HYDROPONIC FODDER: JINSI YA KUOTESHA MAJANI YA MIFUGO KATIKA TREI ZA ALUMINIUM NA PLASTIKI BILA UDONGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HYDROPONIC FODDER: JINSI YA KUOTESHA MAJANI YA MIFUGO KATIKA TREI ZA ALUMINIUM NA PLASTIKI BILA UDONGO

trei la majani ya hydroponic fodder
Safu yetu ya Ushauri wa biashara leo tumepata swali kutoka kwa msomaji wetu aliyeko Kibaha mkoa wa Pwani na aliuliza kupitia watsap kama ifuatavyo;

Tafadhali naomba kufahamu kwa kina hatua mbalimbali za kufuata ili niweze kutengeneza chakula cha kuku kiitwacho hydroponic folder, pia kama mnajua ni wapi yanakopatikana matrei ya aluminium kwa ajili ya kilimo hiki mnijulishe.
Asanteni sana,
JL. Martin
Kibaha.

MAJIBU.
Asante sana ndugu Martin kwa swali lako zuri kabisa, kwanza kabisa chakula hiki, hydroponic fodder (siyo folder), au majani haya ya kulishia mifugo huwa hayatengenezwi kama ulivyotaja hapo juu kwamba unataka kujua jinsi ya kutengeneza hydroponic fodder, bali mbegu huoteshwa na kumea kama mimea mingine yeyote ile isipokuwa tu hii huwa haioteshwi katika udongo kama mimea mingine bali ni katika vyombo maalumu au matrei yaliyotobolewa mashimo kwa chini.

Utaalamu huu wa hydroponikia hautumiki tu katika kutayarisha chakula kwa ajili ya wanyama au mifugo bali pia hutumika katika utayarishaji au uoteshaji wa mbogamboga na matunda mbalimbali pia kwa ajili ya binadamu. Lakini kwa kuwa swali hili msomaji umetaka kufahamu zaidi juu ya namna ya kutengeneza mfumo wa kuotesha hydroponic fodder za kulishia mifugo basi majibu yetu tutajikita zaidi katika eneo hilo la mifugo ambao kwa kiasi kikubwa ni Ng’ombe, mbuzi, kuku, sungura, ndege wengine wafugwao, kondoo nk.


Kilimo cha hydroponic nchini (hydroponic farming in Tanzania) kama ilivyokuwa kwa kilimo cha azolla chakula kingine cha kupunguza gharama za ufugaji, hakijazoeleka sana na wala hakijawa maarufu kutokana na wakulima na wafugaji wengi kutokuwa na ujuzi wa jinsi ya kutengeneza mifumo ya hydroponikia(hydroponic systems)

HATUA ZA KUPITIA UNAPOTAKA KUTENGENEZA MFUMO WA HYDROPONIC FODDER.

Mfumo wa hydroponikia hujumuisha chanja zilizobeba trei kwa ajili ya kuotesha mbegu za kuzalisha hydroponic fodder. Lakini pia kwanza ikumbukwe kwamba kuotesha au kuzalisha majani ya kuliwa na mifugo bila kutumia udongo, hydroponic fodder siyo lazima mtu atumie vifaa vya kisasa sana na vya bei kubwa. Mkulima au mfugaji anaweza kuandaa hydroponic fodder zake kwa kutumia vifaa vinavyoweza kupatikana kwa urahisi kabisa katika mazingira yake anayoishi.


Hii itategemea pia na ukubwa wa kilimo cha hydroponic unachotaka kufanya kwa mfano ikiwa unayo mifugo michache tu kama labda ni kuku 50 na ngombe wawili au watatu huhitaji gharama kubwa sana kutengeneza mfumo wako wa kuzalisha majani mabichi ya hydroponic fodder. Faida za hydroponic pia naamini unazifahamu na zinajulikana na watu wengi siku hizi lakini kwa kifupi tu ni kwamba hydroponic fodder faida yake kubwa kati ya nyingi iliyokuwa nazo ni kumpunguzia mfugaji gharama za uzalishaji hasa zile za chakula kwa zaidi ya asilimia 50%


Sasa hebu tuone hatua zenyewe kamili, ni jinsi gani mtu kwa kutumia tu maji bila ya udongo anavyoweza kuotesha mbegu kwa ajili ya kupata hydroponic fodder au majani yanayoweza kutumika kulisha mifugo karibu aina zote wanaofugwa na binadamu.

