KUBUNI KITU KIZURI NI HATARI! WATU LAZIMA WAKOPI NA KUPESTI, UFANYENINI KUZUIA HILI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUBUNI KITU KIZURI NI HATARI! WATU LAZIMA WAKOPI NA KUPESTI, UFANYENINI KUZUIA HILI?



















Ukibuni kitu au unapobuni kitu/wazo la kutengeneza bidhaa/huduma nzuri, tegemea kwa asilimia kubwa watu wengine kuibuka na vitu vya kwao vinavyofanana na kile ulichokifanya,watafanya kitu kinachoitwa 'kukopi na kupesti'. Nazungumzia hasahasa kwenye tasnia ya biashara. Ukiwa tu na wazo zuri la biashara, ukaliweka katika vitendo na watu wengine wakagundua kuwa wazo hilo lina uwezekano wa kuzalisha faida nzuri, utashangaa utitiri wa watu wengine watakavyoibuka na kulitumia wazo lilelile ulilolianzisha wewe.

Kuna kuiga kwa aina 2, kuiga kubaya(unakopi idea, kitu cha mtu mia kwa mia kama kilivyo) na kuiga kuzuri kunakojenga(kuiga kiubunifu).
Kuiga au kukopi kwa njia hiyo ya kwanza kuna madhara makubwa kiuchumi siyo tu kwa kampuni au yule aliyeibiwa bali hata na kwa jamii na serikali kwa ujumla, kwani uigaji wa namna hii huua vipaji na ubunifu ukizingatia mbunifu alipoteza muda wake mwingi na gharama kufanya ubunifu huo. Hii ndiyo sababu serikali nyingi na hata Umoja wa Mataifa wenyewe jambo hili hawalitaki kabisa na zimewekwa hata sheria mbalimbali kama vile ile ya hatimiliki, hakimiliki na ulinzi wa alama za biashara kusudi kukomesha na kuzuia vitendo vya namna hiyo.

Unaweza ukaiga(kukopi na kupesti), lakini ni lazima uhakikishe unaongeza ubunifu wenye tija kwa watumiaji.
Kuna ule msemo maarufu sana duniani usemao; “You can’t reinvent the wheel”(Huwezi ukagundua upya gurudumu) wakimaanisha, mtu kutaka kugundua kitu kipya kabisa hapa duniani leo hii ni jambo gumu sana. Vitu vingi vimekwisha kugunduliwa na kilichobakia sasa ni kuviongezea ubunifu kusudi kuviboresha zaidi na kuvifanya viwe na uwezo wa kufanya kazi nyingi au kuwa na matumizi mengi zaidi ya vile vya awali.

Kuiga kitu kwa asilimia mia moja ni kosa na tena hata ni aibu kubwa kwa yule anayeiga. Ushindani haumaanishi kukopi mawazo ya mtu mwingine mazima kama yalivyo, bali ni kutoa kitu tofauti na kilichokuwa na manufaa zaidi kwa walaji au watumiaji kushinda kile cha mshindani/washindani wako.

Unaweza ukakuta mtu au kampuni fulani imeiga mawazo ya mtu/kampuni nyingine lakini ikiwa katika kuiga huko kuna kitu(thamani) kilichoongezwa pale, huwezi ukalaumu na kudai kuwa kaiba wazo la mwingine.

Katika mifano ifuatayo huwezi ukaiita ni kukopi na kupesti.
1) Kuiga au kutengeneza bidhaa za aina moja.
Kampuni inaweza ikatengeneza bidhaa au huduma zinazofanana na za kampuni nyingine lakini kukawa na tofauti katika alama(features) au formula(kanuni ya utengenezaji). Mfano mzuri tunaweza tukaupata kutoka makampuni ya vivywaji baridi ya hapahapa kwetu nyumbani Tanzania ya Cocacola, Pepsi, Azam cola na Sayona. Wakati Azam na Sayona wanatoa vinywaji vyao vyenye asili ya cola hukuwasikia Cocacola na Pepsi wakilalamika au kwenda mahakamani kudai wameibiwa wazo la soda zao za cola.

