Kilichomuua Dk Mvungi | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Kilichomuua Dk Mvungi


Hospitali ya Millpark ya Johannesburg, Afrika Kusini, imesema madaktari waliokuwa wakimtibu aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi walibaini kuharibika kwa ubongo wake kutokana na kumwagika kwa maji yanayoutunza ambayo kitaalamu yanaitwa ‘cerebrospinal fluids’ au CCF.

Msemaji wa Hospitali hiyo, Tebogo Nyembezi alisema Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata tatizo la maji hayo yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya kujeruhiwa.
Dk Mvungi (61), alipata majeraha makubwa baada ya kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia jana mchana.
“Maji hayo ambayo ni miligramu 50 tu katika ubongo wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee yakimwagika nusu tu, basi mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na kupata tiba sahihi anaweza kupona,” alisema Nyembezi.
Alisema iwapo mgonjwa atapewa tiba sahihi ndani ya saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya kawaida, lakini saa hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji hayo yanapomwagika ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na kuharibika kabisa.
Mtaalamu wa mishipa na neva za fahamu (neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk Hariff Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao huharibika.
“Haya maji yanaufanya ubongo uelee na usielemee kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au kupungua, ubongo hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema. Soma zaidi habari hii katika tovuti ya Mwananch hapa


0 Response to "Kilichomuua Dk Mvungi"

Post a Comment