MAHITAJI MAKUBWA WAKATI WA UTAYARISHAJI HYDROPONIC FODDER

1.ENEO/BANDA AU NYUMBA
Hapa ni mahali utakapopanga trei  au vyombo vyako utakavyotumia kwa ajili ya kuoteshea mimea(hydroponic fodder). Hydroponic fodder hazihitaji  mwanga mkali kwani zenyewe hujitengenezea nishati na chakula zenyewe kutokana na wanga uliojaa katika mbegu, kwahiyo ni vizuri ukapanga matrei ndani ya eneo lililokingwa na mwanga mkali wa jua.


VITALU: Hiki ni kichanja kinachotumika kwa ajili ya kupanga vyombo au trei zako za hydroponic fodder. Unaweza kutengeneza kwa kutumia material zozote zile kama mbao, mabati au chuma ilimradi kiweze kubeba matrei yako vizuri. Unaweza ukapanga kama ‘ghorofa’ kwenda juu au ukaweka kichanja kimoja tu kulingana na nafasi au ukubwa wa mfumo wako unaotaka kutengeneza. Siyo lazima iwe ni chanja matrei unaweza kuyapanga juu ya kitu chochote kile likichoinuka hata juu ya meza au stuli unaweza kuweka ilimradi tu uhakikishe maji yanapochuruzika hayatuami mahali, yanakwenda moja kwa moja katika chombo au mfereji utakaoyaondosha katika mfumo wako wa hydroponic fodder.

JOTO: Joto nalo halitakiwi kuwa kubwa sana wala kidogo sana bali liwe la wastani tu kuanzia wastani wa nyuzijoto 17 mpaka 25 za sentigredi. Joto linapokuwa kubwa kupita kiasi mbegu huchachuka na kuharibika na likiwa kidogo sana pia mimea huota taratibu mno.

2. MATREI(VYOMBO VYA KUOTESHEA)

trei za fodder

Vyombo kwa ajili ya kutayarishia hydroponic  fodder vinaweza kuwa ni vya umbo lolote lile  ilimradi tu kisiwe ni chombo kinachoweza kushika kutu au kutengeneza kuvu kwa urahisi. Kwa mfano unaweza hata kutumia hata ungo au beseni kama lile la kuogea baada ya kulitoboa matundu kama majaribio ikiwa ndio unataka kuanza kuona jinsi hydroponic fodder zinavyokuzwa.


Lakini aina ya vyombo vinavyokubalika zaidi kitaalamu kutumika katika uoteshaji wa mimea, hydroponic fodder kwa ajili ya kulishia mifugo ni matrei ya aluminium au matrei ya plastiki. Trei la aluminiam ndiyo bora zaidi kuliko hata la plastiki ingawa gharama zake ni kubwa kidogo, halishiki kutu wala kutengeneza kuvu inayoweza kuharibu mimea yako na hatimaye kuwadhuru mifugo na binadamu pia.

Vipimo na ukubwa wa trei la hydroponic fodder au chombo chochote kile utakachotumia kuandalia hydroponic fodder zako itategemea ni kiasi gani cha majani unachotaka kuzalisha na upatikanaji wa vyombo vyenyewe kwa mfano ikiwa vifaa(matrei) ya aluminium unaweza kuyapata kwa urahisi basi yatumie kwani ndiyo bora zaidi kuyatumia na ikiwa vyombo au matrei ya plastic  ndiyo rahisi zaidi kwako kupatikana basi tumia hayo ukifuata taratibu zinazotakiwa kuyafanyia usafi.


Usafi wa trei za hydroponic fodder au vyombo vingine vyovyote utakavyotumia ni  lazima uhakikishe unakuwa ni wa hali ya juu kabisa kabla ya kuotesha mbegu zako na ikiwa utatumia trei au vyombo vya plastiki itakubidi uongeze umakini zaidi katika usafi huo kwani plastiki hushika kuvu kwa urahisi zaidi kuliko aluminiam. Ni vizuri vyombo vyako au matrei ya kutayarishia hydroponic fodder ukayasafisha kwa kutumia mchanganyiko wa maji na dawa ya kuulia vimelea na wadudu wa magojwa kama vile dawa ya chlorine au Hydrogen Peroxide. Clorini ni kama vile dawa unayoona ya kutibu maji(water guard) au hata JIKI ya kufulia nguo na hupatikana kirahisi sana madukani.

