INNOCENT MUNYUKU: UCHESHI, UBUNIFU NA UKARIMU WAKO HAVITASAHAULIKA MILELE. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

INNOCENT MUNYUKU: UCHESHI, UBUNIFU NA UKARIMU WAKO HAVITASAHAULIKA MILELE.

Nakumbuka mwaka 2002, baada tu ya kumaliza mafunzo yangu ya uandishi wa habari, mimi na wenzangu kadhaa tulipangiwa mafunzo ya vitendo katika kampuni ya Mwananchi Communications ltd iliyokuwa ikimiliki magazeti ya Mwananchi  na Mwanaspot. 

Moja kati ya waandishi waandamizi tuliowakuta pale miongoni mwao walikuwepo Marehemu  Innocent Munyuku, Dastan Conrad (kionambali)ambaye pia ni Marehemu, Deodatus Balile, Leah Samike, Joyce Mmasi, Charles Mateso, Anastazia Anyimike, Deus Ngowi, Happiness Katabazi, Sarah Mosi,  Absalom Kibanda.

Wengine ni, Manyerere Jacton, Kulwa Karedia, Zena Chande, Maulid Ahmed, Joseph Zablon, Prudence Costantine, Angela Semaya, Ojuku Abraham, Shadrak Sagat, Midraj Ibrahim, Theodatus Muchunguzi, Usia Nkhoma, Alex Kachelewa na wengineo wengi.

Naweza kusema karibu wanahabari wote wakali unaowajua sasa hivi nchini Tanzania, waliokuwa hai na hata waliokwishatangulia mbele za haki kwa kweli katika kipindi hicho ni jambo la ajabu kabisa walikuwepo pale Mwananchi. 

Juu ya wote hao viongozi waliokuwepo, na ambao kwa kipindi hicho kulikuwa na utamaduni usiokuwa rasmi wa kuwaita “MaChief”  hata ikiwa siyo 'chief editor'  walikuwa ni Mhariri mkuu(Chief Editor) Theophil Makunga, Msaidizi wake Muhingo Rweyemamu,  Mhariri wa habari, Danny Mwakiteleko(marehemu naye).

Kulikuwa pia na “Chief” mwingine ila sikumbuki kama alikuwa mhariri wa makala au ni msaidizi  wa nani, na nakumbuka jina lake moja tu aliitwa Mr. Makaranga. Kila siku asubuhi tulikusanyika ofisini kwenye mkutano kabla ya kuanza kazi(postmortem) na kisha tulianza kupangiwa majukumu ya siku hiyo ambapo kwa wale wageni na tuliokuwa tukijifunza tulipangwa majukumu, “assignment” na wale wakongwe.

Kigari cha kampuni wakati huo kikiwa ni  ‘kihice’ ndicho kilichokuwa kikituzungusha kutupeleka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kutafuta habari. Kama ilivyokuwa kawaida katika nyumba nyingi za habari, unapoingia ukiwa mgeni unapata wakati mgumu kidogo katika kuzoea mazingira na hata taratibu mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa. 

Ukiwa mgeni ni lazima utajikuta ukihitaji kwa kiasi kikubwa kujifunza kutoka kwa wale waliokwishatangulia hapo lakini kwa kweli kila binadamu ameumbwa tofauti na mwenzake, kuna waliokuwa wepesi kuzoeleka na wengine inakuwa vigumu kidogo kuwazoea ili waweze kukupa msaada katika jambo fulani.

Pale Mwananchi kipindi kile kwa kweli kulingana na maoni yangu binafsi na hata maoni ya wanafunzi wengi tuliokuwa pale kwa mafunzo ya vitendo, mtu ambaye tulimuona mwepesi  kumzoea na kumuomba msaada hasa katika maswala ya kompyuta, alikuwa Conrad Dustan, kwa kweli mtu huyu alikuw wa ajabu kila mtu alimpenda kwa moyo wake wa ukarimu na kusaidia usiokuwa na mipaka. Lakini kwa bahati mbaya ule usemi usemao “wazuri hawadumu” hatimaye ulitimia pale kipenzi cha wengi Conrad  Dustan alipoaga dunia baada ya kusumbuliwa na homa. Kila mtu alisikitika.

Baada ya Conrad kuondoka si kwamba kulikuwa hakuna tena watu wazuri Mwananchi, hapana, walikuwepo na nadhani kwa maoni ya mtu mwingine pengine yawezekana walikuwepo watu wengi tu kulingana na mtazamo wao waliokuwa wazuri. Hii ni kwa mtazamo wangu na baadhi tu ya wale tuliokuwa tukifanya mazoezi ya vitendo kwa wakati ule. 

Innocent Munyuku alikuwa kimbilio jingine kwa wanafunzi  wengi kutokana na wepesi wake kumzoea, alikuwa mwazi, asiyependa kuzungukazunguka unapomwendea kutaka msaada wowote ule, mcheshi na mwenye utani mwingi, alipenda kuvaa tai, na mara zote alionekana nadhifu na mchangamfu huku kalamu ikiwa kwenye mfuko wa shati lake. 

Pengine ndiyo maana yeye na mwenzake marehemu Conrad Dustan walikuwa marafiki wakubwa kutokana na tabia zao kushabihiana tabia ya ucheshi, kupenda kusaidia wengine pamoja na kusuluhisha migogoro popote pale ilipotokea. 

Alipenda kuzungumza kwa sauti nzito hivi, anapozungumza kama yuko nyuma yako humuoni, unaweza ukafikiri ni  “jitu kuubwa la miraba minne” linakusemesha, hautaamini macho yako utakapogeuka na kukutana na kijana mwenye umbile la wastani tu.

