TAYARI MALENGO YAKO KIUCHUMI YA MWAKA 2017 UMESHAYAANDIKA MAHALI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

TAYARI MALENGO YAKO KIUCHUMI YA MWAKA 2017 UMESHAYAANDIKA MAHALI?


Ili uweze kufanikiwa maishani ni lazima ujiwekee malengo, na hiyo ni kanuni ya msingi ya kimaumbile ambayo huwezi ukaipinga hata utoe sababu kubwa kiasi gani. Malengo husaidia kuongeza umakini na kuelekeza nguvu katika jukumu husika huku yakimfanya mtu kuwa mbali na mambo yote yanayochangia kutokutimia kwa jukumu hilo barabara.

Kuna wataalamu kama ‘Edwin A. Locke’  aliyewahi kufanya utafiti kuhusiana na jinsi binadamu anavyoweza akatimiza majukumu yake vizuri na kwa ufanisi zaidi pindi anapojiwekea malengo kuliko vile anavyoamua kujifanyia mambo kiholela tu kama wanyama wafanyavyo. Edwin aliyeanza utafiti huo miaka ya 60 na kuuhitimisha baada ya miaka 30 alitumia falsafa ya zamani zaidi ya mwanafalsafa mwingine maarufu aitwaye Aristotle kwamba Lengo lina uwezo wa kusababisha kitendo na hivyo akaanza kutafiti athari za malengo katika shughuli za kila siku za mwanadamu.


Mwisho ilibainika kwamba kuweka malengo kunasababisha athari zifuatazo,

1.  kufanya uchaguzi wa kipi cha kufanya kwanza au kujiwekea vipaumbele.

2.  Kuzidisha juhudi zaidi kwa kile kinachofanyika mfano ikiwa mtu amezoea kulima eka moja kwa siku, atakapojiwekea lengo la kumaliza eka 2 basi atafanya kila linalowezekana kumaliza hizo heka 2.

3.  Uvumilivu: Mtu akishajiwekea malengo, atahakikisha anatimiza alichoahidi licha ya vikwazo vitakavyojitokeza njiani.

4.  Utambuzi: Malengo humfanya mtu kujitambua na hata kubadilisha tabia kutoka tabia alizokuwa nazo zamani na kuwa na tabia mpya zinazoendana au kusaidia kutimiza malengoa aliyojiwekea.  

Binadamu wa rangi zote kutoka mabara yote yanayounda Dunia imedhibitika kwa dhati kabisa kwamba ufanisi wa kile wanachokifanya iwe ni kazi, michezo au hata jambo lolote lile linalohusisha akili basi hutegemea zaidi kujitoa katika kufanikisha lengo husika.

Na kwa kupitia uelewa huo wa kujiwekea malengo, taasisi zote duniani zikiwemo serikali mbalimbali, makampuni na mashirika hutumia njia ya kujiwekea malengo katika kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi.

Hata tunaporudi kwenye biashara zetu, mameneja na wajasiriamali wote hawawezi kukwepa suala la kuweka malengo ya kiuchumi katika biashara zao. Utakuwa unafanya kitu cha namna gani ikiwa utajidanganya eti unaendesha mambo pasipokuweka malengo akilini?. Matumizi mazuri ya muda na kujiwekea malengo ni kama mapacha wawili vile, vitu hivyo viwili huwezi ukavitenganisha.

Hata hivyo kuna wakati malengo huwa yanakumbwa na vikwazo(changamoto) kwa mfano, kuingiliana kwa malengo baina ya mtu mmoja na taasisi kama vile malengo ya meneja yaanaweza yakakinzana nay ale yaliyowekwa na taasisi tuseme labda kampuni lakini kinachotakiwa kufanywa ni kuhakikisha malengo ya mtu binafsi yanaendana na yale ya mtu mmojammoja kwenye taasisi.

