UJIO WA MABILIONI YA MAGUFULI: MJASIRIAMALI UMEJIANDAAJE? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UJIO WA MABILIONI YA MAGUFULI: MJASIRIAMALI UMEJIANDAAJE?

Ngugu  msomaji wa makala hii na mjasiriamali, hivi unayakumbuka yale mabilioni ya Kikwete aliyogawa kwa wajasiriamali kipindi kile alipokuwa akiingia madarakani awamu yakeya kwanza?. Ni vipi uliweza kunufaika na mabilioni hayo? Ulifanikiwa kupata japo sehemu ya fedha hizo?. Na je ikiwa Rais mpya Dr. John Pombe Magufuli ataamua naye kutoa fedha Mamilioni au hata Mabilioni kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake hebu niambie, umejiandaa vipi kuyapata mapesa hayo?
Magufuli, Kikwete na sera za kuwawezesha vijana na wanawake kwa mabilioni

Kama ulikuwa pengine kwa bahati mbaya hukufanikiwa kupata habari za mabilioni hayo kwani naamini kabisa kuwa, wapo watu hata hawakuwa na fununu kwamba kulikuwa na mabilioni yaliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwe kila Mkoa Tanzania Bara shilingi bilioni moja, na Tanzania visiwani shilingi milioni 6 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali hasa vijana waliokuwa katika vikundi kujikwamua na umasikini, sembuse kuambulia kuzipata pesa hizo, basi leo utapata kujua kila kitu kuhusiana na fedha hizo.

Kwa upande wangu binafsi, baada tu ya kupata habari za ujio wa mabilioni hayo ya Kikwete kipindi hicho, nilipata hamasa kubwa nikajua sasa mambo yangu yatanyooka na kuwa safi muda si mrefu. Hata mkopo kutoka taasisi moja ndogo niliokuwa nafuatilia kwa ajili ya biashara yangu ndogo, nilipunguza ‘spidi’ ya ufuatiliaji niliyokuwa nayo nikijua sasa, naenda kupata mkopo wenye masharti nafuu. Hakukuwa na masharti magumu kama vile, kuweka dhamana nyumba, kadi ya gari au mdhamini mwenye nyumba nk. Ila nakumbuka sharti moja lililokuwa gumu kwa watu wengi mpaka ikafika mahali wahusika wakaamua kuliondoa lilikuwa ni sharti la mtu kuandaa Mpango au mchanganuo wa biashara unayotaka kwenda kuendeleza.

Sharti hili lilionekana kuwa kikwazo kwa watu wengi baada ya karibu kila mjasiriamali aliyezihitaji pesa zile kuanza kuzunguka huku na kule kutafuta wataalamu wanaoweza kuandika michanganuo ya biashara. Pesa zilikabidhiwa kwa baadhi ya mabenki ili wazigawe, ikiwemo benki ya NMB nadhani na CRDB kama sikosei na benki zingine kadhaa. Mimi nilifunga safari mpaka benki ya NMB pale Ilala boma nikamuuliza afisa mmoja aliyenikatisha tama kabisa.

Nilifahamishwa kuwa fedha zile zilikuwa zimeshamalizika kitambo na walikuwa wakisubiri awamu nyingine. Cha kushangaza mimi sikuona kama ulikuwa umepita muda mrefu tangu mchakato ule uanze, sasa kwanini ziishe mapema kiasi kile?. Lakini jamaa mmoja niliyekutana naye mtaani aliniambia kuwa fedha zile zilikuwa sawa na tone moja la maji katika bahari kubwa kutokana na sababu kwamba Tanzania ni kubwa na hata kwa mfano kikwete angesema kila raia apate mgawo basi kwa idadi yote kila mwananchi angeliambulia wastani wa shilingi elfu moja(1000) pekee. Kwa kweli kiherehere changu chote kiliishia pale NMB ilala, sikuja kuzifuatilia tena!

Tanzania Bara kila mkoa ulipewa pesa kiasi cha sh. Bilioni moja wakati Tanzania visiwani wao walipewa sh. Milioni sita(6) kwa ujumla, ukichanganya na nyingine sh.milioni 6 iliyotoa serikali ya Mapinduzi ya Zanziba zinakuwa jula shilingi Bilioni 1.2 kwa visiwani.

