USIOGOPE, MABADILIKO YA MAISHA NI KAMA PLASTA IKISHABANDUKA KIDONDA HUPOA CHENYEWE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

USIOGOPE, MABADILIKO YA MAISHA NI KAMA PLASTA IKISHABANDUKA KIDONDA HUPOA CHENYEWE

Kuna wakati unaweza kukabiliwa na uchaguzi mgumu, uamue kati ya mambo mawili ambayo yote yanakuogopesha na kuona kila moja baadaye unaweza ukakabiliwa na matokeo mabaya katika maisha yako. Mara nyingi watu huamua kubaki vilevile walivyo na maisha waliyoyazoea huku wakiahirisha uamuzi muhimu juu ya mustakabali wa maisha yao.

Vipindi hasa vya mwaka mpya unapoanza kama sasa hivi 2017, mara nyingi ndiyo muda muafaka kwa mtu kujichunguza kama kuna jambo lolote maishani mwako ambalo linahitaji kufanyiwa maamuzi muafaka lakini ukawa unasitasita kwa muda mrefu ukihofia kufanya maamuzi(mabadiliko) kwa madai kwamba pengine mabadiliko hayo yanaweza kukuletea balaa zaidi kuliko ambavyo ulikuwa ukiishi zamani.


Kama binadamu tuna mambo mengi tunayoweza kuhitaji kuamua au kufanyia mabadiliko, kwa mfano unaweza ukawa unaishi maisha magumu pengine kwasababu tu kazi unayoifanya hailipi, mshahara ni kidogo nk. maisha na mafanikio kwako unayaona yatabakia kwa muda mrefu kuwa ndoto kwa sababu tu ya biashara uliyokuwa ukiifanya zamani na ambayo mpaka leo hii unaendelea nayo haikupi faida ya kutosha, ni ngumu, haina wateja wa kutosha, ama ni biashara isiyokua kimtaji.

Kimsingi, ugumu wa maisha hautokani tu na maisha tuliyokuwa tukiishi na ambayo tunaendelea nayo mpaka sasa, bali hutokana hasa zaidi na ugumu wa akili zetu kukubali kubadilika.

Sasa Ikiwa Suluhisho Ni Kubadilika, Mbona Watu Huwa ni Wagumu Hivyo Kubadilika?

Sababu kubwa ni kwanini watu huhofia mabadiliko, wakati kubadilika ndiyo suluhisho ni kwamba, watu wanaogopa mno matokeo mabaya yanayoweza kutokea baada ya kubadilika. Kuna mifano mingi sana. Jamaa mmoja yeye anafanya biashara ya kuuza samaki kwa miaka mingi sasa. Lakini kutokana na kuishi mbali mno na Feri(anaishi Kibaha Kongowe) faida karibu yote ya biashara yake huishia njiani kama nauli na ana familia kubwa inayomtegemea.

Watu walimshauri na hata yeye mwenyewe kufikiria kuachana na biashara ya samaki na kuanzisha biashara ya kuuza mkaa ambao huupata karibu na eneo analoishi. Bwana huyu mpaka dakika hii ninapoandika hapa hajaweza kuamua kuachana na samaki japo kila siku husikika akilalamika haimlipi. Anazeeka na biashara ile wakati fursa za biashara nyingine zipo nyingi na zinaendelea kuzaliwa kila leo.

SOMA: Unaijua siri hii ya kufanikisha biashara yako?

Wasiwasi wake mkubwa ni kwamba , Je, akiacha biashara ya samaki aliyoizoea kwanza watu waliomzunguka watamfikiria vipi?, familia itaishije siku atakazokuwa akiiboresha hiyo biashara mpya?, je, na kama hiyo biashara mpya haitaleta faida atafanyaje?.

Kifupi ni kwamba jamaa huyu anajijengea mwenyewe mazingira ya kwamba kuachana na biashara yake ya zamani isiyomlipa vizuri na kuingia biashara mpya asiyokuwa na uhakika nayo kisha kwa bahati mbaya ikaja kuyumba, itakuwa kwake kama ndiyo mwisho wa dunia vile. Anahisi kama hakuna tena kitu kibaya kwake maishani kama hicho.