Lakini kama Azam na Sayona pengine wangeliziita soda zao majina yaleyale ya “cocacola au pepsi” au kutumia chupa zinazofanana kila kitu na zile za kwao, basi bila shaka hapo ni lazima pangetokea mgogoro mkubwa. Vilevile  ijapokuwa vinywaji vyote hivyo hutumia kiasili kimoja yaani “cola” lakini bidhaa zao zina tofauti kubwa katika ladha na hata utakuta formula(kanuni ya uchanganyaji vile viungo) anayotumia kila mmoja ni tofauti na ya mwenzake.

Kingine ni kwamba ujio wa kampuni hizo mbili. Azam na sayona ulisababisha mapinduzi makubwa katika bei za soda na hata vifungashio vyake(packaging). Zamani kabla ya hapo bei za soda zilikuwa na ukiritimba mkubwa lakini makampuni yalipoongezeka wakaanza kushindana vikali mpaka watu tukaanza kupata soda za 500 mpaka 300 ilihali soda ilishafika mpaka 700. Chupa nazo badala ya zile za kioo zilizokuwa zimezoeleka sasa tukashuhudia za plastiki(takeaways) zikitumika kwa wingi. Zamani ilikuwa kupata soda iliyotiwa ndani ya chupa ya plastiki ni ‘ishu’ na hata ulipoipata, bei yake ilikuwa haikamatiki, 1000/= mpaka 1500/= na kuendelea. Leo hii ukitaka mpaka ya sh. 500/= unapata bila shida yeyote.

2) Kuiga kazi za ubunifu wa mawazo(Intellectual properties)
Kazi hizi ni kama vile za uandishi, utunzi wa muziki, filamu, alama mbalimbali kama logo nk. Mfano mzuri ninao mimi mwenyewe. Nilipotoa kitabu, “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA” Kitabu kilitoka sambamba na kampeni niliyoipa jina la; “KUELEKEAUTAJIRI” Kuna watu wengi waliojaribu kuiga wazo lile. Katika blogu kadhaa niliona baadhi ya insha “articles” zangu zikiwa zimekopiwa nyingine nzimanzima kama zilivyo, wengine wakaanzisha blogu zilizokuwa na maudhui kama yaleyale.

Wapo hata waliotunga vitabu vilivyokuwa na maudhui sawasawa na ya kile kitabu nilichotunga, kwa mfano mimi nilisema; Mifereji 7 ya Pesa” wengine wakaita, Mifereji 10 ya pesa, mifereji 12 ya kipato nk. Mfano mwingine ni makala maarufu nilizoandika katika website ya jifunzeujasiriamali wakati huo ikijulikana kama “Kuelekeautajiri”, kama vile; “Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?”“Natengeneza sabuni, shampoo, batiki na Unga wa lishe lakini sioni unafuu wowote wa maisha” na hata makala iliyosema “Rasilimali adimu kuliko zote duniani, ikipotea imepotea huwezi tena ukaipata maisha yako yote”

Waliokopi makala hizo wengine walikopi kama zilivyo lakini pia kuna waliobadilisha heading kidogo au hata kubadili kabisa maneno lakini maudhui yakabakia kuwa ni yaleyale. Mimi binafsi kwa upande wangu hilo halikunipa shida, kwanza nilifurahi na kutiwa moyo kwani ndilo lililokuwa lengo langu kuu, kuhamasisha watu wengi kwa kadiri inavyowezekana kuchukua hatua ya kupigana na umasikini kwa vitendo hasa kupitia shughuli zinazohusisha mawazo au akili zao huku zikiwapa kipato.

Hata katika kitabu hichohicho kama ulikisoma kuna mahali nilitoa ‘ruksa’ ya kukopi, nikihamasisha juu ya kitabu kingine, MICHANGANUO YA BIASHARA NAUJASIRIAMALI” niliandika maneno haya na hapa nanukuu, “Michanganuo yetu ni ruksa kabisa mtu yeyote yule kuiga, ilimradi tu usiige kama ‘mbumbumbu’ kwa asilimia mia moja” mwisho wa kunukuu. Kwa vyovyote vile nisingeliweza kukasirika au kumzuia mtu yeyote yule ambaye angetumia “kuiga kuzuri” au “kukopi kiubunifu” kazi zangu.

