UVUMILIVU NGUZO KUU YA MAFANIKIO KATIKA BIASHARA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UVUMILIVU NGUZO KUU YA MAFANIKIO KATIKA BIASHARA


Siku zinayoyoma na maisha yanakwenda kasi ya ajabu, leo ni Ijumaa ya mwisho kwa mwezi huu Novemba.Tutaanza  kuhesabu siku kuelekea mwishoni mwa mwaka, mjasiriamali jiulize mafanikio yako yakoje mpaka sasa kuelekea mwisho wa  mwaka?  

Katika siku za karibuni nimepokea simu za wasomaji mbalimbali wa kona hii ya wajasiriamali wakiuliza ni kwa namna gani wanaweza kufanikiwa. Wengi wamekuwa kwenye ujasiriamali na bado hawajaweza kupata mafanikio makubwa wanayotamani. 

Leo katika kona ya mjasiriamali tutaona moja ya siri inyoweza kujenga mafanikio katika ujasiriamali, nayo ni nguvu iliyopo katika uvumilivu. Uvumilivu ni hali ya kukubali na kukabili jambo kadiri ya wakati na jinsi linavyotokea.  

Kumbuka kuwa  mafanikio katika biashara si jambo la kulala na kuamka bali ni suala linalohitaji uvumilivu wa kweli. Hivyo kwa wale wajasiriamali wenye kiu ya mafanikio wanahitaji kuzingatia mbinu za ujasiriamali mojawapo ikiwa uvumilivu ili kufanikiwa. 

Lugha ya uvumilivu inaweza isiwe rahisi kueleweka miongoni mwa wajasiriamali, kwani ukweli ulio wazi ni kwamba wengi tunapenda matokeo ya haraka, tungependa kupata  matokeo mazuri mapema, lakini matokeo mazuri na ya kudumu yanahitaji uvumilivu. 

Tuangalie baadhi ya mbinu za kudumu katika ujasiriamali na hasa namna bora ya kuweza kuvumilia. Jambo muhimu la kujiuliza je una malengo gani katika ujasiriamali? Siri ya kufanikiwa ni kujiwekea malengo, usifanye mambo kimazoea ili kupata hela ya kula!

Malengo ni ndoto za kweli juu ya mambo unayotaka uyapate, kwamba katika kipindi cha muda fulani uwe umeweza kufanya jambo fulani. Jiulize umeamua kufanya unayofanya ukiwa na malengo gani hasa ambayo ungependa kuyafikia?

Katika malengo ni muhimu kuwa na uvumilivu, kwani si kila unalopanga litakuja kama unavyotaka. Elewa katika malengo huenda ukakutana na changamoto mbalimbali wakati mwingine ngumu zinazoweza kukwamisha yale uliyoyapanga na hivyo kurudi nyuma. 

Kumbuka mjasiriamali ni vizuri kujiwekea malengo ambayo unaweza kuyafikia na si kujifurahisha. Ndio maana tunasema unahitaji kuwa mvumilivu, usikurupuke kwa kuwa tu umeona mwenzio anafanya jambo fulani na wewe unataka kufuata mkumbo.

Wajasiriamali wote ambao wamefanikiwa walianza na mawazo madogo ambayo yaliwapeleka kwenye mawazo makubwa. Mafanikio katika ujasiriamali hayaji kama upepo bali lazima udhamirie na kuanza harakati za kuelekea unakotaka. 

Yafaa kujiuliza kwa nini unafanya biashara unayofanya, ni kitu gani kilikusukuma uingie katika biashara hiyo na si nyinginezo? Sababu ya wewe kufanya unachofanya kwa sasa ni ni ufunguo wa kufungua mafanikio. Tangu  mwaka umeanza mpaka sasa umefanya nini?

Wengi wameingia kwenye ujasiriamali kwa ajili ya kutafuta mafanikio, na kilele cha mafanikio ni hupimwa kwa fedha na mali wanazopata, je umewahi kujiuliza ni kiasi gani cha kipato au mali unahitaji kupata na utapataje? Je ni kwa mbinu gani halali?

