JINSI YA KUPIKA SUPU NZURI NA TAMU YA BIASHARA (SUPU NA CHAPATI SEHEMU-2) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUPIKA SUPU NZURI NA TAMU YA BIASHARA (SUPU NA CHAPATI SEHEMU-2)

Kupika supu

BIASHARA YA SUPU NA CHAPATI SEHEMU YA 2: SUPU

Katika somo hili tutakwenda kujifunza vitu vifuatavyo;

ü Aina kuu 4 za supu

ü Jinsi ya kupika supu nzuri kwa ajili ya biashara

ü Jinsi ya kupika supu ya kongoro

ü Changamoto za biashara ya supu

ü Siri 5 ili supu ikulipe vizuri

AINA KUU 4 ZA SUPU

Kuna aina nyingi za supu kulingana pia na aina ya nyama zinazotumika kupika supu hizo. Ifuatayo ni orodha ya nyama zinazotumika zaidi kwa supu;

1. Nyama ya Ng’ombe

·      Nyama yenyewe

·      Utumbo

·      Kichwa

·      Makongoro(miguu)

·      Ulimi

·      Mkia

2. Nyama ya Mbuzi

·      Nyama yenyewe

·      Utumbo

·      Vichwa

·      Makongoro(miguu)

3. Nyama ya Kuku

4. Samaki na viumbe wengine wa baharini kama vile Pweza nk.

Watu wanapenda sana supu na supu iliyozoeleka zaidi katika maeneo mengi ni ile ya ng’ombe na mbuzi. Supu hunywewa kama kifungua kinywa muda wa asubuhi lakini pia wapo wanaokunywa supu hata  nyakati za jioni mfano katika vituo mbalimbali vya mabasi(stendi) utakutana na watu wakifurahia kunywa supu na vitafunwa kama chapati, ndizi na maandazi asubuhi hata na jioni.

Bishara ya supu pamoja na kwamba ina uwezo wa kumpatia mtu faida nzuri lakini ina changamoto ambazo mtu asipokuwa makini  nazo anaweza akaona haimlipi kabisa. Tutaziona changamoto hizo baada ya kuona kwanza jinsi ya kupika supu

JINSI YA KUPIKA SUPU NZURI NA TAMU KWA AJILI YA BIASHARA

Mahitaji:

·      Nyama kiasi unachohitaji

·      Maji

·      Chumvi

·      Kitunguu swaumu kilichosagwa

·      Tangawizi iliyosagwa

·      Pilipili manga

·      Kitunguu maji kilichosagwa

·      Unaweza pia kuweka ladha ya supu inayouzwa madukani

·      Viungo vingine ukipenda

Maandalizi:

1.   Osha nyama yako vizuri na kama ni utumbo basi hakikisha unachukua muda wa kutosha kuuosha kwani utumbo huwa na kawaida ya kuwa na mchanga.

 

2.   Katakata vipande nyama yako na uitie kwenye sufuria

 

3.   Tia chumvi kiasi kulingana na wingi wa nyama yako

 

4.   Ongeza viungo vyako vingine kama nilivyotaja pale juu

 

5.   Bandika jikoni sufuria lako bila ya kuweka kwanza maji hadi pale nyama itakapobadilika rangi na maji yake ya asili kuonyesha yanaanza kukauka

 

6.   Ongeza maji kiasi unachoona kitatosha nyama iive na kubaki kama supu kuepuka kuja kuongeza maji supu ikiwa imeshaiva tayari kwani itapoteza ladha

 

7.   Punguza moto uwe wa kiasi wakati supu ikikaribia kuiva kusudi supu ijichuje vizuri na kuifanya iwe na ladha ya kupendeza.

NB: Unaweza wakati wa kuweka viungo ukaongeza mbogamboga na vitu kama njegere, karoti na viazi ulaya kulingana na mapenzi ya wateja wako kwani wengine huwa hawapendi supu iliyotiwa viungo sana.

