MUHAMMAD ALI: UVUMILIVU, NIDHAMU, UJASIRI, MSIMAMO VILIMPA UBINGWA KINSHASA ZAIRE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MUHAMMAD ALI: UVUMILIVU, NIDHAMU, UJASIRI, MSIMAMO VILIMPA UBINGWA KINSHASA ZAIRE

Kuna vitu kadhaa mjasiriamali yeyote yule anayetaka kufanikiwa kimaisha anavyoweza akajifunza kutoka kwa bingwa mweusi mashuhuri zaidi wa ngumi aliyewahi kutokea Duniani na mwanamichezo wa karne ya 20. 


Roho ya kutokukata tamaa kamwe, uvumilivu, Nidhamu ya hali ya juu na Ujasiri vilimfanya Muhammad Ali kuvishinda vikwazo nje na ndani ya ulingo. Vikwazo vya kubaguliwa, kuchukiwa, kudharauliwa kwa sababu ya rangi na dini hasa na watu weupe.
Muhammad Ali wakitaniana na bondia mwenzake Nelson Mandela walipokutana mwaka 2005. Mandela aliwahi kuwa bondia zamani.
Muhammad Ali alipoanza mazoezi miaka ya 50 alikuwa ni mtu mwenye nidhamu ya hali ya juu kwenye mazoezi yenyewe, chakula alichokula, na hata kwa waalimu waliomfundisha. Aliweza kujizuia kunywa pombe, kuvuta sigara na vyakula vya mafuta mengi na sukari ambavyo alikuwa akivipenda. Nukuu yake maarufu inasema hivi;

“Yeyote yule asiyekuwa na Ujasiri wa kutosha kuchukua hatari, kamwe hataweza kufanikisha chochote maishani.”- Muhammad Ali

Ingawa Muhammad Ali alichukiwa sana na jamii hasa ya watu weupe, lakini mwishowe baada ya kushinda mataji ya ngumi ya Dunia mara tatu mfululizo,  kila mtu alikuja kumkubali na huu ni uthibitisho kwamba; 

“Mtu yeyote yule anaweza kuwa chochote kile anachotamani kuwa, endapo tu ataweka jitihada za kutosha na wala haijalishi ana imani gani, kabila gani au ni rangi gani, kila kitu kinawezekana chini ya jua”- Peter

Raisi Barack Obama akitoa salamu zake za rambirambi baada ya kifo cha Muhammad Ali hapo siku ya tarehe 3 june 2016 akiwa na umri wa miaka 74, Obama alitamka maneno yafuatayo;

“Muhammad Ali alikuwa Mkuu….mtu aliyetupigania. Alisimama na akina King na Mandela kipindi kilichokuwa kigumu, akiongea pale wengine waliposhindwa kuongea. Mapambano yake nje ya ulingo yalimgharimu taji lake na msimamo wake hadharani. Yaliweza hata kumjengea maadui kulia na kushoto, na hata kukaribia kumpeleka jela. Lakini Ali alisimama kidete, na ushindi wake umetusaidia kuwa na Marekani tunayoiona leo.”- Barack Obama.


Kama ilivyokuwa kwa binadamu mwingine yeyote yule, hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro na shilingi ni lazima iwe na pande zote mbili, Muhammad Ali hakuwa mkamilifu alikuwa na mapungufu yake, kubwa likiwa ni tabia yake ya kuwatukana maadui zake na kuwatolea maneno makali hata pale alipokuwa ulingoni. Hata hivyo, ubaya wake wote huo ulifunikwa kabisa na mazuri aliyoyafanya huku maadui zake wengi wakijikuta wanakuwa mashabiki wake wakubwa. 

Hata miaka yake ya mwisho aligeuka na kuwa balozi mkubwa wa amani na maridhiano duniani kote baina ya pande zote zinazokinzana siyo tu katika siasa bali na katika imani, dini na matabaka mbalimbali.   

Pambano la ngumi za uzito wa juu mashuhuri zaidi Duniani kati ya Muhammad Ali na George Foreman Kinshasa nchini Zaire Congo(DRC) “Rumble in the jungle” mwaka 1974.

