JE WAJUA SIRI NYINGI ZA MAFANIKIO ZIMEJIFICHA KWENYE MAMBO HAYA 4 MADOGOMADOGO? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JE WAJUA SIRI NYINGI ZA MAFANIKIO ZIMEJIFICHA KWENYE MAMBO HAYA 4 MADOGOMADOGO?


Mafanikio katika jambo lolote lile maishani mwanadamu analolenga kufanya hutokea nje ya uwanja wake wa faraja, kwa kimombo wanasema, “outside of your comfort zone”,. Unataka kuwahi kazini, shuleni au kwenye biashara zako kwa lengo la kuzidisha mafanikio, ufanisi au kipato zaidi, ni lazima ukubaliane na kuachia shuka, kukatisha usingizi wako mtamu wa alfajiri na kupambana na umande wa asubuhiasubuhi kwenye nyasi katika uchochoro unaotoka nyumbani kwako kabla hujafika stendi kupanda basi.


Unataka mwili wako kuwa imara(fiti), ni lazima kwanza uvuje jasho jingi kwa mazoezi nk. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa katika biashara au sekta nyingine zozote zile za kimaisha. Mafanikio yanamtaka mtu kuchukua hatua ambazo mara nyingi haziwezi kumpendeza hata kidogo, na hali hiyo ya kutokupendezwa ndiyo tunayopigana nayo kila siku ndani  ya fikra zetu, na ili tufanikiwe basi ni lazima tushinde vita hiyo ya kifikra kabla hatujaanza kusaka njia kuu za mafanikio katika maisha.


Binadamu mara nyingi tumekuwa tukisaka siri za mafanikio katika mambo yetu mbalimbali tunayoyafanya kama vile, jinsi ya kufanikiwa kibiashara, jinsi ya kupata pesa, kufanikiwa katika masomo, au katika maeneo mengine yeyote yale kwenye maisha. Ukweli ni kwamba majibu ya swali hilo wala siyo magumu hata kidogo kwani siri kuu za mafanikio hujidhihirisha zenyewe katika mifano ya vitu, watu na hata mambo mbalimbali yanayotokea kwenye mazingira yetu ya kawaida kabisa. Mifano hiyo katika maisha ya kawaida ndiyo leo nataka nikutajie katika makala hii, hivyo karibu sana tujifunze pamoja, hakikisha unaisoma makala hii mpaka mwisho kupata manufaa yote yaliyokusudiwa na ukiwa na maoni au mchango wowote ule wa mawazo usisite kuandika mwisho kwenye sehemu ya maoni, nitumie email, jifunzeujasiriamali@gmail.com. Au ujumbe wa whatsapp kwenye 0765553030

1. SHULENI.
Unafikiri ni kwanini serikali duniani ziliweka mifumo ya elimu ambayo kila mtu ni lazima kwanza aipitie kabla hajafanya mtihani wake wa mwisho? Lengo la mtu kwenda shuleni/chuo ni ili aweze kupata elimu na hatimaye baada ya ule muda uliopangwa na serikali kama ni miaka saba, minne au miwili kumalizika basi aweze kufanya mtihani na kufaulu. Serikali inafahamu kabisa kwamba muda uliopangwa mwanafunzi endapo atatia juhudi zake kwenye masomo ni lazima tu atafaulu. Kwa hiyo imeweka mfumo maalumu ili kila anayeutumia aweze kufaulu.


Mfumo huo serikali iliyouweka utakuta ndio kama vile, mitaala mbalimbali(syllabus), ratiba za vipindi madarasani, likizo, ukaguzi, mitihani ya wilaya, Mkoa na ile ya Kitaifa pamoja na mfumo mzima wa uongozi katika shule zenyewe na Wizara husika kwa ujumla. Ni vigumu mno kwa mwanafunzi au mtu yeyote yule kufanya mtihani akaweza kufaulu pasipo kuufuata mfumo uliowekwa kama inavyotakiwa.
MFUMO WA ELIMU UNAMWEZESHA MWANAFUNZI KUFAULU MTIHANI WAKE WA MWISHO


Kama ilivyokuwa vigumu kwa mwanafunzi wa darasa la kwanza kufanya mtihani wa darasa la saba akafaulu, hali ni hivyohivyo ilivyo pia katika upande wa maisha ya mtu ya kawaida anapokuwa na malengo kwenye jambo fulani liwe biashara, kazi au shughuli yeyote ile ya kiuchumi. Haiwezekani kabisa mtu eti leo umejiwekea malengo katika jambo fulani halafu kesho tu au keshokutwa unataka malengo hayo yawe yametimia.