Vilevile viungo kama pilipili na ndimu au limao wateja wana uhuru wa kuchagua wenyewe kama waweke ama la, hivyo viungo hivi viwekwe pembeni kwenye sahani ya supu.

JINSI YA KUPIKA SUPU YA KONGORO

Tofauti na supu ya nyama au ile ya utumbo,supu ya makongoro(miguu ya ng’ombe) ina wateja wake maalumu na ukiweza kuizoesha eneo fulani unaweza kupata wateja wengi wa kudumu kila siku na hasahasa huwa ni wanaume kwani inaaminika kwamba supu hii huongeza nguvu za mwili.

Upishi wake hauna tofauti sana na ule wa supu ya nyama au utumbo isipokuwa tu  hii huchukua muda mrefu zaidi jikoni na maandalizi yake kama ilivyokuwa utumbo unatakiwa uyaoshe vizuri na kurudia kuyaparua kwa kutumia kisu au kiwembe ili kuondoa manyoya yote yaliyobaki kwani wauzaji mara nyingi hawayasafishi vizuri

 

CHANGAMOTO ZA BIASHARA YA SUPU

1. Supu kuwa kidogo kuliko nyama yenyewe

Kama hujawa makini utajikuta kila siku ukimaliza supu/mchuzi wote huku nyama ikiwa bado haijaisha, hii ina maana kwamba unakuwa umezidisha kipimo chako cha supu, umewatilia wateja supu nyingi zaidi kuliko ilivyotakiwa. Wauzaji supu wengi hukimbilia kuongeza maji kwenye sufuria la supu jambo linalosababisha supu hii ya awamu ya pili kuwa nyepesi na isiyokuwa na ladha nzuri kama ile ya awali na mteja anayekutana nayo si ajabu kesho asije tena na atamwambia na mwingine kuwa kwako supu siyo nzuri.

Suluhisho la changamoto hii ni mtu kujitahidi kujenga uzoefu wa kujua kiasi fulani cha nyama  kinatakiwa kitoe supu ujazo gani na hivyo tokea mwanzoni unapoongeza maji kwa ajili ya supu ufahamu kabisa ni maji kiasi gani utatakiwa kuongeza ili mpaka supu inapoiva basi kiasi kinachohitajika tu ndicho kibakie kwenye sufuria lako.

Na pia kiasi hicho cha supu uhakikishe kitatoa idadi ya bakuli ulizokadiria kwamba zitarudisha ghara zako zote na faida juu. Wakati wa kuwapimia wateja supu ni lazima uhakikishe unazingatia sana kipimo kile ulichopanga, usizidishe wala kupunguza na kataa kwa hekima pale wateja wanapokushawishi uwaongezee supu watakavyo pasipo kuongeza pesa.

Wateja wengi wamejijengea imani kwamba supu au mchuzi hauna gharama na kwamba muuzaji anaweza tu kuongeza maji atakavyo kupata supu nyingi, kumbe hawajui kufanya hivyo ndiyo kuwapatia tiketi ya kukuhama kwani supu yako itakuwa na maji mengi tena isiyo na ladha ya kuvutia kabisa. Wafahamishe kwa hekima wanunue bakuli nyingine ya supu kwani nyongeza-nyongeza itakusababishia hasara na mwishowe ushindwe kuwapatia huduma waipendayo.

2. Kutokuendana na muda wateja wanaotaka supu

Supu ya asubuhi inatakiwa iwe tayari mapema kwa kadiri inavyowezekana ili kuwavutia wateja wa aina mbalimbali. Kwa mfano wapo wateja ambao hupenda kuwahi kazini mapema sana na utakuta wanapenda wapate supu hata saa 12 asubuhi, kuna wengine watataka wanywe supu saa 1, saa 2 nk. Kwa hiyo ni juu yako kuhakikisha wote unawaridhisha kwa kuwahi mapema kuivisha supu yako.

