MALARIA, UGONJWA HATARI, ULIOJAA MAAJABU NA CHANZO KIKUBWA CHA UMASIKINI.HUUA KULIKO UKIMWI-1 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MALARIA, UGONJWA HATARI, ULIOJAA MAAJABU NA CHANZO KIKUBWA CHA UMASIKINI.HUUA KULIKO UKIMWI-1

Mwaka 1996 nikiwa ndiyo naenda kuanza kidato cha tano katika shule ya sekondari ya wavulana Songea Boys Secondary school, maarufu kama BOX 2, sikuwa nafahamu mtu anapougua malaria huwa anajisikiaje, zaidi ya kuzisoma dalili zake katika vitabu na kufundishwa na mwalimu wa somo la baiolojia na sayansi kimu.

Nilikuwa natoka Mkoani Kilimanjaro, wilayani Rombo ambapo ugojwa huu kwa wakati ule haukuwa umeenea sana, nadhani hata mpaka hivi sasa unapolinganisha na maeneo mengineyo kama Dar es salaam na mikoa ya Kusini bado malaria siyo tishio sana. Ulikuwa ukisikia mtu anaugua malaria basi ujue katoka nayo Dar au mikoa  ile iliyokuwa na kiwango kikubwa cha Maambukizi ya malaria. Hata tulipokuwa tukisoma shule ya msingi na O lelel mwanafunzi akiugua homa basi ujue ni mafua, tumbo la kuendesha, surua au ugonjwa mwingine wowote lakini siyo malaria.

Wiki mbili tu baada ya kuanza kidato cha tano, nikiwa 'boarding' katika mabweni ya Uhuru nilianza kujisikia mwili kuchoka, homa, na kutaka kulala kila mara hata ikiwa usiku nililala mapema kiasi gani. ‘Prepo’ za usiku sikuwa kabisa na hamu nazo, wenzangu wakienda mimi nabaki ndani ya neti. 

Chakula ambacho ilikuwa ni dona na maharage kasoro siku za 'weekend' ambazo tulipikiwa wali na nyama maarufu kama mpunga, asubuhi saa nne tulipewa uji, na vitafunwa mtu unajitegemea mwenyewe ambapo wengi tulipendelea kununua kwa mamantilie viazi vitamu au mihogo ya kuchemshwa iliyojulikana sana kwa jina maarufu kama“Mayao”  ‘Ulokoni’ ulokoni maana yake ni nje ya maeneo ya shule.

Siwezi kuisahau kamwe siku ambayo shuleni kulikuwa na ‘Debe’ yaani Disko, Wakati wenzangu ‘wakijirusha bwaloni na mademu wa "Tamsala" (mademu wa tamsala au tamso walikuwa ni wanafunzi wasichana kutoka shule jirani ya wasichana songea girls)  mimi nilikuwa nimelala hoi ‘Dom’(bwenini) nikiugulia malaria, huku nikizisikia kwa mbali ngoma kali za wakati huo kama vile 'Salanoki na Famille Kikuta  za General Defao', Twisted wa Keith Sweat, 'Macarena wa Los del  Rio', 'End of The Road wa Boys II Men'  na nyinginezo nyingi.  Bweni letu lililoitwa Uhuru halikuwa mbali sana na Ukumbi huo hivyo kuyafanya masikio yangu kuzisikia vyema ngoma hizo.

Nilikula kwa tabu sana huku kiungulia kikinisumbua mara kwa mara na tumbo kujaa gesi. Baadaye nilikuja kubaini kwamba hali ile ilitokana na malaria. Nilidhoofika sana na kila nilipokuwa naenda zahanati ya shule au hospitali mjini kupima waliniambia nina wadudu wa malaria wawili au watatu. Kwa kweli hali ile ilikuwa ngeni sana kwangu. Dawa pekee wakati huo iliyokuwa rahisi kupatikana ilikuwa ni vidonge vya Chloroquine na mara kwa mara ndivyo nilivyokuwa nikipewa hospitalini nikichanganyiwa na 'antibiotic' nyingine iitwayo Septrine kama sikosei(mimi sina taaluma ya udaktari au madawa naweza kuwa nimekosea spelling).

