WAMACHINGA MFUPA MGUMU DAR ES SALAAM | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WAMACHINGA MFUPA MGUMU DAR ES SALAAM

HABARI NA NIPASHE, IPP MEDIA.
Wafanyabiashara wadodo wadogo maarufu kama 'machinga' jiji la Dar es salaam.
Zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga maeneo yasiyoruhusiwa limebaki kuwa kitendawili kwa Manispaa za jiji la Dar es Salaam.

Pamoja na kwamba Mkuu wa Mkoa, Saidi Meck Sadiki, ameahidi mara kadhaa kuwaondoa wamachinga, ombaomba na watu wote wanaoishi kwenye maeneo siyoruhusiwa; bado ahadi hiyo imeshindwa kutekelezwa.

NIPASHE imeshuhudia wamachinga wakiwa wamepanga bidhaa zao hadi barabarani katika maeneo ya Mwenge, Ubungo, Manzese, Mbezi mwisho, Kimara, Tandika, Tazara, Buguruni Chama, Ilala Boma, Tegeta na kwingineko, bila wasiwasi.

Baadhi ya wananchi wamewatuhumu askari wa jiji kwa kushindwa kuwadhibiti wamachinga na kusema kwamba huenda wanapokea rushwa.

NIPASHE imeshuhudia wamachinga wakiwa wamepanga bidhaa zao hadi kwenye lango la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambako pia ndipo ilipo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alikiri kuzagaa kwa wamachinga katika Manispaa hiyo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.

Msumba alisema mkakati wa kuwaondoa wamachinga na watoto wa mtaani pamoja na baadhi ya wazazi wao, unaendelea na sasa kutakuwa na ushirikishi wa vikundi vya Polisi Jamii, ambao watakuwa wakiwatoza faini ya Sh. 50,000.

Alisema mkakati huo unalenga kuwapeleka wamachinga katika masoko ambayo serikali imetenga kwa ajili ya shughuli hizo.

“Masoko ambayo yametengwa kwa ajili ya Machinga ni Tazara, Kampochea, Tandika na Mbagala Charambe, hivyo askari jamii ambaye atafanikiwa kumkamata machinga basi asilimia 60 ya faini ya kiasi cha Sh. 50,000, ambayo ni sawa na Sh. 35,000 itakuwa yake,” alisema.

Kwa upande wake, Manispaa ya Kinondoni imesema operesheni ya kuwaondoa inahitaji nguvu ya pamoja.
Akizungumza na NIPASHE  jijini Dar es Salaam Msemaji wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera, alisema, zoezi hilo linahitaji nguvu kutoka kwa waandishi wa habari kwa kuelimisha umma na ili wamachinga waweze kuondoka kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.

“Ninyi kama waandishi wa habari mnatakiwa kuelimisha umma kwa ujumla kuhusu tatizo la wamachinga na kutoa ushauri kwa viongozi wafanye nini juu ya hili tatizo kuliko kuuliza kila siku sisi tumechukua hatua gani?” alisema Mhowera.

Hata hivyo alisema, manispaa hiyo haikusanyi ushuru kutoka kwa wafanyabiashara wanaofanyabiashara katika maeneo yasiyo rasmi.

Imeandikwa na Enles Mbegalo, Fransisco Haule na Lucy Thomas (Saut).

0 Response to "WAMACHINGA MFUPA MGUMU DAR ES SALAAM"

Post a Comment