NILIVYOINGIZA PESA KIRAHISI KARIAKOO HATA NIKIWA NIMELALA USIKU KWA MTAJI KIDOGO SANA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NILIVYOINGIZA PESA KIRAHISI KARIAKOO HATA NIKIWA NIMELALA USIKU KWA MTAJI KIDOGO SANA

Nikiwa kwenye biashara yangu ya rejareja napigapiga hesabu

Siyo stori ya mtu mwingine wala riwaya ya kutunga, ni simulizi yangu mwenyewe binafsi ya ukweli ya jinsi nilivyoweza kutengeneza pesa haraka na kwa urahisi hata usiku nilipokuwa nimelala kupitia wazo la biashara ya mtaji kidogo ya rejareja niliyoibuni mwenyewe. 

Faida ilikuwa kubwa ya kushangaza na karibu kila mtu aliyenifahamu akastaajabu. Marafiki zangu wengi walinifuata kutaka kufahamu ni nini ilikuwa siri yangu kubwa ya kupata mafanikio haraka kiasi kile katika biashara ya duka la rejareja tofauti na watu wengi ambapo huwachukua kipindi cha muda mrefu kuona mafanikio ya maana.

Mafanikio katika aina za biashara ndogondogo nyingi hasa katika hatua zake za mwanzo siyo duka la rejareja tu bali hata na biashara za aina nyingine mfano biashara ya chakula, biashara ya nafaka, biashara za ufugaji wa kuku, biashara za kusafiri nje ya nchi nk.hutegemea sana ubunifu kuliko hata mtu kuwa na mtaji mkubwa.

Unaweza kuwa na mtaji kidogo sana au hata kutokuwa na mtaji kabisa lakini kwa kutumia tu ubunifu hatimaye ukaweza kuondoka kwenye hatua duni uliyopo kimtaji na kuweza kujenga biashara kubwa ya ndoto yako tena iliyo na faida ya haraka.

Mbinu na siri zenyewe nilizotumia kutengeneza pesa kirahisi nikiwa mtaa wa msimbazi pale kariakoo kwa mtaji kidogo sana

Sipendi kukuchosha na maelezo mengi mpenzi msomaji na moja kwa moja nitakwenda kwenye pointi. Nikiwa nimehangaika kwa muda mrefu na biashara ndogondogo nyingi za mtaji mdogo ikiwemo kuuza chipsi pale Tandale stendi kwa Mtogole katika fremu za Mzee Kirongo, hatimaye niliamua kujaribu biashara maeneo mengine yenye mzunguko mkubwa zaidi wa watu, hata hivyo kikwazo kikubwa kilikuwa ni mtaji kwani siyo rahisi kuanzisha biashara maeneo ya watu wengi mfano Kariakoo ikiwa kama huna pesa za kutosha kulipia fremu.

Lakini wazo likanijia ghafla akilini, kulikuwa na kaka yangu alikuwa na duka la kontena la rejareja maeneo ya Kariakoo Msimbazi opposite na kilipo kituo cha polisi na palikuwa na eneo la vibanda pia. Nilimuomba kaka niwe naweka biashara ya vinywaji vya rejareja pembeni mwa lile kontena lake usiku muda ambao yeye anakuwa amefunga biashara na namshukuru Mungu alikubali.

Maandalizi ya vifaa na Mtaji  

Kiukweli nilikuwa na pesa kidogo sana mfukoni pengine ya kutosha mlo wa siku mbili tatu tu lakini siyo mtaji hata wa genge dogo. Nilichokifanya nikamwomba kaka awe ananikopesha vinywaji na bidhaa zile tu zenye uwezekano wa kutoka harakaharaka usiku kama vile soda, juisi, malta, keki, biskuti, crisp za viazi na maji ya chupa.

