KAMA FEDHA HAIJWAHI KUWA RAHISI KUPATIKANA KWANINI UCHEZEE PESA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KAMA FEDHA HAIJWAHI KUWA RAHISI KUPATIKANA KWANINI UCHEZEE PESA?

Waheshimiwa, Mwalimu, Mzee Ruksa, Ben, Jakaya na Magu
Ni tangu enzi za dahari, kitu hiki kinachoitwa pesa au fedha hakijawahi kuwa rahisi kupatikana, kila enzi utasikia kuna misemo na lugha mbalimbali kuhusiana na ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa mfano enzi za Mwalimu Julius Nyerere tulisikia misemo kama vile,uhujumu uchumi wakati wa Azimio la Arushaa, uhuru na kazi kipindi cha Uhuru, Siasa ya ujamaa na kujitegemea na hata kufunga mikanda baada ya vita ya Idd Amin Dada kule Uganda.

Zikaja enzi za Mheshimiwa Ali Hassana Mwinyi Rais wa awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukazuka msemo mashuhuri sana ulioitwa RUKSA. Alipoanza kutawala Mzee Benjamin William Mkapa tukasikia, maneno kama vile, Ukapa, uchumi wa sayansi na teknolojia na mengine yaliyofanana na hayo. Rais Jakaya Kikwete yeye aliingia na maisha bora kwa kila mtanzania akimaanisha kila mtu awajibike kuyapata maisha bora. Na Mheshimiwa Rais Joseph Pombe Magufuli misemo karibu inayofanana na ile ya enzi za Mkapa imeibuka ukiwemo huu wa vyuma vimekaza, hapa kazi tu nk.


Maneno na misemo yoote hii inamaanisha kitu gani?
Misemo yote hii katika awamu zote 5 za uongozi ukiitazama kwa umakini haimaanishi chochote zaidi ya Mzunguko wa fedha, nikimaanisha fedha kuingia na fedha kutoka hazina kuu ya serikali na mifukoni mwa wananchi. Kila sera au kaulimbiu ina malengo ya kutaka kuelezea hisia za wananchi au serikali juu ya hali ya kiuchumi iliyokuwepo katika kipindi husika na maneno hayo yanaakisi hali ya kiuchumi iliyopo. Hali kuwa ngumu katika mzunguko wa fedha iwe ni serikalini, katika biashara au mfukoni mwa mtu binafsi maana yake ni kwamba fedha zinazoingia ni chache kuliko zile zinazotoka.


Kiuchumi kuimarisha mzunguko wa fedha au kwa maneno mengine kudumisha mzunguko wa fedha uwe chanya ni lazima serikali, biashara au mtu binafsi achukue hatua za kubana matumizi au kuwa na kitu kinachoitwa nidhamu ya pesa ya hali ya juu. Na zoezi hili ndilo linalofanywa na serikali za awamu mbalimbali katika nyakati tofauti ndipo sasa tunashuhudia misemo kama hiyo kuibuka.

Kwa mfano Serikali inapolegeza sana ukusanyaji wa fedha maana yake inakuwa dhaifu lakini wananchi wananeemeka na hiki ndicho kilichotokea enzi za Mzee Ruksa na Mzee kikwete, serikali inapoamua kubana matumizi, kukusanya fedha kikamilifu na kudumihsa nidhamu ya hali ya juu ya matumizi, serikali huimarika kifedha japo wananchi hupata shida kidogo kwa kuona fedha hamna mifukoni mwao.

Hali kama hiyo ndiyo inayotokea hata katika biashara zetu, biashara kama serikali ilivyo, inapaswa kuingiza pesa nyingi na kwa nidhamu ya hali ya juu ikiwa itataka kuimarika. Kinyume chake ni kuanguka au kufa kabisa.


Somo hili la fedha ni muhimu sana kwa kila mtu, kampuni, taasisi na hata serikali yenyewe. Ni lazima kuelewa kwamba fedha hata siku moja haijawahi kuwa rahisi kupatikana, ukiona imekuwa rahisi basi na ujue kuna matokeo au athari nyuma yake. Fedha inayopatikana kiurahisi nyuma yake ni lazima kuna habari ya utovu mkubwa wa uwajibikaji, wizi, magendo, ujanja ujanja, au uhujumu uchumi wa namna moja ama nyingine.

