Siku ya leo Jumapili
tarehe 1/6/2014 kwangu binafsi ilianza vizuri tu asubuhi, huku mawazoni
nikitafakari mambo mbalimbali yahusuyo maisha yangu kwa ujumla. Lakini
ilipotimu majira ya jioni ghafla hali ilibadilika pale niliposikia redioni
kwamba yule mtoto Nasrah Rashid aliyeishi
ndani ya boksi kwa takriban miaka minne ameaga Dunia!
Naandika makala hii
ningali na simanzi kuu machozi yakinilengalenga. Amefia Hospitali ya Taifa
Muhimbili baada ya madaktari kuhangaika naye usiku na mchana wakitaka kuyaokoa
maisha yake pasipo mafanikio. Najaribu kupata picha ya jinsi mtoto huyu (Malaika)
asiyekuwa na chembe ya dhambi jinsi alivyokuwa akiishi gizani ndani ya boksi
pembeni kukiwa na dimbwi la maji machafu, sielewi shimo hili lilikuwa la kazi
gani.
Kwa kifupi hajawahi
kuonja upendo na furaha tangu amezaliwa kutokana na kuzaliwa mama yake angali
mgonjwa na hatimaye kufa isipokuwa tu
katika zile siku chache za mwisho wa
uhai wake baada ya wasamaria wema kuja kumuibua ‘shimoni’. Ameondoka na
kutuacha kila mtu tukitamani kumpa upendo, ni kama vile amesema, “Kwani
mlikuwa wapi siku zote hizo nikipata mateso yasiyomithilika wala kulingana na
umri wangu?”
Haya ni matokeo ya
binadamu wa siku hizi kutokujali tena hata pale tunapoona kiumbe kama kile
kikiteseka. Bila shaka majirani na hata watu wa karibu, ndugu na jamaa wa
marehemu mama wa mtoto huyu, ni lazima
walifahamu kuteseka kwake kitambpo tu lakini kwa kuwa hakuwahusu sana wakaamua “kupotezea”
mpaka mambo yalivyokuja kuwa magumu zaidi ndipo wakaamua kutoa taarifa.
Hivi jamani nauliza
mtoto huyu alikuwa halii hata majirani wasisikie? Ni maumivu kiasi gani mtoto
huyu alikuwa akiyahisi ndani ya akili yake change? Akili yake ilikuwa
ikifikiria nini? Alikuwa anahisi uchungu na mateso au labda alikuwa akiona ni
maisha ya kawaida tu? Akili yake ilitambua kuwa alikuwa akiteswa?
Hakika MWENYEZI Mungu
ni wa ajabu! Nasema hivyo kwa sababu, mtoto huyu aliweza kuishi kwa muda huo
wote ndani ya boksi hilo katika hali ya mateso yote hayo pasipo kufa. Swali
jingine ninalojiuliza ni kama alikuwa akiugua
homa kwa kipindi chote hicho, na kama alikua akipatwa na homa basi
alikuwa akipona vipi bila matibabu? Nijuavyo mimi kwa kipindi chote hicho
kwenye mazingira duni namna ile ilitosha kabisa kuondoa uhai wake tena mapema
kabisa.
Mtoto Nasrah Rashid aliyeishi ndani ya boksi kwa miaka 4 akiwa amebebwa na baba yake enzi za uhai
wake.
Hebu kama wewe ni
mzazi jaribu kufikiria ni mara ngapi umewahi kumpeleka mwanao mwenye umri kama
huo hospitalini hata kutokana na malaria tu au kikohozi sembuse Neumonia?
Huenda MUNGU alikuwa
na makusudi ya kuuthihirishia umma
mateso makali wanayotendewa watoto wadogo Tanzania nap engine Duniani
kwa ujumla kupitia mtoto huyu. Ndiyo maana hakutaka kumchukua mapema, alisubiri
aje agunduliwe na wasamaria habari zimfikie kila mtu ndipo sasa amchukue kiumbe
wake.
Nakumbuka jinsi
nilivyomuona katika vyombo vya habari siku alipookolewa na siku zilizofuata,
alionekana mzima tu ijapokuwa alikuwa amedhoofika sana. Hata wandishi wa habari
walipojaribu kuzungumza naye, aliweza kujibu vizuri tu na kutia matumaini,
aliweza kuzungumza sentesi chache kama vile “Napenda chipsi” nk.
Ina maana kwamba kama
asingegunduliwa na akaendelea kuishi mle “jehanamu”(kwenye lile boksi) pengine
wiki ile ile ndiyo ingelikuwa mwisho wa maisha yake. Ina maana alikuwa karibu
kufa kiasi hicho? Sijui, ndiyo maana nasema hili lilikuwa kusudi la Mwenyezi
Mungu mwenyewe kufikisha ujumbe wa kilio cha watoto wadogo kwa Wanadamu wa
Ulimwengu huu dhalimu.
Mtoto huyu
namfananisha na Nabii, ni kama vile alitumiwa na Mungu kuwakilisha watoto wenzake kote Duniani na
hususan Tanzania wanaopata mateso makali, siyo kutoka kwa watu baki bali bali
ni kutoka kwa wale watu wanaostahili kuwa walezi wao, kama vile Baba wadogo,
mama wadogo, mama na baba wakubwa, shangazi, mjomba, binamu, bibi, babu na hata
wazazi wao wenyewe wa kuwazaa kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya wazazi
waliodiriki kuwatoa watoto wao wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwa wauaji, kisa
tu, tamaa ya kupata pesa na utajiri wa haraka haraka.
Mateso ya Nasra yawe chachu ya mapambano dhidi ya
mateso ya watoto wengine wadogo wasiokuwa na hatia wanaopata mateso kama hayo.
Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi Amina.
Picha na global publishers
0 Response to "MAAJABU KIFO CHA MTOTO WA KWENYE BOKSI KUMBE ALIKUWA "NABII WA MUNGU""
Post a Comment