SHINDANO LA MCHANGANUO WA BIASHARA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA NA UWEKEZAJI, WAJASIRIAMALI WALIVYOHAMASIKA. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SHINDANO LA MCHANGANUO WA BIASHARA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA NA UWEKEZAJI, WAJASIRIAMALI WALIVYOHAMASIKA.

Tarehe 28 Agosti mpaka 30, lilifanyika kongamano la Wiki ya Huduma za Kifedha na Uwekezaji linalofanyika kila mwaka katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam ambalo lengo lake kuu kwa mujibu wa Meneja mauzo  wa kampuni ya Nuebrand EC inayoandaa kongamano hilo, Cathreen Bukuku  ni kuongeza uelewa wa masuala yahusuyo fedha, kwani watanzania wengi  wamekuwa hawatumii njia salama na zilizokuwa rasmi katika shughuli zao za kila siku za ujasiriamali.

Cathreen Bukuku  kushoto, meneja mauzo Nuebrand 
Katika kongamano hilo lililoaza siku ya Ijumaa, wajasiriamali wengi walifika wakiwa na hamasa kubwa ya kutaka kusikiliza na kujifunza yale waliyokuwa wameahidiwa katika kongamano hilo. Washiriki walikuwa wengi hasa wanawake idadi yao ilionekana kuzidi ile ya wanaume, wengine hata walifika wakiwa na watoto wao wadogo migongoni ilimradi tu wasikose yale yaliyokuwa yametangazwa kutolewa katika kongamano hili.
Jubilee Life Insurance, washiriki.
Kongamano hili limedhaminiwa na kampuni ya NUEBRAND ikishirikiana na Shirika la PESCODE na limeshirikisha Wajasiriamali, wasiokuwa wajasiriamali, Taasisi mbalimbali za fedha kama mabenki pamoja na mashirika/kampuni za Bima.

Amana Bank, moja ya washiriki.
Nilipata bahati ya kuzungumza na mtu mmoja mwanaume  wa makamo ambaye nilikutana naye getini wakati wa kujiandikisha ili tupewe kibali pamoja na fomu maalumu ya kuingilia katika kongamano hilo, akanifanya nicheke na kufurahi sana. Kaka yule wakati akiomba ile fomu ambayo pamoja na vitu vingine ilikuwa pia na ratiba ya masomo  ambayo yangetolewa ndani ya mabanda mbalimbali, alikuwa akitoa msisitizo mkubwa kwa wale wahudumu akitaka kuelekezwa banda ambalo lilikuwa na somo la kutengeneza Wine ya Rosella.

Wahudumu walimuelekeza  kuwa kwa siku ile somo hilo lilikuwa likitolewa katika banda la Tembo, kwani  mabanda yalikuwa yamepangiwa kila moja na masomo yake lakini katika siku zote tatu kila banda linakuwa limepata masomo yote yaliyokusudiwa. Kwa mfano ikiwa banda la Tembo siku ya kwanza limeanza na somo la kutengeneza wine ya rosella basi siku inayofuata muda ule ule litafundishwa somo jingine ambalo lilikwishafundishwa katika mabanda mengine siku iliyopita na Wine ya rosella watakwenda kufundishwa banda jingine madhalani Simba au Swala.

Wajasiriamali wakiingia na kutoka katika mabanda mbalimbali. 
Katika mabanda mengine kwa wakati huo walikuwa na masomo mbalimbali ya utengenezaji bidhaa mfano, chai ya rosella, juisi ya rosella, ukaushaji wa mbogamboga na matunda nk.

Mimi binafsi kilichonipeleka pale siku hiyo ilikuwa ni namna ya kutengeneza Mchanganuo wa Biashara pamoja na Shindano la kuandika mchanganuo wa biashara lakini pia nilivutiwa sana na utengenezaji wa wine ya rosella kwa hiyo nikaamua niende banda lilelile aliloamua kwenda yule kaka kwani masomo yote hayo yalikuwepo siku hiyo. 

Baada tumeshapewa tikiti zetu, fomu, kalamu, maji ya kunywa, kijibandiko mkononi kuashiria umesajiliwa pamoja na vipeperushi kadhaa, mimi na rafiki yangu Yule tulianza safari ya kuelekea kwenye banda letu la Tembo tulilochagua, huku tukiendelea kuzungumza hili na lile.

