JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YAKO, DONDOO HIZI 3 NI MUHIMU SANA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YAKO, DONDOO HIZI 3 NI MUHIMU SANA

DONDOO MUHIMU ZA MPANGO WA BIASHARA HIZI HAPA

Mpango wa biashara au mchanganuo wa biashara, watu wengi wamekuwa wakiona kama ni jambo gumu linalohitaji mtu kuwa mtaalamu wa biashara au mtu aliyebobea katika mahesabu ya biashara ndipo aweze kuandika kumbe ni kinyume chake kabisa.

Wanachoshindwa kufahamu wajasiriamali ni kwamba, kumbe kila mjasiriamali anayeanzisha biashara pasipo hata kujua yeye mwenyewe huwa anakuwa ameshaandaa mpango wa biashara yake kichwani tayari. Tatizo moja tu linakuja pale mtu anaposikia neno JINSI YA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA AU MPANGO WA BIASHARA KWENYE KARATASI.


Kwa kifupi kabisa mpango au mchanganuo wa biashara ni jumla ya mambo  yote na michakato inayotarajiwa kutekelezwa na biashara. Mambo hayo yote uyafikirie kwa kichwa, uyaandike katika karatasi au hata uyarekodi kama sauti, vyovyote vile yataitwa mpango wa biashara. Hivyo kufahamu mtiririko mzima jinsi utakavyoendesha biashara yako ndiyo mpango wenyewe wa biashara na hakuna mtu anayeweza akaanzisha biashara pasipo kufahamu anataka kufanya kitu gani au malengo yake ni nini.

Kwa hiyo ikiwa unataka  kuandika au kuandaa mpango wa biashara utakaokuwezesha kutimiza malengo yako ya biashara uliyojiwekea, yawe ni malengo kwa ajili ya kupata fedha  mahali, benki, kwa wawekezaji au wabia, au ni kwa malengo  tu ya kupanga mkakati imara wa kuikuza biashara yako, dondoo  zifuatazo ni muhimu.

1. Andika mchanganuo mfupi.
Lengo la kutokuandika mpango wa biashara yako kuwa mrefu sana ni kuhakikisha mpango wako unasomwa na hadhira uliyokusudia iusome na kama ujuavyo binadamu hatukuumbwa kusoma mamia ya kurasa, karibu kila mtu anapenda kusoma kitu kifupi chenye maana iliyokusudiwa.

Sababu nyingine ni kwamba, mpango wa biashara siyo kitu cha kubwaga kabatini na kuacha huko mende watafune bali ni kitu unachopaswa kufanya marejeo mara kwa mara na kufanya marekebisho angalao kila wiki au mwezi kulingana na matukio halisi yanavyotokea, kumbuka mpango wa biashara ni dira tu, ukiwa mrefu sana hata wewe mwenyewe utaona uvivu kuupitia.

2. Fahamu vizuri hadhira yako(wasomaji wa mpango wako)
Mchanganuo wako unatakiwa kuandikwa kwa lugha  ambayo ni nyepesi na inayoeleweka barabara kwa wasomaji wako. Mathalani  biashara yako unashughulika na masuala ya kiteknolojia lakini wafadhili au wawekezaji wako ni watu wa kawaida wasioweza kuelewa lugha za kitaalamu basi hakikisha mpango wako unaweka maneno rahisi.

3. Usikubali vitisho kutoka kwa watu.
Wamiliki wa biashara na wajasiriamali wengi duniani kote siyo wataalamu wa biashara na wala wengi wao hawana digirii za biashara, kama ulivyokuwa wewe na mimi, wanajifunza kadiri muda unavyokwenda na biashara zao zinavyokua. Kigezo kikubwa cha mtu kuandika mpango wa biashara yake ni ikiwa anaifahamu vizuri biashara husika, utayari wa kuifanya na kuipenda.


Kuna watu wengine wakiwemo na baadhi ya wataalamu wa biashara, kutokana tu na uvivu hudai mipango ya biashara ni kupoteza wakati, ni jukumu gumu na lisilokuwa na faida. Lakini wao wenyewe katika biashara zao kila siku hupanga mikakati na namna watakavyoboresha zaidi biashara zao, hukubali kwa shingo upande kuwa mpango wa biashara ni muhimu lakini wakati huohuo huponda.

Kitu wasichotambua tu ni kwamba duniani huwezi ukafanya jambo lolote lile pasipo mipango likafanikiwa vizuri. Unapofahamu vizuri ni nini kinachotakiwa kuwa katika mpango wako wa biashara, hata usipoandika katika karatasi, bado unaweza ukapanga kichwani mwako na ikatosha kuitwa ni mpango wa biashara.

Hatua nane( 8)za kuandika mpango wa biashara yako.
Kwa haraka haraka hebu tutazame hatua nane au unaweza kuziita vipengele vinavyounda mchanganuo wa biashara kwa mujibu wa kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, kitabu ambacho pamoja na masomo mengine mengi ya ujasiriamali, kimeelezea kwa undani kabisa jinsi ya kuandka mchanganuo/mpango wa biasha yeyote ile pamoja na michanganuo yenyewe halisi ya  biashara mbalimbai iliyokamika.

