MAKTABA YA VITABU INAYOTEMBEA MASHULENI MWANZA(LITTLE TRAVELLING LIBRARY) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAKTABA YA VITABU INAYOTEMBEA MASHULENI MWANZA(LITTLE TRAVELLING LIBRARY)


Ni  ubunifu wa vijana wawili ndugu, Innocent Junior na Innocent senior walioamua kuanzisha Ujasiriamali wa kijamii baada ya kuhitimu Elimu yao ya chuo kikuu katika chuo kikuu cha Mt. Augustine. Hutumia matoroli kama maktaba ya vitabu kwa watoto wa shule za awali na msingi Mkoani Mwanza. 

Soma pia: Teknolojia itakayowakomboa wasanii wa video na muziki Tanzania. 

Vijana hawa baada ya kubaini matatizo mbalimbali  yanayowakabili watoto wadogo wanafunzi wa shule za msingi katika kupata vitabu vya kujisomea, tatizo la lugha hasa kutoifahamu vyema lugha ya kiingereza, kutokuwa na ari ya kujisomea vitabu, ukosefu wa mazingira mazuri ya kujisomea, shida ya umeme hasa nyakati za usiku, ukosefu wa mikoba mizuri ya kuhifadhia na kubebea vifaa vya shule kama madaftari, kalamu nk. waliamua kuanzisha shirika lisilokuwa la kiserikali lijulikanalo kama, “My Little Traveling Library” au Maktaba inayotembea.

Vijana hawa huenda mashuleni wakiwa na matoroli yao yaliyobeba vitabu, na baada ya kuomba ruksa kutoka mamlaka husika, hugawa vitabu hivyo bure kwa watoto wanafunzi ili kuwajengea utamaduni mzuri wa kujisomea maishani mwao. Wanafunzi hao baada ya kusoma vitabu hivyo hatimaye huvirudisha na kuazima tena vitabu vingine.

Watoto wakifurahia vitabu.
Wanawatofautisha watoto katika makundi ‘grades’ kuanzia grade 1 mpkaka grade 8 ambapo grade 8 wanakuwa wameshaweza kusoma na kuelezea kile walichokisoma mbele ya darasa(representations). Hali hii imeongeza mahudhurio na ufanisi wa watoto katika mashule wanakohudumia.

Katika kuinua ufahamu na ari ya wanafunzi kupenda kujifunza, My little travelling library pia wameanzisha mashindano ya kusoma baina ya shule na shule na hata madarasa kwa madarasa. Mbali na hayo pia wameanzisha timu ya mpira, picnics, klabu za midahalo(debates) pamoja na kuonyesha video mbalimbali za masomo muhimu kama ya sayansi kwa kutumia projekta.
My Little Travelling Library inadhaminiwa na mradi wa Kampuni ya simu ya Tigo ujulikanao kama “Tigo Digital Change Makers” ambapo wao ni washindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2014.

Soma na: David Adjae, mbunifu majengo wa kimataifa aliyezaliwa Tanzania.

Ili Taasisi hii iweze kujitegemeza yenyewe, wameanzisha mradi mwingine wa kutengeneza na kuuza mabegi mazuri kwa ajili ya kubebea vifaa vya shule vikiwamo vitabu na zana zingine za darasani. Mikoba hii au mabegi yametengenezwa kwa vitambaa, maarufu kama “Mashuka ya Kimaasai.”

Mabegi hayo yakitengenezwa.
Kitu kingine kizuri cha ubunifu katika mabegi hayo ni kwamba yameunganishwa na mfumo maalumu wa umeme-jua ‘solar’ ambao humuwezesha mtoto nyakati za usiku kuunganisha balbu ambayo huwaka na kumuwezesha kusoma bila shida.

Kwa habari zaidi kuhusiana na Asasi hii ya My Little Traveling Library unaweza ukatembelea website yao hii hapa.

Sikiliza makala hiyo katika sauti kama ilivyotolewa na Redio Deutsche welle Ujerumani siku ya Jumatano tarehe 25 may 2016.  


CHANZO cha makala haya ni Tovuti ya My Little Travelling Library pamoja na Redio DW Ujerumani idhaa ya kiswahili.  

0 Response to "MAKTABA YA VITABU INAYOTEMBEA MASHULENI MWANZA(LITTLE TRAVELLING LIBRARY)"

Post a Comment