Aliniambia hivi; “Unasikia bwana, mimi nina muda mchache sana na sijui kama kesho naweza tena kuhudhuria hapa, kilichonileta hapa mimi si kingine bali ni hicho ‘KILAJI’ tu” Akimaanisha kutengeneza wine. Nilicheka na kumuambia si utani hata mimi ijapokuwa pia nilivutiwa na mchanganuo wa biashara lakini pia hiyo wine nilikuwa na hamu kubwa sana ya kufahamu namna ya kuitengeneza. Sote tulicheka mara tukajikuta tumefika banda la Simba.

Tulikaa na kuanza kumsikiliza Mkufunzi kutoka kampuni moja ya Bima ambaye alikuwa amekwisha anza tayari kuelezea, hivyo sikupata fursa ya kufahamu jina lake, na hata baada ya kumaliza sikukumbuka tena kuulizia jina lake na kampuni aliyokuw a ameiwakilisha. Alikuwa akielezea namna  Bima mbalimbali zinavyofanya kazihasa Bima ya vitu, bima ya magari, na bima ya nyumba ambayo alisema hii hujumuisha pia na vitu vilivyomo ndani kwa mfano, samani, Tv, Compyuta, simu za mkononi nk.

Mtaalmu huyo alizitaja hatari mbalimbali ambazo  biashara, mtu au hata wateja wanazoweza kukumbana nazo kuwa ni pamoja na moto, wizi, majanga mbalimbali ya asili nk. Lakini pia alibainisha kwamba zipo hatari nyinginezo kwa mfano katika biashara ambazo huwezi ukazikatia bima madhalani, hatari inayotokana na ushindani katika biashara, kuondokewa na mfanyakazi/wafanyakazi na kutokuwa na ujuzi wa kutosha katika biashara husika nk.

Aliongeza kuwa, hatari  mbalimbali katika biashara au maisha kwa ujumla unaweza ukakabiliana nazo kwa kutumia moja kati ya njia kuu nne zifuatazo;
1.  Kwa kuondokana nazo kabisa, hii ni kwa kuamua kuachana kabisa na biashara husika.
2.  Kukubali, hii ni kwa kukubaliana na matokeo njia ambayo ni hatari sana hasa kwako mwenyewe kani hapa ndipo hukuta mtu anaamua kujiua au kupata msongo mkubwa wa mawazo ambao hatimaye hupelekea kumuua.
3.  Kupunguza hatari, kwa njia malimbali kama kuweka walinzi, fire extinguisher, nk.
4.  Na njia ya nne ambayo ndiyo muafaka zaidi ni Kuhamisha Hatari/Transfer risk au kwa maana nyingine kukata bima (INSURANCE)  Unaipa kampuni ya bima kazi ya kukulindia mali zako ikiwa hatari itatokea basi usije ukapatwa na msongo wa mawazo.
Mtaalamu huyo alisisitiza kwamba Bima ni kitu muhimu sana  maishani kwa mtu mwenyewe kama bima za maisha na afya pia katika vitu na mali kama kwenye biashara zetu, nyumba na magari. Watu huja kugundua umuhimu wa bima wakati wameshachelewa, yaani wakati wamekwishapata hasara baada ya majanga kutokea.”Angalia usijekumbuka shuka kungali kumekucha”

Baada ya somo la Bima kumalizika, tulipumzika saa moja na baadae tulirudi kuendelea na somo jingine jipya ambalo sasa lilikuwa ni “JINSI YA KUANDAA MCHANGANUO WA BIASHARA”. Mwalimu/mkufunzi katika somo hili alikuwa Bwana Luther Monko Majoji kutoka taasisi ya VICOBA ya  PESCODE. Bwana Luther alianza kwa kuelezea maana ya Mchanganuo wa Biashara kuwa ni, Maelezo ya kina yanayoelezea hali halisi ya biashara  kule inakotoka, ilipo na kule inapopaswa kuwepo wakati ujao.



