SIRI YA MAFANIKIO UFUNDI WA KUTENGENEZA FRIJI MAJOKOFU NA AC (VIYOYOZI) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIRI YA MAFANIKIO UFUNDI WA KUTENGENEZA FRIJI MAJOKOFU NA AC (VIYOYOZI)

Nafasi mpya za kazi nchini Tanzania zinavyozidi kuwa chache watu nao ndivyo wanavyobuni njia tofauti za jinsi ya kupata pesa bila ya kuvunja sheria za nchi. Ufundi wa mitambo mbalimbali ikiwemo na ufundi wa mafriji(jokofu) na ac(kiyoyozi) ni fani inayolipa kutokana na huduma hiyo kuwa na mahitaji makubwa sana hususani sehemu za miji yenye joto kali kama Dar es salaam. Dar hakuna mtu asiyetumia friji.


Karibu kila nyumba yenye umeme hukosi friji, feni na hata friza kubwakubwa, magari mengi nayo makubwa kwa madogo hufungwa ac system(air conditioner) au kwa jina jingine viyoyozi. Vinywaji moto na vinywaji baridi ni maneno ya kawaida yaliyotawala maeneo mengi hasa nyakati za joto na jua kali miezi ya kiangazi.


Kwenye maduka na migahawa utasikia wateja wakisema, “Nipe soda ya baridi sana iliyo karibu kuganda”, wateja wengine wakifika dukani na kukuta vinywaji vyako kama maji, juisi au soda havina ubaridi sahihi wa kutosha nao utasikia wakisema, “Nipe ela yangu niende pale kwa mangi vitu vyake ni baridi sana” nk.  

Katika ulimwengu huu wa ajira na kazi siku hizi, watu na hasa kundi la vijana wanaomaliza masomo katika shule na vyuo mbalimbali huamua kujiunga na vyuo vya ufundi kama Veta au vile vya watu binafsi ili kupata ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kupata ajira au kazi na hivyo kuwa na njia nzuri ya kupata pesa. Kazi Tanzania siku hizi kama huna ujuzi wowote itakuwia vigumu mno kuipata.

Jinsi ya kupata pesa kupitia ufundi wa kutengeneza vifaa vya kupoozea hewa (Home air conditioning & room air conditioning)

Ujasiriamali haupo tu kwenye biashara za kawaida za kuuza bidhaa na huduma, au kutengeneza bidhaa. Ufundi pia wa kutengeneza vifaa vilivyoharibika(repairing) unahitaji mtu kuwa mbunifu na mtundu, vitu ambavyo ndiyo viungo vikuu katika suala zima la ujasiriamali.

Katika makala hii ambayo ipo katika kipengele kilichoanzishwa rasmi kwa ajili ya stori za watu waliofanikiwa katika biashara mbalimbali nimeamua kumzungumzia kijana mmoja niliyemshuhudia mwenyewe binafsi akipata mafanikio makubwa kupitia kazi ya ufundi wa kurepea vifaa mbalimbali vya kupooza kama vile friji, freezer, majokofu, viyoyozi(ac) pamoja na mafeni ya ukutani na yale ya mezani.

Si lengo langu kuelezea kwa undani sana utaalamu wenyewe wa kiufundi wa kutengeneza hivyo vifaa, lakini mimi nia yangu ni kuelezea ule ubunifu niliouona kwa huyu kijana ambao ulimuwezesha kuinuka haraka kimaisha hata watu wakabaki wakishangaa. Kijana huyo kama walivyokuwa vijana wengine baada tu ya kumaliza kozi yake ya ufundi kutoka chuo cha veta, mwanzoni aliidharau kazi ya ufundi akaenda kufungua biashara nyingine ambayo alikuwa hana uzoefu nayo wa kutosha wala hakuwa ameifanyia utafiti wa kina.


Baada ya miezi michache alishuhudia biashara ile ikimfia mikononi huku asijue cha kufanya ni nini. Ndipo alipogutuka na kukumbuka kumbe anayo fani aliyosomea ya ufundi mafriji na vifaa vingine vya umeme. Huku akiwa hata hela ya kula inampiga chenga, alinunua vifaa vya ufundi, tool box kwa fedha kidogo alizouza baadhi ya mali za ile biashara iliyokufa. Pasipokuwa hata na eneo maalumu la kufanyia kazi ya ufundi(workshop) alianza kutembea maeneo mbalimbali ya ilala na temeke akiulizia watu waliokuwa na vifaa vyao vilivyoharibika.

