MAPITIO YA KITABU, THINK AND GROW RICH KWA UFUPI(UCHAMBUZI SANIFU) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAPITIO YA KITABU, THINK AND GROW RICH KWA UFUPI(UCHAMBUZI SANIFU)


Amini usiamini kitabu hiki “Think and Grow Rich”  ni moja kati ya vitabu  ambavyo vimewafanya watu wengi sana duniani hususani Wamarekani kutajirika, siyo kutajirika kifedha tu bali na hata katika nyanja nyinginezo za kimaisha, kwa mfano inasemekana mtu kama raisi wa marekana ni lazima asome kitabu hiki na kukielewa ndipo anaweza kushinda kinyanganyiro hicho. Ni miongoni mwa vitabu vilivyouza nakala nyingi sana duniani kote, zaidi ya nakala milioni 15. Pamoja na kwamba  kimeandikwa miaka mingi iliyopita kabla hata ya kuja  kwa kompyuta za kisasa lakini maudhui yake hayajachuja na pengine hayatachuja mamia ya miaka ijayo.

Maelezo mafupi.
Think and Grow Rich kama jina  linavyojieleza ni kitabu kinachohusisha fikra (mawazo) na kupata utajiri. Maudhui yake hasa ni jinsi binadamu  anavyoweza kubadilisha fikra au maono yake kuwa  kitu halisi  kinachoweza kushikika kama mali au fedha.

Mtunzi wake Napoleon Hill hakubaliani kabisa na dhana kuwa mafanikio  /utajiri ni bahati, urithi, au kutumia nguvu fulani za giza kama wengi miongoni  mwetu tunavyofikiria leo, bali ni matokeo ya mipangilio madhubuti ambayo imewekwa na binadamu mwenyewe  kwa kutumia akili yake aliyopewa  na Mwenyezi Mungu.

Wazo la kukitunga kitabu hiki halikuwa la Napoleon Hill mwenyewe, bali lilitoka kwa mtu mwingine tajiri aliyejulikana kama Andrew Garnegie. Napoleon hapo kabla  alikuwa mwandishi  wa habari na katika pitapita yake  mitaani ndipo alipokutana na huyu bwana, Andrew Carnegie ambaye alimwalika Napoleon katika makazi yake ya kifahari. Andrew Carnegie alikuwa na wazo kichwani mwake siku nyingi kwamba, Mafanikio ni lazima yana kanuni zake na kanuni hizo zingeweza kuandikwa na hata zikasomwa na kila mtu anayependa kufanikiwa/kutajirika.

Carnegie alihitaji  mtu ambaye angeweza kufanya utafiti wa kina kuthibitisha kanuni hizo ikiwa kama kweli zipo na zingeweza kuandikwa, ndipo akamwita Napoleon Hill na kumuuliza kama angeweza kuifanya kazi hiyo. Alimuuliza Napoleon endapo alikuwa tayari kupoteza miaka 20 akitafiti swala hilo naye bila ya kipingamizi alikubali “ndiyo” na kazi ikaanza.

Kazi yenyewe ilikuwa ni kuhakikisha anawafanyia usaili matajiri na watu  mashuhuri wakubwa nchini Marekani  miaka hiyo ya 1930  zaidi ya  mia tano ili kufahamu  siri za mafanikio yao. Andew  Carnegie kwa kuwa alikuwa  naye ni mtu tajiri na mashuhuri alimuandikia Napoleon Hill barua za utambulisho kwa watu mashuhuri wenzake wakati huo kama Kina Henry Ford, Thomas Edison, F.w. Woolworth na wengineo. Napoleo Hill aliifanya kazi ile kwa miaka ipatayo 20 na kufanikiwa kupata kanuni maalumu ambazo matajiri wote na watu wenye mafanikio huzifuata pasipo hata ya wengi wao kujua.Mwaka 1928 aliweza kukamilisha kazi hiyo iliyochukua vitabu vikubwa vinane.

Kitabu cha Think and Grow Rich  ni ufupisho wa vitabu hivyo 8 vilivyotokana na utafiti huo.Napoleon Hill mwenyewe katika kitabu hiki hazitaji siri hizo moja kwa moja bali amesisitiza mtu kukisoma kitabu kizima na ndipo ndani yake atakapokutana na siri hizo moja baada ya nyingine, anasema “utakapokutana na siri zenyewe utajua tu, simama kwa muda kidogo, unapokutana nayo, chukua glasi ya maji kwanza ujipongeze kwani  wakati huo ni muhimu sana katika maisha yako”.

Pesa na Roho.
Ndani ya kitabu mwishoni, Napoleon anaelezea sababu iliyomfanya aandae kitabu hiki, kwamba ni kutokana na  mamilioni ya watu kote marekeani miaka hiyo ya 1930 kuwa katika  lindi kubwa la woga wa umasikini. Kumbuka miaka  hiyo marekani  na dunia kwa ujula ilikumbwa na mdororo mkubwa wa uchumi (Greet Depression) baada ya vita ya II ya dunia, mithili ya ule uliotokea hivi karibuni.

Uhusiano uliopo kati ya  maswala ya kiroho na kupata utajiri kwa Wamarekani ni jamba la kawaida tofauti na sehemu nyingine kama huku Africa. Kwa Wamarekani  ni maadili yao, kwamba utajiri  ni  matokeo ya akili/fikra, ubunifu pamoja na uvumilivu. Hivyo Napoleon anahitimisha kwamba, utajiri na mafanikiko huja kutokana na akili/fikra na wala siyo vinginevyo:- Ukweli huo uligundulika miaka zaidi ya 70 iliyopita na bado mpaka hivi sasa zama za mawasiliano ukweli huo unabeba mana ile ile.

Hamu (Shauku)
Kiungo kingine katika kupata utajiri Napoleon anasema ni hamu kubwa ya kufanikisha jambo. Anaelezea habari ya mtu mmoja aitwae Edwin E. Barnes ambaye hakuwa na chochote zaidi ya shauku kubwa ya kutaka kuwa Mbia (Partner) na tajiri  mvumbuzi maarufu Thomas Edson, mwishowe huyo bwana alitimiza  ndoto yake hiyo na akafanikiwa pia  kuwa tajiri mkubwa, hakuanza  na kitu zaidi ya hamu kubwa ya kutaka kuwa mbia wa Edson.

Kwa ufupi  hivyo ndivyo Napoleo Hill alivyotunga kitabu chake, Think and Grow Rich Chenye sura 15 ambazo kila moja imebeba hatua moja kuelekea utajiri isipokuwa sura ya kwanza na ya 15 kwa maana hiyo kitabu kizima kina hatua 13 za kuelekea  utajiri kwa mujibu wa Napoleon Hill mwenyewe. Sasa tuangalie kila sura pamoja na hizo hatua 13 kwa ufupi zinasema  kitu gani, Ili kuendelea kusoma kinachofuata, bonyeza maandishi yafuatayo;



0 Response to "MAPITIO YA KITABU, THINK AND GROW RICH KWA UFUPI(UCHAMBUZI SANIFU)"

Post a Comment