JINSI YA KUONGEZA FAIDA BIASHARA YA KUINGIZA NYIMBO NA KUCHAJI SIMU ZA SMARTPHONE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUONGEZA FAIDA BIASHARA YA KUINGIZA NYIMBO NA KUCHAJI SIMU ZA SMARTPHONE

Sekta ya mawasiliano hususani katika kipengele cha simu za mkononi nchini Tanzania imekuwa ikikua kwa kasi kubwa tangu kuanza kwake miaka ya 90 mwishoni wakati tuliposhuhudia ujio wa simu kubwa za mkononi aina ya Motorola ambazo baadae kidogo watu waliziita kwa jina la utani kama “miche ya sabuni” lakini jina hilo mche wa sabuni lilikuja baada ya kuingia aina nyingine za simu mpya zilizokuwa na umbile dogodogo mfano, siemen, Ericson na Nokia.


Nyakati hizo ndiyo tulishuhudia maneno kama, siemen ya dole gumba, twangapepeta, Nokia ya kitochi, ‘jeneza’ na simu yeyote ile ya mkononi kuitwa mobitel hata kama ilikuwa inatumia mtandao wa kampuni tofauti na mobitel kama vile tritel, Vodacom na Celtel

Mabadiliko hayo yalikuwa yakitokea kwa haraka kiasi kwamba ukinunua tu simu kabla hata haijachakaa, tayari inakuwa imekwishapitwa na wakati, unatamani kununua toleo jingine tena . Hamna tofauti na iivyo sasa unapoona makampuni kama TECNO, Samsung, na Apple wanavyotoa matoleo tofautitofauti kila kukicha na kila toleo likiwa bora zaidi kushinda lile lililopita.

Tukiachana na historia hiyo sasa tuangalie jinsi kuibuka kwa kasi kwa sekta hii kulivyoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa ujumla hasa kwa wafanyabiashara wadogowadogo. Miji yote kuanzia Dar es salaam na hata mikoani kila kona viliibuka vibanda vidogo vidogo maarufu kama vibanda vya kupigisha simu ambavyo wingi wake ulitokana na idadi ndogo ya watu waliokuwa wakimiliki simu za mkononi kwa wakati huo, wachache waliokuwa na simu walikuwa na watu wengi waliotaka kuwasiliana nao, lakini kwa kuwa hawakuwa na simu zao binafsi iliwabidi waingie katika vibanda hivyo ili kuweza kuwapigia na kuwasiliana nao. Taratibu vibanda hivi vilianza kutoweka kadiri idadi ya watu wanaomiliki simu za mkononi nayo ilivyozidi kuongezeka.


Badala yake viliibuka vibanda vingine kwa ajili ya kuchajia simu na betri za simu kwa kutumia kobe sambamba na huduma zingine mbalimbali kama vile, kuuza vocha za simu jumla na rejareja, kuingiza nyimbo katika simu, kuuza kava za simu, kuuza vifaa mbalimbali vya simu za mkononi kama earphones, vioo, betri, housing, protector, covers charger za simu, power banks, touch, memory cards, flash nk. Vilevile katika vibanda hivyo utakuta wengine wakitoa huduma za kusajili line za mitandao ya simu mbalimbali kama vile mitandao ya Vodacom, Tigo, Airtel, Zantel, Halotel, Smart, TTCL na mingineyo pamoja na huduma za kurudisha namba za simu zilizopotea(kuswap)

Kuna huduma nyingine kama vile, kudownload nyimbo mpya na kuziburn katika CD au DVD au kuweka katika flash na memory cards japo kisheria hii haikubaliki kabisa lakini kuna wakati watu walikuwa wakidownload sana. Wateja wengi hupendelea kudownload nyimbo za dini, kudownload nyimbo mpya za kibongo, kudownload nyimbo za bongo flava, nyimbo za Injili, Qaswida nk.


Huduma zoote hizo pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya mawasiliano ya simu za mkononi zimebadilisha maisha ya vijana wengi wa Kitanzania na watu wote walioamua kujiingiza katika biashara hizi, zimetoa ajira za muda na za kudumu pamoja na kuongeza mapato ya serikali kutokana na kodi na tozo mbalimbali.

Ubunifu utakaokufanya uongeze mapato yako(faida) kama unafanya biashara ya kuuza na kutoa huduma ndogondogo za simu za mkononi na smartphones.