Jumla ya fedha zilizotolewa zote ni karibu shilingi bilioni 43.7  na wajasiriamali walionufaika walikuwa elfu 74.5 tu. Hapo ni jinsi gani unaweza kuona pesa hizi zilikuwa kidogo kiasi ambacho ni watu wengi walihisi zilikuwa ni kiini macho kwa kutokuonekana wazi zilikokwenda. Lakini pia kulikuwa na changamoto kubwa ya urasimu pamoja na kutokuwajibika kwa wale waliopewa dhamana ya kuzigawa kwa wananchi.

Mfano mmoja wapo ni Rais Jakaya mwenyewe pale alipoagiza kukutanishwa na angalao watu wawili au watatu walionufaika na mikopo yake hiyo katika kila Wilaya ili kujiridhisha kama kweli walikuwa wananufaika  alipokuwa akifanya ziara mikoani “Nia yangu ni kuthibitisha, “to demonstrate”, kuwa mikopo hii inakuwa na tija” Alisema Rais Kikwete alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kilombero mwaka 2008.

Kama hiyo haikutosha, Rais Jakaya Kikwete tena hapo mwaka 2009, baada ya kuchoshwa na malalamiko ya wananchi juu ya mabilioni yake hayo, alitaka arejeshewe fedha zake hizo alizozitoa kwa ajili ya kuinua maendeleo ya wananchi ikiwa zilikuwa hazijafanyiwa kazi kama ilivyokuwa imekusudiwa. Hayo aliyasema alipokuwa akitembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara(BET) ya 33.

"Fedha hizo ni zangu kama mmeshindwa kuzizungusha kwa wananchi naomba mzirudishe kwa kuwa nilizitoa kwa nia ya kuwasaidia wananchi wangu ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha," Alisema Rais Kikwete na kuongeza kwamba madhumuni ya kutoa fedha hizo yalikuwa ni kuwasaidia wananchi wake pamoja na kuleta tija kwa maendeleo ya nchi na wala siyo watu wachache jambo ambalo limekwenda kinyume na utaratibu.

Inasemekana mpaka Kikwete anaondoka madarakani fedha hizi bado nyingine zilikuwa hazijagawiwa kwa wananchi, hata hivyo pia wananchi wenyewe kwa upande wao, hawakupenda kuzirejesha pesa hizo, mfano ni pale mwanzoni mwa mwaka huu Wabunge walipohoji juu ya fedha hizo na serikali kujibu kuwa, baadhi hazijagawiwa na waliogawiwa wengi hawajazirudisha na idara ya ukaguzi wa ndani ina mpango wa kufanya ukaguzi kujua ni kina nani waliokopeshwa ili ichukue hatua stahiki.

Mimi binafsi katika uchunguzi wangu mtaani, nilifanikiwa kuzungumza na kijana mmoja aliyechukua mkopo akiwa Wilayani Kibaha, anajitapa kuwa hakuna hela aliyoifaidi kama ile ya Mabilioni ya JK kwani hakuona umuhimu wa kuzirejesha; kwanza kutokana na kuwa zilitolewa na serikali, pili anasema hata watu wa benki wenyewe hawajawa na msukumo wa kuzifuatilia kama ilivyokuwa kwa fedha zingine. Kwingineko anasema hata maafisa wenyewe wa benki huwahamasisha waliochukua mikopo hiyo kutokurudisha kwa maslahi wanayoyajua wao wenyewe.

Ikiwa hali yenyewe ndiyo hiyo basi, Ujio mwingine wa Mabilioni ya Dr. Magufuli, Mjasiriamali Umejipanga vipi?

Hakuna ajuaye ikiwa Rais mpya Dr. John Pombe Magufuli atakuja na sera gani juu ya kuwawezesha wafanyibiashara wadogowadogo hususani vikundi vya akina mama na vijana, lakini ni lazima atakuwa na mpango wake. Hata kama hatakuja na utaratibu mpya lakini kama tulivyoona katika makala haya bado yale mabilioni aliyotoa Kikwete mengine hayajagawiwa.