Kwa mfano, ukiona mfanyakazi katika biashara yako “anatanua sana” nikiwa na maana kwamba anatumia fedha ovyo, basi ujue anaihujumu biashara yako, atapata wapi fedha kirahisi namna hiyo? Na hali ni hivyohivyo katika taasisi zingine na serikalini pia. Wema usizidi uwezo, mweleze msaidizi wako wa kazi ukweli kwamba fedha haijawahi kuwa rahisi hivyo kupatikana, na ikiwezekana mtimue mapema kabla hali kwako haijawa tete zaidi. Michezo michezo yake mwishowe wote, wewe na yeye mtajikuta mkiomba mia ya kula.

Tunashuhudia viongozi kadhaa wa serikali na taasisi za umma waliokosea katika matumizi ya fedha au kushindwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha za serikali miaka mingi iliyopita wakiwajibishwa sasa mahakamani, kosa la kushindwa kusimamia fedha halijawahi kumwacha mtu yeyote yule salama, usipowajibika sasa, utawajibika hata baada ya kifo chako, wanao, wajukuu au hata vitukuu watakuja kuwajibika kwa makosa yako hayo kwa kisingizio bandia cha laana ya mabibi na mababu.


Ni wangapi wanaowajibika kwa makosa ya kipesa waliyotenda wazazi wao huko nyuma? Inawezekana leo unaishi katika lindi la umasikini wa kutisha kwa sababu tu mzazi hakuwa na nidhamu ya pesa. Kinachotakiwa sasa ni wewe kutorudia makosa hayo vizazi vyako navyo vikaendelea kuipata ‘laana hiyo’.

Enzi zitapita, zitakuja nyingine lakini hakuna enzi hata moja utakuja kusikia eti fedha imekuwa rahisi kupatikana bila ya kufanya kazi kwa nidhamu na maarifa. Ili uweze kudumisha mzunguko mzuri(chanya) wa fedha katika vyanzo vyako inatakiwa kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu na ubanaji matumizi, hakuna njia ya mkato hata kidogo na hii ni kila mahali popote pale duniani, usije ukaona nchi zilizoendelea ukafikiri walitapanya ovyo mapato yao, wasingefika pale walipo.

Kabla hujanunua itu chochote kile hebu jiulize kwanza, “Hivi kitu hiki ninachonunua au kulipia, kina manufaa gani kwangu na hasa katika kuongeza mzunguko wangu wa fedha badalaa ya kuupunguza?”
………………………………………….
Ndugu msomaji wangu, nashukuru kwa kuchukua muda wako wa dhamani kusoma hapa, hayo ni machache lakini mengi zaidi tumeyaweka katika vitabu vyetu hivi hapa chini pamoja na machapisho mengineyo mbalimbali katika private blogu yetu ya Michanganuo na kundi la whatsapp la michanganuo online.

Vitabu hivi unaweza kuvipata kimojakimoja au vyote kwa pamoja ukiwa popote pale kwa njia mbili zifuatazo.

1. SOFTCOPY(PDF) kupitia email yako unavidownload na kusoma katika simu au kompyuta yako

2. HARDCOPY(VYA KARATASI). Unaletewa kitabu/vitabu popote pale ulipo Dar es salaa kwa gharama ya ziada ya sh. 2000/=. Kama upo mikoani unaweza ukaagizia kwa mtu anayefika Dar au ukatuma fedha na sisi tukatuma vitabu kwenye basi.

SIMU:     0712202244
WASAP: 0765553030
JINA:       Peter Augustino Tarimo


TUPO MBEZI KWA MSUGURI KARIBU NA STENDI YA DALADALA

Softcopy sh. 10,000/=
Harcopy  sh. 20,000/=


Softcopy sh. 5,000/=
Harcopy  sh. 10,000/=


Softcopy sh. 3,000/=
Harcopy  sh. 5,000/=0 Response to "KAMA FEDHA HAIJWAHI KUWA RAHISI KUPATIKANA KWANINI UCHEZEE PESA?"

Post a Comment