Alifuatia na kuelezea  umuhimu wa kuandika Andiko la Biashara au kwa lugha nyingine Mchanganuo/mpango wa Biashara kabla au wakati umeshaanza biashara. Alisema kwamba umuhimu wa kuandika mpango wa biashara, ni  kumuwezesha mjasiriamali kuwa na dira sahihi ya biashara yake, kubaini kabla matatizo na vikwazo mbalimbali vinavyoweza kuja kutokea hapo baadaye na hivyo kuchukua hatua mapema au kuamua kuachana na biashara hiyo kabisa endapo vikwazo hivyo ni vikubwa mno kuvimudu. Umuhimu mwingine ni kufahamu hali ya soko ikiwa kweli lipo na litalipa, sekta husika pamoja na vipengele vingine muhimu kama fedha, usimamizi na ratiba ya uzalishaji.

Umuhimu mwingine ni katika kuwavutia wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali kama vile mabenki na taasisi za mikopo wakati utakapohitaji kukopa au kuongeza mtaji wa biasara yako ili iwezekukua zaidi. Wadau hao watahitaji uwashawishi ni namna gani umejipanga kwa kuwaonyesha mchanganuo wako na siyo kwa maneno matupu.

Vile vile mchanganuo wako wa biashara utakusaidia ikiwa utakopa fedha benki au kutoka taasisi yeyote ile, uweze kuzielekeza katika zile shughuli za kibiashara ulizokusudia kuzifanya pekee na wala siyo kwingineko kokote kule ukizingatia ya kwamba hela ya mkopo siyo yakwako ni ya watu, na faida unayoipata unatakiwa kwanza uhakikishe unarejesha mkopo pamoja na riba yake wakati huo huo unatakiwa pesa hiyohiyo ukuze mtaji pamoja na gharama nyinginezo kama vile mishahara na kodi ya pango.

Alisema pia ya kwamba mchanganuo unakufanya ufahamu  ikiwa ni kiasi gani cha fedha kinachohitajika katika biashara iwe mpya au ya zamani iliyokwisha anzishwa.
MTIRIRIKO WA MCHANGANUO WA BIASHARA.
Bwana Luther akielezea kwa kifdupi jinsi mtiririko wa mpango wa biashara unavyopaswa kuwa alisema kuwa mpango wa biashara unaanza na;
1.  JALADA LA NJE, ambapo juu yake utaandika aina ya biashara, anuani na jina la muandaaji.
2.  Muhtasari, ufupisho wa mambo yote yaliyopo ndani ukijumuisha, dira malengo, bidhaa, soko, fedha, utawala pamoja na bajeti.
3.  Malengo ya biashara.
4.  Masoko.
5.  Usimamizi
6.  Fedha na
7.  Ratiba ya uzalishaji bidhaa au huduma.
Hatimaye somo la mchanganuo wa biashara lilimalizika na tukapewa maelekezo juu ya shindano la kuandika mchanganuo ambapo kila mshirikia aliyependa kushiriki alitakiwa mara baada ya kumaliza semina akachulue fomu ya kushiriki mlangoni na kisha atakwenda kuandaa mchanganuo wa biashara yake na kisha tarehe 15 au 15 Septemba atatakiwa kurudisha fomu  katika kijiji cha Makumbusho Kijitonyama Dar es slaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni. Washindi katika shindano hili watapewa ruzuku kwa ajili ya kuendeleza biashara zao ambapo wa kwanza atapewa kitita cha shilingi za Kitanzania 2,000,000/= wa pili sh. 1,500,000/= na watatu sh. 1,000,000/=

Hebu sikiliza sauti(audio) ya mkufunzi huyo Bw. Luther Monko Majoji akitoa mada.


UTENGENEZAJI WA MVINYO WA ROSELLA (WINE)
Somo lililofuata lilikuwa ni namna ya kutengeneza mvinyo wa Rosella kwa vitendo, somo lililowasilishwa na, Bibi Stella Matutina Mwombeki, mama mjasiriamali anayemiliki kampuni ya kutengeneza mvinyo (wine ya rosella) iitwayo “MATUTINA NATURAL PRODUCTS” iliyo na makazi yake huko Mbezi Beach jijini Dar es salaam, aliianzisha tangu mwaka 2007 na hujihusisha pia na utengenezaji wa vitu vingine kama vile,garlic paste, ukaushaji wa mbogamboga na viungo.

Maua na mmea wa Rosella.