Kikwazo kingine katika kutimiza malengo ni pale unapokuta lengo linahitaji mtu kujifunza maarifa mapya, mtu anapokuwa amejiwekea lengo la kufanikisha jambo fulani anaweza kujisahau au kutokuona umuhimu wa kujiongezea maarifa au taarifa mpya kuhusiana  jambo hilo. Suluhisho lake ni kwa mtu huyo kujiwekea lengo jingine la kujifunza katika tasnia husika ili kutimiza lengo la msingi alilojiwekea.


Kuna watu wanaoweza wakakudanganya kuwa eti unaweza ukafanikiwa bila ya kujiwekea malengo lakini ukweli ni kwamba wao wanajaribu kutazama zaidi yale mapungufu yanayoweza kutokana na mtu kujiwekea malengo. Changamoto kubwa kwenye kuweka malengo watu hao hudai kuwa wakati mwingine huwa hayawezi kutimia kama unavyoyapanga, lakini ukweli ni kuwa kuweka malengo hakuna mbadala zaidi ya mtu kuchunguza mahali ulipokosea katika malengo yako yaliyoshindwa ukajipanga upya na kuweka malengo mengine sahihi zaidi(soma sifa za malengo mazuri ndani ya kitabu, MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA).

Changamoto nyingine hutokea pale malengo unayotekeleza unapokuwa umewekewa na mtu mwingine. Inatakiwa hata kama malengo yamewekwa labda na taasisi au mtu mwingine basi mhusika uridhie kwa moyo wako na kukubali kuyatekeleza huku ukifahamu fika faida utakazopata baada ya kutekeleza malengo yenyewe.

Katika kitabu, MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA, mada hii ya kujiwekea malengo hasa ya kiuchumi imeelezewa kwa undani kabisa, kwanza malengo ni kitu gani, mifano ya malengo, tofaui ya malengo na vitu vingine kama Dira, Maono, Ndoto na Dhamira. Pia kimeelezea kwa ufasaha kabisa jinsi au namna mtu/taasisi anavyoweza akajiwekea malengo nk.


Kitabu hiki ni kizuri sana hasa kwa mtu anayetaka kuuanza mwaka huu wa 2017 akiwa na mtazamo mpya kifikra na kiuchumi. Kama unafanya biashara, umeajiriwa au upo katika harakati za kuingia katika biashara au ajira basi kisome kitabu hiki utapata manufaa makubwa.

Kwa yule pia anayefuatilia kwa karibu kampeni yetu msimu huu ya KUJIRUDISHIA TENA UKUU WAKO ULIOPOTEZA(MAKE YOURSELF GREAT AGAIN) sina shaka yeyote kwamba umeshapata kitabu hiki kwani ni muhimu mno katika kukufanya tuweze kuwa sambamba katika kampeni hii.

Unaweza kukipata kitabu hiki kikiwa katika mfumo wa kitabu cha kawaida cha karatasi au mfumo pepe(softcopy) katika email yako.

Bei ya kitabu cha karatasi ni Sh. 4,000/= na Softcopy ni Sh. 3,000/=. Kwa mawasiliano piga au tuma sms kupitia namba hizi hapa, 0712202244  au  0765553030. Kama unahitaji softcopy usisahau kutuma email yako na pesa shilingi elfu tatu kupitia moja ya namba hizo popote pale ulipo tunakutumia baada ya muda mfupi. Kwa maelezo zaidi na taarifa za vitabu vingine unaweza ukatembelea ukurasa huu hapa, SMART BOOKS TANZANIA.


Usikubali mwaka huu mpya wa 2017 kuendelea kubaki nyuma, amka usingizini na ujirudishie tena mambo yako yote mazuri uliyokuwa nayo zamani. Inawezekana na wengi wameweza. Jiwekee malengo yako mwenyewe achana na malengo ya kuwekewa, hata wahenga hawakukosea waliposema "akili ya mwenzio changanya na ya kwako" 

Mwandishi na Mhamasishaji wako,

Peter A. Tarimo   

0 Response to "TAYARI MALENGO YAKO KIUCHUMI YA MWAKA 2017 UMESHAYAANDIKA MAHALI?"

Post a Comment