TAJIRI BILIONEA WA MADAWA YA KULEVYA ALIYETOROKA JELA “ASIYECHUKUA HATARI HAFANIKIWI” | JIFUNZE UJASIRIAMALI

TAJIRI BILIONEA WA MADAWA YA KULEVYA ALIYETOROKA JELA “ASIYECHUKUA HATARI HAFANIKIWI”

Kumbe hata mhalifu namba moja Duniani, Joaquin El Shapo au Guzman, kwa jina la utani ‘Shorty’ au mtu mfupi, anafahamu dhana hii kuu katika suala zima la ujasiriamali. Ujasiriamali unaweza ukatumika katika karibu kila nyanja ya kimaisha hata katika shughuli haramu kama hii ya biashara za madawa ya kulevya.

Mtu usipochukua hatari  yaani kufanya jambo ambalo mwisho wake hauna uhakika asilimia mia moja ikiwa utaishia kupata faida ama hasara kamwe mafanikio katika ujasiriamali hautayaona.(Simaanishi kwamba uhalifu nayo ni njia halali ya kujipatia kipato)

Kauli ya mhalifu huyo, ‘Zungu la unga’, na mtu anayesakwa mno na Marekani aliitoa punde tu  baada ya kutoroka gereza lenye ulinzi mkali(maximum security) kushinda yote nchini Mexico, alikokuwa ameshikiliwa kwa takribani mwaka mmoja. Guzman hii si mara yake ya kwanza kutoroka jela, mara ya kwanza mwaka 2001 alitoroka tena baada ya kuwahonga walinzi wa jela kiasi kikubwa cha pesa wakamtia kwenye pipa la taka alilotumia kutorokea. Safari hii mnamo siku ya jumamosi usiku saa 2 katika bafu la kuogea alizama katika handaki lililokuwa limechimbwa chini kwa chini na mainjinia wake, kazi waliyoifanya kwa muda unaokadiriwa kufika mwaka mmoja.

Handaki hilo kwa ndani.
Handaki hilo lilianzia katika jumba moja jirani na gereza alimokuwa Guzman ambalo ujenzi unaonekana ulikuwa ukiendelea kwa nje kumbe kwa ndani ndipo kazi ya kuchimba ilikuwa ikifanyika. Handaki hilo lililokuwa na urefu upatao maili moja kutoka gereza lilipo kwenye bafu la kuogea mpaka alipoibukia lina upana wa  futi 2 na nchi 3, na urefu wa futi 5 na inchi6, urefu unaolingana na ‘Shorty’ mwenyewe linakadiriwa kugharimu kiasi cha Dola milioni $50.

Sehemu ya kuingilia kwenye handaki.
Ndani kulikuwa na kila kitu muhimu kuanzia taa za umeme, mitungi ya hewa ya oxygen, toroli la kubebea mchanga na pikipiki kwa ajili ya kusafiri haraka wakati anatoroka kutoka gerezani mpaka jumba lilipokuwa maili 1. Inakadiriwa pia udongo(kifusi) uliotokana na kazi hiyo unafika tani 3,250 na ulihitaji magari zaidi ya 379 kuubeba lakini ajabu ni kwamba  hakuna ripoti yeyote iliyoweza kuzifikia mamlaka kutoka kwa waliohusika na ulinzi katika eneo hilo la gereza mpaka anafanikiwa kutoroka.

‘Akitweet’ katika account inayosadikiwa kuwa ni ya mwanawe, Guzman alimjibu kwa matusi makali  mtangaza nia wa chama cha Republican, Bilionea Donald Trump kwamba, atamfanya ayameze matamshi yake aliyoyatoa juu yake. Trump hapo kabla alikuwa amesema  kwamba; Guzman  anafaa kulaumiwa kwa kila jambo baya linalotokea Mexico na kuongeza kwamba angeweza kumpiga teke la “makalioni”. 

Kufuatia tishio hilo Trump ameogopa na kwenda FBI kuomba uchunguzi ufanywe juu ya hiyo akaunti ya twiter. Hakuishia hapo, Mhalifu huyo pia alitweet kwa raisi wa nchi hiyo na kumwambia hivi; “Na wewe usiniite mhalifu, kwani nawapa watu ajira, tofauti na wewe mwanasiasa mwoga”

Mtangazania wa Republican, Bilionea Donald Trump.
Pia aliposti, “Kamwe usiseme haitakaa itokee, hii dunia inazunguka. Katika maisha haya asiyechukua hatari yeyote hawezi kufanikiwa ( 'Never say never, this world keeps turning. In this life, he who risks nothing cannot win')

Aliwataja pia watu maadui zake aliosema ndiyo wa kwanza kuuwawa kwasababu walichekelea yeye afie jela, mmoja wao ni El Chabelo mhalifu wa madawa ya kulevya mwenzake anayedai alimsaliti.

