MECHI KALI YA KIHISTORIA: UHOLANZI VS SPAIN, MASHABIKI WASHANGAA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MECHI KALI YA KIHISTORIA: UHOLANZI VS SPAIN, MASHABIKI WASHANGAA


Ni maajabu, kila mtu haamini kilichotokea, baada ya mabingwa watetezi wa kombe la Dunia kuchapwa kama watoto wa chekechea, mabao 5 kwa 1 tena baada ya kuongoza kumiliki mpira ‘(ball possession)’ katika kipindi chote cha kwanza pamoja na kupata bao la kuongoza katika dakika ya 27.


Kila mtu alifikiri kuwa Uholanzi ingelifungwa mabao mengi zaidi katika kipindi cha pili lakini matokeo yake yaligeuka kuwa kinyume kabisa kwani hata kabla ya kipindi hicho cha kwanza kumalizika Waholanzi walisawazisha mnamo dk. Ya 44, bao lililowekwa kimiani kwa kichwa safi kabisa na Nahodha wa timu hiyo, ‘Robin Van Persie’ huku golikipa wa ‘spain’ akibaki akitazama tu.

Ni kama vile Waholanzi walikuwa wakiwasoma miamba hao wa kombe lililopita la Dunia Bondeni A.Kusini kwani ilipofika kipindi cha pili tu, dakika za mwazoni, ‘Arjen Robben’ akaifungia timu yake goli la pili. Hii ni moja kati ya mechi nzuri kabisa mashabiki wameishuhudia katika kombe hili la Dunia la mwaka 2014 na pengine itabakia kuwa historia kutokana na jinsi watu wengi walivyokuwa wakitabiri bingwa mtetezi Uhispania kufanya vizuri.

Kadiri muda ulivyokuwa ukienda Wahispania walizidi kuchanganyikiwa hasa kipa wao, jambo lililosababisha walambwe tena bao jingine dakika ya 64, bao hilo lilifungwa na ‘Stefan de Virji.’ Bao la nne lilipachikwa wavuni na ‘Robin Van Persie’ kwa mara ya pili sasa na kufanya matokeo yasomeke 4-1. Kama vile Robin Van Persie na  mwenzake Arjen Robben walikuwa wamepanga kupachika mabao mawilimawili katika mechi hii, ‘Arjen’ naye katika dakika ya 80 karibu na mchezo kumalizika aliifungia timu yake ya Uholanzi bao la tano na ambalo ndilo lililokuwa la mwisho katika mechi hii.

Bao la pekee walilopata Uhispania lilikuwa ni lile lililofungwa kwa mkwaju wa penalty iliyopigwa na ‘Xabi Alonso’ mnamo dakika ya 27 katika kipindi cha kwanza, baada ya mchezaji wao Diego Costa kuangushwa chini.









0 Response to "MECHI KALI YA KIHISTORIA: UHOLANZI VS SPAIN, MASHABIKI WASHANGAA"

Post a Comment