Alianza kwa kuuliza swali, “Ni nini maana ya neno mjasiriamali?. Washiriki mbalimbali walinyosha vidole na mmoja akajibu, “Mjasiriamali ni mtu mwenye ujasiri wa mali ambaye hutumia ubunifu kuanzisha biashara”. Mkufunzi alikubaliana naye kuwa alikuwa sahihi, baada ya kutoa maana yake, na kusema kuwa; “Mjasiriamali ni mtu anayeanzisha biashara kwa lengo la kupata faida na wakati huohuo kuwa tayari kupata hasa endapo itatokea”

Baada ya hapo alianza kuelezea namna ya kuandaa wine ya rosella, na kusema kuwa Rosella ni maua ya mti wa rosella au kwa jina jingine hujulikana kama Choya na  ambao hupatikana zaidi katika mikoa ya Singida na Dodoma lakini pia hata hapa Dar es salaam huweza kuota lakini unahitaji maji mengi sana.
Akielezea zaidi kwa vitendo Bi Stella alisema kuwa angefundisha kutengeneza wine ya rossela katika lita tano kutokana na ufinyu wa vifaa vilivyokuwa pale pamoja na muda, ila vipimo ambavyo angetupa pale ni vipimo vinavyotosha kuandaa wine katika lita 20 hivyo katika lita 5 itabidi kugawanya vile vipimo ya lita ishirini katika sehemu nne za lita tanotano.

Mahitaji ya kutengeneza wine katika lita 20
·       Rosella grammu 200
·       Maji lita 20
·       Sukari kilo 6
·       Ndimu 4 au kama ni limao ziwe 2
·       Majani ya chai vijiko  vya chai 4
·       Hamira vijiko 4 vya chai.
Vifaa.
1.  Dumu au ndoo yenye mfuniko wa kufunga vizuri.
2.  Jiko la mkaa, au la gesi.
3.  Sufuria la kuchemshia maji.
4.  Ndoo 2
5.  Mwiko 1
6.  Vijiko viwili vya chai.
7.  Kisu.
8.  Chujio.
9.  Mrija wa kutolea hewa.
Alitutia moyo kwa kusema kuwa kila kitu kinawezekana, kwani yeye alipoanza alianza na lita 20 na hakuanza kuuza mbali bali aliwauzia watu wa karibu waliomzunguka. Akizidi kubainisha alituambia hivi; “Msiogope Wine inalipa”

Vile vile alitutajia faida za Rosella na wine kwa ujumla kwa kusema kwamba, mmea wa rosella unaojulikana kwa jina la kisayansi kama “Rosella Hibiscus Sabdarifer”, una faida nyingi katika mwili wa binadamu kama vile;

·       Huongeza damu mwilini.
·       Hushusha shinikizo la juu la damu ‘high blood pressure’ na kuondoa mafuta mabaya mwilini au ‘cholesterol’
·       Husaidia kupunguza athari zitokanazo na unywaji pombe(Hangover)
·       Husaidia kupunguza unene.
·       Huchochea kinga za mwili, kutokana na kuwa na vitamin c kwa wingi na pia husaidia kutibu mafua.
·       Chai yake ikinywewa mara kwa mara husaidia kuzuia maambukizi ya kibofu cha mkojo pamoja na kurahisisha usagaji wa chakula tumboni.


Chai ya Rosella.
Alizitaja pia faida za wine mwilini kuwa ni; kusaidia mwili usizeeke haraka, akitoa mfano alisema kuwa watu duniani walikuwa wakishangaa ni kwanini Wafaransa hawazeeki au kufa haraka wala kupata magonjwa ya mara kwa mara, wataalamu wakafanya research (utafiti) na kubaini kuwa ni kwa sababu Wafaransa hupendelea zaidi kutumia wine. Kila mtu katika nyumba yake utamkuta ana wine na huitumia kidogo kabla na baada ya chakula kwa kiasi kidogo na wala siyo kunywa kwa ajili ya kulewa.

Faida nyingine alizitaja kuwa ni pamoja na;
·       Kusafisha mafuta mwilini hasa yale yanayozunguka moyo.
·       Inasafisha ini, figo na kutoa gesi tumboni.
·       Hupunguza unene, mfano kina mama wenye matumbo yaliyomwagika hasa baada ya kuzaa wakitumia kidogokidogo hupungua, alitoa ushuhuda yeye mwenyewe kuwa alikuwa mnene sana baada ya kuzaa lakini alipotumia sasa yupo fiti.
·       Huondoa msongo wa mawazo(stress/tension)
·       Huongeza CD4.
·       Huongeza nguvu za kiume.
·       Husaidia kina mama wanapofikia umri wa kukoma hedhi(menopause)
·       Husafisa kizazi.
·       Husaidia kutibu kikohozi
·       Hutibu Pressure na
·       Wine iliyokomaa pia hutumiwa kuoshea vidonda.
Baad ya kuelezea faida za wine na rosella tuliendelea na somo letu ambapo sasa alianza kuelezea vitendo, au jinsi ya kuchangavya vile vitu.