Hii ni sababu kubwa sana inayotufanya kila siku tulalamike kwamba, kujiwekea malengo ni sawa na kupoteza muda, sasa bila malengo utaendeshaje maisha yako? Hata roboti ili liweze kutimiza wajibu wake ni lazima lipangiwe malengo na mmiliki wake katika mfumo wa kielektroniki au kompyuta, yale ni malengo!

Tatizo hapa ni je, UNATUMIA MFUMO GANI KUTIMIZA MALENGO YAKO? Huwezi ukasema utaamka tu ufanye chochote kitakachotokea mbele yako. Vinginevyo basi serikali zingetangaza kwamba hakuna haja ya mifumo ya kielimu badala yake siku ya mtihani mtu yeyote anaweza ‘from no where’ tu akafika shuleni/chuoni na kuja kujifanyia zake mtihani wa mwisho hata ikiwa wakati wa maandalizi yeye alikuwa akilea mtoto au akiuza karanga mtaani(kumradhi sana msomaji sina dhamira mbaya ya kunyanyapaa makundi tajwa).

Malengo yanahitaji kuwekewa mfumo thabiti wa kuyatekeleza sawasawa tu na serikali zinavyoweka mifumo ya elimu kusudi wanafunzi waweze kutimiza malengo yao ya kielimu. Umefungua biashara yako, weka mfumo wa kupata wateja kama kutangaza kwenye social media, magazeti nk., Weka mfumo wa kuuza kwa kufungua matawi(outlets) sehemu mbalimbai na usikimbillie tu kumtafuta mchawi anayekuloga au chumaulete usiyeweza kuelezea anakuibiaibiaje hela zako, inawezekana chumaulete ni wewe mwenyewe, vile tu huna mfumo wa kubaini kama ni wewe. Mfumo sahihi ungeweza kuwa ni kuweka daftari la mahesabu kujua kila senti inakokwenda na inakotoka ni wapi.

2. MWANZI WA KICHINA
(CHINESSE BAMBOO TREE)
Hii ni stori ya kusisimua mno katika ulimwengu wa kusaka mafanikio yenye ujumbe na funzo kubwa sana kwa watu wa makabila yote duniani, siyo kwa wachina tu peke yake. Mti huu, Mwanzi wa Kichina au Chinesse Bamboo tree kama unavyojulikana kote duniani ni kielelezo kizuri sana cha jinsi mafanikio ya binadamu yalivyokuwa ni jambo linalohitaji uvumilivu, subira na msimamo.


Mti huu kama ilivyokuwa miti mingine yote duniani mara unapopandwa ardhini humea na kuota. Katika mwaka wake wote wa kwanza huwezi ukaona mabadiliko yeyote yale ya maana kwani huota taratibu sana. Mwaka wa pili mti huu wa mwanzi napo bado huonekana ukisuasua tu ardhini bila kuonyesha maendeleo yeyote yale ya kutia moyo na hata mwaka wake wa tatu na wanne pia bado kamti haka kanaoonekana ni kadogo tu.

Mwishowe sasa mti huu unapofikisha mwaka wake wa tano (5)- maajabu makubwa hujitokeza. Ghafla mti huanza kuota kwa kasi ya ajabu! Mwanzi wa Kichina sasa huota futi 80 kwenda juu katika kipindi cha wiki sita (6) tu

Sasa hebu pata somo hapo, hivi Mwanzi huu wa Kichina ni kweli huota futi hizo 80 zote katika kipindi hicho cha wiki 6 tu? Au miaka minne ulikuwa ukijiotea ndani kwa ndani? Bila shaka na hicho ndicho kilichokuwa kikifanyika. Mwanzi wa Kichina kwa miaka yote 4 hujitengenezea mifumo imara ambayo ni mizizi, majani, shina, na hata seli na tishu mbalimbali, mifumo ambayo hatimaye hutengeneza fursa kubwa ya baadae kuja kuota ghafla na kuishangaza dunia. Mti huu usingelikuwa umetumia muda mrefu wa kutosha kutengeneza misingi imara(mfumo), tusingeliweza pia kuja kuyaona matunda unaokuja kuonyesha baada ya miaka 5 kupita.