Lengo kuu katika makala hii ilikuwa ni kukudokezea mbinu kadha ambazo nimegundua zinaweza zikamfanya mtu anayejishughulisha na biashara ndogondogo za kutoa huduma kwa watumiaji wa simu za mkononi akazidisha faida anayopata mara nyingi zaidi ya ile aliyozowea kuipata kila siku katika kibanda chake au kama ni duka, kioski na katika miavuli kwenye baraza za nyumba maeneo mbalimbali, stendi na maeneo mengine ya wazi.


Simu za kisasa za mkononi maarufu kama Smartphones kwa sasa hivi ndiyo habari ya mjini kila mahali. Kwa lugha nyingine unaweza ukasema simu hizo sasa ndiyo ‘zinatrend’ hapa Tanzania na duniani kwa ujumla. Hii inafanya mahitaji ya huduma mbalimbali zinazohusiana na simu hizo kuwa spesho na zilizokuwa na uhitaji wa kiwango cha juu sana. Kuna watu wengi mpaka sasa hivi ambao bado hawana simu hizi lakini wana mpango wa kuzimiliki hapo baadae. Kwa ujumla kila mtu anatamani kununua simu hizo hata kama siyo leo wala kesho lakini ni lazima ipo siku.

Kuna watu pia wanaomiliki simu hizo lakini bado hawajaweza kufahamu kutumia kila kipengele kilichopo katika simu hizo, watu hao wanahitaji sana mtu wa kuwaelekeza chapchap, wengine si kama ni mambumbumbu hapana, hawana tu muda mwingi wa kuanza kukaa na kubonyabonya wakijifunza, wanataka njia ya haraka ya kujifunza ambayo ni kwa kupata maelekezo kutoka kwa mtu aliyekwisha ‘master’ kuelewa vyema jinsi ya kutumia smartphones. Unaweza kushangaa hata mwingine hajui awashie tochi wapi au aongeze mwanga wa kioo wapi.


Nilijaribu kufanya utafiti kidogo kwa kutembea vibanda kadhaa nikijidai kama nahitaji huduma za kujiunga intanet, kufungua e-mail,  kujiunga na facebook, kujiunga instagram, kujiunga na whatsapp, kubadilisha kioo, kukata line, kubadilisha line, nk. Karibu kila kibanda nilichopita wanakuambia, “sisi tunachaji simu tu” au “hapa tunaweka miziki kwenye simu tu”. Ni vibanda vichache sana nilivyokuta wameweka vibao vilivyoandikwa; “Tunaunganisha intaneti, e-mail, instagram, facebook, whatsapp, badoo, twitter, youtube na telegram

Kama wewe unatoa huduma za simu, jifunze jinsi ya kuunganisha huduma hizi zote nilizozitaja hapa na nyinginezo ambazo sikuzitaja hapa lakini zinahusiana na smartphones au Intaneti kwa ujumla. Siyo kazi ngumu kujifunza vitu hivi, waweza hata kumlipa mtu fedha kidogo akakuelekeza siku mbili, tatu, ukishafahamu vizuri nenda katika kibanda au kioski chako na uweke bango linalosomeka vizuri maandishi yanayotaja huduma zote hizo. Utashangaa kuona wateja wakiongezeka siku hadi siku kuhitaji huduma hizo, usisahau pia kuweka na charger kwa ajili ya smartphones kwani nyingi huwa hazikai na chaji muda mrefu.

…………………………………………………………


Ndugu msomaji wa makala hii kwanza nikushukuru kwa muda wako halafu nikuombe tena kushea makala hii kwa wale unaowathamini. Kama unapenda kujifunza biashara na ujasiriamali kwa kina zaidi unaweza kupata moja ya vitabu vifuatavyo hapa chini pichani kwa gharama kidogo. Unaweza pia kujipatia vitabu vyetu vingine bure bila malipo na kwa maelezo yake zaidi unaweza ukayapata katika ukurasa huu hapa; SMART BOOKS TANZANIA   

Mawasiliano kwa ajili ya kupata vitabu hivi ni haya hapa;

simu:          0712202244
whatsapp:  0765553030

jina:           Peter Augustino Tarimo

1
2


3


0 Response to "JINSI YA KUONGEZA FAIDA BIASHARA YA KUINGIZA NYIMBO NA KUCHAJI SIMU ZA SMARTPHONE"

Post a Comment