JINSI YA KUUZA WAZO LAKO LA BIASHARA AU BUNIFU KWA WAWEKEZAJI NA WATU WENGINE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUUZA WAZO LAKO LA BIASHARA AU BUNIFU KWA WAWEKEZAJI NA WATU WENGINE


Mawazo ya biashara kama kazi zingine zozote zile zinazotumia akili katika kubuni, zina thamani na zinaweza zikauzwa sawasawa kama vile huduma na bidhaa za kawaida zinavyoweza kuuzwa.

Wazo la biashara laweza kuwa ni biashara yeyote ile lakini pia hapa tunatazama wazo la biashara kwa muktadha mpana zaidi tukijumuisha pia na ubunifu wa aina nyinginezo kama vile wa kazi za kisanii pamoja na ugunduzi mbalimbali kwa mfano hata ubunifu wa kisayansi, majina ya biashara, nembo mbalimbali za biashara nk.

Sababu zinazoweza kukufanya uuze wazo lako la biashara au ubunifu ni hizi zifuatazo,
1.  Kubuni na kuliendeleza wazo la biashara kunagharimu rasilimali nyingi ukiwemo muda pesa na hata kujitoa kikamilifu. Changamoto hizo zote zinaweza zikamfanya mtu akaamua ni bora akamuuzia mtu mwingine yeyote yule aliyekuwa tayari kwenda kuliendeleza wazo hilo.

SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara unayoipenda.

2.  Kuanzisha biashara mpya kutokana na wazo jipya ulilolibuni kunaambatana na hatari mbalimbali kama vile, kushindwa kutimiza malengo ya biashara, kufilisika na hata kukosa muda wa kutosha. Hivyo kuepukana na hatari hizo unaweza ukaamua kuliuza wazo lako.

3.  Unaweza pia ukauza ubunifu au wazo lako la biashara kutokana na kukosa maarifa ya kijasiriamali, ujuzi pamoja na nguvu za kiushindani kwenye biashara.

4.  Lakini pia unaweza kuuza wazo lako la biashara ikiwa lengo lako kubwa wakati wa kulibuni lilikuwa ni kupata faida ya haraka na katika muda mfupi.

5.  Ikiwa wewe  shughuli yako rasmi ni ya kuchunguza fursa mbalimbali zilizoko kwenye jamii na kuwaandalia watu, makampuni na wawekezaji mawazo ya biashara, bila shaka ni lazima ubadilishane nao mawazo hayo kwa pesa.

Ili sasa uweze kuuza wazo lako la biashara au ubunifu katika jambo lolote lile ni lazima ufuate hatua hizi zifuatazo.

1.  Tafuta mwanasheria.
Hatua ya awali kabisa ni kumtafuta mwanasheria anayefahamu masuala ya mikataba ya kibiashara na sheria ya hakimiliki, hii ni hatua muhimu sana ikiwa hutaki kuja kujutia hapo baadae. Mwanasheria atakuwa na wewe wakati wa kusaini mikataba, na pia kukusaidia kuchunguza kitaalamu makubaliano yenu ikiwa kama kuna hila zozote na hivyo kukufanya wewe uweze kuwa upande salama zaidi na wenye faida.

2.  Wekea ulinzi wazo/ubunifu wako.
Hatua nyingine ya kufuata hata kabla hujaingia kwenye meza na wawekezaji wako watarajiwa ni ya wewe kuhakikisha kwamba sheria za nchi zinakutambua wewe kama mmiliki halali wa wazo au ugunduzi husika.

SOMA: Kwanini kubuni kitu ni hatari?

Kwa mujibu wa kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, vyombo vinavyohusika na ulinzi wa hakimiliki ya ubunifu wa kiakili kwa hapa Tanzania ni kama vile COSOTA, BRELA na BASATA, vyombo hivi hulinda, hakimiliki ya ubunifu wa kazi za kisanaa, ugunduzi, hatimiliki, majina ya biashara na alama za biashara.

3.  Tathmini na kutambua thamani halisi ya wazo lako.
Ukishatambua wazo lako lina thamani kiasi gani, sasa panga bei utakayoliuza. Thamani ya pesa ya wazo hilo katika soko ni kiasi gani? Na ni jinsi gani utakavyokokotoa thamani hiyo. Unaweza ukamtafuta mtaalamu wa biashara na makadirio au hata wewe mwenyewe unaweza ukathaminisha tu kwa kuangalia fursa ya soko iliyokuwepo kutokana na wazo hilo.

