HUJUMA ZATAJWA KUUNGUA SOKO LA WAMACHINGA MCHIKICHINI/KARUME | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HUJUMA ZATAJWA KUUNGUA SOKO LA WAMACHINGA MCHIKICHINI/KARUME



Waathirika wa moto ulioteketeza soko la wafanyabiashara wadogo, maarufu kama soko la mchikichini au soko la Karume wamelalamika kuwa huenda zikawa ni njama zilizosababisha kuungua kwa soko hilo kwani hata mamlaka zinazohusika ikiwemo zima moto hawakuonekana kufanya jitihada za kutosha wakati moto huo ulipozuka jana tarehe 11 majira ya saa nne na nusu usiku.

Jifunzeujasiriamali ilitembelea  eneo la tukio leo majira ya saa 10 jioni na kujionea hali halisi ilivyokuwa ambapo mpaka wakati huo bado moto ulikuwa ungali ukiwaka katika baadhi ya maeneo hasa yale yaliyokuwa maalumu kwa biashara za viatu. Mfanyabiashara mmoja anayefanya shughuli za kuhifadhi mizigo ya wafanyabiashara kwa jina moja la Costa, alisema kwamba muda huo wa saa nne usiku alishuhudia moto huo ukianzia maeneo ya katikati karibu na yalipo mabanda ya mamantilie akafikiri moto ule ungedhibitiwa tu lakini kadiri muda ulivyopita ukazidi kusambaa.

Anasema cha ajabu moto ule ulimshangaza kwani ulisambaa haraka sana katika staili ambayo utadhani kuna mtu alikuwa akiufukiza chini kwa chini kuelekea kulikokuwa na mabanda ya nguo na viatu. Costa anaendelea kusema kuwa Gari la faya lilipofika waliingiwa na matumaini wakidhani sasa moto ungedhibitiwa lakini walishangaa kusikia eti gari la faya lisingeweza kupenya katikati ya vibanda kutokana na kutokuwa na barabara pana.” Kwa nini hata wasingelilazimisha hata kuharibu baadhi ya mabanda ilimradi tu gari limepenya katikati” anauliza Costa kwa hasira. Waliishia kuzima kandokando ya soko tu kuzuia moto usishike nyumba za jirani na upande wa kiwanda cha bia Tanzania Breweries.

SOKO LA WAMACHINGA MCHIKICHINI LIKITEKETEA KWA MOTO
Mfanyabiashara mwingine ambaye ni mlemavu wa mguu yeye amesema kwamba hasara waliyoipata ni kubwa, lakini hawezi kuvunjika moyo kwani ameshapitia majanga mengi likiwemo la mwaka 2007 la kuhamishwa na aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam katika maeneo ya biashara ya vibanda yaliyokuwa eneo la Msimbazi Kariakoo, “Wakati ule wa Kandoro ilikuwa hivihivi, tulibaki bila chochote na kama ningekuwa na roho ndogo basi hata ningejiua lakini kidogokidogo nilianza tena mpaka nikazoea”  Alisema mfanyabiashara huyo ambaye hapo awali alikuwa na kibanda kwenye kona jirani na baa maarufu ya Sabasaba iliyoko Msimbazi eneo linalotazamana na kituo cha polisi Msimbazi. 

Costa anasema walijitahidi kuokoa baadhi ya mali zisiteketee lakini tatizo lilikuwa vibaka nao kuwaibia pindi walipokuwa wakienda kurudia kutoa mali zingine, anasema polisi nao walikuwa wakiwakataza kuokoa mali kwa hofu ya kupoteza maisha au kupata majeraha ya moto. 

Watu wengi walisikika wakikumbuka suala la bima huku wengine wakihoji ikiwa hata wafanyabiashara wadogowadogo kama wamachinga wanaweza kujiwekea bima kama ilivyokuwa kwa biashara kubwa.

Nyakati za mchana walionekana watu mbalimbali wakiondoa baadhi ya mabaki ya mabanda yao yaliyoungua huku wengine ambao inasemekana wala siyo waathiriwa wakijikatia mabomba ya nguzo za chuma bila wasiwasi wowote, utathani ni wahusika vile. Inasemekana mabomba hayo huenda kuyauza kama chuma chakavu.


Hata hivyo mamlaka zinazohusika jijini Dares salaam likiwemo jeshi la polisi zimekwishatoa tamko leo jioni wakiwataka wafanyabiashara hao kuwa watulivu huku uchunguzi kamili ukifanyika kubaini chanzo halisi cha moto huo, na ikiwa kulikuwa na hujuma za aina yeyote ile kutoka kwa taasisi au mtu yeyote yule.

0 Response to "HUJUMA ZATAJWA KUUNGUA SOKO LA WAMACHINGA MCHIKICHINI/KARUME"

Post a Comment