Alikuwa akipata mteja, huenda mpaka alipokuwa anaishi na kubeba vifaa vyake vyote vya ufundi kama mtungi wa gesi, filter, waya za kopa, capacitor, condactor, condenser, meta ya kupimia na fyuzi mbalimbali. Mwanzoni hakuwa na msaidizi kabisa na aliweza kumudu kubeba kila kitu mwenyewe alipokuwa akienda kwa mteja kwa kuhakikisha mtungi wa gesi uliokuwa kitu kizito kuliko vifaa vingine anatumia aina ya mitungi midogomidogo inayobebeka kwa urahisi.

Mbinu nyingine kijana huyu aliyoitumia na iliyompatia umaarufu mkubwa eneo lile alilokuwa akifanyia shughuli zake ni uaminifu, alikuwa hana longolongo kama za mafundi wengi wengine, ukimpa friji yako, anaipima akishatambua tatizo ni nini, hukueleza bila kuficha chochote, hata kama kifaa kilichoharibika ni kidogo yeye hatakudanganya ni kompresa imekufa ili ajinufaishe kwa fedha nyingi, atakutajia tu kilekile kilichoharibika hata kama kinauzwa elfu mbili. Atakuchaji hela yake ya ufundi kama elfu tano au kumi tu basi.

Ndani ya kipindi kifupi sana aliweza kununua pikipiki kwa ajili ya kubebea vifaa vyake na ili aweze kufanya kazi maeneo mengi zaidi na yaliyokuwa mbali na lile eneo alilozoeleka. Kidogo akafungua ofisi yake mwenyewe ambapo sasa baadhi ya kazi alikuwa akizifanyia pale pale kwenye workshop aliyofungua. Watu walimuamini sana kijana yule hata ikawa ukimsikia mtu yeyote akilalamika friji yake au ac imeharibika basi huchelewi kumwambia aende kwake.


Ile pikipiki na ofisi(workshop) vilikuwa nyenzo kubwa sana kwake na “vilimboost”  haraka kiasi ambacho aliweza sasa kupata wateja wengi alioshindwa kuwahudumia kikamilifu akiwa peke yake. Ndipo sasa akaona umuhimu wa kumtafuta msaidizi. Alifunga safari mpaka kijijini kwao alipokwenda kumchukua mdogo wake wa kuzaliwa tumbo moja aliyekuwa amemaliza shule karibuni akaja naye kwa lendo la kuja kumfundisha shughuli za ufundi pamoja na kuwa kama msaidizi wake.

Walipiga kazi na mdogo wake mambo yakazidi kunyooka siku hadi siku mpaka akaanza sasa kuuza spea vya kutengeneza vifaa vya kupoozea kwenye kile chumba alichokodi kwa ajili ya kufanyia kazi za ufundi. Alichokifanya ni kugawanyisha chumba mara mbili kwani kilikuwa kikubwa kidogo. Sehemu moja ikawa duka la vifaa na nyingine ikabakia kuwa kama workshop kisha nje barazani walipanga mafriji yaliyosubiri kutengenezwa na yale waliyokuwa wakiyauza.

Muda si muda mdogo mtu naye aliielewa vizuri kazi ya ufundi ikawa sasa kaka mtu anashinda dukani na kwenye workshop huku mdogo wake akizunguka kwa pikipiki mitaani akitengeneza mafriji na vifaa vya wateja. Naye alikuwa ‘mkali’ utafikiri ni kaka yake, ni vitu vichache sana vilivyomshinda na hata ilikuwa ameshindwa kitu mara moja humpigia kaka yake simu na kuja ‘kusolve’.

Ninavyoandika hapa kwa sasa kijana yule anamiliki gari tatu ikiwemo moja ya kwake ya kutembelea, pikipiki kamwachia mdogo wake. Amejenga na kufungua tawi eneo jingine tofauti na lile la mwanzoni. Lakini kitu kingine nilichogundua kilichangia mafanikio yake ya haraka ni mkopo, katika shughuli zake hizi aliwahi kukopa benki moja na fedha hizo ziliweza kumpa msaada mkubwa sana kwenye safari yake hiyo ya mafanikio kupitia shughuli za ufundi mitambo hususani ufundi wa vifaa vya kupoozea na umeme.

.................................................................................................

Ndugu msomaji, kama unahitaji kupata maarifa sahii kuhusiana na kuanzisha na kuendesha biashara pamoja na Ujasiriamali kwa kina, pata moja kati ya vitabu hivi kwenye ukurasa huu wa SMART BOOKS TANZANIA, unaamua mwenyewe ununue softcopy au hardcopy.

ASANTE SANA,
Peter A. Tarimo
SELF HELP BOOKS




0 Response to "SIRI YA MAFANIKIO UFUNDI WA KUTENGENEZA FRIJI MAJOKOFU NA AC (VIYOYOZI)"

Post a Comment