Na zaidi ya hapo niligundua tena kwamba, kumbe kile nilichokuwa nikikifanya kilikuwa ni kitu kizuri na ndiyo maana watu wengine nao wakaanza kukopi ‘idea’ yangu. Matokeo kwa ujumla ya kampeni ile na Kitabu hicho cha Mifereji 7 ya Pesa bila shaka yeyote mimi huwa siachi kusema kuwa pengine ndiyo yaliyokuja kuleta mwamko uliokuwepo sasa wa watu wengi hasa bloggers na waelimishaji mbalimbali kupitia vitabu, kwenye magazeti na semina kutoa elimu ya ujasiriamali, kujikomboa kiuchumi na maendeleo binafsi kwa jamii.

Kampeni ile ilisambaa mithili ya moto wa nyika, nikawa napigiwa simu nyingi sana watu wakitaka kufahamishwa zaidi juu ya kampeni ile “kuelekeautajiri”. Nilifanya kosa moja kubwa sana na ambalo nitalijutia siku zote, baada ya kuona watu wakinisumbua sana juu ya kampeni hiyo, niliamua kuisitisha ghafla(soma makala hii kwanini nilisitisha kampeni hiyo) na kubadilisha jina na hata muonekano mzima wa blogu zangu nikidhania pengine watu walikuwa wamenielewa vibaya. Baada ya kubadilisha majina na kuita “jifunzeujasiriamali” hakuna tena mtu aliyehangaika kunifuatilia.

Muziki na Filamu.
Muziki na filamu navyo ni hivyo hivyo, hauwezi ukakopi muziki au filamu ya mtu mwingine kama ilivyo na ukabaki salama. Lakini maudhui ni ruksa na hata mtindo na vionjo hauwezi ukamlaumu mtu eti kaiga vyakwako. Rege kapiga Bob Marley, rege kapiga Lucky Dube, rege kapiga Jimmy Cliff, rege hiyo hiyo kapiga Alpha Blondy. Lakini hamna hata mmoja aliyelalamika kuibiwa mtindo huo na mwenzake.

Lucky Dube kwa mfano alipiga wimbo uitwao “One love” jina linalofanana sawasawa na la wimbo wa Bob Marley nao unaoitwa jina hilohilo, lakini ukizisikiliza rekodi hizo zote mbili wala hazifanani kabisa kimdundo japo zote ni reggae na hata mashairi hayafanani isipokuwa jina tu na pengine maudhui yake yanaweza yakafanana.

Cheki pia, hata kuna filamu kama vile, Tarzan, au Titanic, filamu hizo zimewahi kuchezwa na watu tofauti wengi na ijapokuwa maudhui na majina zinafanana lakini tofauti zake ni kubwa.

“Templates”(Themes) za blogu na tovuti.
Hizi ni violezo au kwa maana nyingine unaweza ukazifananisha na daftari lililokuwa tupu halijaandikwa bado kitu chochote ndani. Baadaye daftari hilo unapoandika na kuchora vitu ndani yake tunalinganisha na unapoweka ‘contents’, vitu, maandishi, picha, sauti nk. kwenye blogu/mtandao/tovuti/website, vyovyote vile utakavyoita na hatimaye vitu hivyo visomwe, kusikilizwa au kuonwa na watu/hadhira.

‘Theme hizi/templates’ hutengenezwa na watu mbalimbali wenye ujuzi wa lugha ya kompyuta(coding) na kisha baadaye kuziuza au kuzitundika bure mtandaoni kwa mtu yeyote atakayehitaji basi aweze kuzitumia. Blogu nyingi hapa Tanzania hutumia hizi templates za bure.

Sasa tukichukua mfano, A blogu yake ametumia template ya bure, B naye akija akatumia template ileile, A hawezi kwa namna yeyote ile kulalamika na kudai kuwa eti B kakopi wazo lake. Wakulalamika hapa angekuwa ni yule mtengenezaji wa hiyo template lakini mtengenezaji mwenyewe keshasema template yake itumiwe na mtu yeyote anayeihitaji tena bure.

Hata za kununua bado huwezi ukamlaumu mtu kwani watu tofauti wanaweza wakanunua template hiyo hiyo moja. A kitu ambacho angeliweza kukifanya ili awe na haki ya kudai watu wasikopi template yake ni kutengeneza template yake kuanzia moja “from the scratch” akitumia “code” zake mwenyewe na isitoshe akaikatia hatimiliki, kwa hapa kwetu ni pale BRELLA.

