KUFA AU KUANGUKA KWA BIASHARA YAKO NDOGO FANYA VITU HIVI 9 KUJIEPUSHA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUFA AU KUANGUKA KWA BIASHARA YAKO NDOGO FANYA VITU HIVI 9 KUJIEPUSHA?

1. Jiandae kuanguka.
Unapojiandaa kwa maanguko haina maana kuwa unafahamu kwamba utaanguka hapana. Kuna usemi maarufu usemao, “Wakati wa amani, ndiyo muda mzuri wa kufanya mazoezi kujiandaa na vita” Usisubiri mpaka biashara ife ndipo uanze kujiuliza imekufa kufaje kwani mafanikio au kuanguka kwa biashara yako kunakutegemea wewe na kupo chini ya uthibiti wako, wewe ndiye utakayeamua kufeli au kufanikiwa kwake. Jiandae kwa vyote, mafanikio, lakini pia usiache kujiandaa na maanguko.

Jiandae kuanguka lakini huku ukifanya kila jitihada zilizopo ndani ya uwezo wako kuhakikisha unazuia usianguke na kamwe hautaanguka. Sababu moja kubwa inayowafanya wajasiriamali kushindwa ni kwa sababu wanaogopa kushindwa(woga), na kwa hiyo woga huo wa kushindwa huwasababisha washindwe kuwa wabunifu katika biashara zao. Wengine hudhani kwamba kuhofia sana kushindwa kunasaidia kumfanya mtu ajitume zaidi na zaidi lakini hilo siyo kweli hasa kwa upande wa ujasiriamali. Inaweza ikawa  kweli katika upande wa ajira.

SOMA: Kutafuta soko la bidhaa zako kunahitaji ubunifu.


Unapohofia sana maanguko, kunakufanya uwe makini kupita kiasi jambo litakalokufanya pia uogope kujaribu mambo mengi na hivyo kupoteza fursa nyingi za kukufanya ufanikiwe. Wajasiriamali wa kweli “huogelea katika bahari hiyo hiyo iliyojaa maanguko pasipo kuhofia kitu chochote”. Kujiandaa kisaikolojia kutakufanya  hata ukianguka uweze kuinuka tena upya haraka bila kuchelewa.

2. Kuwa makini sana na maamuzi unayoyafanya.
Wewe ni mjasiriamali na hivyo ndiye rubani wa biashara yako. Kwa hiyo mafanikio ya kesho ya biashara yako  yatategemea kwa kiasi kukubwa maamuzi unayoyafanya leo. Hivyo usije ukafanya maamuzi ya kukurupuka; ikiwa una mashaka na uamuzi unaokaribia kuufanya,, basi tafuta wataalamu wa ushauri ili uweze kujadiliana nao juu ya hayo maamuzi.

Ni bora kuahirisha mpaka umepata suluhisho kuliko biashara yako kuja kufa kirahisi. Kabla hujafanya maamuzi muhimu, tafuta kwanza taarifa nyingi kwa kadiri itakavyowezekana, zitathmini vyema na kupima uzuri na ubaya wake, jadiliana na washirika wako wa karibu na mwisho fanya maamuzi moyo wako utakayokuambia ufanye.
3. Chunga sana mtiririko wako wa fedha.
Kwenye kitabu, “Mifereji 7ya pesa na siri matajiri wasiyopenda kuitoa”, Toleo jipya la 2016, kuna Sura iliyoongezwa pale inayosema “HESABU MUHIMU KULIKO NYINGINE ZOTE KATIKA BIASHARA” Sura hiyo imezungumzia kwa kina sana juu ya uhai wa biashara yeyote ile ambao ni PESA TASLIMU(CASH). 

Kuna vitu vingi sana kuhusiana na mzunguko wa pesa ambavyo wajasiriamali tunavichukulia rahisirahisi kumbe vinatugharimu vibaya sana na mara nyingi inakuwa ndiyo chanzo cha kuanguka kwetu kibiashara.

“Mzunguko wa pesa ni sawa na damu katika mwili wa binadamu”, “pesa ni mfalme” (cash is aking) nk. Hayo ni baadhi tu ya maneno ambayo bila shaka yeyote ile hakuna mtu ambaye hajawahi kukutana nayo mahali katika ulimwengu wa biashara. Hii yote ni kuonyesha ni jinsi gani pesa na hasa ‘pesa taslimu’ ilivyokuwa muhimu katika uhai wa biashara.