Chloroquine zilinitesa zaidi ya homa yenyewe ya malaria, kwanza nilipatwa na muwasho mkali hasa maeneo ya siri na mwili mzima, muwasho uliofanana na vitu vinavyochomachoma mithili ya sindano au miiba midogomidogo. Hali hiyo inasemekana ni mzio, ‘allergy’ inayotokana na vidonge hivyo na huwapata baadhi ya watu tu, kwani nilishangaa sana kuona kuna wanafunzi wengine walikuwa wakitumia hawapatwi na muwasho wowote.

Kupunguza muwasho ijapokuwa kwa upande wangu wala sikuona kama inanisaidia lolote madokta walipendekeza mtu utumiapo chloroquine basi utumie sambamba na Vidonde vingine vilivyojulikana kama PiritonMara ya kwanza kula chloroquine nilipata nafuu lakini wala hazikupita wiki mbili hali ile ikarudi tena, niliendelea kuteseka na malaria kwa kipindi kirefu huku nikitumia chloroquine mara kwa mara, kwa kipindi karibu cha mwaka mmoja mzima. 

Kwa kweli nilichanganyikiwa, sikujua nitumie dawa gani, wenzangu wengine walinishauri labda ningetumia quinine ingenisaidia. Sikuthubutu kuzitumia pasipo kuandikiwa na daktari hivyo ikanibidi niende kwa dokta mmoja aliyejulikana kwa jina, Dokta Hyera aliyekuwa na zahanati yake maeneo ya pale Matogoro karibu na Songea TTC Chuo cha ualimu. Dr. Hyera alinipima nikamuelezea historia ya malaria yangu kisha aliniandikia kutumia vidonge vitatu ambavyo baadaye nilikuja kugundua kwamba vilikuwa SP, Sikumbuki vilikuwa Fansida au Metakelfin lakini kwa wakati ule dawa hizi ndiyo zilikuwa zinaanza anza kutumika, hazikuwa zimezoeleka sana.

Nilishangazwa sana, kwani siku chache baada ya kutumia dawa zile nilijisikia tena mwenye afya njema kama nilivyokuwa kabla sijaondoka Kilimanjaro. Sasa nilikuwa nimeshaingia kidato cha sita lakini nikiwa karibu mwaka wote wa kidato cha tano nikiwa sijasoma kikamilifu.

Tatizo la malaria pale shuleni halikuwa likinisumbua mimi peke yangu, nilichojifunza ni kwamba wanafunzi wengi waliotoka mikoa isiyokuwa na maambukizi mengi ya malaria karibu wote walikuwa wakisumbuliwa kama mimi, lakini wale waliozaliwa palepale Ruvuma au kutoka mikoa kama Morogoro na Dar. hawakuwa wakisumbuliwa kwa kiasi kikubwa. 

Tena wapo wanafunzi wengine hata walifikia hatua ya kuhama shule kwenda kusoma katika shule za mikoa walikotoka. Kila mara ungesikia kuna mwanafunzi kalazwa hoi katika zahanati ya shule na hata wakati mwingine kuna waliofariki kwa malaria kali.

Hamna hata siku moja nililala pasipo kufunga chandarua(neti),  lakini labda nafikiri neti za wakati ule hazikuwa zikiwekewa dawa kama ilivyokuwa siku hizi. Tangu kutibiwa na Dr. Hyera nikaanza kutumia metakelfin na kuachana na chloroquine. Sasa hivi nikawa nakaa muda mrefu kidogo pasipo kupata malaria na nilipotumia dawa nilipona haraka kuliko enzi za klorokwin. Lakini athari nilizozipata kipindi hicho, kiuchumi na kimaisha kwa ujumla mpaka leo hii bado zinanitesa, hazijafutika.