Kwa mfano tovuti yangu hii, jifunzeujasiriamali.com, template yake niliitengeneza mwenyewe tangu mwanzo bila usaidizi wowote na hata watu wengine siku hizi huniuliza “mbona huibadilishi, imepitwa na wakati, kwanza siyo mobile friendly” lakini huwa nawajibu “nitabadilisha tu taratibu” na kweli sina haraka nayo kwasababu moja tu, “inanikumbusha mbali sana, kipindi sijui chochote kuhusu maswala ya mitandao na wala sina laki tano za kumlipa mtaalamu wa tovuti.”

Unapokuwa umeuwekea ubunifu wako hatimiliki, unayo haki ya kumshitaki mtu yeyote anayekuibia na kukopi ‘idea’ au kitu chako na akakulipa pesa nzuri.

Usije ukaogopa kutumia template ya bure au hata ya kununua mtandaoni iliyokwisha kutumiwa na mtu mwingine tayari kwa kuhofia eti utaonekana umekopi na kupesti, hakuna kitu kama hicho katika dunia hii ya utandawazi. Ilimradi imekuvutia, wewe download au nunua, jiwekee blogu/website yako ipendeze.

Unapokopi kitu/idea ya mtu mwingine, epuka kukopi pale kwenye kitovu(roho) ya ule ubunifu ilipo. Roho au kitovu cha ubunifu kwa mfano kwenye soda za cola kipo katika formula(kanuni) ya uchanganyaji wa viungo, jina halisi la soda na vitu kama nembo. Kwenye utunzi au kazi yeyote ile ya maandishi roho ipo kwenye yale maandishi na mpangilio wake mzima na wala siyo katika maudhui yake ndiyo maana ukikopi kazi ya mtu mwingine neno kwa neno ni kosa kubwa. Kwenye blogu au tovuti roho ipo kwenye ‘contents’, kile kilichomo ndani, na kama ni template basi ipo kwenye hatimiliki yake.

Hakuna kitu “Search enginesmfano google wanachokichukia kama mtu kukopi kazi iliyokwishatolewa na mtu mwingine pasipo kuomba idhini ya mwenyewe. Lakini hata siku moja sijawahi kusikia google wamempiga mtu ‘penalty’ kisa eti katumia template aliyokwishatumia mtu mwingine, watakupiga penati wakibaini umekopi maandishi ya mtu mwingine.

Magari na vyombo vya moto.
Mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 kulizuka ushindani mkali baina ya makampuni makubwa ya magari duniani. Volkswagen ndiyo iliyoanza kwa kuja na ubunifu wake ambapo iliamua kuitoa tena upya gari yake ndogo aina ya “Beetles” iliyopata umaarufu mkubwa sana miaka ya 60 na 70 huko nchini Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Lilikuwa ni wazo zuri sana na wakafanikiwa kuliteka soko kwa kasi ya ajabu! Kila mtu alikuwa na shauku ya “ku-experience way back” lakini katika muonekano na hisia mpya.
Gari ndogo aina ya Volkswagen beetles mpya. 
Haikuchukua hata muda mrefu, wapinzani wao BMW nao wakaona wasibakie nyuma. Wazo ni lilelile lakini wao wakaitoa tena upya gari yao ndogo iliyowahikutamba miaka ya 60 na iliyojulikana kama Mini Cooper S, Mini Cooper zilitamba sana nchini Uingereza miaka hiyo ya 60. New Mini Cooper S lilikuwa ni wazo lilelile waliloanzisha Volkswagen.
New Mini Cooper S(gari ndogo iliyotolewa upya na BMW) 

Washindani wengine FIAT nao hawakukubali kuchelewa, mara moja kwa kutumia wazo lililoanzishwa na Volkswagen la kurudisha mtindo wa zamani wa magari, wakalizalisha tena upya gari lao dogo la Kiitaliano, Fiat 500, gari lililotamba mno miaka ya 50 na 60.

Fiat 500 toleo jipya la iliyokuwa fiat500 ya miaka ya 50.
Wateja hupendelea sana vitu vya namna hii, hasa ushindani wa kiubunifu usiomuumiza mtu mwingine lakini unaochochea maendeleo na ndiyo maana ukaona makampuni yote matatu ya magari yakitumia wazo lilelile moja lililoanzishwa na Volkswagen bila kujali ni nani aliyelianzisha.