Mti wa ajabu, chinnese bamboo tree huota futi 80 kwa wiki 6 tu

Kanuni ya mti huu hufanya kazi pia kwetu sisi binadamu sawasawa tu na inavyofanya kazi kwa mwanzi huu wa Kichina. Yeyote yule anayeweka uvumilivu mkubwa na subira huku akitekeleza kwa vitendo ndoto na malengo yake kidogokidogo kila siku na kukabiliana na changamoto bila ya kukata tamaa kirahisi, anajijengea msingi imara(mfumo) ambao hatimaye kuna siku dunia huja kushangaa mithili inavyofanya kwa Mwanzi huu wa Kichina.


Hakumna mafanikio rahisi, Siri ya mafanikio kimaisha ni kwamba, chochote kile tufanyacho huenda taratibu mwanzoni jambo linaloweza kutuchanganya na kutupa wakati mgumu sana. Lakini yote hayo mwishowe huja kuzaa matunda. Napoleo Hill katika kitabu chake, THINK & GROW RICH anasisitiza kwenye Sura ya 9 ya kitabu hicho kwamba, Kwa uvumilivu na msimamo usioyumbishwa kirahisi na kitu chochote kile, mafanikio ni dhahiri.

Kuwa na malengo na kuendelea kuamini katika kile unachokifanya hata kama huoni matokeo ya haraka.

3. WANAMUZIKI KAMA KINA DIAMOND, ALI KIBA NA WENGINEO.
Tunavutiwa sana na mafanikio ya wanamuziki au wasanii wakubwa kama kina Naseeb Abdul au Diamond, Ali Kiba na wengineo lakini unaijua siri iliyoko nyuma ya mafanikio yao makubwa? Ni MSIMAMO, Napoleo hili katika kitabu Think and Grow Rich au Fikiri Utajirike kwa Kiswahili anataja  katika sura ya 9 kwamba mfano mzuri kabisa wa nguvu ya msimamo ni biashara ya burudani, anasema kwa mfano watu kutoka pande mbalimbali za dunia humiminika Hollywood Marekani kusaka umaarufu, mapenzi, nguvu na kila aina ya mafanikio lakini kinachomfanya mtu aweze kupenya na kufanikiwa kuingia pale ni msimamo wake wa kuendelea kupambana bila kuchoka.

DIAMOND VS ALLY KIBA


Vipi kama Diamond baada ya kukitoa kibao chake cha Tatizo kwetu Mbagala kama angeliridhika na mafanikio  yaleyale halafu akabweteka na kukaa kimya bila kutoa mfululizo vibao vingine vikali kama vile Nenda kamwambie.., You are My number one, Wakawaka na nyinginezo? Msimamo wake wa kuendelea kufanya kazi nzuri hata baada ya kupata mafanikio kidogo ulimfanya kuja kuwa star, nyota mkubwa kote nchini Tanzania, Afrika na Duniani kwa ujumla. Katika kutimiza malengo yako hakikisha yale matendo mazuri unayoyafanya basi unayarudiarudia kila mara.


Kufanya tendo moja tu zuri mara moja na kuona tayari umewini hakutoshi,wala hakuna atakayeguswa na kitendo chako hicho kimoja. Ukitaka kuvuta hisia za watu wengi ni lazima kwanza uonyeshe msimamo, urudie mambo mazuri kila siku yaonekane ndipo ushindi utakuja. Umefungua biashara yako leo na unataka uanze kuona mauzo makubwa siku hiyohiyo, haiwezekani, ni lazima kwanza uuze elfu 5, elfu 10 na hata elfu 50 kisha itakuja kufika siku unashangaa unauza laki tano mpaka milioni na kuendelea. Hiyo ndiyo siri ya utajiri au jinsi ya kupata pesa, siri ya mafanikio katika biashara  yeyote ile ni uvumilivu.

4. MICHEZO YA BAHATI NA SIBU
Makampuni yanayoendesha michezo ya kubahatisha hutangaza zawadi nono kwa washindi wanaofanikia kupita lakini, je unafahamu fedha hizo hutolewa na nani? Mchezo wa bahati na sibu wanaoshiriki huwa wengi na kile kiasi cha fedha wanazotoa ni kidogokidogo lakini kutokana na wingi wao jumla yake hufika mamilioni ya shilingi na hizi ndizo fedha zinazotumiwa na makampuni hayo kulipa washindi na wao kupata faida.

