AJIRA SIYO LAANA, NI MTAJI WA UHAKIKA KULIKO AINA NYINGINE ZOTE ZA MITAJI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

AJIRA SIYO LAANA, NI MTAJI WA UHAKIKA KULIKO AINA NYINGINE ZOTE ZA MITAJI

Ajira siyo laana.
Kwa miongo mingi sasa Duniani, kumekuwepo na mjadala mzito juu ya ajira na shughuli za kujiajiri binafsi au unaweza ukasema kumiliki biashara mwenyewe. Njia zote hizi mbili, kufanya kazi ya ajira na kumiliki mradi wa kiuchumi, ni njia za kumfanya binadamu aweze kupata kipato kinachomuwezesha kuishi hapa duniani.

Katika mjadala huo, kila upande, iwe ni wale waliokuwa upande wa ajira au wanaotetea suala la kujiajiri, kila upande unavutia kamba kwake. Lakini mara nyingi upande ule wa ajira binafsi au kumiliki biashara ndio upande unaoonekana kuwa na nguvu na hata kufika mahali ambapo karibu kila mtu hushawishika na kuamini ya kwamba kuajiriwa ni kama vile laana na kujiajiri au kumiliki mradi wa kiuchumi ndiyo “habari ya mjini.”


Kujiajiri binafsi ni kweli kwamba ndiyo njia sahihi na ya uhakika zaidi inayoweza kumhakikishia mtu kipato kuliko ajira lakini hakuna kitu chochote duniani kisichokuwa na faida na hasara zake. Kwamfano wakati kujiajiri au kumiliki biashara kunatazamwa kama njia bora zaidi ya kufikia uhuru kipesa, kuna changamoto nyingi zinazoambatan na kuendesha biashara tofauti na upande wa ajira ambao mwajiriwa akishaingia mkataba na mwajiri basi, kazi yake kubwa inabakia kutekeleza yale anayotakiwa kuyatekeleza akisubiri mshahara wake, haumizi kichwa pesa zitatoka wapi wala ni vipi faida itakavyopatikana.

Je, Inawezekana kila mtu duniani akajiajiri binafsi?
Dunia kwa jinsi ilivyoumbwa, karibu kila kitu, viumbe hai na hata vile visivyokuwa na uhai hutegemeana. Ni lazima kitu fulani kiwepo ndipo na kitu kingine nacho kiweze kuwepo. Hebu tutazame mifano michache ifuatayo;

Uislamu na Ukristo.(Religious diversity)
Natumia dhana hii nyeti sana ya dini kuonyesha uzito wa vitu tofauti vinavyotegemeana hata ikiwa katika mazingira ya kawaida inategemewa haviwezi kabisa kutegemeana.
Uislamu na Ukristo, kila kimoja kingelipenda mwenzake atoweke duniani kusudi chenyewe kiweze kuenea maeneo yote duniani. Lakini kwa bahati mbaya asili haiwezi ikaruhusu jambo la namna hiyo kutokea.

Dini zote hizi mbili zitaendelea kuwepo duniani milele na milele na wala hamna moja itakayoweza kumtokomeza mwenzake ili iendelee kuwepo. Hivi ndivyo Mungu alivyoumba Ulimwengu. Moja ikitoweka basi na ujue nyingine haitakuwepo tena. Duniani kungelikuwa na dini moja tu, basi hiyo wala isingelikuwa na jina, kwanza haingekuwepo kwa sababu hamna nyingine ya kuitofautisha nayo.

Mimea na Wanyama(Ecosystem)
Kila siku wanasayansi hupiga kelele; “Jamani msikate tena miti ovyo, msiue tembo,…msifanye uvuvi haramu….!” Wanajua kitu kimoja hutegemea kingine na kinapotoweka basi kile kinachotegemea nacho hakipo tena. Unaweza ukauliza, “kwani Tembo wana kazi gani, kwanza ni waharibifu wakitoweka sisi binadamu tuna hasara gani?” Akitoweka Tembo ujue kuna viumbe wengine wengi na mimea ambavyo navyo vitatoweka. Kwa mantiki hiyo athari hizo huenda mpaka kwenye kuathiri hali ya hewa, maziwa, mito na hata bahari na matokeo yake ndiyo kama hayo tunayoyashuhudia sasa hivi, ukame, joto kuongezeka sambamba na kina cha bahari.

