THAMANI YA PESA KUJIANDIKISHA KUPIGA KURA NI SHILINGI NGAPI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

THAMANI YA PESA KUJIANDIKISHA KUPIGA KURA NI SHILINGI NGAPI?


Simaanishi hata kidogo ni kiasi gani cha fedha mtu anachotakiwa atoe kwa afisa anayehusika na kuandikisha  vitambulisho vya kupiga kura ili ampitishe mlango wa nyuma kwenda kujiandikisha hata kama amekuta foleni ndefu kiasi gani. Wala sina maana kwamba ni shilingi ngapi mtu anazotakiwa alipwe na mgombea au chama fulani cha siasa ili aweze kumuuzia kitambulisho chake kwa madhumuni ya kuja kujiongezea wapiga kura siku ya uchaguzi.

Jana nilipokwenda kujiandikisha ili nipate kitambulisho kwa ajili ya kuja kupiga kura, njiani na hata kabla sijaanza safari ya kuelekea huko nilifikiri sana juu muda ambao ningeutumia mpaka namaliza zoezi hili. Niliwahi kuwasikia watu wengine wakisema, inaweza hata ikakuchukua siku nzima  kuanzia asubuhi mpaka jioni kabla hujafanikiwa kukipata kitambulisho chenyewe.

Akilini nilijaribu kufanya hesabu  kwa kufikiria kwa mfano  kama mtu ataamua kukokotoa gharama zote atakazotumia mpaka amepata kitambulisho kile inaweza ikafika gharama kiasi gani? Nikianza na muda nikasema, kwa mfano ikiwa nitatumia masaa 6 na masaa hayo nilipaswa niwe katika biashara yangu ambayo niliifunga muda naenda kituo cha kujiandikisha, ni sawa na faida yote ambayo ingepatikana ndani ya masaa hayo 6. 

Kama toka asubuhi mpaka jioni huwa napata faida, mfano sh. 30,000/- ina maana kwamba kwa hayo masaa 6 ni kadirio la sh. 15,000/- Kwa ujumla gharama zote ambazo zingeambatana na zoezi hili zingeweza kuhesabiwa kama ndiyo dhamani halisi kipesa ya kitambulisho kile.

Lakini  bado  niliendelea kujiuliza, kama basi dhamani ya kitambulisho hiki ni sawa na muda unaotumika kukipata pamoja na gharama zote zinazoambatana na upatikanaji wake, kwanini basi hata watu wenye uwezo tu, kwao shilingi laki moja, mbili kwao siyo tatizo nao walikuwemo kwenye foleni ya kujiandikisha?

Ajabu nyingine ni kwamba, walikuwepo pia na watu wakawaida  tu ambao maisha yao hutegemea zaidi muda wao, kwao mtaji ni muda, akisha upoteza siku hiyo basi ujue na kula hakuna tena.

Nakumbuka kwenye foleni hiyo jana tulikuwa mchanganyiko wa kila aina ya watu, walikuwepo wanafunzi hasa washule za sekondari wengi wakiwa ni kuanzia  ‘form two’ na kuendelea, na utawajua tu kwa stori zao mfano kuna wawili waliokuwa nyuma yangu walinivutia sana, nilibaini kuwa walikuwa wanafunzi waliomaliza la saba katika shule ile miaka miwili mitatu iliyopita, mara zote walikuwa wakipiga stori za walimu wao wa zamani kwa kuwataja majina yao ya utani, jinsi walivyokuwa wakichapa bakora na hata mwalimu mkuu alivyokuwa akimiliki gari na sasa akaja kubadilishwa cheo na mambo yake kuzorota.

Walizungumzia pia “mademu” waliosoma nao huku wakiwataja waliokwishaolewa na wengine wanaodai walikutana nao njiani wakiwa na watoto walipowaambia mambo vipi wakawajibu, “We shika adamu yako, hebu niamkie” Ina maana kwamba wasichana hukua upesi kushinda wavulana na hata kuwahi kuanza maisha kabla yao.

