JE, WAJUA KITU BINADAMU ANACHOPENDA KULIKO VYOTE DUNIANI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JE, WAJUA KITU BINADAMU ANACHOPENDA KULIKO VYOTE DUNIANI?

Watu wanaweza wakawa na majibu tofauti mengi  kuhusiana na swali hili kwamba, ni kitu gani ambacho wanadamu hupenda kuwa nacho kuliko kitu kingine chochote kile hapa chini ya jua. 

Simaanishi ile kanuni maarufu ya “Maslow’s hierarchy of needs” ya hatua za mahitaji ya binadamu, kwani ingelikuwa ni hiyo basi tungelisema binadamu anahitaji zaidi chakula na malazi ili aweze kuishi.

Kwa mtazamo wa wengi jibu linaweza likawa ni moja kati ya vitu hivi vifuatayo(vimetajwa baadhi tu) kabla hatujaangalia jibu sahihi ni lipi la ni kitu gani binadamu anachopenda zaidi kuliko vitu vingine vyote hapa Duniani.

PESA.
Bila shaka yeyote, idadi kubwa ya watu ni lazima watajibu kwamba, kile wanachopenda zaidi maishani mwao wawe nacho ni PESA, au kwa maneno mengine wanapenda kuwa na utajiri utakaowawezesha kununua kila kitu wakipendacho. Binafsi siwezi nikabisha hilo ingawa sina hakika ikiwa pesa ina uwezo wa kununua kila kitu hapa duniani.

KAZI NZURI.
Wengine watataja, wangependa kuwa na ajira nzuri waipendayo  yenye kulipa ujira mnono, tena ikiwezekana serikalini kabisa, kusudi waweze kuwa na ulinzi wa kutosha wa ajira zao na siyo tena mara leo kazi ipo keshokutwa unaambiwa imeota majani. Pamoja na marupurupu ya uzeeni baada ya kustaafu kazi.

BIASHARA NZURI.
Wapo watakao kuambia, wao kitu wanachotamani sana kuwa nacho maishani mwao kuliko kitu kingine chochote kile, siyo kingine bali ni kumiliki biashara ya ndoto zao, wawe mabosi wao wenyewe na mwishowe kuwa na uhuru kifedha utakaowawezesha kufanya jambo lolote maishani pasipo kumtegemea mtu mwingine yeyote yule wala kuhofia kesho watakula nini ikiwa leo watatumia kiasi kikubwa cha fedha. Ina maana kuwekeza katika vitegauchumi vya uhakika vitakavyowatiririshia pesa hata ikiwa wamelala usiku au hata baada ya kufa.

MUNGU.
“Kuna  faida gani, ikiwa mtu atapata kila kitu hata kama ni Dunia yote, na kisha akaipoteza Roho yake? “ Hiyo ni moja ya kauli utakazojibiwa na wale ambao wao kwao kila kitu ni Ufalme wa Mbingu tu, hawataki kitu kingine chochote kile. Hawataki pesa, magari, mali, wala chochote zaidi ya kupalilia maisha yao baada ya kifo kwa kumtumikia Mungu wakiwa hapa Duniani.

KUFANYA JAMBO LA KUKUMBUKWA MAISHANI.
Mwingine yeye shauku yake kuu maishani ni kufanya jambo fulani  liwe ni la kijamii, kisiasa, kisayansi, kisanaa ama katika nyanja nyingine yeyote ile,  ambalo  ni “tofauti” linalowagusa watu na litakalobadilisha maisha ya wengi. Mwishowe jambo hilo liweze kukumbukwa vizazi na vizazi hata baada ya mtu huyo kuwa amekwishaondoka duniani. Iwapo akifa ameshatimiza jambo hilo basi ataridhika mchango wake ameshautoa.

CHOCHOTE WASICHOKUWA NACHO
Kuna watakaojibu kiujumla kwa kusema kwamba  wanachokipenda zaidi ni kile wasichokuwa nacho,  mathalani, ikiwa mtu hana pesa atakuambia anataka pesa kushinda kila kitu kingine, ikiwa mtu ni mgonjwa atakuambia anahitaji afya kushinda kila kitu kingine. Kikongwe atakwambia anataka ujana na Mtoto atakuambia anataka kuwa mtu mzima. Hali kadhalika na kwa mtu mpweke atakuambia anahitaji mpenzi au rafiki zaidi ya chochote kile.

Orodha ni ndefu ya vitu ambavyo watu wanaweza kukuambia kuwa ndivyo wanavyotamani zaidi kuwa navyo maishani na hivyo kazi ya kujua kwamba ni kitu gani hasa kimoja ambacho hupendwa zaidi na watu wengi kuwa ngumu. Kwa bahati mbaya katika vitu vyote vilivyotajwa hapo juu hamna hata kimoja ambacho unaweza ukasema ndicho kinachopendwa zaidi na watu.

Kwa mfano ikiwa utasema ni pesa elimu kubwa, kazi nzuri, biashara nzuri au umaarufu, mbona basi  tunashuhudia kila siku watu wenye vitu hivyo wakijiua na hata wengine kuishi maisha ya kuhuzunisha? Hilo linazidi kunitia shaka kwamba katika vitu vyote hapo juu hakuna jibu sahihi hata moja.

JIBU SAHIHI NI LIPI BASI?
Ikiwa wewe ni mdadisi vya kutosha utagundua yakwamba katika vitu vyoote vilivyotajwa na watu hapo juu, kwamba ndivyo ambavyo wangetamani kuwa navyo maishani mwao kushinda kitu kingine chochote kile, vina uhusiano moja kwa moja na kitu kimoja tu kinachoitwa  FURAHA.

Halafu kwa makusudi kabisa kuna kitu kingine kimoja ambacho sikupenda kukitaja ijapokuwa kimlolongo kilipaswa hata kiwe ni cha kwanza;  ‘KUPENDWA’.

Binadamu kwa asili tunapenda sana KUPENDWA na kuthaminiwa,upendo namaanisha  wa aina zote mbili, ule wa kawaida kama wa mzazi na mtoto na ule wa mtu na mpenzi wake mfano wanandoa. Hali hii ya kupendwa ndiyo humfanya mtu kuhisi FURAHA. Hivyo basi unaweza ukasema kwamba katika kila kitu, wanadamu tunapenda zaidi FURAHA kuliko  kitu kingine chochote kile, ndiyo maana kila mtu ana kitu chake maishani atakachokutajia anakipenda lakini nyuma ya kitu hicho ndipo FURAHA yake ilipojificha.


Inasemekana kwamba mtu anapokuwa amekamilisha kila kitu alichokuwa akikitaka maishani mwake, haoni tena sababu ya kuishi na yupo tayari kufa muda wowote. Maisha huwa na maana tu pale mtu anapokuwa namalengo ya kukamilisha. Hii ndiyo kusema kwamba, mtu mwenye furaha ya kweli moyoni mwake haogopi kifo kwani tayari anakuwa ameshakamilisha kilichomleta Duniani.

Mpendwa msomaji, wewe kuna kitu gani unachopenda kushinda vyote katika maisha yako hapa Duniani?.   

1 Response to "JE, WAJUA KITU BINADAMU ANACHOPENDA KULIKO VYOTE DUNIANI?"