokitafuta siku zote ni furaha katika nafsi zao, na si hivyo tu bali wote pia wanahusika kwa namna moja ama nyingine katika mazingira ya kazi nikiwa na maana pale shughuli au biashara zinapofanyikia.


Kwanza kabla hatujaingia ndani zaidi kwenye mada yetu hii, hebu tutazame furaha ni nini? Furaha ni hali ya hisia au akili inayomtokea binadamu pale anapojisikia vizuri aidha kiafya, bahati, kiusalama, kiimani, kiuchumi au kwenye mafanikio mengine yeyote yale. Hii ndiyo kusema kwamba furaha ni suala la mtu binafsi zaidi. Sasa tunapoongelea furaha kwa mtu yeyote yule awe ameajiriwa au mjasiriamali hutegemea sana vigezo viwili vkubwa, watu huweza kuwa na furaha kutokana na vigezo hivyo 2 ambavyo ni;

·       Mazingira wanayofanyia kazi
·       Mazingira yao binafsi

Mada yetu hii itakwenda kujikita zaidi katika kigezo cha kwanza ambacho ni mazingira mtu anayofanyia kazi. Sasa basi Mwajiriwa au tuseme mfanyakazi anawezaje kuwa na furaha? Zipo pia njia kuu tatu ambazo mwajiriwa yeyote yule anaweza akaijenga furaha yake juu yake navyo ni hivi hapa chini;

1)  Kwa kutokufanya kazi!

2)  Kwa kujenga uvumilivu na mshikamano na taasisi/kampuni anayofanyia kazi pamoja na watu waliopo pale.

3)  Mahitaji yake kuendana sambamba na malengo yake.

Hebu sasa tujaribu kuzifahamu vizuri zaidi njia hizo tatu mtu aliye katika ajira anazoweza akapata furaha;


1.“Kutokufanya kazi”
(Mtu kufanya kazi uipendayo ni sawa na kutokufanya kazi)
Bila shaka kila mtu angependa kufanikisha kitu fulani katika fani yake aliyochagua maishani. Watu wanataka kuleta tofauti katika fani hizo huku wakikidhi mahitaji yao ya kimaisha . Jambo hili hasa ndiyo kiini cha maisha yenye furaha kamili kazini(katika ajira).


Watu hulitumia neno KAZI A au AJIRA wakimaanisha kile mtu anachokifanya ili kujipatia riziki au kuishi lakini wakati mtu unapofanya kile kitu(kazi) unayoipenda unakuwa haufanyi tena ‘KAZI’ aslani, hapo ni sawa na hujaajiriwa, bali unafanya kazi hiyo kwasababu unaipenda, UNA MAPENZI NAYO na inakufanya uwe na FURAHA.

Lakini kwa bahati mbaya sana mara nyingi mahitaji ya binadamu yale ya muda mfupi ya kila siku hufunika shauku hiyo(mapenzi hayo kwa kazi) na hatimaye kufanikiwa kuizima kabisa ndoto nzuri uliyokuwa nayo awali. Kutimiza mahitaji ya muda mfupi ambayo kwa kiasi kikubwa hutokana na kuiga kutoka kwa watu wengine au rika kuna msukumo mkubwa na mahitaji hayo huzunguka juu ya vitu hivi vikubwa vifuatavyo;

·       Pesa
·       Faida
·       Ubora wa maisha
·       Cheo/nafasi na malaka

Vitu nilivyovitaja hapo juu huonekana kuwa vya kuvutia mno kiasi kwamba watu wengi hulazimika kuamini kwamba hivyo ndivyo malengo ya ajira/kazi ambayo kimsingi hawaipendi au hawana furaha nayo, wanaifanya kwa vile tu kazi hiyo inalipa vizuri. Hebu jaribu kufikiria inaingiaje akilini kumkuta injinia au daktari akifanya kazi ya uhasibu? Au Mtaalamu aliyebobea katika masuala ya kiuchumi akifanya kazi ya siasa?.


Matokeo au zao la ajira ndilo hugeuka kuwa lengo kuu la ajira kwani pesa au cheo ni zao tu la ajira na siyo lengo. Na kwa namna hii yale mapenzi na kazi yanakuwa tayari yamekwisha uwawa. Sasa watu wanaweza kuwa na AJIRA zilizokuwa na FURAHA ikiwa tu wataacha kuruhusu haya mahitaji ya muda mfupi kuwaendesha.