Wale wanaocheza huona kama vile hawapotezi kitu chochote kutokana na sababu kwamba wengi wao hutumia fedha za ziada ambazo hazipo katikika bajeti zao baada ya kutoa matumizi yao yote ya msingi ingawa pia kuna baadhi ya watu wachache ambao wamefanya michezo hiyo kimakosa kama ndio kazi zao. Lakini ni kitu gani kinachotokea baada ya maelfu ya watu kucheza? Fedha kidogokidogo wanazozichanga huwawezesha washindi wachache kugeuka mamilionea ghafla huku na makampuni husika pia yakineemeka.


Mfano huu wa michezo ya bahati na sibu funzo lake ni kwamba mambo makubwa yote maishani hutokana na vitu vidogovidogo sana kama fedha hizi kidogo wanazocheza watu bahati na sibu. Ili kutimiza lengo kubwa ni lazima lengo hilo ulivunjevunje katika malengo madogomadogo kwanza  na unapokuwa ukiyatimiza hayo malengo madogomadogo ndiyo unatimiza lile lengo lako kubwa.

…………………………………………………..


Mpendwa msomaji wa blogu hii, na huo ndio mwisho wa makala hii ya leo. Endelea kufuatilia makala zijazo na ikiwa utapenda kupata mafunzo ya kina zaidi ya biashara na ujasiriamali, napendekeza kujiunga na huduma zetu nyinginezo zifuatazo;

1. GROUP LA MICHANGANUO ONLINE
Ada ni sh. Elfu 10 na unapata fursa ya kujiunga na group pamoja na masomo, vitabu na semina mbalimbali zilizokwishatayarishwa zifuatazo;

1.  Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI kwa lugha ya Kiswahili.

2.  Masomo 11 ya semina kamili ya jinsi ya kuandika mpango wa biashara.

3.  Kifurushi maarufu cha michanganuo 3 ya ufugaji wa kuku(MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACKS)

4.  Kitabu mashuhuri zaidi duniani, HOW TO WRITTE A BUSINESS PLAN kwa lugha ya kiingereza, ndio kinachotumika vyuo vikuu vingi duniani.

5.  Mfululizo wa Tafsiri ya kitabu mashuhuri cha THINK & GROW RICH kwa Kiswahili.

6.  Kuunganishwa na blogu ya kulipia ya michanganuo bure.

7.  Vielezo(Templates) za michanganuo ya biashara inayokuwezesha kuandika michanganuo kwa muda mfupi.

8.  Masomo yote yaliyopita katika group la whatsapp la MICHANGANUO NA MZUNGUKO WA FEDHA.

9.  Mfumo mpya wa usimamizi wa duka la rejareja(2 IN ONE STORE MANAGEMENTA SYSTEM) unaomwezesha mmiliki wa duka dogo la rejareja au la kati kuthibiti mapato yake pasipo msaidizi kudokoa hata senti 5

10.      Somo muhimu sana la mzunguko wa fedha.

11.      Ukurasa mmoja wa mchanganuo.

Siyo lazima uwe na WHATSAPP ndipo uweze kupata masomo haya kwani pia tunatuma kupitia email na blog maalumu ya private. Namba za malipo ni 0712202244  au  0765553030 jina hutokea Peter Augustino Tarimo. Unaweza kutuma ujumbe wa simu wa kawaida au wa whatsapp kupitia 0765553030 kutujulisha kama umeshalipa na sisi tutakutumia item zako zote muda huohuo pamoja na kukuunganisha katika group.


2. VITABU  MBALIMBALI VYA BIASHARA NA UJASIRIAMALI
Unaweza pia kujipatia softcopy au Hardcopy za vitabu vinavyoonekana majalada yake hapo chini kutoka kwetu; Bei ya vitabu vyote vitatu SOFTCOPY ni sh. 18,000/= lakini pia ukihitaji kimojakimoja unaweza kupata kwa sh. elfu 10 hicho cha kwanza, elfu 5 cha pili na elfu 3 hicho cha tatu.

1

2

3

HARDCOPY cha kwanza ni sh. Elfu 20, cha pili elfu 10 na cha tatu sh. Elfu 5, ukiwa dar tutakuletea mpaka ulipo ila utaongeza sh elfu 2 za nauli na ukiwa mikoani agiza mtu anayefika Dar akuchukulie au tunaweza pia kutuma kwa njia ya basi na utaongeza gharama za usafiri kutegemea na basi au mkoa ulipo.

SANTE SANA

Peter A. Tarimo.
Self help books tz


2 Responses to "JE WAJUA SIRI NYINGI ZA MAFANIKIO ZIMEJIFICHA KWENYE MAMBO HAYA 4 MADOGOMADOGO?"