KUMRADHI SANA MTEJA WETU WA MANZESE TIP TOP | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUMRADHI SANA MTEJA WETU WA MANZESE TIP TOP


Tumekuwa tukiwasiliana kwa meseji ya simu tokea jana mchana tarehe 24/12/2015, kwa bahati mbaya ‘sikuisave’ namba yako kwenye simu yangu nikitegemea ‘kuisave’ baadaye na pia nikijua kwakuwa namba ipo katika meseji basi hamna tatizo. Leo baada ya kunielekeza nikuletee kitabu Manzese Tip Top na nikakuahidi kuwa kitabu kipo njiani kinakuja, nilikuwa nimemtuma msaidizi nikampa na ile namba uliyokuwa ukiwasiliana nayo namimi kusudi akifika tip top akupigie na kukupatia kitabu.

Kosa kubwa nililofanya, baada ya kumpa ile namba nilifuta meseji ya mwisho uliyonitumia kwa hiyo ikawa namba yako niliifuta. Baada ya kama  dakika 45 hivi kupita nilishikwa na butwaa kumuona yule niliyemtuma kitabu akirudi huku mkononi akiwa ameshika kile kitabu kama alivyoondoka nacho.

Kumuuliza akanijibu kuwa alipofika Magomeni Mikumi alishuka kutoka gari la Mwananyamala alilokuwa amepanda ili atembee mpaka Usalama kupanda daladala zinazokwenda Manzese, baada tu ya kumaliza kona ya ilipo sheli ya mafuta, alipigiwa simu na alipojaribu kupokea, akaja mtu nyuma yake na kumpora ile simu kisha akatimua mbio kuvuka barabara huku akitokomea maeneo ya ilipo hospitali ya Magomeni. Anase alikosa hata ujasiri wa kupiga kelele kwa jinsi mwizi yule alivyokuwa akijiamini, mara tu baada ya kuvuka bara bara wala hakuonekana kuwa na wasiwasi, alikuwa akitembea utadhani hajaiba vile!

Nisingeandika yote haya kwenye blogu na kwa kweli hakukuwa na mantiki wala maslahi yeyote kwa wasomaji wengine lakini nimelazimika kuandika kutokana na jinsi tukio lenyewe lilivyokaa, kwanza sikuwa tena na namba ya yule mteja na hata nilipojaribu kutizama vizuri katika simu yangu sikufanikiwa kuipata, nikajaribu kucheki kwenye orodha ya simu nilizopigiwa nikakumbuka kumbe hakuwa amewahi kunipigia  tulikuwa tukiandikiana meseji tu.

Nikabaki sina tena namna yeyote ile ya kuwasiliana na mteja wangu huyu, njia pekee iliyokuwa imebakia nikadhani labda baada ya kusubiri kwa muda mrefu ‘angenitext’ tena kwa meseji lakini kumbe kama unavyojua tena tabia za wateja” hata kama ingelikuwa ni mimi binafsi kwa kweli nisingelikuwa tena na moyo wa kutuma meseji kwani ningejisikia kama vile ni kitu cha kuomba kumbe natoa pesa yangu. Na kwa kweli hakuwasiliana tena na mimi mpaka hivi ninapoandika ujumbe huu.

Kwa hiyo lengo langu kuandika haya hapa siyo jingine bali kubahatisha labda mteja wangu huyu anaweza kwa bahati akasoma hapa, basi aweze kufahamu kilichotusibu kwani nafahamu ni maswali mengi kiasi gani aliyojiuliza baada ya kutokumuona mtu aliyemuahidi anamletea kitabu cha “JIFUNZE MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI”. Basi nakuomba kwa dhati ya moyo wangu na kama umesoma hapa tafadhali fahamu kuwa  hatukuwa na nia mbaya kutokukufikishia kitabu, kwa niaba ya SELF HELP BOOKS COMPANY LTD, narudia tena, “TUSAMEHE” na ikiwa tutapata njia yeyote ile ya kuwasiliana na wewe basi tutarekebisha makosa haya haraka sana na tunaahidi  hayatajitokeza tena kwa mteja yeyote yule.

Asante,
Ni mimi Peter Augustino
Mtendaji mkuu, SHBPL.

0 Response to "KUMRADHI SANA MTEJA WETU WA MANZESE TIP TOP"

Post a Comment