KUMBE NELSON MANDELA ALIKUWA MPENZI WA VITABU VYA ELIMU YA MAFANIKIO! | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUMBE NELSON MANDELA ALIKUWA MPENZI WA VITABU VYA ELIMU YA MAFANIKIO!


Unaweza ukafikiria labda elimu  na vitabu vya mafanikio binafsi, Self Help books ni jambo la juzijuzi tu, lakini kumbe hapana siyo hivyo. Hebu fikiria mwaka 1969 Aliyekuja kuwa Rais wa Afrika ya kusini isiyokuwa na ubaguzi wa rangi Hayati Nelson Mandela alimwandikia mkewe Winnie Madikizela Mandela barua ifuatayo(orijino ipo chini yake) wakati akiwa kifungoni katika gereza la kisiwa cha Robben Island. 



Juu ni sehemu ya barua Nelson Mandela aliyomwandikia mkewe Winnie kumpa pole kwa ugonjwa wakati alipokuwa gerezani Robben Island

Juu ni barua hiyo original.

Katika barua hiyo Mandela alikuwa akimpa mkewe pole kutokana na tatizo la kuzimia mara kwa mara lililokuwa likimsumbua, tatizo hili lilikuwa likisababishwa na tatizo jingine la moyo ambalo Mandela katika barua  anasema alikuwa anafahamu kuwa Winnie alikuwa nalo. Hata hivyo Mandela akashukuru kwamba Daktari wa familia alikuwa akilishughulikia tatizo hilo kwa karibu na kwamba tatizo tayari lilikuwa limeshapatiwa ufumbuzi. Mandela aliomba aendelee kupewa taarifa za matokeo ya vipimo kutoka kwa daktari huyo na akamtakia mkewe uponaji wa haraka na kila la heri katika maisha.


Katika aya iliyofuatia, Mandela alipendekeza kwa mkewe vitabu 2 ambavyo vingemfaa na kumpa tulizo wakati huo mgumu, vitabu alivyopendekeza mkewe akavisome katika maktaba za manispaa ya mji ni, THE POWER OF POSITIVE THINKING na THE RESULT OF POSITIVE THINKING, vyote vikiwa vimeandikwa na mwandishi mwanasaikolojia wa Kimarekani aitwaye Norman Vincent Peale. Alimwambia kuwa yeye hajaweka  umuhimu mkubwa kwenye suala la dini mwandishi analojadili bali yeye zaidi anazingatia yale maoni mwandishi aliyozungumzia kuhusiana na masuala ya kimwili na kisaikolojia katika kitabu hicho.


Mandela akinukuu kutoka katika vitabu hivyo alimsisitizia Winnie pointi muhimu  kwamba, “Tatizo kubwa halipo katika ulemavu wa mtu bali lipo zaidi katika mtazamo wake kuelekea ulemavu huo, Mtu anayesema nitapona ugonjwa huu na kuishi maisha ya furaha, tayari kwa kusema hivyo anakuwa ameshapona nusu yake” 

Karibu na mwisho wa barua hiyo, Madiba alimsifia mkewe kwa kumwambia hivi; “Katika vipaji ulivyokuwa navyo, kinachonivutia zaidi mimi ni ujasiri wako na kujitambua, Hii hukufanya wewe kuwazidi wengine na mwishowe itakuletea mafanikio makubwa. Endelea kulitunza hili muda wote akilini….”


0 Response to "KUMBE NELSON MANDELA ALIKUWA MPENZI WA VITABU VYA ELIMU YA MAFANIKIO!"

Post a Comment