Ili supu iweze kuiva mapema ni lazima pia maandalizi yake yafanyike mapema hata ikiwezekana siku moja kabla na usiku wa kuamkia siku yenyewe. Maandalizi siku moja kabla ni pamoja na jiko-kununua mkaa au gesi, ununuzi wa mahitaji mengine yote vikiwamo viungo pamoja na usafi wa vyombo na mazingira.

Nyama kwa ajili ya supu inafaa zaidi inunuliwe usiku ama alfajiri ikiwa freshi na watu wengi hununua moja kwa moja kutoka machinjioni ambapo kwenye miji mingi kama Dar es salaam uchinjaji wa ng’ombe na mbuzi huanza saa 4 usiku mpaka saa 11 alfajiri, ni juu yako kuamua utanunua saa ngapi ili supu yako isichelewe.

Ikiwa unatumia nyama iliyolala kwenye friji basi utainunua buchani siku moja kabla ili uanze kuichemsha kuanzia saa 10 au saa 11 alfajiri. Hata hivyo nyama nzuri itakayotoa supu yenye ladha ya kupendeza zaidi ni ile ya siku hiyohiyo ambayo haijalala.

Vitafunwa navyo viandaliwe mapema ikiwezekana kuwe na mtu maalumu kabisa kwa ajili ya kazi hiyo na siyo yuleyule anayeandaa supu ukute ndiye huyohuyo anayeandaa na vitafunwa. Kufanya majukumu yote mawili mtu mmoja mara nyingi husababisha ucheleweshaji usiokuwa wa lazima na hii siyo sifa njema kwa wateja wako.

3. Supu kutokwisha kwa wakati

Unategemea supu iliyopikwa kumalizika kwa siku moja lakini kutokana na sababu mbalimbali unaweza kukuta haiishi na hata  wakati mwingine inabaki mpaka siku inayofuata jambo ambalo si zuri kwani supu ni chakula kinachoharibika upesi na ikilala ni rahisi wateja kutambua hata kama utaihifadhi vizuri namna gani.

Sababu kubwa kwanini supu hubaki ni wateja kuwa wachache mno au kukisia kwa makosa kiasi cha supu unayopika kulingana na idadi ya wateja uliokuwa nao. Ili kuhakikisha kila siku supu yako inaisha, jitahidi kupika kiasi cha supu inayolingana na idadi ya wateja uliokuwa nao tu huku ukiendelea kuvutia wateja wapya mpaka pale watakapoongezeka basi ndipo na wewe uongeze kiasi cha supu unayopika.Hili litawezekana kwa kudumisha huduma kila siku bila ya kukosa wateja wakuzoee.

Kuna njia mbili kubwa unazoweza kutumia kuhifadhi supu iliyobaki isiharibike, ya kwanza ni kuitia katika friji na ya pili kuipasha moto vya kutosha kila baada ya masaa 6 kuisha.

4. Kuchagua  saizi mbaya ya bakuli za supu

Bakuli za kunywea supu wateja zinapaswa kulingana na kipimo ulichoamua kutumia. Ikiwa umeamua kuuza supu ya shilingi 1,500 basi bakuli zisijekuwa ni za supu ya sh. 2,000/= nikimaanisha zisiwe oversize kwani wateja wana tabia ya kuhisi wanapunjwa bakuli isipojaa vizuri mpaka juu, hivyo basi nunua bakuli ambazo ukipima kipimo chako inajaa hadi juu kuepusha ushawishi wa kuongeza kiasi cha supu. Halikadhalika pia zisije kuwa ndogo mno ukawapunja wateja watakimbilia kule wanakouziwa kwa haki. Pima supu inayokulipa na siyo itakayokusababishia hasara.

 

5. Ukataji wa vipande vya nyama

Idadi ya vipande vya nyama ni kitu cha muhimu sana, ni lazima idadi iendane na idadi ya bakuli za supu unazohitaji ili kurudisha gharama zote na faida juu. Kuna wengine hukatakata kabisa idadi ya vipande kabla ya kuanza kuchemsha supu na wengine huamua kuchemsha kwanza nyama mapande makubwa makubwa na kisha kuja kukatakata vipande vidogo wakati wa kumhudumia mteja supu.

