HATUA SITA (6) ZA KUANZISHA BIASHARA YA REJAREJA(DUKA) - SEHEMU YA II | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HATUA SITA (6) ZA KUANZISHA BIASHARA YA REJAREJA(DUKA) - SEHEMU YA II

DUKA LA REJAREJA

HATUA 10 ZA KUANZISHA BIASHARA YA REJAREJA (DUKA)

SEHEMU YA II
Katika makala nyingine kwenye blogu hii iliyosema, Hatua10 za kuanzisha biashara ya duka la rejareja, Sehemu ya kwanza, tulizitaja hatua 6 peke yake, jambo lililosababisha wasomaji wengi kutaka kuzijua hatua nyingine 4 zilizobakia. Leo tutamalizia hatua nyingine 4 zilizobakia kusudi kuwaondolea dukuduku wasomaji na wafuatiliaji wa blogu hii.

7. Kuchagua eneo la biashara (duka)
Watu husema Biashara ya  duka la rejareja ni eneo”  Eneo utakalochagua kuweka duka lako, litaathiri kila kitu utakachofanya katika biashara yako yote. Mafanikio au kuanguka kwa bishara ya duka la rejareja kunategemea  kwa asilimia kubwa sana sehemu ulipoiweka biashara hiyo.

SOMA: Mbinu hizi 2 za uendeshaji duka la rejareja kwa mafanikio hazipo mahali pengine popote pale.

Usikurupuke wakati wa kufanya uamuzi wa eneo utakaloweka biashara yako ya duka, chukua muda  wa kutosha kufanya utafiti na kuwa mvumilivu. Ukigundua eneo halifai, basi ni bora ukaahirisha na kuangalia uwezekano wa eneo jingine kuliko baada ya muda mfupi kuja kuanza kuzozana na mwenye nyumba akurudishie kodi au hata biashara yako kufia njiani.


Usikubali presha za madalali ambao hutumia ujanja kwa kukuambia eti, eneo/fremu fulani inagombewa na watu zaidi ya watatu na wewe ni wa nne, hivyo ukichelewa kidogo tu hutaikuta. Zifuatazo ni baadhi ya dondoo za kuzingatia wakati ukitafuta eneo utakaloweka duka lako la rejareja;

Wateja: 
Hakikisha eneo lina wateja wa kutosha; bidhaa utakazouza zitategemea aina ya wateja walioko pale. Mara nyingi sana maduka ya rejareja huhitaji maeneo yaliyokuwa na wakaazi wanaoishi majumbani, wapita njia kwa mfano eneo la stendi ya basi au sokoni panapokusanyika watu wengi. Kila kundi lina aina zake za bidhaa tofauti na lingine, kwa  mfano duka la mtaani kwenye makazi ya watu utahitajika uweke zaidi vyakula kama nafaka na mahitaji  ya nyumbani, na stendi utaweka zaidi vinywaji baridi na vitafunwa “bites” kushinda vitu vingine.

SOMA: Tumia siri hii kuongeza mauzo x2 ya soda, maji, juisi na sigara.

Chagua eneo ambalo unajua kabisa wateja wako unaolenga watanunua bidhaa unazokusudia kuzipa kipaumbele, mathalani, usije ukachagua eneo la stendi halafu ukajaza mchele na unga, wapita njia na wasafiri siyo rahisi wakanunua vitu hivyo.

Eneo kuwa na idadi kubwa sana ya watu siyo ishara kuwa na wateja nao ni wengi, la hasha, inawezekana pale wanapita njia tu, kwa mfano maeneo ya posta mpya Dar es salaam kuna umati mkubwa sana wa watu, lakini hauwezi ukaenda kukita duka lako la nafaka pale ukamuuzia mtu, vitakudodea….


