SOKO LA TIKITI MAJI KIWANDA CHA BAKHRESA CHA KUTENGENEZA JUIS ZA MATUNDA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SOKO LA TIKITI MAJI KIWANDA CHA BAKHRESA CHA KUTENGENEZA JUIS ZA MATUNDA

Niiahidi kumalizia maswali yaliyoulizwa na wasomaji wetu siku chache zilizopita na maswali niliyokuwa naendelea nayo yalikuwa ni maswali kutoka kwa msomaji wetu wa Songea Mkoani Ruvuma. Tayari maswali yake mawili tulishayajibi na niliahidi kujibu swali la tatu hapa, ila Swali hilo la tatu sitaweza kulijibu kutokana na kugundua kwamba linafanana mno na lile la pili hivyo nadhani kwa kusoma majibu ya swali hilo la pili lililosema, Kijana waumri mdogo anaweza akaanzisha biaashara kubwa ikafanikiwa? Atakuwa amesharidhika.


Leo nitajibu swali jingine la msomaji mmoja yeye hakutaja anatokea wapi, aliuliza kama ifuatavyo;

“Habari ya jioni, mimi ni mkulima nina heka 3 za matikiti maji. Yamebakiza siku 7 kukomaa na yako vizuri sana! Natafuta soko kwenye kiwanda cha Bakhresa cha juisi za matunda ila nashindwa kwani sina mawasiliano na hichi kiwanda. Unaweza ukanisaidia?” 

Kabla sijaweka majibu niliyompa msomaji huyu kwanza nitaelezea kidogo kuhusiana na dhana nzima ya utafutaji wa masoko ya biashara zetu iwe ni bidhaa, ama huduma na bila ya kujali huduma na bidhaa hizo zinatokana na shughuli za shamba, kilimo na ufugaji au biashara za kawaida tu za uchuuzi, viwanda na biashara za jumla jumla.


Kumbuka pia kwamba shughuli yeyote ile unayoifanya ni biashara ilimradi tu lengo lako liwe ni kukidhi mahitaji fulani ya wateja. Hii ni kwa mujibu wa maelezo ya biashara katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI. Katika kitabu hicho hicho pia, kinazungumzia mchakato mzima wa biashara kuwa ni mchakato wa kutafuta soko au “Marketing” kwa kimombo.

Hivyo kwa kifupi tu niseme kwamba unapotaka kuyakidhi mahitaji fulani ya wateja ni lazima tangia mwanzo mpaka mwisho wa mchakato wako huo uhakikishe kwamba unalo soko la uhakika la bidhaa au huduma zako. Vinginevyo biashara au mchakato wako huo utakuwa na uwalakini na hapo sasa ndipo unakuta mtu unaanza kujiuliza mwenyewe, “Mungu wangu tu, ona nitauza wapi bidhaa zangu hizi, zinanidodea.”

Kitu ambacho ni muhimu sana kufanya kama mjasiriamali au mfanyabiashara unayechipukia ambacho kitakusaidia sana kuhakikisha unalifahamu barabara soko lako unalolenga kuwauzia bidhaa au huduma zako, ni kufanya utafiti wa biashara yako au unaweza kufanya mchanganuo wa biashara yako. Tafadhali vitu hivi visikuchanganye hata kidogo, unaweza kusema; “huyu mtu anazungumzia utafiti mara mchanganuo wa biashara, sasa nishike kitu gani?” 


Ndugu msomaji wangu wala visikuchanganye, utafiti wa biashara na mchanganuo wa biashara au mpango wa biashara ni kitu kimoja hichocho na tena unaweza ukakutana na majina mengine mengi mahali kwingine kama vile, mpango mkakati wa biashara, andiko la biashara, andiko la mradi, upembuzi yakinifu,  business plan nk. ni majina tu, na kitabu kimeyaelezea vyema pamoja na tofauti zake ndogondogo.

Hakuna tofauti na jinsi ulivyokuwa mchele, mchele baada ya kupikwa unakuwa na majina meengi, utakuta kuna wali, ubwabwa, biriani, pilau, mseto na majina chungu nzima lakini bado ni mchele tu uleule ambao lengo la kuuandaa ni ili watu waweze kula na kushiba. Halikadhalika mchanganuo nao lengo lake pamoja na mengine mengi ni kutathmini au kubaini soko lako kwa uhakika kabisa kabla hata wateja wenyewe hawajagundua kwamba utawauzia kitu gani.

MAJIBU YA SWALI
Jinsi mkulima huyu atakavyoweza kupata soko la kuuza matunda yake ya matikiti maji katika viwanda vya kutengeneza juisi vya mwekezaji Said Salim Bakhresa.

Ndugu mkulima ni kweli kwamba Bakhresa Food Products imeanzisha viwanda kadhaa vinavyozalisha juisi kutokana na matunda halisi yanayolimwa hapahapa nchini kama vile maembe, mananasi, pera, passion, na nyinginezo ingawa sina uhakika sana ikiwa kama wanazalisha pia na juisi inayotokana na tikiti maji(water mellon). Nasema sina uhakika na juisi za matikiti kutokana na uzoefu wangu binafsi kwani sijawahi kuziona zikiuzwa madukani hata aina kutoka nje ya nchi.


Sababu kubwa inayotolewa kwanini juisi ya tikiti maji isiwepo kirahisi sokoni kama ilivyokuwa kwa matunda mengine kama embe, nanasi na passion ni kuwa, juisi ya matikiti maji ni vigumu kuihifadhi katika vifungashio ikadumu kwa muda mrefu pasipo kupoteza uhalisia wake hasa ile hali ya urojorojo.

