MAWIMBI YASIYOONE ALIYOTABIRI MWANASAYANSI ALBERT EINSTAIN YANASWA, NI BAADA YA MIAKA 100 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAWIMBI YASIYOONE ALIYOTABIRI MWANASAYANSI ALBERT EINSTAIN YANASWA, NI BAADA YA MIAKA 100

Hatimaye Wanasayansi wa Marekani wakishirikiana na wenzao wa Ulaya wamefanikiwa kuyanasa mawimbi yasiyoonekana  kwa macho ya kawaida wala darubini za kawaida. Mawimbi hayo yanayojulikana kama “Gravitational waves” yalitabiriwa na  mwanasayansi anayesemekana kuwa mashuhuri zaidi kuwahi kutokea duniani na aliyewahi kugundua mambo makubwa mno, Albert Einstain.


Mnamo mwaka 1915, Einstain katika Kanuni yake maarufu ijulikanayo kama “General Relativity” inayoelezea uhusiano wa vitu vyote vilivyokuwepo ndani ya Ulimwengu, aligundua pia kuwepo kwa nguvu fulani ya mawimbi, ‘gravitational waves’ ambayo huweza kuzalishwa na kitu chochote kile kilichokuwa kwenye mwendo wa kasi  tukiwamo na hata sisi binadamu, nyota, jua, na maumbo mengine yote yaliyokuwepo angani.

Nguvu hizi huwa kubwa kadiri kitu kinachohusika kinavyokuwa kikubwa zaidi na kwa kasi kubwa. Mawimbi hayo husambaa mithili ya mawimbi yanayotokea unapotupa jiwe katika maji. Lakini jambo la ajabu pamoja na Einstain kutabiri mawimbi hayo yasiyoonekana kiurahisi miaka 100 iliyopita, hakuna mtu yeyote aliyeweza  kuthibitisha uwepo wake wala ni kwa nini nguvu hizo zipo.


Wanasayansi mbalimbali katika vipindi tofauti walijaribu kuunda vyombo vya kuyanasa mawimbi hayo  lakini haikuwezekana mpaka hivi leo ambapo kwa mara ya kwanza kabisa jaribio lililopewa jina la “Advanced Laser Interferometer Gravitational Wave Observation(VIGO)” limeweza kuyanasa na kuyapima mawimbi hayo na mpaka sasa ninapoandika, Wanasayansi hao wanaendelea na kazi ya kuchanganua ‘data’.
Mwanasayansi katika uchunguzi huo.
Majaribio hayo yamefanyika katika maeneo tofauti Duniani yakiwamo Marekani, Italia na Ujerumani na katika kila moja watalinganisha matokeo yake kuona ikiwa taarifa(data) zinafanana na hivyo kuthibitisha kwa uhakika kabisa pasipo shaka kuwa alichotabiri mwanasayansi Albert Einstai katika kanuni yake mashuhuri “General Relativity” miaka 100 iliyopita kilikuwa sahihi kwa asilimia 100%.
Mawimbi hayo"gravitational waves".
Kufanikiwa kuthibitisha uwepo wa mawimbi hayo kuna umuhimu mkubwa katika uchunguzi wa anga za juu pamoja na kufahamu namna Ulimwengu ulivyotokea, kitendawili ambacho kimekuwa kigumu kuteguliwa na wanasayansi kwa muda mrefu sasa. 

Ugunduzi huu pia utasaidia katika uchunguzi wa maeneo mengine ya ulimwengu katika anga za mbali kabisa ambazo vyombo vya kawaida “telescope” haviwezi kuona na pengine kugundua mifumo mingine ya Sayari inayofanana na huu wa jua letu ambao labda kuna sayari zilizokuwa na uhai kama ilivyokuwa Dunia yetu. Kwani mpaka sasa hivi katika mfumo wetu huu wa sayari hakuna mahali popote palipogundulika kuishi viumbe hai.

0 Response to "MAWIMBI YASIYOONE ALIYOTABIRI MWANASAYANSI ALBERT EINSTAIN YANASWA, NI BAADA YA MIAKA 100"

Post a Comment