Muda ule maafisa wanaoandikisha walipokuwa wakipata ‘lunch’ ndani,  pale nje watu wengi tulikuwa hatuna mbavu kwa vicheko; vijana watatu, huwezi ukawaita vijana sana kwani wanaonekana umri wao ni zaidi ya miaka 35 hivi, wakionekana kabisa kuwa walikuwa wamelewa pombe au ulevi mwingine wowote ule, na mavazi yao na hata haiba zao zilialiashiria kabisa kwamba ni wapiga debe, au vijana wanaokaa katika vijiwe vya stendi za mabasi.

Awali walikuwa kwenye mistari lakini waliposikia zoezi limesitishwa kwa muda nao mmoja wao alichomoja akakimbilia nje ya geti la shule.Punde kidogo alirudi ameshikilia vifuko viwili laini vya lambo mikononi ndani vikiwa  na chakula. Wenzake mara moja walimfuata kisha wakatafuta mahali wakakaa na kuanza kula ilikuwa ni ugali na samaki wa mafungu wakukaangwa, walionyunyiziwa kitu mfano wa chachandu. Maneno waliyokuwa wakitamka na staili zao zilimfanya kila mtu awakodolee macho. Katika mistari pia walikuwepo Watanzania wenye asili mbalimbali wakiwamo waarabu na hata wasomali.

Cha kujiuliza hapa ni kwamba, kitambulisho hiki  thamani yake ni kiasi gani hasa mpaka watu wahamasike kiasi hiki?. Mtu mmoja wa makamo jana wakati ule tunalumbana juu yawalioingia mlango wa nyuma alimtania yule askari polisi na kumwambia hivi; “Afande, hivi unaweza kunijibu ni kwanini zoezi la kujiandikisha huchukua zaidi ya wiki moja wakati siku ya kupiga kura, watu huenda siku moja tu na kura kuanza kuhesabiwa siku hiyohiyo?. Askari alicheka tu wala hakumjibu kitu.

Ni nini kilichowasukuma watu kujitokeza namna hii?, je, ni mwamko wa watu kutambua umuhimu wa kupiga kura, au kuna sababu nyinginezo? Kuna wanaosema kwamba, watu wamehamasika kutokana na umuhimu wa kitambulisho chenyewe kuwa, mbali na kutumiwa kupigia kura lakini pia kimekuwa muhimu sana hasa katika masuala mbalimbali kama vile shughuli za kibenki na kujisajili sehemu mbalimbali.

Watu wengi ambao walipuuzia zoezi kama hilo miaka iliyopita kwa muda wote wa miaka mitano au kumi wameonja ‘joto ya jiwe’ kwa kushindwa kupewa huduma kiurahisi katika taasisi mbalimbali za serikali na hata zile za kibinafsi.

Mfano mmoja ni rafiki yangu yule niliyemtaja jana kuwa alijihimu siku ya kwanza kabisa ya kujiandikisha, mimi nikashindwa kwenda. Kipindi kile cha vitambulisho vya Taifa yeye alipuuzia, siku za hivi karibuni akaja kujaribu kukifuatilia lakini vikwazo alivyokutana navyo nusu akate tamaa ya kufuatilia.

Mpaka sasa hivi ninavyoandika haya makala ni zaidi ya miezi miwili hajafanikiwa kukipata, kwanza kabisa tofauti na ilivyokuwa kwa watu tuliowahi muda zoezi la kawaida lilipofanyika, sasa mtu analazimika kwanza aende Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo ‘RITA’ kupata cheti cha kuzaliwa kama hana. Ni mchakato mrefu, siyo rahisi tena kama mwanzoni.

Leo taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi ni kwamba muda wakuandikisha umeongezwa siku nne ili kila mtu aweze kujiandikisha. Binafsi ninaamini kabisa, hakuna mtu atakayebaki tena labda iwe mwenyewe hataki kufanya hivyo. Thamani ya kitambulisho hiki huwezi ukaithaminisha kwa pesa hata kidogo. Usipokipata sasa kuna wakati utakuja kukihitaji hata kwa milioni ukikose, shauri yako.

0 Response to "THAMANI YA PESA KUJIANDIKISHA KUPIGA KURA NI SHILINGI NGAPI?"

Post a Comment