Kibaya hapo ni kama mmoja wao angelitoa gari linalofanana kila kitu kwa asilimia mia moja na mwenzake. Lakini kila mmoja kwa kutumia wazo la kuzalisha tena upya magari yao ya zamani na katika muonekano mpya wa kisasa, hakukuwa na tatizo lolote hapo na huwezi ukawalaumu BMW wala FIAT kwa kudai wamekopi na kupesti.

HITIMISHO.
Kuiga kupo kila mahali na kutaendelea kuwepo nyakati zote. Nchi zilizoendelea wangezuia kabisa kuiga, sidhani nchi kama hizi za kwetu huku kungelikuwa na maendeleo yeyote. Njia za kuzuia ‘uigaji mbaya’ zipo kama vile, kuuwekea ubunifu hatimiliki, hakimiliki kwa kazi za utunzi na usanii, kulinda kwa kusajili alama za biashara nk. Njia hizi hupunguza tu na wakati mwingine kuzuia kwa muda watu kukopi kazi za watu wengine. Simaanishi kwamba hazisaidii hapana, lakini kufanya kwake kazi vizuri kunategemea zaidi wazo au kitu kilichobuniwa iwe ni kweli umekibuni na wala siyo kwamba na wewe ulikikopi kutoka mahali pengine na kisha ukadai umekibuni.

Njia pekee na ya uhakika zaidi inayoweza ikakusaidia kupambana na waigaji watakaokopi kazi zako ni kuhakikisha unakuwa bora muda wote katika biashara au chochote kile unachokifanya. Waigaji watakapobaini haukatishwi tamaa wala kutikisika na kukopiwa kazi zako, basi wenyewe ‘watasarenda’ na kukuacha ukisonga mbele kifua mbele.

Kwa upande mwingine, ‘kuiga kuzuri’, ndiko kunakoleta ushindani na hatima yake maendeleo kupatikana kwani vinginevyo duniani kusingelikuwa na kitu kipya. Vitu vingi vipya ni vilevile vya zamani vilivyoboreshwa au kuongezewa madoido(features) zaidi.
........................................................................................................

Mpenzi msomaji wa blogu hii ya Jifunzeujasiriamali, kuna mambo mengi zaidi na makubwa yanayotarajiwa kuja nyuma ya blogu yako hii, hivyo nakuomba sana usikose kuwa na sisi kila mara. Pia ikiwa utahitaji vitabu kutoka kwetu juu ya ujasiriamali na biashara basi usisite kuwasiliana nasi au tembelea ukurasa huu wa SMARTBOOKSTZ. 'Jipatie free of charge' kitabu cha 'Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio' pamoja na vitabu vingine vizuri 25 kwa kujiunga hapa na kuweka e-mail yako

Mawasiliano yetu ni haya yafuatayo;

SIMU:             0712 202244, 0765 553030 na 0689 303098
TELEGRAM:   0712 202244 au @petertarimo
E-MAIL:          jifunzeujasiriamali@gmail.com    

2 Responses to "KUBUNI KITU KIZURI NI HATARI! WATU LAZIMA WAKOPI NA KUPESTI, UFANYENINI KUZUIA HILI?"

  1. Unasema kuiga kiubunifu siyo vibaya, wewe hujawahi kukopiwa kitu ukaona machungu yake, niliwahi kufunga biashara yangu ya nguo mwananyamala hivi hivi baada ya jamaa mmoja kuona nilivyokuwa nauza akajaniwekea pembeni biashara kama ileile. Ningekuwa mchawi ningemloga.

    ReplyDelete
  2. Kwanza hebu naomba ondoa hilo neno 'uchawi' kwanza maanake hizi imani imani mara nyingi sana ndizo hutufunga hata tusiwe na ujasiri wa kuthubutu kufanya vitu. Ikiwa unaamini uchawi ni dawa basi hata ujasiri wa kupambana nae kibiashara usingeliweza kuwa nao.Ulipaswa kujiamini na siyo kukimbia na kumwacha. Wewe tayari alikukuta na wateja wako, ni mbinu gani aliyoitumia kuwateka? Ikiwa ulikuwa unawapa huduma stahiki kwa bei stahiki sidhani kama huyo jamaa angelikuwa na ubavu wakukungoa, badala yake yeye ndiye angelifunga virago baada ya miezi michache. Ulipaswa uwe mvumilivu kidogo na siyo siku mbili tatu tu ukakimbia. Asante

    ReplyDelete