Uwezekano wa kufikika na kuonekana kwa urahisi;
chagua eneo wateja wanaweza kufika bila matatizo, iwe ni kwa miguu ama usafiri kama wa gari, pikipiki, bajaji n.k. Je, panaonekana kwa urahisi na wateja? Pasiwe ni mahali palipojificha itakusaidia hata kimatangazo, patakuwa panajitangaza penyewe vitu kuonekana na kuwavutia wateja kwa urahisi.

SOMA: Mchanganuo wa biashara ya duka la rejareja.

Taratibu za mipango miji.
Wapo watu wamewahi kulia machozi na hata wengine kufikia hatua ya kuzimia baada ya kutakiwa wavunje mabanda yao waliyokuwa wamejenga maeneo ya mji ambayo serikali imepiga marufuku. Hata ikiwa unapanga sehemu, ulizia kwanza kwa kina kama eneo lile halina marukufu yeyote iliyowekwa na serikali za mitaa au serikali kuu.

Majirani na washindani wako.
Biashara za majirani wako zinazofanana na ya kwako zina uwezo wa kuathiri biashara yako kwa namna moja ama nyingine. Chunguza eneo unalotaka kufungua duka lako. Maduka mengine yanayokuzunguka yakoje?

Ukigundua pana ushindani mkali sana, na uwezo wako kiushindani pengine kimtaji ni mdogo, basi ni bora hata ukaangalia uwezekano wa eneo jingine lenye ushindani kidogo zaidi. Vilevile angalia eneo  lenye biashara ambazo zitategemeana na ya kwako kwa mfano kama pana mama ntilie wengi au migahawa basi duka la rejareja la vyakula ndiyo mahali muafaka.

Masuala binafsi.
Jiangalie binafsi ikiwa wewe ndiye utakayeuza mwenyewe dukani, umbali kutoka unapoishi, masuala ya chakula n.k. Mathalani eneo ulilochagua ni mbali sana na unapoishi  jambo litakalokufanya upoteze muda mwingi njiani pamoja na foleni,  kama ni mjini basi ndiyo balaa kabisa.

SOMA: Biashara ya duka inavyoweza kukutoa kimaisha ukiwa mjanja.

Jaribu kuchagua eneo la karibu na unapoishi, vilevile suala la chakula lina athari kubwa katika matumizi yako ya kila siku. Athari hizo  husababisha faida kuwa kidogo, hakikisha unapata njia nafuu ya kujipatia mlo wako wa mchana uwapo dukani aidha kwa kununua mahali ambapo bei siyo kubwa sana au uletewe kabisa kutoka nyumbani. Kwa hiyo utaona ikiwa eneo ni karibu na unapoishi, itakuwa ni jambo rahisi sana.

Huduma za Kijamii.
Chunguza vitu kama umeme, maji na sehemu ya kujisaidia(choo), uwezekano wa kupita gari la kuzima moto “fire” ikiwa moto utazuka kwa bahati mbaya pamoja na mahali ambapo wateja wanaweza wakapumzika au hata kujificha mvua na jua. Hakikisha pana umeme wa uhakika kwani duka la rejareja friji ni kitu muhimu sana, ulizia ikiwa nyumba ina deni Tanesco kwani wenye nyumba wengine wanapoleta mpangaji siku hiyo hujiunganishia umeme wa wizi kinyemela na baada ya siku mbili tatu unakatika kama kawaida.

SOMA: Aina za bidhaa za duka zilizo na faida ndogo lakini zinaotoka haraka haraka.

Usalama.
Angalia matukio ya uhalifu katika eneo husika  ukubwa wake ukoje.
Yapo maeneo mengine huwezi ukaweka duka na kisha jioni ukalale nyumbani, ni lazima wezi usiku na wasipovunja mlango basi watachimba ukuta kwa nyuma na kuzama ndani  kisha kukomba kila kitu. Vilevile usalama wako binafsi wakati wa kurudi nyumbani usiku, je, hamna wimbi kubwa la vibaka kama “watoto wa mbwa mwitu” n.k.?.