Ajira na biashara binafsi(kujiajiri) ni vitu viwili vinavyotegemeana sana.
Ukimkuta mtu anakuhubiria kuwa ajira ni mbaya, ajira ni utumwa, ajira haifai kabisa, hebu mchunguze vizuri, je, nyumbani kwake hana hata housegirl? Kama ni mwanamume, labda amemfungulia mkewe mradi mfano wa saluni, je, hiyo saluni mkewe huwa anashinda hapo mwenyewe na kufanya kila kitu peke yake wateja wanachohitaji?

Nijuavyo mimi asilimia kubwa ya watu matajiri, huufikia utajiri baada ya kufungua miradi ya biashara zaidi ya mmoja. Katika kitabu nilichoandika kiitwacho, “MIFEREJI7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA” jambo hili nililielezea kwa kina sana. Na huwezi ukahudumia mradi zaidi ya mmoja pasipokuwa na wasaidizi ambao ni lazima tu uajiri watu, penda usipende, vinginevyo basi utajiri uusikie tu kwa wenzako. Au pengine iwe utajiri huo unaupata kama urithi au umeshinda bahati na sibu, mambo ambayo ni adimu mno kutokea, katika watu tuseme labda 1000 hutokea watu wa namna hiyo 2 au 3, sasa hebu fikiria ni wangapi watabahatika?


Kwa upande mwingine napo, kwa kuwa siyo rahisi kila mtu akawa na rasilimali za kufungua biashara au mradi binafsi wa kiuchumi, utakuta wale wasiokuwa na biashara hutafuta kazi za kuajiriwa kutoka kwa wale wenye miradi/biashara au katika taasisi za uma. Hilo hutokea moja kwa moja ‘automatiki’ kabisa na wala siyo kwa mtu kulazimishwa. Unahitaji pesa kwa ajili ya kuendeshea maisha, huna mtaji wala mradi wowote, utaishije kama siyo kuomba kazi ya ajira mahali?

Suluhisho.
Kuajiriwa na kuajiri kulikuwepo tokea enzi za dahari, na vitu hivi viwili vitaendelea kuwepo huku vikitegemeana mpaka pale Ulimengu utakapofikia tamati. Cha kuzingatia hapa ni kwamba, binadamu unapozaliwa mpaka siku ya kufa kwako, hapo katikati hutokea mabadiliko mengi. Kuna kipindi utaajiriwa na kuna kipindi utaajiri watu. Nyakati hazilingani na wala siku kamwe hazigandi. Aliyeajiriwa leo siye atakayeajiriwa kesho.

Kuna nyakati fulani watu kama kina Steve Jobs, Reginald Mengi, Aliko Dangote na wengine wengi waliwahi kufanya kazi za ajira katika maisha yao iwe ni serikalini au makampuni binafsi, lakini walichotilia maanani ni kuwa, ajira ilikuwa ni kazi ya mpito kwao na chanzo kikuu cha mtaji wa kuanzishia miradi yao ya kibiashara. Mwenyezi Mungu hawezi tu kukuumba tangu unatoka tumboni mwa mama yako wewe uwe ni mtu wa kuajiri watu tu hapana, ni lazima kuna wakati fulani utawatumikia watu wengine hata ikiwa ni kwa kazi ya kujitolea. Hata mwanamfalme wa Uingereza kabla hajatawazwa rasmi kuwa mfalme au malkia, hupangwa kwanza kazi za kuwatumikia watu kama raia wengine wa kawaida.

Na hii ndiyo maana nasema; “Ajira siyo laana, bali ichukuliwe kama chanzo kizuri kuliko vingine vyote vya mitaji ya kuanzisha miradi na biashara binafsi.

……………………………………………………………………….
Mpenzi msomaji, sasa hivi vitabu vyetu vyote unaweza ukavipata moja kwa moja mtandaoni kwenye simu yako ya mkononi(smartphone), tablet au kompyuta ya mezani kupitia;
·       E-mail yako au
·       Telegram

Wasiliana na sisi kupitia;
Simu:   0712 202244 / 0765 553030 /  0689 303098

E-mail: jiunzeujasiriamali@gmail.com

Kucheki vitabu vya biashara na ujasiriamali vya kiswahili tembelea SMARTBOOKSTZ


Kudownload/kupakua kitabu cha bure cha kiswahili pamoja na vitabu vingine vizuri 25 katika lugha ya kiingereza bonyeza hapa kujiunga na blogu hii.

0 Response to "AJIRA SIYO LAANA, NI MTAJI WA UHAKIKA KULIKO AINA NYINGINE ZOTE ZA MITAJI"

Post a Comment