Kwa kweli mimi binafsi Munyuku alikuwa moja kati ya waandishi walionivutia sana hasa katika lugha aliyokuwa akitumia katika habari na makala alizokuwa akiandika, alipenda kutumia misamiati  iliyomwacha hoi kila mtu na mfano ni neno ‘Busati’ alilokuwa akimaanisha safu yake katika makala za michezo kwenye magazeti mbalimbali ya michezo na burudani aliyowahi kuandikia likiwemo Mwanaspot. 

Waandishi wengi wameandika juu ya Munyuku baada ya kuaga Dunia, ingawa watu husema kuwa binadamu tunapenda kumsifia mtu pale anapoaga dunia lakini kwa Munyuku sidhani kama anapewa sifa za uwongo.
 
Innocent Munyuku, Mzee wa Busati kapumzike kwa Amani
Katika gazeti la Mtanzania la Jumapili ya tarehe 23 Novemba 2014 Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhino Rweyemamu katika sehemu ndogo ya  makala yake ndefu juu ya kifo na maisha ya Innocent Munyuki alivyofanya naye kazi, amemuelezea kama ifuatavyo juu ya sakata la kuuzwa kwa nyumba za serikali jinsi alivyoliibua na Muhingo akiwa mhariri wake wakati huo kabla hajawa Mkuu wa Wilaya;

“Hadi kesho naushangaa ujasiri wako. Katika hili, Inno ulistahili tuzo. Natamani sana wale wanaofundisha  “Investigative Journalism“ (uandishi wa habari za uchunguzi) wangeyajua haya wakakuita katika madarasa yao  ukawapa mfano halisi wa ulichokifanya. Ni wachache wa namna yako kama wapo.


Naweza kuwa nakosa maneno sahihi. Lakini mtaniwia radhi kueleza haya, niliyatunuku utu na heshima kwa innocent-ucheshi wake na utukutu wake kazini lakini uchapakazi mzuri kazini wa kimapinduzi. Innocent , kuondoka ni ombwe kwa wanaokufahamu na wasiokufahamu.


Hukuwa mwandishi tu kama wengi wanavyosema , ulikuwa mhariri na mtaalamu wa lugha. Ulikuwa mpatanishi na msuluhishi. Hukuwa na fedha bali ulikuwa na roho iliyoshiba. Hukukubali uhitaji ukutawale. Uliweza kutawala nafsi yako.


Ulifanya kile ulichoamua kufanya. Si wengine walichotaka ufanye. Hukuwa mtu wa mkumbo na ndiyo maana wengi hawakuelewa ujumbe wako wa mara kwa mara katika post zako. Ni wachache sana waliofahamu siku ulipokuwa na shida.


Na hata  pale ulipolazwa Hospitali ya Temeke kwa tatizo la ini, ni wachache walioweza  kujua. Nilipata bahati tu ya kuelezwa na rafiki yako Charles Mateso. Sina uhakika kama ulimtuma lakini nilipofika wodini, niliweza kukiona kile ulichotaka kuniambia. Ulinieleza kidogo tu, kwamba ini lina tundu. Ulitaka kusema mengine hukuweza. Mimi nakuzidi umri,  nilijua unataka kuniambia nini.


Ulijua uzito wa tatizo lako la mwili, lakini ulizingatia nadharia kwamba ukikutana na Mungu usimwambie ukubwa wa tatizo lako, bali unapopambana na tatizo, liambie ukubwa wa Mungu wako. Nilikwambia muache Mungu aitwe Mungu. Na tukakubaliana, tukacheka na siku zote tano ulizokaa hospitalini hapo, tuliweza kuwa karibu na mimi na familia yangu. Kwa bahati nzuri nilikuwa naishi National Housing  Temeke,Dar es salaam.


Inno, nakutakia safari njema. Safari ambayo wote lazima tutaifanya. Ni safari ya kumaliza kazi. Wewe umemaliza kazi. Umepigana vita vizuri. Na umeishikilia imani yako. Imani inayothibitishwa na wingi wa watu waliojitokeza kukuaga.


Uliotuacha, sote tunatambua kwamba tupo nasi safarini.
Wewe umetangulia, sisi bado kidogo. Tupo hapa kusherehekea ushindi wako. Tupo kukuaga tukimwomba Mungu akupumzishe sehemu unayostahili Amina.”

Mimi binafsi naamini kabisa kwamba "kichwa hiki" Innocent Munyuku kutokana na uwezo mkubwa wa akili na ubunifu aliokuwa nao, ni dhahiri kabisa bado ndoto zake za maisha alikuwa hajazikamilisha.Baada ya miaka zaidi ya 15 akichapa kazi katika makampuni mbalimbali ya habari, bila shaka alikuwa akipanga jambo lake mwenyewe kubwa la kutimiza maishani. 

Kwa bahati mbaya Mwenyezi Mungu amemchukua kabla hajatimiza lengo lake hilo, na ni funzo kwetu sisi sote tuliobakia kuwa ijapokuwa hatujui siku wala saa lakini tusichoke kuhangaika katika kuyatimiza malengo yetu tuliyojiwekea maishani hata ikiwa itatuchukua muda gani. 

Marejeo kutoka blogu mbalimbali na magazeti ya New Habari (2006) Limited



0 Response to "INNOCENT MUNYUKU: UCHESHI, UBUNIFU NA UKARIMU WAKO HAVITASAHAULIKA MILELE. "

Post a Comment