Vifaa muhimu nilivyohitaji kwa ajili ya kuanza ilikuwa ni friji na kwa kuwa sikuwa na fedha za kununua ikanibidi niazime friji la kampuni ya pepsi. Kifaa kingie muhimu lilikuwa ni kabati la mbao na kioo kwa ajili ya kupanga zile bidhaa ndogondogo. Hili nilitumia kabati la zamani la kuuzia chipsi, nikalipeleka kwa fundi akalipiga msasa na kuliwekea carpet jipya kusudi liwe na muonekanao mzuri wa kuvutia wateja

Pia nilitafuta matenga 2 ya nyanya ya mbao pale shimoni sokoni Kariakoo kwa ajili ya kuyafanya kama stendi ya kabati langu. Kitu kingine cha msingi niliazima viti 2 vya chuma nikanunua na benchi moja kwa ajili ya kukaa wateja na stuli moja niliyokalia mwenyewe na wakati mwingine kuigeuza kama meza ya wateja.

Muda wa jioni ulipofika kuanzia saa 1 nilianza maandalizi kwa kuchukua bidhaa dukani kwa kaka, tulikuwa na daftari maalumu la kurekodi bidhaa zote nilizokopa na kisha kuanzia saa 2 mpaka saa 4 muda yeye anafunga duka lake ulikuwa ni muda wa mimi kupangapanga vitu kwenye kabati na vinywaji katika friji langu la pepsi. Ilinibidi kuchanganya kila kitu humohumo mpaka maji na malta ingawa maafisa wa pepsi hawakuwa wakipenda kabisa suala hili lakini kwa kuwa ilikuwa ni usiku hawakuweza kunizuia.

Kazi ya kuuza ilianza saa 4 mpaka asubuhi saa 1 kaka anapofika kufungua kontena lake. Akifika kama kawaida tulichukua daftari letu na peni kisha tukafanya hesabu na kumlipa fedha za mauzo ya bidhaa nilizochukua jana usiku. Alinipigia hesabu kwa bei ya kununuli na mara chache alizidisha kidogo ili na yeye apate faida kidogo lakini alihakikisha ananiachia faida kiasi fulani.

Usiku mauzo yalikuwa mazuri sana na mara nyingi niliishiwa vinywaji vyote kabla ya kupambazuka. Wateja ulipofika usiku wa manane walimiminika kutoka maeneo mbalimbali ya jiji kuja kutafuta hasa chipsi na vinywaji baridi kwa kuwa maeneo mengi muda huo yanakuwa yamefungwa.

Wateja wengi walitoka Kariakoo sokoni, Magomeni kwa  Macheni ilipokuwa club maarufu ya usiku na madereva wa teksi na daladala. Jirani yangu kulikuwa na mzee mmoja muuza chipsi tulimwita kwa utani “Mzee Shebe” (Mzee Shabani). Karibu kila siku ikifika saa 8 usiku Shebe alikuwa keshamaliza chipsi zote, mishikaki, kuku na mayai.

Miezi michache ilinibidi nimwajiri kijana msaidizi (Christopher) maana nilipata wazo la kujenga kabisa banda la mabati ya kontena kusudi niwe nafanya biashara usiku na mchana. Nakumba kioski changu sikujihangaisha kuweka mlango kwani tulikuwa tukifanya kazi masaa 24 kwa kupokezana. Siku nilikuja kuona umuhimu wa kuchomelea mlango ni siku ambayo kulitokea maandamano jijini Dar es salaam polisi wakaamuru kila mtu afunge biashara yake. Kwangu ilikuwa shughuli pevu kwelikweli, ikanibidi siku ya pili yake nimwite fundi haraka sana aje kuniwekea mlango wa chuma.

Ndani ya mwaka mmoja niliweza kumuajri mfanyakazi wa pili (Dada Mese) kwa ajili ya kuuza masaa ya mchana kwani binafsi nilikuwa nahudhuria kozi fulani na hivyo nisingeliweza tena kumpokea mfanyakazi wa usiku.