Baada ya masomo nilirudi nyumbani Kilimanjaro, huku mwili ukiwa umedhoofu sana. Nakumbuka hata mama yangu mzazi alishtuka kuniona, nikaanza dozi moja ya kula malimao, dozi hii niliambiwa na mtaalamu mmoja wa dawa lishe kwamba ingesafisha sumusumu zote mwilini zilizotokana na madawa ya malaria niliyokuwa nikitumia karibu miaka 2. Kwa siku nilipaswa kula zaidi ya malimao 12, sikumbuki vizuri ilikuwa ni dozi ya malimao mangapi tena lakini kama ningemaliza dozi nzima si chini ya malimao 120. 

Dozi hii nayo almanusura imalize uhai wangu kwani baada tu ya kuitumia kwa muda wa siku nne hivi, siku moja tukiwa shambani mimi dada yangu na mama yangu, ghafla nikasikia kizunguzungu na kuanguka chini, niliamka baada ya dakika kama 5 hivi, baadaye niligundua huenda ikawa ni ile asidi  ya malimao ilikuwa imezidi kwenye damu na kwa kuwa mwili ulikuwa umedhoofu,( nilifikisha kilo 45, kutoka kilo 70) yakanizidi nguvu. 

Nilisitisha dozi mara moja na hali ile haikuja kunirudia tena mpaka hivi leo. Nikawa sasa nakula vyakula vya kawaida tu mpaka mwili uliporudi hali yake ya kawaida. Nilikaa nyumbani karibu mwaka mzima wala sikusikia dalili yeyote ile ya malaria isipokuwa tu siku za mwanzo baada ya kurudi nilisikia dalili na baada ya kupima nikaenda kununua Sp duka moja na nilipotumia zile dalili zikatoweka. Nadhani walikuwa ni wadudu wa malaria niliotoka nao Songea.

Baadaye nilihamia jijini Dr es salaam, ambako nilianza tena upya kusumbuliwa na malaria. Nikiwa naishi mitaa ya Manzese, nakumbuka nilianza tena kuzisikia dalili kama zile zile nilizokuwa nazipata nikiwa Songea, sikuhangaika wala kwenda kupima nikaanza matumizi ya dozi ya SP. Baadae niligundua kitu kimoja kwamba kumbe ile dozi ya Sp mtu ulitakiwa kurudia pindi ambapo wiki moja ilikuwa imemalizika lakini mimi baada ya dozi ya kwanza tu sikuwa narudia tena hadi dalili zilipokuwa zikinirudia tena. Vile vile unatakiwa kula idadi ya vidonge kulingana na uzito wako. 

Hali ile kumbe ilikuwa ikinifanya malaria isiishe kikamilifu jambo lililofanya niwe naumwa mara kwa mara. Nilipata ushauri kutoka kwa watu wengi, wengine wakinishauri kutumia dawa chungu kama mchunga, muarobaini ama majani yeyote yale ambayo ni machungu. Mboga zangu zikawa kila wakati ni mchunga na hata nilienda kwa Wamasai ambao walinipatia dawa chungu.

Juhudi zote zile ziligonga mwamba, nikawa kila mara natumia dozi ya Malaria ambayo mara nyingi ilikuwa ni metakelfin(SP). Chloroquine japo wakati huo ilikuwa haijapigwa marufuku rasmi hata ungelinishikia panga katu nisingeliitia mdomoni kwangu tena nikikumbuka vile ilivyokuwa ikinitesa kwa muwasho.

Kitu kilichonistaajabisha sana ni kwamba, wakati naanza kutumia Metakelfin(SP) kwa Dr, Hyera nikiwa pale Songea kabla sijamaliza shule, dawa hiyo ilinitibu vizuri sana! Lakini baada tu ya kuwa nimeitumia kwa muda fulani tangu niliporudi nyumbani Kilimanjaro na baadaye Dar. SP ilianza kuonekana hainisaidii chochote.