Matrei pia yanatakiwa yawe na matobo upande wa chini ili kupitisha maji unaponyweshea mimea yako maji. Matrei au vyombo hupangwa juu ya vichanja au maumbo yaliyotengenezwa kwa ajili hiyo ndani ya chumba au eneo ulilotayarisha.

3.MBEGU ZA HYDROPONIC FODDER
Mbegu kwa ajili ya utayarishaji wa hydroponic fodder zinaweza zikawa ni za nafaka aina yeyote ile imeayo lakini nafaka zinazopendekezwa zaidi kitaalamu na zinazotoa kimea au majani bora yenye virutubisho vingi kwa wanyama ni mtama, ngano na shayiri. Mbegu nyingine zinazofaa ni Mahindi, Ulezi, Uwele nk.


Matayarisho ya mbegu za hydroponic fodder.
Mbegu zinatakiwa zichaguliwe zile tu zilizokuwa bora kwa maana ya mbegu ambazo hazijatobolewa na wadudu wala zisizokuwa na makapi . Mbegu zilowekwe kwa muda wa masaa 2 katika maji ya dawa (chlorine)  na zisafishwe vizuri kwa  maji safi na kusuuzwa ili kuondoa kabisa uwezekano wa kuota kwa kuvu au viini vingine vya magonjwa vitakavyoweza kuathiri uotaji wa fodder zenyewe, au hata kusababisha magojwa kwa wanyama watakaokula hydroponic fodder zako. Unaweza kutumia ndoo za kawaida za plastiki au beseni wakati wa uoshaji au utakapoloweka mbegu zako.Hakikisha pia mbegu zako hazina sumu yeyote wala kemikali hatarishi inayoweza kudhuru wanyama na binadamu.

4. MAJI
Maji safi na salama yatahitajika wakati wa kuziosha mbegu na kunyweshea mimea ya hydroponic fodder. Maji yanayotiririka chini ya trei siyo vizuri kuyakinga na kuyatumia tena kwa ajili ya kumwagilia mimea ya hydroponic kwani  yanaweza yakawa ni chanzo cha mazalia ya viini vya magonjwa kwa mimea hiyo na mifugo pia kama fangasi na bacteria kutokana na sukari inayotoka kwenye mbegu zinazomea.

Utahitaji pia kuwa na bomba dogo au hata kubwa kwa ajili ya, unywesheaji wa maji kwani maji hayatakiwi kumwagiwa mengi kama vile ufanyavyo katika bustani ya kawaida ya udongo bali ni matone madogomadogo juu ya majani mithili ya mtu anayenyunyizia dawa ya kuulia wadudu.

5. MBOLEA YA HYDROPONIC FODDER
Suala la kutumia virutubisho au mbolea ya hydroponics kwa ajili ya kustawisha na kuongeza uzito wa majani yako ya hydroponic ni mjadala ambao mpaka sasa hivi kuna watu wanaosema ni sahihi kutumia mbolea(virutubisho), hydroponic nutrients na wengine hukataa kwa madai kwamba kwasababu hydroponic fodder huchukua muda mfupi sana kuvunwa siku 4 mpaka siku 7 tu, mbolea za chumvichumvi zinaweza zikawa na madhara kwa wanyama yanayoweza kusababisha hatimaye matatizo kwa afya ya binadamu watakaokwenda kutumia nyama au mazao ya wanyama hao.

Hivyo huamini kutokutumia kabisa virutubisho vya aina yeyote ile kwa ajili ya kukuza mimea ya hydroponic fodder. Kwa wale wanaotumia virutubisho hivyo sanasana hutumia mbolea za maji mfano ‘booster’ kupulizia fodder mara zinapoanza kumea. Hata hivyo usipotumia virutubisho vyovyote vile bado fodder zako zitaota vizuri tu na kukua kwani zinatumia chakula na nguvu ya nishati kutoka katika akiba ya mbegu zinazooteshwa.


MCHAKATO MZIMA WA KUPANDA HYDROPONIC FODDER ULIVYO

Mchakato huanza na usafi wa matrei au vyombo vinavyotumika kwa kuviosha na maji ya dawa (sterilization) ili kuzuia kuvu na wadudu wanaoweza kusababisha magojwa. Tumia chlorine au hydrojen peroxide. Mbegu baada ya kusafishwa kwa maji ya dawa hulowekwa kwenye maji masafi kwa muda wa masaa 12 mpaka 24 ili kuzizimua ziweze kumea kwa urahisi . Usiloweke zaidi ya masaa hayo kwani zinaweza kuanza kuharibika au kuoza.

