MAMA HUBEBA WATOTO WAO KIPINDI KIFUPI LAKINI MIOYO YAO HUWABEBA MILELE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAMA HUBEBA WATOTO WAO KIPINDI KIFUPI LAKINI MIOYO YAO HUWABEBA MILELE

Ikiwa leo ni siku ya mama duniani, watu wengi katika nchi nyingi duniani wamekuwa wakiwakumbuka mama zao, upendo waliokuwa wakiwaonyesha walipokuwa wadogo mpaka hata sasa hivi ukubwani pamoja na kujitoa hata pale kulipokuwa na hatari kubwa kiasi gani.

Siyo kama kina baba hawana upendo kiasi hicho kwa watoto wao, lakini kusema ule ukweli kina mama ndiyo waliokuwa na dhamana kubwa zaidi pengine kutokana na kazi ya ulezi kuwa inafanywa na wao zaidi na muda mwingi hujikuta wakiwa na watoto hasa wanapokuwa wadogo.

Nakumbuka sana mama yangu mzazi tukiwa wadogo alikuwa mara kwa mara akitusimulia jinsi ambavyo kitendo cha yeye na baba kutaka kuachana kilivyokuwa kigumu kutokana na kufikiria suala la watoto wake ambao ni sisi. Anasema kuna nyakati walifikia hatua ya kuachana baada ya kutokuelewana lakini alipowaza juu yetu watoto na kututazama tulimtia huruma mno kiasi cha kuahirisha uamuzi wake.


Wazazi wote mama na baba wana umuhimu wa kipekee kama mwanamuziki huyu hapa chini, mwanamama Doly Parton alivyoimba katika kibao chake hiki maarufu katika mtindo wa Country, “I remember mama and Daddy most of all” akimaanisha “Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote”.

Kwa heshima ya siku hii ya mama nimeyatafsiri mashairi ya wimbo huo yote kuanzia mwazo hadi mwisho katika lugha ya kiswahili, pamoja na kuweka audio na video ya wimbo huo.


Popote pale ulipo ukihangaika na maisha, iwe unafanya ujasiriamali, au hata umeajiriwa mahali, wazazi hasa mama ni watu wa kukumbuka sana. Inawezekana kiuchumi hali yako ni duni unashindwa kuwapa chochote lakini walao chukua muda kuwatafakari na kuwaenzi moyoni mwako. Na wala haijalishi kama wameshatangulia mbele za haki au bado wapo hai.

Audio ya wimbo Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyoteVideo ya wimbo Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Mashairi ya wimbo, "Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote" wa 'Dolly Parton'.

Nawakumbuka Nawakumbuka Nawakumbuka mama na baba zaidi ya kitu chochote.

Nayakumbuka  malisho na mashamba ya ngano ya dhahabu.

Nawakumbuka ndege waimbao na miwa mitamu mno

Nakumbuka vitu vingi sana ambavyo mara nyingi hujirudia akilini

Lakini namkumbuka mama na baba zaidi ya vyote

Naukumbuka mkate wa tangawizi, aliokuwa akioka mama yangu

Na naikumbuka midoli ya kutengenezwa nyumbani, ambayo baba alikuwa akitengeneza.

Ndiyo nakumbuka vitu vingi, ambavyo hujirudia akilini mara kwa mara.

Lakini nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Na nyumba yetu ndogo kijijini, walijawa na upendo.

Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Na vitu vyote walivyofanya, kufanya maisha yawe ya furaha kwetu.

Ndiyo nakumbuka vitu vingi sana ambavyo hujirudia akilini mara kwa mara.

Lakini nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Nakumbuka peremende baba alizokuwa akileta, nakumbuka nyimbo mama alizokuwa akiimba.

Oh nakumbuka vitu vingi, ambavyo hujirudia akili mara kwa mara.

Lakini nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Na jinsi walivyokuwa wakitufunza sisi watoto, yaliyokuwa mema na mabaya.

Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Jinsi walivyotumaini na kusali, kusudi waishi watuone tukikua.

Oh nakumbuka vitu vingi ambavyo hujirudia akilini mara kwa mara.

Lakini nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote.

Nawakumbuka, Nawakumbuka, Nawakumbuka mama na baba zaidi ya vyote, zaidi ya vyote.
 .................................................................................................

0 Response to "MAMA HUBEBA WATOTO WAO KIPINDI KIFUPI LAKINI MIOYO YAO HUWABEBA MILELE"

Post a Comment