Kwa kweli sijafanya utafiti kufikia hatua ya kuonana na wahusika katika viwanda hivyo vya makampuni ya Bakhresa lakini kwa taarifa nilizokuwa nazo, kampuni ya Bakhresa ina viwanda vya juisi za matunda maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Dar es salaam, Pwani na katika mikoa ya kanda ya ziwa. Kwa mfano kuna kiwanda cha juisi kilichopo Mwandege Mkuranga katika mkoa wa Pwani na kwa msimu ulioanza Novemba mwaka huu kwa mujibu wa afisa uhusiano wa kampuni hiyo bwana Hussein Sufiani, kiwanda kina matarajio ya kununua matunda kutoka kwa wakulima yenye thamani ya shilingi zipatazo bilioni 7 sawa na zaidi ya tani 70,000 za matunda mbalimbali.

Kama uonavyo ndugu msomaji, mzigo tani zaidi ya sabini elfu siyo mchezo hata kidogo, hapa unahitajika utaratibu uliopangika vizuri baina ya wadau wote wanaohusika yaani wakulima wenyewe, uongozi wa kiwanda pamoja hata na serikali au vyama vinavyohusiana na maslahi ya wakulima katika eneo husika na siyo tu suala la mtu mmoja au wawili kuamua wanataka kwenda kuuza matunda katika kiwanda.

Si kama nabeza mkulima mmoja mmoja kuuzia kiwanda matunda hapana, ila ninachotaka kueleza hapa ni kwamba, mahitaji ya kiwanda chochote kile ni makubwa, huwezi kufungua kiwanda kikubwa ukategemea kubangaiza malighafi, ni lazima ujipange aidha kwa kuzalisha malighafi zako binafsi za kutosha au ukawa na wateja kabisa wanaoeleweka watakaoingia na wewe mkataba wa kudumu kukuuzia malighafi kusudi kiwanda kisije kikakaukiwa malighafi njiani, kwani itakuwa ni bonge la hasara huku ukiwa umeshawekeza mabilioni yako kibao ya shilingi.

Ndugu yangu kama nilivyotangulia kusema sina nia ya kukukatisha tamaa, ila kukueleza kile kilichokuwa wazi, ushauri wangu ni kwamba kwa kuwa umechelewa sana kuhakikisha soko la matikiti yako mpaka yanafikia kukomaa ndipo unaanza kutafuta soko, hata hivyo kiasi cha matikiti uliyokuwa nayo ni kidogo sana kuogopa kuwa utashindwa kuyauza. Kwa heka mbili, tatu unaweza hata kuyapeleka masoko mbalimbali yaliyoko Dar na yakaisha kwa muda mfupi tu.

Kuhusiana na soko la makampuni tanzu ya Bakhresa, nadhani ni vizuri zaidi ukatafuta mawasiliano nao kupata uhakika iwapo kama wananunua au la, au pia unaweza ukawasiliana na chama cha wakulima wa matunda Tanzania UWAWATA wakakupa ufafanuzi zaidi kwani mara nyingi viwanda vikubwa huwa wananunua matunda kutoka kwa wakulima waliosaini nao mikataba maalumu.


Ulichokifanya ni sahihi kabisa, kufanya utafiti wa soko la matikiti yako, ila kosa moja dogo ulilolifanya ni kuchelewa kufanya utafiti wenyewe, kazi hii ulipaswa kuifanya kabla hata haujaanza kuandaa shamba kwa ajili ya kuotesha mbegu za matikiti yako. Hata hivyo utakuwa umeshajifunza, wakati ujao hakikisha kazi hii nyeti ya kufanya utafiti wa soko la bidhaa zako unaifanya mapema iwezekanavyo na unaendelea kufanya hivyo katika kila hatua utakayoendelea kuwa mpaka umeuza bidhaa zako zote. Na katika utafiti huulizi sehemu moja tu, kwa mfano unakuja kuuliza kwangu, majibu nitakayokupa changanya na mengine utakayopata sehemu nyingine na mwisho wa siku unakuwa na taarifa zote muhimu zitakazokuwezesha kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa/huduma zako. Kumbuka soko ni kitu muhimu pengine kushinda vigezo vingine karibu vyote kwenye biashara na si zoezi la siku moja bali mchakato tangu unaanza wazo mpaka unauza.

……………………………………………………………......

Ndugu msomaji wangu, mwezi huu wa Desemba ni mwezi wa kutathmini malengo yetu tuliyojiwekea katika mwaka huu unaomalizika wa 2017 kuelekea mwaka 2018. Nakuomba tuwe pamoja kwani kuna mambo mengi tutakumbushana na mengine tutapanga hapahapa pamoja kama tulivyofanya kipindi kinachomalizika hata kama ikiwa yalikuwa ni mambo machache lakini naamini sote tulikuwa tukifanya mambo kwa malengo.

Vitabu ni muhimu muda wote na naendelea kukukumbusha kwamba kama hukusoma vitabu hivi hapa chini angalau jipatie hata softcopy moja au zote kwa pamoja, ni uchaguzi wako lakini hakikisha umesoma angalao kimoja kabla hatujauaga rasmi huu mwaka.






Kwa vitabu zaidi au maelezo kuhusiana na hivi tembelea;  SMART BOOKS TANZANIA

0 Response to "SOKO LA TIKITI MAJI KIWANDA CHA BAKHRESA CHA KUTENGENEZA JUIS ZA MATUNDA"

Post a Comment