Uamuzi wake wa kuachana na biashara ya samaki na kuanza biashara nyingine itakayompa uhuru kifedha na kimaisha ungeliweza kuwa rahisi tu kama asingelifikiria zaidi mambo mabaya(hasi) yanayoweza kuja kutokea. Lakini ukweli ni kwamba suala la matokeo wala haliwezi likawa na uzito kiasi hicho, hebu fikiria ni mara ngapi katika maisha yako uliwahi kuona kabisa sasa huna tena pa kutokea lakini muda ulipofika ukashangaa mambo yamepita salama?

Hata ulipokuwa shule ya msingi au sekondari, hebu kumbuka ulipofanya kosa kubwa, wakati unasubiri siku ya jumatatu paredi(mstarini) uitwe mbele na mwalimu mkuu na kupewa adhabu kali ya viboko, unashangaa siku hiyo wala mwalimu mkuu mwenyewe hatokei shuleni, unasikia eti mara amesafiri kikazi na wala hupewi tena adhabu yeyote, mambo yanayeyuka kimyakimya. Maisha ndivyo yalivyo. Sasa hebu niambie, ingelikuwaje kama ungeliamua kujinyonga kwa hofu?

Watu wengi huamua kwa woga kuendelea kuvumilia, huku wakifanya vitu/shughuli zisizowaridhisha hata kama zitagharimu muda wote  wa maisha yao badala ya kuamua kubadilika na kufanya vile vitu wanavyovipenda maishani na vilivyo na uwezo wa kuwapa faida zaidi.

Unapoamua na kujitoa kiukwelikweli, ukajiambia “sasa basi inatosha, mimi ninao uwezo wa kukabiliana na chochote kile kitakachojitokeza mbele ya safari yangu hii ya mabadiliko kutoka hali duni niliyokuwa nayo zamani(kazi au biashara)”. Hakika kweli utakuwa umefanya uamuzi wa busara na hakuna lolote lile baya litakalokupata, na hata kama ikiwa hautafanikiwa kwenye hiyo biashara au kazi yako mpya, MAISHA YATAENDELEA TU WALA HAUTAKUWA NDIYO MWISHO WA DUNIA.

Mabadiliko ni kama vile unavyofungua plasta kutoka katika kidonda ambacho bado ni kibichi hakijapona sawasawa, panauma ghafla kwa nguvu lakini plasta ikishabanduka tu, unapata ahueni na mambo yanakwenda kama kawaida

Maisha mtu unaishi mara moja tu, na sidhani kama ungependa miezi 12 ijayo uje useme tena, “laiti ningelijua, ningelifanya hivi au vile. Fanya leo, fanya sasa hivi, wakati ndiyo huu.

Hebu nikupe zoezi kidogo ambalo hata na mimi nalifanya sasa hivi na nitakupa mrejesho wangu baadae hapo chini kwenye sehemu ya maoni.

1.  Chagua jambo moja ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikuumiza kichwa chako kufanyia maamuzi, jambo lolote lile, laweza hata kuwa ni kazi, biashara, eneo unaloishi, matumizi ya kileo, kufanya ibada, kuachana na nyumba ndogo/mchepuko nk. Amua kufanya mabadiliko/maamuzi sasa hivi kabla hata haujamalizia kuisoma makala hii.

2.  Ukiweza, weka maoni yako hapo chini kwenye kisanduku cha maoni, ukitueleza kuwa unakwenda kubadilika sasa hivi. Siyo lazima uweke jina lako hapo au utambulisho wako wowote ule, unaweza kutumia ‘Anonymous’

3.  Kitu kingine muhimu ni kwamba, kama makala hii ina kitu chochote kile chenye manufaa kwako, tafadhali, ingekuwa jambo jema sana kama ukimshirikisha/ukiwashirikisha na wale wote unaowajali kupitia mtandao wa kijamii wowote ule iwe ni facebook, twitter, google nk. Usisahau pia kuwajuza kuhusiana na kampeni yetu inayoendelea ya,

 #JIRUDISHIEUKUUWAKOTENA au #MAKEYOURSELFGREATAGAIN

Ukihitaji vitabu vyako vya biashara na Ujasiriamali kwa lugha ya Kiswahili, usisite kutembelea ukurasa ufuatao, >>SMARTBOOKSTZ

Mhamasishaji na mwandishi wako,

Peter A. Tarimo

0712 202244
0765 553030


0 Response to "USIOGOPE, MABADILIKO YA MAISHA NI KAMA PLASTA IKISHABANDUKA KIDONDA HUPOA CHENYEWE"

Post a Comment