Tukawa jumla watu watatu sasa ila mimi jukumu langu kubwa likiwa kama meneja, naenda kununua bidhaa asubuhi kila siku vijana wanapiga kazi. Hapa sasa ndipo nilipojifunza wakati mwingine kwa uchungu mkubwa mambo mengi juu ya usimamizi wa duka kwani ndipo penye “kupigwa” na kila aina ya changamoto za biashara ya rejareja.

Kufupisha mlolongo wa mambo, stori hii katika picha za rangi nilizopiga tangu siku za mwanzo wa biashara hii nikiwa na kabati langu kuu-kuu la chipsi na friji la kuazima Pepsi nimezishea kwenye kitabu changu kiitwacho, MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA kuanzia ukurasa wa 10

Katika kitabu hiki nimeelezea kwa kirefu mbinu mbalimbali nilizotumia kufanikiwa na ni wapi pia nilifanya makosa mbalimbali yaliyonigharimu hata sasa hivi kutamani laiti ningalikuwa na uelewa/maarifa niliyokuwa nayo leo hii.

Kwa kifupi kabisa vitu 2 vikubwa vilivyonibusti sana mpaka biashara yangu ya rejareja ikakua haraka namna ile  ni hivi vifuatavyo ;

1. Eneo zuri la biashara/Location

Msimbazi Kariakoo bila shaka yeyote kila mtu angependa kuwa na biashara eneo kama lile. Katika biashara za rejareja hasa duka eneo lililo na pilikapilika nyingi za watu kama Kariakoo ni hot Cake sana, linaweza kukufanyia maajabu watu wakadhani labda umetumia madawa ya kienyeji (ndumba) kumbe ukweli wala hamna kitu kama hicho.

2. Ubunifu

Mara nyingi pale unapoona mambo hayawezekaniki kabisa basi ujue hapo ndio mpenyo wako ulipo na fursa ya biashara itakayobadilisha maisha yako kwa kutumia ubunifu. Sugua akili yako kupata majibu yaliyojificha ndani mambo yawezekane

Nilipoona sina kabisa uwezo wa kukodisha fremu ya malaki ya pesa Kariakoo, sikusubiri mpaka niwe na uwezo huo bali nilianza tu na kidogo nlichokuwa nacho mkononi, friji la pepsi moja la kuazima na kabati kuu-kuu la chipsi.

Kwa kutumia fursa iliyokuwepo muda ule ya kuanzisha vibanda mitaani niliweza hatimaye kuanzisha biashara yangu ya kwanza ya rejareja ya maana pasipokuwa na mtaji wowote ule mkubwa. Nikagundua kumbe kuanzisha biashara yenye faida elfu 20,000, elfu 30 na hata elfu 50 kwa siku moja lilikuwa ni jambo linalowezekana kabisa

Ubunifu mwingine naweza nikasema ulikuwa ni ile hali ya kutengeneza pesa hata pale nilipokuwa nimlala usiku. Mimi niligundua kwamba muda watu wanafunga biashara zao kariakoo usiku saa 3 –saa4 ulikuwa muda mzuri na mimi kuanza kuuza bidhaa zangu kwani Kariakoo hakuna usiku wala mchana, wateja wapo masaa 24 hasa wa bidhaa nilizozilenga.

Kingine ni kuweka wasaidizi, wakati nikiwa nimelala usiku, kijana aliendelea kuuza na hivyo pesa kuingia nikiwa usingizini. Aina za biashara ndogondogo nyingi watu huogopa sana kuajiri vijana lakini hapa niligundua mbinu ambazo mtu unaweza ukazitumia na wala usihofie kitu chochote kuajiri watu hata ingelikuwa ni biashara ya mtaji wa 50,000 au hata biashara ya kufanya ukiwa nyumbani pasipokuwa na fremu mahali popote

Sisemi kila mtu atumie ubunifu niliotumia mimi la hasha, kuna ubunifu wa aina nyingi mtu unaweza ukafanya fedha zikaingia ukiwa umelala. Tumeanza kampeni kwenye Mastermind group letu la Michanganuo-online na blogu yetu hii kuibua bunifu mbalimbali za kibiashara usikose kufuatana nasi kila siku.