Pikipiki aliyotumia kusafiria shimoni hadi alipoibukia.
Mashuhuda mtu na mkewe  Lorenzo na Maria wanaoishi jirani na jumba linalojengwa alimotorokea walisema kwamba walishangazwa kuona miezi sita iliyopita akija mtu mgeni na eneo lile akajitambulisha kwa jina la ‘El Pastor’ (mchungaji kondoo)na kudai alikuwa anahamia pale kufanya ujenzi wa nyumba.
Chumba alimoibukia na kubadilisha nguo kabla ‘hajasepa’
Walieleza jinsi jinsi mtu huyo alivyoingia kwenye jengo hilo la matofali mwanzoni mwa mwaka huu na kisha baadaye kuanza msururu wa kazi za ujenzi. Mtu huyo mrefu, mnene na anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 50, mara kwa mara alionekana kuingiza ndani na kutoa nje ya ‘saiti’ hiyo vifaa vya ujenzi akitumia gari yake nyekundu aina ya 4×4 na Pick up nyeupe. Walisema; “Hakuwa mwenyeji wa eneo hili kabisa lakini mara zote alionyesha urafiki wa hali ya juu. Alitueleza kwamba alikuwa akijenga nyuma mpya kwenye hicho kiwanja lakini kamwe hatukuona mabadiliko yeyote ya nje”.
Jengo lililotumika kuchimba handaki na El pastor linavyoonekana kwa nje.
Siku ya Jumamosi ambayo ndiyo siku El Chapo alipotoroka, wanandoa hao wanaeleza kuwa waliona gari mbili ‘luxury’ sana aina ya 4×4 zikiingia kwenye kile kiwanja na siku iliyofuata asubuhi waliziona tena zile gari zikiondoka pale zikiwa sambamba na magari mengine mawili ya El Pastor.


Gereza la Altiplano linavyoonekana kwa mbali.
Awali Guzman alipokamatwa mwaka jana serikali ya Marekani iliiomba sana serikali ya Mexico impeleke akafunguliwe mashtaka Marekani kwa hofu kuwa ni lazima angetoroka lakini Rais mpya wa Mexico Enrique Peña Nieto aliyekuwa ameingia madarakani akiapa kutokomeza magenge ya wauza madawa alikataa na kudai safari hii asingeweza kutoroka tena. Serikali ya Mexico imeweka dau la dola milioni 3.8 kwa atakayefanikisha kumkamata.

El Shapo, (Guzman) ‘akila bata’ uraiani baada ya kutoroka.
Soko lake kubwa la madawa ya kulevya lipo Marekani. Ni miongoni mwa watu matajiri zaidi Duniani akimiliki mtandao mkubwa wa biashara ya madawa ya kulevya Duniani uitwao 'Sinaloa Cartel' , pia ana  jeshi binafsi  hatari lililokuwa na uwezo wa kumuua mtu yeyote anayeingilia maslahi yake na ana uwezo wa kuwahonga maafisa wengi katika serikali ya Mexico kufanikisha mipango yake. Mashabiki na wafuasi wake wanaokadiriwa kufikia milioni 3.2 huwa anatoa misaada mbalimbali pamoja na pesa na wengi humsaidia katika harakati zake za kujificha serikali isimkamate hasahasa eneo analotoka la Sinaloa.

Jarida la Forbes mwaka 2009 liliwahi kumweka miongoni mwa matajiri wakubwa duniani kama kina Bill Gates na Warren Buffet, na lilisema alikuwa na utajiri uliofikia Dolla Bilioni 1.

Anamiliki pia ndege binafsi pamoja na timu ya mainjinia mahiri walio na vifaa vya kisasa kabisa wanaomwezesha kutengeneza miundombinu mbalimbali ya kujificha na kutoroka hasa mahandaki na njia za chini kwa chini za kuingiza madawa nchini Marekani.

Kimwana, mrembo aliyezaa naye mapacha.
Kamuoa pia mrembo mmoja mwenye asili ya Marekani na Mexico, Emma Coronel, na amezaa naye watoto mapacha wawili ambao mama yao alikwenda kuwazalia nchini Marekani ili wawe raia wa nchi hiyo.

CHANZO: DAILY MAIL ONLINE  

0 Response to "TAJIRI BILIONEA WA MADAWA YA KULEVYA ALIYETOROKA JELA “ASIYECHUKUA HATARI HAFANIKIWI”"

Post a Comment