Usisubiri mpaka usikie wanaanza kugawa ndipo uanze kukimbia kimbia kutafuta wataalamu wa kukuandikia mpango wa biashara kama wengi walivyofanya kipindi cha JK.

Naandika kama utani vile, lakini ndugu yangu baadaye haya yanaweza yakaja kuwa na maana. Hebu tu, hata pasipo kuwa na mawazo ya mabilioni ya Magufuli kichwani, tafakari na kujiuliza ikiwa utapata mtaji labda kuanzia milioni kadhaa(  ) kutoka mahali popote pale, mpango wako ni nini?, utafanya biashara gani?. Jaribu kutengeneza picha ya mchanganuo kichwani mwako ni jinsi gani utakavyozitumia fedha hizo kujikwamua na umasikini.

Hapa namaanisha kuwa muda wote kuwa “updated” kuhusiana na maswala yahusuyo pesa, kuwa na elimu sahihi juu ya fedha, haikuhitaji wewe kukaa darasani tena, kwani siyo lazima.

Unaweza ukapata ufahamu huo kwa njia mbalimbali mbadala na moja wapo ni kama hivi unavyosoma kupitia blogu hii. Njia nyingine ni semina na makongamano mbalimbali, na vilevile unaweza ukasoma vitabu mbalimbali na napendekeza ikiwa utahitaji vitabu basi usikose vitabu kutoka kampuni ya "SELF HELP BOOKS TANZANIA LIMITED", wana vitabu vizuri, mfano ni kitabu kilichobeba kila kozi ya ujasiriamali ndani yake na kwa ubora wa hali ya juu, yaani ni kila kitu ndani ya kitabu kimoja, “JIFUNZE UJASIRIAMALI NA MICHANGANUO YA BIASHARA hautajutia pesa yako kamwe.

Wana kitabu pia “online book” ambacho unaweza kukinunua hata dakika hii hii unaposoma hapa, “Miferejiya Pesa”. Cha kufanya tu ni kwambba, unatuma sh. 3,000/- kwenye namba hizi, 0712 202244 au 0765 553030 pamoja na meseji yenye anuani ya barua pepe yako(e-mail address). Na kisha unapakua(Unadownload) kitabu chako chini ya dakika 5.

Kumbuka ndugu msomaji wangu, dunia tunakoelekea sasa, unahitaji kila kitu kufanya katika mtizamo wa kibiashara, na zaidi ya hapo kijasiriamali zaidi, mathalani unafanya muziki, huwezi tena kufanya katika ule mtizamo waliokuwa nao wanamuziki enzi zile za kina NUTA jazz na Sikinde, bali itakubidi uende sambamba na akina AY, Ali Kiba, Diamond, Lady JD  na wengineo, kwa kuwa na mameneja(menejimenti), timu inayolipwa mishahara kukamilisha majukumu mbalimbali ya kampuni pamoja na promosheni au kujitangaza kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii  na katika ‘level’ za kimataifa.

Tuseme pia unafanya kilimo, siyo tena kama kile cha kutegemea jembe la mkono kwa ajili ya kujikimu chakula cha familia tu, bali kilimo cha kisasa kinachohusisha mashine kama matrekta na maksai, mbegu bora, umwagiliaji, kuongeza thamani katika mazao unayovuna na hatimaye soko la uhakika.

Yoote haya unahitaji maarifa ya kifedha, ufahamu wa maswala ya msingi kabisa kama vile, faida na hasara, mzunguko wa fedha taslimu "cash flow" , mipango ya biashara, hisa, mitaji, mizania katika biashara, kutafuta masoko nk. Na utavijuaje vitu hivyo?, Ni kwa njia ya kujifunza peke yake na wala siyo vinginevyo.

Asante sana kwa kusoma makala hii na uendelee kubarikiwa.


0 Response to "UJIO WA MABILIONI YA MAGUFULI: MJASIRIAMALI UMEJIANDAAJE?"

Post a Comment