Umewahi kujiuliza kwa nini baadhi ya wajasiriamali wanashindwa kufikia ndoto zao? Umeshawahi kujiuliza kwanini kuna wajasiriamali waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa? Hawa wamefanikiwa vipi na hawa wameshindwa vipi?

Amka ndugu mjasiriamali, malengo ni silaha ya kukupeleka kule unakotaka. Acha kufanya mambo kimazoea kwakuwa tu unapata hela ya kula na kulipa ada, elewa kuwa malengo yenye kufaa yanaweza kukupeleka mbali na kupata zaidi ya unachopata.

Pamoja na kujiwekea malengo, ni muhimu sana tena sana kufanyia kazi yale ambayo unataka kuyafikia. Wapo ambao wana mipango mizuri vichwani mwao lakini katika utekelezaji wake huwa ni mzigo kwao, maneno na matendo yao hayawiani!

Ili ufanikiwe unahitaji kuamka na kutafuta namna ya kuweza kutekeleza yale yote uliyojipangia. Kujiwekea malengo yoyote bila kutafuta namna ya kuyafikia ni sawa na bure. Kaa chini uumize kichwa ni kwa namna gani utaweza kuyatimiza yale unayoyataka.

Mbinu wa pili, fanya yale unayoyaweza. Tunapozungumzia ujasiriamali ieleweke kwamba ni uwanja mpana sana, si swala la kununua na kuuza bidhaa tu peke yake. Sasa katika mikakati yako ya ujasiriamali inawezekana umejipanga kufanya mambo mengi.

Inashauriwa uanze na jambo dogo kabla ya kukurupuka na kuanza yale usiyoyamudu. Fanya jambo ambalo liko ndani ya uwezo wako na kadiri utakavyofanikiwa ndipo ujipe nafasi ya kwenda kwenye jambo lingine lililo juu zaidi ya lile uliloanza.

Kwa mfano, kama umeamua kufanya biashara ya kusindika vyakula jaribu kujipanga vema kadiri ya uwezo ulio nao na mahitaji ya soko yalivyo. Hapa maana yake lolote unalofanya hakikisha unafanya kwa hatua bila kukurupuka au kufuata mkumbo.

Pamoja na kufanya yale unayoyaweza kwa kuanzia na mambo madogo ukielekea katika mambo makubwa, unashauriwa kuwaza makubwa. Kuwaza makubwa maana yake usiwaze mambo ambayo yanayoweza kukukatisha tamaa au kukurudisha nyuma.

Mbinu ya tatu, elewa matatizo yameumbwa. Wajasiriamali wengi wanapenda kupata mafanikio bila kukumbana na vikwazo vyovyote katika yale wanayoyafanya. Yafaa kukumbuka kuwa matatizo yameumbwa kwaajili ya kila mtu la muhimu ni kuyakabili.

Badala ya kukata tamaa na kuogopa kushindwa, ni vizuri ukajipanga vema ili uweze kukabiliana na matatizo mbalimbali ambayo yanaweza kujitokeza. Haiwezekani ukafanya shughuli zako bila kukumbana na matatizo yoyote.

Pamoja na kutafuta njia za kuweza kukabiliana na matatizo, ni muhimu kuwaepuka wale wote ambao wanaweza kuwa chanzo cha wewe kutofanikiwa, wapo watu ambao wanaweza kukukatisha tamaa kwamba huwezi kufanikiwa katika jambo fulani.

Mtu anaweza kukwambia kwamba, aha wewe unataka kuanzisha biashara fulani utapoteza fedha zako bure kwani fulani alianzisha biashara kama hiyo lakini alishindwa. Kaa chini utafakari maneno yanayoweza kukukatisha tamaa na kurudi nyuma. 