·       Tumia chumba maalumu kisiwe na mwanga sana ambacho hamna mtu atakaye ingia mara kwa mara.
·       Kwanza unachemsha maji(zingatia sana usafi)
·       Toboa mfuniko wa chombo na uweke mrija wa hewa kisha ziba kwa nta ya mshumaa eneo ulikotobolea huo mrija wa hewa. Unaweza ukatumia ‘air lock’ ambazo hutoka nje ya nchi au mpira unaotumika kwa ajili ya dripu.

·       Kata ndimu/limao na kisha ukamue juisi yake kwenye kikombe.
·       Koroga hamira, hamira tumia hamira maalumu za wine zinazopatikana katika masupermarket, hizi ni hamira kama za mandazi ila ni spesheli kwa wine, zina flavor/ladha ya wine.
·       Tia rosella yako kwenye yale maji ya moto yanayochemka na kisha yakishabadilika rangi kuwa juisi uipue.
·       Kabla hujaanza kutia mchanganyiko wa vitu vyako kwenye hiyo juisi acha kwanza ipoe kidogo, joto la kadri kama nyuzijoto 30c hivii. Ikiwa hutaki wine, ni juisi tu, basi hapa unaweza ukaweka sukari na baada ya kupooza katika friji ukaanza kuinywa kama kawaida.
·       Chuja juisi yako ya rosella.
·       Chuja majani chai.

·       Anza kuweka juisi ya ndimu, mchanganyiko wa majani chai na maji au ile juisi ya rosella iliyochujwa kwa chujio, halafu weka mchanganyiko wa hamira huku ukikoroga kwa mwiko.

·       Ukimaliza funika chombo chako na kisha ncha ya pili ya ule mrija wa hewa unauingiza kwenye  chombo kingine kama ndoo au chupa yenye maji kusudi hamira itakapoanza kuchachua kutoa hewa basi hewa ile itoke kama povu ndani ya chombo hicho pasipo kuruhusu hewa kuingia ndani ya hombo chako cha wine.

·       Wine mpaka iwe tayari kutumiwa inakaa miezi 9. Baada ya mwezi mmoja, unafunua chombo chako kisha unaichuja kwa kitambaa safi au mfuko, halafu unairudisha tena katika chombo kilichosafishwa vizuri na kuifunika kwa ule mfuniko wenye mrija wa hewa. Baada ya miezi 2 tena unafanya vile vile, kila baada ya miezi 2 mpaka mwezi wa 9 inakuwa haina hewa tena. Ukianza kuiuza ikiwa na miezi labda 2 au 3 inakuwa bado na hewa na chupa utakayoweka inaweza ikalipuka au kupasuka kutokana na hewa.

·       Baada ya miezi 9 unaichuja vizuri kabisa, unaweza hata ukatumia kifaa kiitwacho ‘filter’ kinachouzwa, itaonekana ‘clear’ pasipo kuwa na uchafu wa aina yeyote tayari kwa ‘kuipack.’ (Ufungashaji) katika chupa zilizokuwa safi na kuweka lebo tayari kwa kuuzwa au matumizi.

*Aidha siyo lazima ikae miezi 9 lakini miezi 9 ndiyo muda ambao inakuwa imechachuka vizuri zaidi na hewa yote imetoka.
Wine haiharibiki wala haina tarehe ya mwisho ‘expire date’ endapo utaifunika vizuri isiingize hewa. Ukienda ulaya zipo hata zenye umri wa miaka 300 na kadiri inavyokuwa na miaka mingi ndivyo thamani yake nayo inavyokuwa kubwa.

Bibi Stella anasema kwamba chupa za kupack wine yake huagiza Afrika ya kusini, zamani walikuwa wakizipata Sido lakini kwa sasa hawana. Anasema ‘package’ ufungashaji ndiyo siri kubwa itakayo kufanya uuze wine yako. Kwa mfano alisema ukipaki wine yako katika chupa labda ya plastiki inaweza isipate wateja kwani wine ina heshima yake na wanywaji wake huvutika zaidi zinapokuwa katika chupa maridadi za kioo.