Hakikisha muda wote biashara yako inaingiza pesa nyingi kuliko vile inavyotoa. Ni lazima utumie mbinu na mikakati itakayowashawishi wateja wako kukulipa mapema na wakati huo huo kwa upande wako kuchelewesha malipo kwa wale wanaokudai.

5. Usiogope Mabadiliko.
Ifanye biashara yako kuendana na mabadiliko. Katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kubwa, mjasiriamali unatakiwa uwe mbunifu kwa kubadilisha mambo mabaya yanayoambatana na mabadiliko hayo kuwa fursa badala ya kuyatazama kwa jicho la maafa. Kumbuka mabadiliko ni rafiki na siyo adui.

6. Ongeza bajeti yako ya masoko na mauzo.
Lengo la kutafuta soko ni ili kuwafahamu vizuri wateja wako kusudi uweze kuwahudumia vizuri zaidi, bidhaa au huduma unazozalisha na mwishowe kufanya mauzo makubwa. Lakini kosa moja kubwa wenye biashara wengi wanalofanya ni kupunguza bajeti ya masoko na mauzo kipindi mambo yanapokuwa magumu au biashara kudorora. Badala ya kufanya hivyo zidisha bajeti yako ya masoko kuhakikisha wateja na washindani wako wote wanaendelea kujua uwepo wako.

7. Jenga mahusiano mazuri na wafanyakazi wako.
Waheshimu na kuwahudumia vizuri watu unaofanya nao kazi, na wao pia utaona wakikurudishia heshima na huduma kama ulizowatendea. Wafanyakazi ni sehemu ya biashara yako hivyo watendee kwa kadiri unavyopenda na wao waitendee biashara yako. Wape zawadi bila ya wao kutegemea katika sikukuu zao za kuzaliwa au hata pale wanapofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kazini.
8. Kuwa makini unapoajiri mfanyakazi/wafanyakazi.
Upo usemi usemao “Ajiri taratibu lakini fukuza haraka”, maana yake ni kuwa, kamwe usije ukachukulia rahisirshisi wakati wa kuajiri mfanyakazi, weka umakini wa kutosha kuhakikisha unaajiri mtu sahihi. Ni bora ukatumia hata gharama kubwa kumpata mfanyakazi aliyekuwa bora kuepusha kuja kuiumiza biashara yako kwa muda wa kipindi kirefu kijacho.

Vivyo hivyo ikiwa mfanyakazi utaona “anazingua” usifanye naye mzaha hata kidogo, haraka muondoe kabla mambo hayajaharibika. Usipofanya hivyo anaweza hata akawaambukiza ubaya wafanyakazi wengine ikiwa wapo wengi na wao wakaanza kuharibu kazi.

9.Tunza wateja uliokuwa nao.
Kwenye biashara yupo bosi mmoja tu, na anao uwezo wa kumtimua kazi mtu yeyote katika kampuni/biashara kuanzia mmiliki mwenyewe kwa kuamua kutumia pesa zake mahali pengine. Mteja ndiyo rasilimali kubwa katika biashara yako kushinda rasilimali zingine zote kwani bila yeye na biashara nayo haipo. Wataalamu wa biashara wanatanabahisha kwamba “NI VIGUMU MNO KUMPATA MTEJA MPYA KULIKO KUMTUNZA MTEJA ULIYEKUWA NAYE TAYARI”

Wateja wako uliokuwa nao ndiyo kitu muhimu zaidi katika ukuaji wa biashara yako ndogo, hivyo watunze  kwa kuwatendea mema na wao watakwenda kukutangaza vizuri na biashara yako kwa watu wengine huko mitaani.

Swali ninalokuachia ni hili hapa;

Ni nini kitakachotokea ikiwa wateja wako watakuhama?  


……………………………………………………………...

Nakutakia biashara njema, na endapo utataka kujipatia vitabu mbalimbali vinavyotolewa na Self Help Books tembelea Blogu/ukurasa huu, SMART BOOKS TANZANIA

Mhamasishji na Mwandishi wako;

Peter A. Tarimo.

0 Response to "KUFA AU KUANGUKA KWA BIASHARA YAKO NDOGO FANYA VITU HIVI 9 KUJIEPUSHA?"

Post a Comment