Nilianza kuingia kwenye mtandao wa intaneti wakati huo tena intaneti ikiwa ndiyo kwanza ipo katika hatua zake za mwanzo kwa hapa kwetu, Google haikuwa maarufu kama ilivyokuwa sasa, nakumbuka nilikuwa nikitumia sana 'search engine' ya Yahoo, nikaanza kutaipu neno malaria. Nilijifunza Malaria kwa kina sana, nikazifahamu dawa zote zinazotumika kutibu malaria kuanzia 'Halfan' mpaka dawa moja ambayo nilifikiria pengine ndiyo ambayo ingeliweza kuwa suluhisho la malaria yangu iitwayo'Piperaquine'. 

Kwa mujibu wa website mbalimbali nilizotembelea ni kwamba Piperaquine iliyokuwa kundi moja na dawa zingine kama Quinine na chloroquine, inafanya kazi tofauti kidogo, na sifa yake kuu ni kwamba ina uwezo wa kuviua vijidudu vya malaria vinavyojificha kwenye ini na ambavyo kwa dawa za kawaida haviwezi kuuwawa. Huwa tu malaria inatoweka kwenye damu lakini mayai ya wadudu hao hujichimbia katika ini na huja kuibuka baada ya kipindi fulani na kuanza tena kumpa mgonjwa dalili za malaria.

Gonjwa jingine hili hatari linaloenezwa na mbu kama hukulisoma nalo lisome hapa.


Niliamini kabisa kwamba malaria yangu haikuwa ya kawaida nikajisemea “Ni lazima malaria yangu itakuwa kwenye ini”. Sasa nilianza kufanya utafiti mwingine wa kuipata dawa hiyo, kila duka la dawa nililokwenda nikawa naambiwa dawa ile 'piperaquine' haipatikani, lakini kila nilipoingia kwenye mitandao nilikuwa nikipata maelekezo yake kuwa ndiyo dawa pekee iliyokuwa na uwezo wa kufuta malaria sugu ya kwenye inni. Nilishangaa sana kwanini serikali ya Tanzania haikuwa imeona umuhimu wa kuagiza dawa hii ambayo nilidhani ndiyo uliokuwa muarobaini wa malaria inayojirudia rudia.

Nilifikia hata hatua ya kutaka kuiagiza dawa hiyo mtandaoni kutoka Marekani au Ulaya lakini kikwazo kilikuwa ni jinsi ya kupata Credit/Debit Card, kumbuka wakati huo miaka ya 2003 kurudi nyuma hata mabenki ya hapa sijui kama kulikuwa na moja iliyokuwa na huduma ya namna hiyo. Sina uhakika kama kulikuwa na benki iliyokuwa na huduma hizi za Master Card na VISA. Nusu nifunge safari ya kwenda jiji la Nairobi nikidhania labda ningekwenda kuikuta dawa hiyo katika 'mapharmacy' makubwa huko.

Nilipokuwa nafanya juhudi hizi zote siyo kwamba sikuwa na imani na madaktari au hospitali za hapa nyumbani, la hasha ila nilishajiaminisha mwenyewe kwamba tatizo la malaria kama mtu usipokuwa makini mwenyewe, ukasema utegemee hospitali unaweza ukapoteza maisha. 

Kwanza nilikatishwa tamaa na dawa ya Sp ambayo mwanzoni ilikuwa ikinitibu vyema ilipoanza kukataa kunitibu vizuri, pili niliona sasa ikiwa serikali haioni umuhimu wa kuagiza Piperaquine dawa pekee ambayo niliamini ndiyo ingeliweza kuniponya malaria yaliyokuwa yakinisumbua kwa takribani miaka mine sasa, basi hakuna tena umuhimu wa kwenda hospitalini.

Mwishowe niliamua kwenda hospitali ya Magomeni na Dokta mmoja nilimuelezea tatizo langu kwa kirefu, alinishauri kwanza nisiwe tena natumia dozi yeyote ya malaria pasipo kwanza kupima na pili nihakikishe baada ya kumalizia dawa atakazoniandikia nirudi tena hospitalini nikafanye vipimo kuangalia ikiwa malaria imemalizika.