4.  Weka kiwango cha chini cha thamani utakachouza wazo lako.
Kabla hujakaa mezani na mnunuzi wa wazo lako la biashara, na tayari umekwishafahamu thamani ya wazo lako, sasa weka kiwango cha chini cha bei utakayouza, chini ya bei hiyo ni kwamba hautauza kabisa.

Hii itafanya kazi ya kuliuza wazo lako kuwa rahisi kwani unafahamu kwa uhakika ni kitu gani unachokitaka. Kwa mfano tuseme umejiwekeamalemgo kwamba, albamu yako ya nyimbo za injili au nyingine zozote zile kiwango chake cha chini cha kuuza ni shilingi milioni ishirini(20,000,000/=). Ikiwa promota atakupa milioni 18, katu huwezi kukubali, ni lazima iwe ni kuanzia milioni 20 au juu ya hapo.

5.  Chagua ni mfumo  upi mauzo yatafanyika
Mfumo au njia ya mauzo maana yake ni kwamba, utataka ulipwe kupitia mtindo upi?, utapokea pesa taslimu au kwa cheki?, je ni kwa malipo ya papo kwa hapo au ni kwa kupitia mfumo wa mrahaba?. Hilo litategemea zaidi wewe na mnunuzi wako mtakavyokubaliana.

6.  Tambua malengo yako.
Unaweza kujikuta unaingia katika majadiliano ya mkataba na watu wajanja watakaokupa ahadi tamu tamu zisizoweza kuja kutekelezwa kamwe kusudi tuwewe uweze kukubali kuuza wazo lako na hili limewahi kuwakuta watu wengi hapa Tanzania hasa watunzi wa kazi za kisanii kama muziki na filamu. Kabla hujaingia kwenye meza ya majadiliano, fahamu kabisa malengo yako ni nini, jua kile unachokihitaji na usiyumbeyumbe.

7.  Watambue kabla wanunuzi wako watarajiwa.
Hatua ya saba ya kuuza wazo la biashara au ubunifu wako ni kuwatambua kwanza wanunuzi wako watarajiwa, makampuni, wawekezaji, au hata watu binafsi waliokuwa na uwezekano wa kununua wazo hilo. Kisha waorodheshe wote katika karatasi.

SOMA: Kufanya utafiti wa soko la biashara yako.

8.  Andika na utume kwa kila mteja mtarajiwa andiko la biashara la mapendekezo yako.
Ukisisitiza zaidi faida na mambo ya kimsingi ya wazo hilo, kikubwa hapa ni wewe kuuza faida za wazo lako kuamsha hisia za mvuto wa wazo lako kwa wanunuzi watarajiwa.

9.  Kutana na wanunuzi watarajiwa walioonyesha kuvutiwa.
Ikiwa wazo lako linaonekana lina fursa ndani yake wanunuzi watarajiwa watakaovutiwa nalo watawasiliana na wewe na kufanya majadiliano ya biashara na wewe lakini kumbuka usisahau kufanya hivyo chini ya mwanasheria wako. Pia usionyeshe papara yeyote na kama unaona hutaweza kujadiliana vizuri unaweza hata ukamchukua mtu mwingine mwenye ujuzi zaidi.

10.      Uza wazo lako au hamia kwa mnunuzi mwingine aliyevutiwa.
Ikiwa mambo yatakwenda kama yalivyo tokea hatua ya kwanza mpaka ya 9, basi unaweza ukauza wazo lako. Ikiwa siyo, usipoteze muda wako nenda tena kwa mnunuzi mwingine aliyeonyesha dalili za kutaka kununua, kumbuka hapa una orodha ya wale wanunuzi watarajiwa ulioandika kwenye karatasi.
……………………………………………………………………......

Ndugu msomaji wa blogu hii, ikiwa unapenda kujifunza kwa kina kabisa kuhusiana na kuanzisha na kuendeleza biashara yeyote ile, jipatie kitabu hiki cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI kwa bei ya shilingi 20,000/= hardcopy  au shilingi, 10,000/= softcopy


Pia tuna vitabu vingine 2, vifuatavyo,

MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA Tsh. 10,000/=hardcopy na sh. 5,000/=softcopy




MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA Tsh. 5,000/=hardcopy na sh. 3,000/=softcopy.


Wasiliana nasi kwa namba za simu 0712 202244  au 0765 553030


Tunayo pia MASOMO YA SEMINA ya jinsi ya kuandika michanganuo ya biashara kwa njia ya e-mail na blogu maalumu, kiingilio ni Tsh. 10,000/=

0 Response to "JINSI YA KUUZA WAZO LAKO LA BIASHARA AU BUNIFU KWA WAWEKEZAJI NA WATU WENGINE"

Post a Comment