Baada ya kuzitoa kwenye maji uliyolowekea, zisuuze na kuzitandaza moja kwa moja katika trei ulizoandaa kwa makadirio ya kina cha robo inchi kutoka sakafu ya trei au chombo unachotumia. Funika kwa kutumia mifuko, magunia au  kitambaa kwa muda wa siku moja zitakapokuwa zimeanza kumea kisha zifunue ziendelee kuota.

Mwagilia maji kwa njia ya kunyunyizia kila siku mara 3 mpaka 4 ukitumia bomba linalotoa matone madogomadogo kama lile la kunyunyizia dawa ya kuulia wadudu. Umwagiliaji wa hydroponic fodder ufanyike mchana tu na wala siyo usiku kuepusha umande na ubaridi unaoweza kutengeneza kuvu.


UVUNAJI WA HYDROPONIC FODDER
Ikiwa umeotesha hydroponic fodder kwa ajili ya kulishia kuku(aina zote) basi utavuna baada ya siku nne 4. Na ikiwa umetayarisha kwa ajili ya kulishia ng’ombe, mbuzi, kondoo, sungura nk. utavuna mimea yako baada ya siku 7 mpaka 9.


Wastani wa uzito wa hydroponic fodder baada ya siku 7 mpaka 9 ni mara 7 ya uzito wa mbegu zilizotumika kuotesha. Hii ina maana kwamba ukiotesha kilo moja ya mbegu utavuna hydroponic kilo 7 baada ya siku hizo 7 mpaka 9. Uvunaji wa hydroponic  fodder hufanyika kwa kuviringisha ‘mkeka’ wenye mchanganyiko wa mizizi na vimea vya mbegu za hydroponic tayari kwa ajili ya kulisha mifugo wako. Mifugo kwa kawaida hula kila kitu kuanzia mizizi, mabaki ya mbegu na majani(vimea) hawaachi kitu chochote kile.

Naamini ndugu yangu Martine wa Kibaha Pwani majibu haya yatakuwa yamekuridhisha na unaweza sasa ukafanya majaribio ya kutayarisha hydroponic fodder hata ikiwa ni kwakutumia sinia, beseni au ungo na mbegu za mahindi, mtama au ngano kisha baadae ukaamua kuandaa kiasi kikubwa zaidi cha mimea hii ya kulishia mifugo hasa kuku isiyohitaji udongo kabisa.

……………………………………………..
MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACK
Kwa mahitaji ya michanganuo ya kuku aina zote, wasiliana na sisi, tuna michanganuo ya kuku wa mayai, kuku wa nyama na kuku wa kienyeji. Kifurushi kizima bei yake ni shilingi elfu 10 tu na tunakutumia kwa njia ya email kama PDF files au softcopy. Pamoja na offa ya kujiunga na group la MICHANGANUO-ONLINE bila malipo ya ziada.

SIMU:     0712202244
WASAP: 0765553030

Vitabu pia vinapatikana tembelea, SMART BOOKS TANZANIA 

6 Responses to "HYDROPONIC FODDER: JINSI YA KUOTESHA MAJANI YA MIFUGO KATIKA TREI ZA ALUMINIUM NA PLASTIKI BILA UDONGO"

  1. I want you to thank for your time of this wonderful read!!! I definately enjoy every little bit of it and I have you bookmarked to check out new stuff of your blog a must read blog! Airco

    ReplyDelete
  2. I have read your article; it is very informative and helpful for me. I admire the valuable information you offer in your articles. Thanks for posting it. Aluminium ramen en deuren

    ReplyDelete
  3. I wish for the great of success in all of our destiny endeavors

    ReplyDelete
  4. Their team presented helpful ideas for new features discuss that enhanced the quality of the product.

    ReplyDelete
  5. I am unable to read articles online very often, but I’m glad I did today. This is very well written and your points are well-expressed. Please, don’t ever stop writing. marquise diamond exporter

    ReplyDelete
  6. Ahsante na nashukuru sana kwa mafunzo haya, ila nina swali kwenye mbegu. Swali langu ni unaoyesha aina moja ya nafaka katika trei au unachanganya nafaka tofauti tofauti kwenye trei unayooteshea.

    ReplyDelete