2. Kwa kujenga uvumilivu na mshikamano na taasisi/kampuni anayofanyia kazi pamoja na watu waliopo pale.
Tumezoea kuona kwamba mtu anapoajiriwa mahali au kujiunga na taasisi fulani mwanzoni kabisa huonyesha heshima na kutoa sifa zote nzuri kwa kampuni/taasisi na uongozi wake  mzima. Lakini taratibu huanza kuleta upinzani na kuonyesha kutokujali tena. Na mwishhowe huanza kuonyesha chuki waziwazi na kuanza kusaka ajira nyingine mpya.


Suala ni kwamba uongozi umebadilika? Au kampuni imebadilika? Hakuna hata kimoja kilichobadilika kati ya hivyo 2, Sasa ni kitu gani kilichobadilika? Jibu ni MTAZAMO! Hilo tu basi. Kila taasisi au binadamu sawasawa na ilivyokuwa kwa mtu na mchumba wake wanapooana, mwanzoni kabisa wanapokutana kila mmoja huonekana mzuri mbele ya mwenzake na sababu kubwa ni kwamba kila mmoja kati yao anataka aonyeshe ubora wake wa kiwango cha juu kabisa mbele ya mwenzake, lakini kadiri uhusiano huo unavyokua siku hadi siku kila upande hujifunza kuhusiana na mwenzake na ikiwa mmoja kati yao tuseme labda ni mwajiriwa atashindwa kuendana /kushikamana au kuvumilia mtazamo wa mwajiri, taassisi au kampuni anayofanyia kazi basi ujue kutoridhika nako huanza kukua taratibu huku furaha nayo ikitoweka.

Hakuna taasisi au kampuni  iliyokuwa kamilifu kwa asilimia 100% na wala pia hakuna mwajiriwa aliyekuwa mkamilifu kwa kiwango cha asilimia mia moja 100%. Kikubwa kinachotakiwa hapa ni kuvumiliana na kuchukuliana mitazamo tofauti. Ili kuwepo na furaha katika kazi yeyote ile mtu anatakiwa kutazama mambo kwa jicho la tatu au kuvaa viatu vya mtu mwingine. Kwa kufanya hivyo tunakuwa na uwezo wa kuelewa mambo kwa kina zaidi  na kuendana na mitazamo ya watu wengine katika taasisi tunazofanyia kazi. Kuumizana mioyo na kuchanganyikiwa kunaweza kuepukwa huku majadiliano yenye manufaa yakipewa nafasi.

3. Mahitaji kwenda sambamba na malengo.
Kwa mtu aliyeajiriwa kuna vitu hivi muhimu viwili

1)  Maisha ya kazini
2)  Maisha binafsi.

Ni utamaduni na tayari imeshazoeleka kwamba mfanyakazi anapaswa kuvitenganisha vitu hivi viwili awapo kazini lakini kwakweli ili mwajiriwa mahali aweze kuwa ni mtu mwenye furaha vitu hivi viwili havipaswi kabisa kutenganishwa. Kwanini? Sababu kubwa ni kwamba waajiriwa hutafuta kazi hizo kwa malengo ya kutosheleza mahitaji au malengo yao binafsi hivyo hakuna umuhimu wowote ule wa kutenganisha kazi na maisha binafsi na ni jambo muhimu malengo na mahitaji hayo kuendana sambamba na maisha ya kazi.


Hili huhitaji mabadiliko makubwa ya kimtazamo kutoka kwa waajiri au makampuni kuelekea maslahi ya wafanyakazi wao na vilevile pia kwa waajiriwa wanatakiwa kuwa na muelekeo wazi usiokuwa na upendeleo kuhusiana na vipaumbele vya kazi na vile vyakwake binafsi.