1. Muhtasari tendaji.
Huu ni ufupisho wa mpango wako mzima wa biashara, kurasa moja mpaka 2, ni sehemu muhimu sana unayotakiwa kuiandika kwa umakini kumfanya msomaji wako avutike kusoma mpango wako mzima.

2. Maelezo kuhusu biashara/kampuni
Hapa unaeleza, mfumo wa biashara kisheria, mfano kama ni kampuni yenye dhima ya ukomo, ubia au ya mtu binafsi, historia ya kampuni ikiwa biashara siyo mpya, wamiliki na sehemu ilipo.

3. Maelezo kuhusu bidhaa au huduma .
 Ni kitu gani unachouza na ni mahitaji gani hasa ya wateja unayokidhi, unawatatulia tatizo gani linalowasumbua?

4. Soko lengwa.
Unawauzia kina nani? Soko lako muhimu ni kundi gani, onyesha ikiwa lipo kundi moja tu au makundi zaidi ya moja na uyaelezee.

5. Mpango wa masoko na mauzo(Mikakati)
Eleza mbinu na mikakati mbalimbali utakazotumia ili kulifikia soko lako lengwa.


6. Vitendo na upimaji wa matokeo
Sehemu hii unaelezea vitendo hasa hasa vile vinavyohusika na uanzishaji wa biashara yako, mpango peke yake bila vitendo hauna maana yeyote, taja vitendo, mtu atakayehusika pamoja na bajeti yake ni kiasi gani.

7. Utawala na nguvukazi
Tumia sehemu hii kuelezea timu itakayohusika kwenye biashara yako, historia zao, ngazi ya elimu na sifa za mtu utakayependa kumuajiri.

8. Masuala yahusuyo fedha
Mwisho ni sehemu ya fedha ambayo wengi hudai ni ngumu lakini siyo kweli ingawa kwa asiyekuwa na uelewa wake ana haki ya kusema ni ngumu. Na hasa kwa biashara mpya hesabu zake ni rahisi sana. Kwa kawaida makisio ya fedha hufanywa ya kila mwezi kwa mwaka mzima wa kwanza na kisha kwa mwaka katika miaka miwili inayofuata.

Kisia  mauzo, gharama za mauzo mfano mishahara nk., ripoti ya faida na hasara, mtiririko wa pesa taslimu, mizania ya biashara, sehemu na muhimu za biashara.

Vielelezo
Hii hauwezi ukasema ni sehemu au kipengele cha mpango wa biashara lakini ni sehemu muhimu ambayo ndiyo unayotakiwa kuweka vile vitu ambavyo usingeliweza kuviweka kwa undani katika mpango wako, vitu hivyo ni kama vile, chati na majedwali marefu ya makisio ya hesabu zako, nyaraka mbalimbali za kisheria kama usajili wa biashara nk.na picha na vielelezo mbalimbali vinavyoelezea bidhaa zako.

………………………………………………………………………..
Mpenzi msomaji wa makala hii, kwa muda mrefu sasa umekuwa ukisoma nadharia nyingi kuhusiana na namna ya kuandika mpango wa biashara na faida zake, lakini yamkini umekuwa ukijiuliza, “Mpango wa biashara unanisaidiaje katika biashara yangu wakati hata taasisi za fedha hapa kwetu mara nyingi huwa haziangalii mipango ya biashara ili kukukopesha?”

Nataka nikutie moyo kwamba mpango wa biashara thamani yake haipo kwenye kuomba mikopo tu peke yake, mpango wa biashara ni zana muhimu iliyokuwa na uwezo wa kumfanya mjasiriamali aweze kuendesha biashara yake kwa ufanisi mkubwa.

Tena siyo lazima uandike mpango wa biashara kwenye karatasi ndipo ukusaidie hapana, kufahamu tu akilini ni kitu gani kinachotakiwa kufanya, ni hatua zipi ufuate wakati wa kuendesha biashara yako inatosha. Na hili utalifahamu pindi utakapopitia na kusoma michanganuo mbalimbali halisi iliyokwisha andikwa tayari, wala haitakuchukua muda mrefu jinsi unavyofikiri.

Self Help Books Tumekuandalia kitabu kizuri kilichokuwa na maelezo ya kutosha juu ya namna ya kuandaa mipango ya biashara kutoka A-Z, isitoshe kina michanganuo kamili unayoweza kuichukua kama mifano na vielelezo wakati utakapokuwa ukiandaa mpango wa biashara yako, angalizo ni kwamba usikopi, bali tumia kama vielelezo kwani kila biashara ni tofauti, biashara ‘X’ mazingira, soko na kila kitu ni tofauti na biashara ‘Y’.
KITABU CHA MPANGO WA BIASHARA(BUSINESS PLAN BOOK)
Ununuapo kitabu hiki, unapata na ofa ya kuingia ‘SEMINA HII YA MICHANGANUO YA BIASHARA’bure.
Bei ya kitabu ni sh. elfu 10 softcopy na sh.elfu 20 hardcopy

Ukitaka kuona vitabu vingine vya Self help books fungua, SMART BOOKS TANZANIA


Peter A. Tarimo
Self Help Books Tanzania

0712202244   &  0765553030

0 Response to "JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA YAKO, DONDOO HIZI 3 NI MUHIMU SANA"

Post a Comment