Muhammad Ali akimwangusha chini Foreman.
Baada ya kuona sifa zilizomfikisha Muhammad Ali kileleni sasa tuone pambano mashuhuri na lililokuwa na umuhimu mkubwa hasa kwa bara letu la Afrika kutokana na sababu kwamba lilipiganwa katika ardhi yetu ambayo pia ndiyo asili ya Muhammad Ali mwenyewe. Pambano lilifanyika iliyokuwa Zaire ya zamani sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo chini ya Rais Mobutu Seseseko.

Pambano la ngumi kati ya mfalme wa ngumi Duniani, Muhammad Ali na George Foreman(Ramble in the Jungle) lililofanyika jijini Kinshasa Zaire(Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo sasa) mwaka 1974 ndilo pambano la ngumi la uzani wa juu mashuhuri zaidi kuwahi kufanyika Duniani.


Sababu za pambano hilo kuwa mashuhuri kiasi hicho zinatokana na ukweli kwamba lilikuwa ni baina ya mabondia wawili mashuhuri na ambao sifa zao zilitofautiana. Foreman akionekana kama mzalendo aliyekuwa ametoka kuliwakilisha Taifa lake katika michuano ya Olimpiki na kurudi akiwa na medali ya dhahabu, huku Muhammad Alli yeye akichukuliwa kama bingwa mweusi ambaye alikuwa amegadhabishwa mno na tabia ya watu weupe ya kuwadharau na kuwabagua watu weusi.

Sababu hizo ndizo hata zilizomfanya Muhammad Alli ambaye hapo awali alijulikana kama Cassius Clay kubadilisha dini kutoka Ukristo kwenda Uislamu. Hadi kufikia katikati ya mwaka 1974, Muhammad Alli alikuwa ameshawapiga mabondia wote wa uzani wa juu na sasa pambano lake hili na Foreman alitaka aendelee kuwa bingwa. Kwa upande wa mafanikio katika kipindi hicho basi angeweza kuwa wa pili baada ya Floyd Patterson.


Madai ya meneja wake kutaka bondia wake Muhammad Alli alipwe jumla ya dola million tano yalimshitua sana mdhamini wa pambano hilo Don King ambaye hapo kabla hakuwa amewahi hata siku moja kudhamini pambano la pesa nyingi kiasi hicho. Hata hivyo Don King aliahidi kufanya kila lililowezekana kuzipata pesa hizo.

Kwa kutumia ujanja na mbinu mbalimbali katika mkanda wa video alioutuma kwa aliyekuwa Raisi wa Zaire, Dikteta Mobutu Seseseko, alifanikiwa kumshawishi mpaka akakubali kutoa dola milioni 10 ambazo zilitosha kuwalipa mabondia wote wawili. Kiasi kingine kilichobakia kufanikisha pambano hilo ilitoa kampuni moja ya Kiingereza.
Mobutu akiwa na Muhammad Ali 1974 jijini Kinshasa.
Mobutu ni mtu aliyependa sana sifa na kwa hivyo aliliona pambano lile kuwa lingeitangaza nchi yake na yeye mwenyewe Dunia nzima. Tabia yake ya kuutukuza Uzungu ilimfanya aibatize Zaire “Ubelgiji ya Congo”. Kuna wakati aliwahi kuwafungia wahalifu 300 katika uwanja mmoja wa michezo kisha akaamuru wauwawe 50, na waliosalia waachiwe wakawasimulie raia wengine. Kwa mtindo wake huo, Zaire ilifikia mahali ikawa na kiwango cha chini sana cha uhalifu.

Tukirudi katika pambano, Foreman alikuwa ni bondia mwenye uwezo mkubwa, katika raundi za pili tu za mwanzo, alikuwa ameshawatoa  kwa ‘Knok out’ wapinzani wake mara 8; na kati ya mapambano yake 40 alikuwa ameshashinda 37.

Muhammad Alli baada ya kujiandaa vilivyo kambini kwake huko Pennisylvania, alisafiri na kuwasili Zaire wiki mbili kabla ya mpambano kusudi apate muda wa kutosha kuyazoea mazingira. Alichagua nyumba iliyokuwa maeneo ya nje kidogo ya jiji la Kinshasa kama kilomita 40 hivi.