Ni rahisi zaidi kutamka kwa maneno kuliko kutenda, ingawa ni jambo linalowezekana mwajiriwa kuwa na furaha lakini bado ni waajiriwa wachache mno wanaokuwa na furaha kamili katika kazi zao. Hata ikiwa kama waajiri wangependa wafanyakazi wao wote kuwa na furaha, lakini siyo jambo rahisi kutokana na kushindwa kurekebisha mifumo yao ya rasilimali watu  kumfanya kila mfanyakazi kuwa na furaha, vilevile pia siyo rahisi kila mfanyakazi ataweza kuwa na mapenzi na kazi au kuwa na uvumilivu kama ilivyotajwa katika vitu au vigezo vingine 2 vilivyotangulia hiki cha mahitaji.

Vigezo vyote hivi vikiwekwa pamoja hulifanya suala la mwajiriwa mwenye furaha kuwa ni kitu adimu na hivyo kuibua mjadala mzito wa ikiwa mwajiriwa anaweza akawa na furaha kazini. Lakini yote kwa yote ,WAJIRIWA WANAWEZA KUWA NA FURAHA KAZINI pale vigezo hivyo 3 vilivyotajwa na kuelezewa hapo juu vinapofikiwa.

Baada sasa ya kumaliza suala la ikiwa mwajiriwa anaweza akawa na furaha kazini au la, turudi tena rasmi katika ule utafiti  wa kustaajabisha  wa wataalamu juu ya ikiwa kama MWAJIRIWA MWENYE FURAHA KAZINI, UFANISI WAKE UNAZIDI WA YULE ASIYEKUWA NA FURAHA KAZINI. Safari hii tunakwenda kuangalia matokeo yake, ni nini walichogundua kilichowaacha midomo wazi watu wengi?

Tangu kale dhana kwamba mfanyakazi mwenye furaha ndiye aliye na ufanisi zaidi kushinda yule asiyekuwa na furaha imekuwepo kila mahali kote duniani, lakini ni ukweli wa kushangaza kwamba dhana hiyo siyo kweli, MFANYAKAZI MWENYE FURAHA HAIMAANISHI KUWA NI MFANYAKAZI MWENYE UFANISI. Utafiti huo kuhusu athari za furaha kwenye makampuni ulifanyika na watu wawili, Profesa  Andre Spicer wa chuo cha biashara London Carl Cadestrom wa chuo kikuu cha Stockholm.

Katika matokeo yao Andre na Carl walisema tabia ya waajiri/makampuni kuhimiza furaha kama njia ya kuzidisha ufanisi/uzalishaji hakuna uwezo wa kuleta furaha halisi inayoweza kupatikana kutokana na vitu vizuri tunavyotegemea. Utafiti huo walioufanya katika supermarket moja ulibainisha kwamba kadiri wafanyakazi walivyokuwa na hasira ndivyo pia ufanisi wao ulivyokuwa mkubwa.

Wanasema kwamba hasa mtu anapokuwa hana furaha kisha ukajaribu kupandikiza furaha ndani yake ndiyo unazidi kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Kutaka kuwa na furaha kwa kukusudia kutafanya kazi kinyume na ulivyotazamia.


Pia walibainisha kwamba watu walio na furaha mara nyingi huingia mikataba mibovu, wakati mtu anapokuwa katika hali ya hasira huingia mikataba kwa ufanisi zaidi. Hivyo kuwa na furaha muda wote hakuwezi kuwa kuzuri katika kila hali kwenye ajira zetu ingawa pia kuna wakati furaha inaweza ikasababisha baadhi ya vitu kufanyika kwa ufanisi.

Walihitimisha kwa kusema kwamba waajiriwa hawatakiwi kutegemea sana furaha kwenye ajira zao kwani wanaweza kuishia kujihisi kukata tamaa zaidi pale watakapokuta hawaipati furaha hiyo na badala yake furaha ni kitu kinachokuja chenyewe bila kukilazimisha.  
 ......................................................................

Kwa vitabu vya  Biashara na ujasiriamali katika lugha ya kiswahili fungua; SMART BOOKS TANZANIA

Kujiunga na Group la masomo ya kila siku na semina za jinsi ya kuandika michanganuo ya biashara lipia sh. elfu 10 kupitia namba 0712202244  au  0765553030 halafu tuma pia na anuani yako ya email ukifuatia na ujumbe wa "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO"

0 Response to "WAFANYAKAZI KWENYE KAZI ZA AJIRA WENGI HAWANA FURAHA, UPO UKWELI WOWOTE AU NI UZUSHI MTUPU?"

Post a Comment