Kwenye ujasiriamali usikubali kuwa mtu mwepesi wa kukata au kukatishwa tamaa, hata kama mambo hayaendi vile unavyotaka unahitaji kupambambana, kumbuka unapokubali kushindwa maana yake unakubali kubaki hapo ulipo ambapo ni mbaya zaidi.

Mbinu ya nne, kuwa na matumizi mazuri ya kipato unachopata. Mjasiriamali unashauriwa kuwa makini na matumizi yako. Hakikisha mara zoye unakuwa na bajeti inayoainisha mapato yako na matumizi yako na hivyo kusimamia hapo.

Wajasiriamali wengi wameshindwa kupiga hatua kwa kushindwa kudhibiti vema matumizi yao. Mara nyingi matumizi yao yamekuwa yakizidi mapato yao, sasa unategemea mtu wa aina hiyo kupata mafanikio gani?

Baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakisema kwamba, vipato wanavyopata ni vidogo kiasi kwamba wanashindwa kufanya jambo lolote la maana. Sawa inawezekana unapata kipato kidogo lakini yafaa kujiuliza hicho kidogo unachopata unakitumia vipi?

Katika hili la matunizi, wajasiriamali wanashauriwa wakati wote kukumbuka kuacha kuchanganya matumizi binafsi na yale ya biashara. Matumizi binafsi yafaa yawekewe bajeti yake tofauti na matumizi ya biashara.

Mbinu ya tano, jiamini unaweza. Katika hali yoyote uliyonayo katika ujasiriamali ni muhimu kuamini unaweza, ipende nafsi yako na kile unachofanya. Amini una jukumu ambalo unapaswa kulifanya katika jamii inayokuzunguka, mchango wako unahitajika !

Hakuna mjasiriamali ambaye alizaliwa ili asipate mafanikio, wote wana nafasi ya kupata mafanikio wanayotamani. Jambo muhimu kwa wajasiriamali ni kukaa chini na kutafakari ufanye nini kama kuna jambo linalokusumbua na kukurudisha nyuma, usikate tamaa.

Mafanikio katika ujasiriamali ni jambo la kila mtu, lakini ili ufanikiwe unahitaji kuamka na kupambana, ni muhimu pia kujenga mahusianao mazuri na wengine. Kama leo hii dunia imekuwa kijiji kwa njia ya teknolojia, wajasiriamali hawana budi kuwa pamoja.

Mbinu ya tano, jipime umefanya nini kujenga mafanikio. Baada ya mihangaiko ya hapa na pale, kule na huko wakati mwingine kushindwa hata kulala au kuhatarisha maisha yako katika safari mbalimbali, jiulize je umefanikiwa kupata kile ulichotaka?

Lazima ifike mahali ujifanyie tathmini ya kile amabacho umefanya kwa siku, juma mwezi au mwaka, epuka kufanya mambo kimazoea kwakuwa tu unapata hela ya kula na kukidhi mahitaji yako mengine, ni muhimu kwa wajasiriamali kujipima wenyewe. 

Tunapozungumzia kupima mafanikio katika biashara yafaa kutofautisha na ile hali ya wewe kukidhi mahitaji yako ya msingi kama vile chakula, mavazi, malazi na matibabu. Hata wasio katika ujasiriamali wanaweza kukidhi mahitaji haya ya msingi.

Lakini kwa mjasiriamali kupima mafanikio ni kuangalia mtiririko mzima wa kile ambacho umekifanya kwa kipindi fulani. Unapojifanyia tathmini ya mafanikio yako pia ni moja ya njia ya kuweza kuangalia pale ambapo ulishindwa, na kujua nini kifanyike. 

Karibu juma lijalo kwa mada nyingine ya namna bora ya kuendeleza biashara. Mwandishi ni mshauri wa Biashara anayepatikana kwa Simu: 0715/0754 363800 Barua pepe: james@nikuze.com 
 CHANZO: NIPASHE

0 Response to "UVUMILIVU NGUZO KUU YA MAFANIKIO KATIKA BIASHARA"

Post a Comment