Tangu siku hiyo nikaanza kufuatilia yale aliyonielekeza yule dokta huku nikihakikisha najilinda vilivyo na mbu. Ijapokuwa tatizo la malaria halikumalizika kabisa lakini nilipata ahueni kubwa na ndipo nilipobaini kuwa kumbe dhana nyingi nilizokuwa nazo juu ya malaria huenda nyingine hazikuwa sahihi sana.

Nilichogundua mimi binafsi ni kuwa mwili wangu ni miongoni mwa wale watu ambao kinga yao ya malaria ipo chini sana jambo linalosababisha mara tu mtu aumwapo na mbu mwenye vijidudu vya malaria basi mwili hauna uwezo wa kujikinga nao, na hili nililigundua tangu nikiwa Songea pale ambapo kuna baadhi ya wanafunzi tuliosoma nao walipokuwa wakikusikia ukilalamika  una malaria walikuwa wakishangaa na hata wengine wakisema walikuwa hawajui malaria inauma vipi.

Ukaja ujio wa dawa ya Artemisinin pamoja na mseto wake na dawa nyinginezo, mara ya kwanza kabisa zilianza kuletwa artemisinin peke yake vidonge ambavyo havikuchanganywa na dawa nyingine yeyote ile.(Nimesema mimi siyo mtaalamu wa dawa hivyo inawezekana majina haya naweza nikawa nakosea spelling). Baada ya kusikia kuna dawa ya malaria ya Kichina imeingia mpya na inatibu haraka pasipokuchosha mwili sana mara moja nikaanza na mimi kuitumia. 

Ni kama vile vile ilivyokuwa kwa ujio wa SP. Matibabu ya malaria kwa kutumia Artemither yalikuwa ni ya kushangaza mno, ukianza tu kumeza vile vidonge vya mwanzo, taratibu dalili zilikuwa zikitoweka mpaka unamaliza dozi malaria nayo kwaheri huku husikii uchovu wowote kama zilivyokuwa dawa zingine.

Mshangao mwingine tena ulinikuta baada ya kipindi kifupi tu, kila nilipopata malaria nikatumia Artemether nilishangaa mbona siponi kama zamani?. Hali kama hiyo hiyo nayo ilimkuta mke wngu ambaye kwa wakati huo alikuwa mjamzito Daktari mmoja akapendekeza aitumie kwani haina madhara makubwa. Ulikuwa ni mtihani, mama aliendelea kulalamika maumivu ya kichwa na mgongo hata mara baada ya kumalizia ile dozi. Haraka sana nilimwahisha hospitalini wakamuwahi kwinini na ndiyo ikawa salama yake.

Nilijiuliza haya malaria kwanini ni kigeugeu hivi? Hata dalili zake unaweza leo ukasikia kichwa kinauma siku nyingine yanakuja kwa staili nyingine  mfano badala sasa ya kichwa unashangaa ni tumbo tu linauma na kuendesha, wewe kama hautakwenda hospitalini kupima maabara unaweza ukdhania labda umekula chakula kichafu ukaanza kumeza flajin kumbe ni mdudu wa malaria. Siku nyingine utasikia tu kiungo labda mguu, mkono, shingo au hata kiuno kikivuta wewe bila kupima ukaanza kusema “oo..nililala vibaya”, kumbe tayari ni mdudu wa malaria.


Baadaye serikali nayo ilianza kutangaza kuwa matumizi ya zile dawa za Artemether peke yake bila ya kuchanganya na dawa nyingine yeyote yalikuwa hayafai tena kutokana na wadudu wenyewe wa malaria kutengeneza usugu. Zilianza kutumika dawa mseto ambazo sasa artemether ya kichina huchanganywa na dawa nyinginezo kuifanya iwe na uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na mdudu wa malaria na moja kati ya hizo ni ile iitwayo ALU.



0 Response to "MALARIA, UGONJWA HATARI, ULIOJAA MAAJABU NA CHANZO KIKUBWA CHA UMASIKINI.HUUA KULIKO UKIMWI-1"

Post a Comment