Wateja hupendelea urahisi, ninaposema urahisi simaanishi bei
, bali wepesi katika kupata bidhaa au huduma , pasipokuwa na milolongo,
usumbufu na ukiritimba usiokuwa na maana
Naandika mada hii kutokana na uzoefu wangu binafsi katika
biashara zangu hususani hii ya vitabu. Wakati
tukiuza vitabu vya ‘MIFEREJI 7 YA PESA’ tuliamua pamoja na kuuza vitabu vya
kawaida vilivyochapwa katika karatasi vilevile tuuze kwa njia ya mtandao (online) nikiwa namaana, tunamtumia
mteja kitabu kikiwa katika mfumo wa faili la PDF kupitia E-mail (barua pepe) yake na kisha yeye ‘hudownload’ na kukisoma hapohapo au
hata kukihifadhi katika hard disk, flas, cd nk. kwa ajili ya kukisoma baadae.
Hii lakini ni kwa yule mteja mwenye uwezekano wa kupata intaneti tu.
Uamuzi huu, ulinishangaza! Wateja wengi na kutoka sehemu
mbalimbali nchini walitupigia simu wakitaka
watumiwe kitabu kwa njia hiyo. Kaka mmoja jina lake la mwanzo Rajab, wa Tarime
hakuamini kama kweli baada ya kutuma sh. 3,000/ kwa njia ya M-pesa angeweza
kukisoma kitabu katika muda usiozidi dakika 5. Aliniambia mwanzoni alikuwa na
wasiwasi labda ni matapeli wa mtandaoni.
Niligundua kitu kimoja, wateja hawapendi shida, hupendelea
bidhaa au huduma waipate katika hali ya
kuvutia, upatikanaji wake uwe rahisi na usiokuwa na vikwazo. Kadiri
utakavyoifanya biashara yako kuwa rahisi kupatikana ndivyo na wateja nao
watakavyokuwa wengi, hali kadhalika na wewe ndivyo utakavyojipatia fedha zaidi.
Urahisi hautumiwi katika
biashara ya vitabu tu peke yake kama nilivyotolea mfano kwa upande wangu, ni
katika kila biashara. Wateja katika biashara ya aina yeyote ile, hiyo ni tabia
yao. Uwe unauza karanga, ubuyu, maji, supermarket, au chochote kile, hakikisha
bidhaa/huduma zako, mteja anakuwa na urahisi katika kuzipata.
0 Response to "WATEJA HUPENDELEA URAHISI"
Post a Comment