Alipoulizwa kama wine yake huuza katika Supermarket kubwa kama Nakumatt alisema bado yeye hajawa tayari kusupply huko kwani hajajipanga vyakutosha, alisema unaweza ukapeleka oda huko  una chupa zako labda 100 wakakuambia ulete lita elfu 10 katika masupermarket yote ya Nakumatt, unapeleka mara ya kwanza ya pili huna, watakuona mbabaishaji.

Pia alisema inatakiiwa unapoanza kuzalisha basi uwe na kazi nyingine ya kukuwezesha kuishi kwani itabidi usubiri miezi 9 na inakubidi ili usije ukakaukiwa na wine basi utengeneze angalao kila mwezi au baada ya miezi 2 au 3.

Wakati wote zoezi hili lilipokuwa likiendelea yule rafiki yangu, “mzee wa kilaji” tuliyekutana mlangoni, mara tu somo la wine lilipoanza ‘aliruka’ akaenda kukaa kiti cha mbele karibu na mkufunzi, na mara kwa mara nilimuona akinyosha mkono akiuliza maswali kwa umakini wa hali ya juu!

Hata kabla somo halijamalizika vizuri baadhi ya washiriki walianza kujinunulia wine ya Matutina hasa iliyokuwa ikiuzwa sh. 4,500/= kwani pia ilikuwepo na kubwa ya sh. 10,000/=

Bibi stella kuhusiana na wale wasiokunywa pombe au wenye imani zinazokataza kutumia vileo alisema kuna wine isiyokuwa na kilevi na hutengenezwa kama hihii ya kilevi lakini kuna chombo maalumu ambacho hupatikana nje ya nchi ambacho hutumika kuondoa Alcohol mpaka inabadilika na kuwa 0%Alcohol. Hata yeye katika sampuli alizoleta pale darasani kwa ajili ya kutuuzia kulikuwepo pia na hiyo wine isiyokuwa na kilevi.

Kwa kweli muonekano wa chupa za wine za huyu mama hauwezi ukautofautisha na ule wa wine zingine zitokazo nje ya nchi kama vile za Afrika ya kusini, Ufaransa na hata Uholanzi.
Aina ya chupa za wine (siyo za Stella)

Wine zake kwa sasa alisema huzisambaza katika maduka ya reja reja ya kawaida na supermarket ndogondogo jijini Dar es salaam hasahasa katika maeneo ya Mwenge, Tegeta, Tangibovu na Tabata Segerea huku akijipanga kwa ajili ya kuuza katika masupermarket makubwa na nje ya nchi, bidhaa zake zina ubora uliopitishwa na vyomb vyote husika serikalini kuanzia, Manispaa, TRA, TFDA naTBS.

Mbali na kutengeneza mvinyo Bibi Stella pia hujishughulisha na kilimo cha rosella, ana mashine ya kukaushia ambapo pia huitumia kukaushia rosella kwa wajasiriamali wengine wasiokuwa na kifaa hicho kwa malipo,ukiwa na rosella yako anakukaribisha uende ukakaushe kwake pamoja na huduma zozote zingine zinazohusiana na rosella. 

Alitutia moyo kwamba hakuna jambo lisilowezekana ukiwa na nia ya dhati, na ikiwa kuna mtu yeyote ambaye angependa kufahamu zaidi juu ya utengenezaji wa wine au hata soko la wine basi ni ruksa kumpigia simu kumuuliza kwa msaada wowote ule, au anaweza akafika kiwandani kwake Mbezi Beach, Tangi Bovu na pia alitupa namba zake za simu ambazo ni 0756368844 na 0782368844, STELLA MATUTINA MWOMBEKI.


Msikilize Stella Mwombeki mwenyewe hapo chini alipokuwa akitoa mada juu ya namna ya kutengeneza mvinyo/wine ya Rosella. (SEHEMU YA 1)




Picha za semina ni kwa hisani ya tovuti ya Amana bank pamoja na blogu ya charaz.blogspot.com   


0 Response to "SHINDANO LA MCHANGANUO WA BIASHARA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA NA UWEKEZAJI, WAJASIRIAMALI WALIVYOHAMASIKA."

Post a Comment