8. Nunua bidhaa kwa jumla.
Ili duka la rejareja liweze kufanikiwa ni lazima bidhaa zinunuliwe kutoka maduka ya jumla kwa bei ya chini na kisha ziuzwe kwa bei ya juu kidogo kusudi kupata faida. Ni lazima uyafahamu maduka yanayouza bidhaa utakazouza yanayouza kwa bei nzuri, linganisha bei za maduka tofauti kubaini ni lipi lenye bei nafuu zaidi ukizingatia pia ubora wa bidhaa zenyewe isije kuwa rahisi kumbe ni bidhaa feki za “mchina”.

9. Weka sera na taratibu za duka lako.
Hata kabla hujafungua duka lako ukiwa bado upo kwenye hatua ya mipango, huu ndio wakati mzuri wa kuweka taratibu na sera zitakazoongoza duka lako. Kwa kuanisha matatizo kabla hayajajitokeza kutakusaidia kuja kukabiliana nayo kwa urahisi zaidi kuliko yanapokuja kukushitukiza. Amua kabla, jinsi utakavyotatua matatizo mbalimbali yatakayohusiana na wateja, mfanyakazi/wafanyakazi ikiwa kama utawaweka na wadau wengine wowote wale  ili kuzuia makosa pindi yatakapokuja kujitokeza. Baadhi ya mifano ya sera/taratibu unazoweza kupanga ni kama vile:-

·       Kiasi cha faida kwenye bidhaa.
·       Suala la nyongeza kwa wateja.
·       Ni muda gani utakaoruhusu mteja kukaa na deni
·       Mteja akishanunua bidhaa ana ruhusiwa kuirudisha au la, na ni katika mazingira yapi ataruhusiwa kurudisha?
·       Utakubali mteja kuweka fedha kidogo kidogo kabla hajachukua bidhaa?
·       Muda wa kufungua na kufunga duka na siku za sikukuu.

Unaweza ukasema “nitalitangaza vipi duka?” ukiwa na maana kwamba ukishafungua ni basi, wateja watajileta wenyewe tu. Ni kweli kuwa duka la kawaida hauhitaji kwenda kwenye TV, Redio au magazetini kulitanganza, lakini  unaweza ukalitangaza duka lako hata kwa majirani watakaokuzunguka tu na ukashangaa kuona tofauti kubwa.

Baadhi ya njia unazoweza kutumia kulitangaza duka lako la rejareja ni kama hizi zifuatazo;

·       Weka mpangilio mzuri na unaovutia wa bidhaa zako pamoja na kutengeneza mandhari nzuri itakayowavutia wateja.
·       Weka bango juu ya paa la duka lenye maandishi ya jina la duka au weka kibao mbele ya duka kinachoonyesha pana duka.
·       Unaweza pia kugawa vipeperushi kwa watu walio karibu na duka kuwajulisha aina za bidhaa unazouza, bei pamoja na punguzo kama lipo.
·       Kuwa na mkakati wa kutoa huduma nzuri kwa wateja kusudi wakija waende kuwaambia na wenzao.

....................................................................................................

Je, unataka kuanzisha biashara ya rejareja au tayari unayo na ungependa kuifanyia mapinduzi makubwa ndani ya muda mfupi iwezekanavyo?

Kama jibu ni ndiyo, basi kitabu hiki hapa chini kitakuwa msaada mkubwa katika safari yako hiyo ya kuibadilisha biashara yako au kuianzisha...
kitabu cha duka la rejareja

jinsi ya kuanzisha biashara ya duka

Ukikihitaji wasiliana nasi kwa namba 0712202244  au 0765553030, tuna softcopy kwa njia ya email shilingi elfu 5 na pia vitabu ya karatasi kwa bei ya shilingi elfu 12 na unaletewa mpaka pale ulipo kwa wale wakazi wa Dar.


6 Responses to "HATUA SITA (6) ZA KUANZISHA BIASHARA YA REJAREJA(DUKA) - SEHEMU YA II"