Foreman pamoja na wapambe wake, wao walichagua nyumba eneo katikati ya jiji la Kinshasa. Kutokupendelea kwake kutembelewa na wageni wasio rasmi kulimfanya amuweke mbwa getini wa kulinda. Muhammad Alli kwa upande wake aliitumia kila fursa aliyoipata kuwa karibu na watu akidhihirisha mapenzi yake kwa Uafrika.

Kila alikoenda alizungukwa na kundi kubwa la watu. Siku nne kabla ya pambano Foreman aliumia juu ya jicho lake ikabidi pambano liahirishwe mpaka  Oktoba 30, jambo lililosababisha kuwe na tetesi kuwa Mobutu alikuwa amewazuia kuondoka nchini humo.

Hatimaye Foreman alipona na “miamba” hao wawili wakaingia ulingoni mwezi Mei 20 1974 majira ya saa 10 za usiku za huko Afrika ya Kati. Ulipangwa muda huo kusudi uweze kuendana sawasawa na muda wa jioni kule Marekani ambako watu walikuwa wakisubiri kwa shauku kubwa kuushuhudia  mpambao huo wa kukata na shoka katika televisheni zao.

Uzito wa Foreman uliuzidi ule wa Muhammad kwa paund kadhaa, kabla ya raundi ya kwanza kuanza watu walikuwa wakiimba kwa vifijo nyimbo za kumshangilia  Muhammad Alli, walitamka maneno “Boma Yee……” Wakimaanisha , “Alli muue Foreman…..!”

Katika raundi ya kwanza Muhammad Alli aliachia makonde mfululizo akitumia mikono yote miwili, staili ambayo kwa kawaida mabondia huitumia mwishoni mwa mchezo mpinzani anapokuwa ameshachoka.

Mbinu hiyo ilizaa matunda lakini hata hivyo Foreman naye akajibu mashambulizi kwa kurusha makonde kadhaa ya nguvu. Katika raundi ya pili, Foreman alimkimbiza Muhammad na kumlazimisha arudi hadi kwenye kona.
Muhammad ali akiwa kwenye kona.
Muhammad pale kwenye kona aliamua kubadili mbinu na kuanza kubakia kwenye kamba muda wote. Aliiegemea kamba kwa nyuma jambo lililomfanya Foreman amfuate, Muhammad alirudi mbele na kumpa kipigo tena na tena.

Katika dakika za mwisho za raundi hiyo, Muhammad alikuja juu kwa kasi ya ajabu na kuutikisa kwa makonde mazito mwili wa Foreman uliokuwa umeshaanza kuchoka.

Raundi za sita na saba zilienda taratibu huku Foreman akijaribu bila mafanikio kumtoa Muhammad kwa ‘knok out’. Karibu na mwishoni mwa raundi ya nane Muhammad alikusanya nguvu zake zote na ujasiri, akajitayarisha kurusha ngumi ya mkono wa kushoto!  Kila mtu alifikiri lile ndilo lingekuwa shambulio la mwisho.

Badala yake, Muhammad aliachia ngumi ya mkono wa kulia iliyomwacha Foreman na kamba ya ulingo wakigaagaa kwa mpepesuko.


Muhammad alimpokelea kwa mikono yote miwili huku akimimina makonde mfululizo, akiitumia ile staili aliyokuwa ameanza nayo katika raundi ya kwanza.

Konde moja zito lilitua sawia katikati ya paji la uso wa Foreman likamfanya aruke kwa kupepesa mikono mithili ya “parachute” linapochomoka ndani ya ndege inayotaka kuanguka.

SOMA: Mabuti ya Nelson Mandela aliyosahau Tanzania mwaka 1962 haya hapa.

Washangiliaji walishikwa na uwendawazimu! Muhammad Alli alikuwa ameshinda tena kwa mara ya pili ubingwa wa Dunia wa ngumi za uzito wa juu kwa staili iliyowaacha watu hoi na kuwastaajabisha.
Muhammad ali baada ya kumshinda Foreman kwa ‘KO’.
Dakika moja baadaye Mbingu zilimimina mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo na radi. Mvua hiyo kama ingelikuwa imenyesha kabla ya pambano ingelilazimu liahirishwe tena.


Vyanzo: Tovuti na mitandao mbalimbali.

0 Response to "MUHAMMAD ALI: UVUMILIVU, NIDHAMU, UJASIRI, MSIMAMO VILIMPA UBINGWA KINSHASA ZAIRE"

Post a Comment