Je, ungependa pia kujua ni changamoto zipi nilikutana nazo mbali na mafanikio na sasa natamani laiti muda ule ningelikuwa na maarifa na uelewa niliokuwa nao sasa hivi? Basi usikose nakala ya kitabu chako cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA

Utafahamu kila kitu kusudi nawewe usijerudia makosa wala kuchukua muda niliochukua mimi kugundua ni kipi kinachofanya kazi na ni kipi hakifanyi kazi.

Kitabu hiki unaweza kukipata kwa njia mbalimbali kama ifuatavyo;

1.   Kukidownload sasa hivi hata kabla hujazima simu au kompyuta yako hii, Bofya hapa na kisha fanya malipo (Tsh. 6,000/=) kwa mtandao wako wa simu.

2.   Kupata nakala ngumu ya karatasi (Hardcopy) kama upo Dar es salaam ni sh. 16,000/= tunakuletea mpaka ulipo unalipia na kupokea kitabu chako

3.   Kupata nakala ngumu ya karatasi (Hardcopy) kama upo mkoa mwingine wowote ni sh. 26,000/= Tunakutumia kwa njia ya basi mpaka ulipo.

Kwa maelezo zaidi au shida yeyote wakati wa kununua kitabu kwa mtandao wa simu wasiliana nasi kupitia; Watsap/Call: 0765553030 au 0712202244, Peter Augustino Tarimo

 

HUDUMA ZETU NYINGINE

1. MasterMind Group la Michanganuo-online

Ndani ya group hili tunajifunza Michanganuo ya biashara na UBUNIFU kila siku. Kujiunga na group unalipia Kitabu cha Michanganuo ya Biashara & Ujasirimali pamoja na Michanganuo mingineyo mbalimbali ya OFFA, vitu tutakavyokutumia punde ulipiapo shilingi 10,000/= na hii ni ada ya mwaka mzima. Namba za kulipia ni 0765553030 au 0712202244, Peter Augustino Tarimo

2. Huduma ya kuandikiwa Mchanganuo wa Biashara yako

Tunaandika Business Plan kwa ajili ya biashara yeyote ile kubwa na ndogo. Gharama zetu ni nafuu kushinda kwingineko na tunachaji asilimia 1% tu ya mtaji mzima wa biashara tunayoandikia. Karibu sana tukutengenezee plan inayoendana na biashara yako halisi na siyo kukopi na kupaste. Kuona sehemu ndogo ya Mihutasari ya kazi za watu na makampuni tuliyowahi kufanya nao kazi bofya hapa>>Our Portfolio.

 

 

 

SOMA NA HIZI HAPA;

1.   Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala.

2.   Jinsi ya kujua faida ya duka la rejareja kila siku jioni unapofunga hesabu

3.   Unajua biashara yenye faida kubwa nay a haraka mara 2 ya mtaji utakaowekeza?

4.   Biashara ya mtaji wa million mbili (2) ninayoweza kufanya ni ipi? naomba msaada

5.   Kama una biashara ndogo ya mtaji mdogo, hizi hapa njia 11 za kuibusti

6.   Mchanganuo wa biashara ya genge la kisasa la matunda, mbogamboga na vyakula

 

2 Responses to "NILIVYOINGIZA PESA KIRAHISI KARIAKOO HATA NIKIWA NIMELALA USIKU KWA MTAJI KIDOGO SANA"

  1. Hongera Sana kwa hatua hiyo nimejifunza pakubwa kupitia story yako

    ReplyDelete
    Replies
    1. Pia Asante sana Anonymous, kwa kusoma makala hii ubarikiwe !

      Delete