Napenda kuimba na kila
nionapo au kusikia mtu akiimba , huwa “automatically nakuwa attention” kutaka
kufahamu, ni nani na anaimba nini.
Nimewahi kumuona akipita
njiani hasa maeneo ya Buguruni huku akiimba(akighani) mashairi matamu, hunikumbusha enzi zile Redio Tanzania,
RTD sasa TBC walipokuwa na vipindi vya kughani mashairi. Kila nilipokuwa
nikimuona nilikuwa najiuliza maswali
mengi juu ya huyu dada, moja likiwa, ni kwa nini huwa anaimba mtaani, na ikiwa
kama kipaji chake hiki amewahi kujitangaza mahali popote pale. Nilinuwia kwamba
iko siku moja lazima nimuite na kumuuliza.
Leo nilipomuona tu akipita
kama kawaida yake akiimba mashairi, sikuweza kujizuia na kwa kuwa alikuwa
akipita karibu kabisa na kazini kwangu, nilimfuata na kumuomba asogee barazani,
Hakukataa akakubali. Kitu cha kwanza nilimuuliza iwapo anatoza shilingi ngapi
kwa shairi moja akanijibu ni shilingi 500/-Sikuchelewa nikamwambia aanze mara
moja, naye hakukawia akaanza. Ile sauti kama ya Tausi, kidogo kidogo ikaanza
kuwakusanya majirani walioisikia mpaka wakajaa tele! Angalia video chini akiimba,
Baada ya kuimba ndipo na
mimi nikamuomba anijibu maswali yangu niliyokuwa nikijiuliza kila siku.
Alilitaja jina lake kuwa ni Amina Hassan na kwamba alianza kughani mashairi
siku nyingi, hakumbuki ni lini lakini anasema ni tangu akiwa mtoto na wala hakuna mtu aliyemfundisha bali
alikuwa akipenda sana kusikiliza kipindi cha mashairi redioni, na ndicho
kilichomvutia na yeye kutunga na kuimba. Video hapa chini akieleza,
Ameniambia kwamba amewahi
kupelekwa pale karibu na Tazara, akimaanisha redio ya Taifa TBC na marehemu Halima Mchuka kupitia kwa Muhidin
Maalim Gurumo, akafanyiwa mahojiano, lakini pamoja na kuonekana kuwa anacho kipaji kikubwa, kikwazo cha yeye
kuweza kuendelezwa ama hata kushirikishwa na wasanii wakubwa kilikuwa ni tatizo
lake la kiafya linalomsumbua.
Nilimuomba ataje ni tatizo
gani, akasema huwa akikaa kwenye msongamano wa watu mara nyingi anapatwa na
ugonjwa wa kuanguka, lakini tatizo hili anasema halimzuii kufanya kazi yake hii
ya kuwaburudisha watu kwani kama ilivyokuwa kwa mtu yeyote mwenye tatizo hili
huwa haiwezi kumtokea kila wakati, ni ugonjwa wa kawaida kama magonjwa mengine
ila tatizo ni watu kutokuelewa na kuwa na unyanyapaa.
Nilipotaka kujua Amina
Hassan anakoishi, alitaja kwamba,
anaishi na wazazi wake wote wawili pamoja na ndugu zake wengine maeneo ya
Uwanja wa ndege, Karakata, ukifika Karakata tu ulizia kwa KALA. Anasema hana
simu ya mkononi, na mtu yeyote akitaka kuwasiliana naye anaweza kufika maeneo
hayo aliyotaja na kumuulizia atampata. Video hii hapa chini akitoa mawasiliano yake.
Maoni ya mwandishi.
*Ugonjwa wa kuanguka au Kifafa
kitaalamu hauwezi kuambukiza, ni ugonja unaotokana na hitilafu katika mishipa
ya fahamu hasahasa katika ubongo na uti wa mgongo. Si vizuri kuwanyanyapaa
wenye tatizo hili wala kuhusisha matatizo yao na maswala ya kishirikina.
Tuwajali wenye ugonjwa huu na kuthamini kazi wanazozifanya kwani wanaweza
kufanya kazi sawasawa na watu wengine licha ya ulemavu waliokuwa nao.
0 Response to "MSICHANA ALIYEJALIWA UWEZO WA AJABU WA KUIMBA MASHAIRI "
Post a Comment