Mimi huwa napendelea zaidi aina ya kwanza ya ukataji kwani huepusha kuchafua mazingira ya sehemu unayouzia supu kila mara kuchafua kibao cha kukatia nyama hukaribisha inzi. Kama hesabu zako zinasema kila mteja atapata vipande 3 basi usizidishe wala kupunguza labda tu mteja mwenyewe alipie vipande vya ziada.

6. Wateja wanaopenda wauziwe mchuzi (supu tupu) isiyokuwa na nyama.

Wauzaji wengi hii huifanya kwa kuwauzia wateja supu tupu kwa nusu bei au hata chini ya hapo lakini hii mara nyingi inavuruga mahesabu ya supu na hazitatoka idadi ya bakuli ulizopanga zitoke matokeo yake supu inaleta hasara. Unaweza kufanya hivyo ukijua tu kwamba kuna kiasi cha supu ya ziada itakayobaki baada ya idadi ya bakuli ulizopanga kuisha.

7. Nyama kuiva kupita kiasi

Wakati ukisubiri wateja waje unaweza ili wasikute supu ikiwa imepoa, unaamua kuacha sufuria la supu kwenye moto jikoni ikiendelea kuchemka muda mrefu. Hali kama hii husababisha nyama kuiva sana na kuwa teketeke huku supu ikikakamia na kupungua ujazo wa awali uliopima kwamba utatoa idadi ya bakuli zitakazokupa faida. Suluhisho la tatizo hili ni kuwa na vifaa bora hasa jiko la gesi ama jiko unaloweza kulitumia kupasha supu yako haraka mteja anapokuja.

Supu inapokuwa tayari imeiva, ipua sufuria na uiweke pembeni ukisubiri wateja. Mteja akija na kukuta imepoa basi washa jiko haraka na upashe kiasi kile unachompimia tu kwa kutumia sufuria nyingine ndogo. Funika sufuria kubwa la supu vizuri kwa mfuniko usioruhusu wadudu kama nzi wala vumbi kuingia ndani yake .

SIRI 5 ILI SUPU IKULIPE VIZURI.....................


·      Je, ungependa kuzijua siri hizo 5 ni zipi?

·      Na je, ungependa pia kushiriki katika kuandika mchanganuo wa biashara hii ya mgahawa mdogo wa supu na chapati hatua kwa hatua katika group letu la masomo ya kila siku la Michanganuo-online?

Basi jiunge na group hilo leo uweze kujifunza na masomo mengine yaliyopita zaidi ya 100 tuliyoyaweka katika channel yetu ya Telegram

Ndani ya group pia unapata mfululizo mzima wa somo hili la chapati laini na supu, siri za kupika chapati laini na tamu.

Ada ya mwaka mzima ni Tsh. 10,000/=

Unatumiwa pia na zawadi ya vitabu na michanganuo ya biashara mbalimbali

Namba za malipo ni 0712202244 au 0765553030 Peter Augustino Tarimo, kisha tuma neno,"Niunge na Mastermind group 2023"

Michanganuo inaanza leo tarehe 16/12/2022 usiku saa 3-4


Kumbuka masomo na michanganuo ndani ya group ni kila siku, na unaweza kuamua kufuatilia baadhi ya masomo na michanganuo ile unayotaka tu, somo kama hulihitaji hulazimishwi kujifunza.

Masomo na michanganuo itabakia kwenye channel ya group kwa muda kabla ya kuondolewa ili kutoa nafasi kwa wanachama wapya kuyapata kiurahisi.


0 Response to "JINSI YA KUPIKA SUPU NZURI NA TAMU YA BIASHARA (SUPU NA CHAPATI SEHEMU-2)"

Post a Comment