MJASIRIAMALI UNAWAHITAJI WATEJA WOTE, CCM NA UKAWA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MJASIRIAMALI UNAWAHITAJI WATEJA WOTE, CCM NA UKAWA


Katika mchakato unaoendelea wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa kuwapata Rais, Wabunge, na Madiwani, kumekuwa na ushabiki mwingi hasa katika pande mbili kuu, nikiwa na maana ya Chama Tawala CCM na vile vya Upinzani vinavyowakilishwa na Umoja wa Katiba au UKAWA ingawa pia kuna vyama vingine kadhaa ambavyo havijajiunga na Umoja huo kama vile TLP na ACT.

Huko mitaani nako Wananchi nao utakuta wamegawanyika, wengine wakishabikia CCM, wengine UKAWA, na wengine katika vyama vilivyosalia. Jana mchana nikiwa nimekaa mahali fulani niliona gari moja la kampeni likiwa limesimama kando kando ya maduka huku wahusika wakiwa wanaingia, mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, duka kwa duka, wakiwa wameshikilia mabango(posters) waliyokuwa wakiyabandika katika kuta, milango, katika nguzo za umeme na simu na mahali pengine popote pale walipoona panafaa kubandika.

Si hivyo tu walikuwa pia wakigawa vipeperushi na beji kwa watu mbalimbali. Uzuri ni kuwa hawakuwa wakibandika tu hovyo hovyo pasipo ridhaa ya wahusika, walikuwa wakiwaomba wenyeji waliowakuta pale wakikubali basi ndipo na wao hubandika.

Kuna baadhi ya sehemu, nyumbani na hata baadhi ya maduka na biashara ambapo walikataliwa, nadhani wengine ni kutokana na misimamo yao kuwa tofauti na ya kile chama wale wahusika walichokuwa wakikipigia debe. Lakini inawezekana pia wengine walikataa tu hata ikiwa mirengo yao wanayosimamia ilikuwa sawa na hayo matangazo na hapa hasa ndipo mimi ninapotaka kupazungumzia zaidi.

Kwa maoni yangu binafsi nadhani hata kitaalamu inaweza ikawa ni sahihi, sidhani kama ni jambo zuri kuhusisha moja kwa moja ushabiki wa kisiasa au hata jambo lolote lile lenye kuleta mihemko kama vile dini katika biashara unayoifanya.

Suala hili limeelezewa kwa undani zaidi katika kitabu cha “SIRI YA MAFANIKIO YA BIASHARA YA REJAREJA”,  kilichoandikwa na Peter Augustino na kuchapishwa na Self Help Books Publishers ltd. Ni katika ukurasa wa 36-38, kwenye somo linaloosema;  “MAKOSA YATAKAYOKIMBIZA WATEJA DUKANI KWAKO NA KUDHANI UMELOGWA” chini ya kipengele kilichoandikwa; ‘Kubandika Matangazo ya Ajabuajabu’

Hii ni sehemu(kipande) tu ya kitabu hicho inayozungumzia makosa yanayoweza yakakimbiza wateja katika biashara yako na wewe  ukadhani labda umelogwa.

Kumbuka katika biashara yako ndogo wewe unahitaji wateja kutoka kila upade ili uweze kukua pasipokujali huyu ni CCM, huyu ni UKAWA, huyu ni TLP, ACT au huyu ni Muislamu, huyu ni Mkristo, huyu ni Mhaya, yule ni Mngoni, Mzaramo nk. au tabaka jingine lolote lile. Kuna watu huwa wanakwazika kwa jambo dogo sana, madhalani yeye anashabikia CCM, atakapofika kwenye biashara yako kwa lengo la kununua kitu kisha akakutana na bango linaloshabikia UKAWA, basi mteja huyu kuna mawili, umkose kabisa au hata akinunua basi siku nyingine itakuwa vigumu kurudi tena katika biashara yako kwani yeye moja kwa moja anajenga chuki na ile biashara yako.

Hawezi kuitofautisha na wewe. Kwa kuwa anachukia ule upande wa pili ambao wewe ndiyo unaoshabikia, ndivyo hivyo hivyo atakavyoichukia na biashara yako. Kwa hiyo kwa mtindo huo hebu fikiria ni wateja wangapi utakuwa umewakwaza kuja kukuungisha?

Si jambo baya kuonesha upo upande gani, lakini wewe pima kwanza, ukiona madhara yanayoweza kutokana na wewe kuonesha ushabiki katika biashara yako kupindukia ni makubwa na yatakayoweza kukuletea athari mbaya basi huna sababu ya kufanya hivyo.

Kuna watu wamewahi kupata hasara kubwa kutokana tu na ushabiki, zinapotokea vurumai, mahasimu huzilenga zaidi biashara na mali za wale mahasimu wao  waliokuwa mstari wa mbele zaidi wakishabikia. Kama upo tayari kukabiliana na yote hayo endapo yatatokea  basi siyo vibaya kuonesha ukereketwa wako hata ikiwa ni kwa kuzungushia bendera za chama chako nyumba nzima. 

0 Response to "MJASIRIAMALI UNAWAHITAJI WATEJA WOTE, CCM NA UKAWA"

Post a Comment