BIASHARA HII ILIYOSAHAULIKA NATAMANI KUIFANYA LAKINI SIFAHAMU MCHANGANUO WAKE (USHAURI) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA HII ILIYOSAHAULIKA NATAMANI KUIFANYA LAKINI SIFAHAMU MCHANGANUO WAKE (USHAURI)

Kama ilivyokuwa kawaida kwa kipengele hiki cha Zungumza na mshauri, huwa baadhi ya majibu ya maswali wanayouliza wasomaji wa blogu hii tunayaweka moja kwa moja kwenye blogu kama makala za kawaida, kuna maswali mengine mengi ambayo huwa tunawajibu wasomaji moja kwa moja kwenye inbox zao. Katika majibu tunayoyaweka hapa kama haya ya leo tunafanya hivyo lakini bila ya kutaja kabisa jina la muuliza swali wala kutaja utambulisho wake wowote ule, tunatumia jina lisilokuwa halisi kwa mfanao katika majibu ya leo tumetumia jina la Salma ambalo ni la kubuni siyo jina halisi la aliyeuliza swali.


Muuliza swali la leo aliuliza kama ifuatavyo;


Asante sana kaka Peter kwa kunifumbua macho kuhusiana na ujasiriamali, kitu ambacho nakipenda sana lakini bado ninazo changamoto. Makala zako hasa hii ya Biashara zilizosahaulika hususani biashara ya kuuza supu ya kuku wa kienyeji kwa kweli imenihamasisha mno. Nimepata wazo jipya ambalo naomba tu Mungu anisaidie niweze kulitimiza kutokana na kwamba mtaji wangu ni mdogo sana. Ninao kuku wa kienyeji kama mia hivi na hapo kabla sikuwa nawaza kabisa juu ya biashara zilizosahaulika kama hii ya supu ya kuku. Natamani sana kuifanya lakini changamoto yangu kubwa na ambayo ningehitaji ushauri kutoka kwako ni jinsi ya kuweka mpangilio wa biashara hii. Naomba sana mawazo yako nahisi biashara hii itaweza kunitoa na kuondokana na hali ngumu ya kiuchumi.
AHSANTE SANA.


Hellow Dada “Salma”,
Kwanza kabisa nashukuru sana kwa kuwa msomaji wa makala katika blogu ya jifunzeujasiriamali, tena pia nimefurahi kwa kuniambia makala hizo mfano wa hii ya biashara zilizosahaulika imekuhamasisha kwa kiasi kikubwa.

Umeniambia tayari unao mradi wa kuku wa kienyeji 100 na nadhani hilo ni jambo zuri, hiyo kijasiriamali siyo hatua ndogo hata kidogo, tayari wewe unao mtaji mkubwa tu ambao kama utajitahidi zaidi kutega vyanzo vingine vya mapato unaweza kutoka na kuwa mtu mwingine tofauti kabisa baada ya kipindi kifupi.

SOMA: Kuanzisha biashara nikiwa nasoma, nipeni ushauri nina wakati mgumu.

Salma tayari wewe ni mjasiriamali wala usiwe na shaka kuhusiana na hilo, unachohitaji zaidi ni uthubutu tu, hebu zidisha ujasiri wako uweze kupiga hatua zaidi ya pale ulipokuwa na kulingana na swali lako nadhani hiyo ndiyo shida yako kubwa kwani tayari mtaji unao kitu ambacho kwa kiasi kikubwa ndicho kinachowasumbua wajasiriamali wengi wadogo na wala siyo maarifa kama wengi wanavyodai, mimi kwa maoni yangu kuna wakati maarifa nalazimika kuyaweka nafasi ya pili.

Kuhusiana na mchanganuo wa biashara, umetoa mfano wa biashara kama za supu nk. mbona siyo kitu kigumu? Maana ya mpango wa biashara au mchanganuo siyo kitu cha ajabu sana, mtu yeyote yule anayeanzisha biashara au aliyewahi kufanya biashara yeyote ile basi na ujue moja kwa moja ameshafanya mchanganuo wa biashara kichwani mwake, ni vile tu huwa hatujui kama tunafanya michanganuo ya biashara vichwani mwetu.

Kitendo cha kufikiri ni mtaji kiasi gani unahitaji, biashara yako utaifanyia eneo gani, utaweka mfanyakazi au utakaa mwenyewe kwenye biashara, utanunua wapi bidhaa zako au malighafi, utauza bei shilingi ngapi, faida utapata kiasi gani nk. huo ndiyo mchanganuo wenyewe wa biashara, "so, almost every person do a business plan at a certain time in his/her lifetime" Tatizo huja pale mtu unapomwambia juu ya mpango wa biashara wa kuandika katika makaratasi, watu wengi hawapendi lakini ni kwa vile tu hawaelewi faida zake.

SOMA: Jinsi mpango wa biashara unavyoweza kuongeza mafanijio ya biashara yako.

Hivyo dada Salma nisingependa kukuchosha sana na mlolongo wa maelezo wakati wewe shida yako ni mchanganuo wa biashara ya supu ya kuku wa kienyeji. Kwa kuwa tayari unafanya biashara, suala la mchanganuo wa biashara haliwezi likawa gumu kwako hata kidogo, unaweza kama nilivyokutajia hapo juu ukafikiria tu kichwani masuala yote yanayohitajika kutekeleza biashara ya supu na ukawa ndiyo mpango wako wa biashara, au pia unaweza ukaamua kutafuta mchanganuo wowote ule ulioandikwa ukaupitia na ukapata picha mchanganuo wa biashara unakuwaje na kisha ukaandaa wa kwako.

Sisi tunacho kitabu kiitwacho MICHANGANUO YA BIASHARA NAUJASIRIAMALI, ndani yake kuna michanganuo ya biashara mbalimbali iliyoandikwa kwa lugha ya kiswahili ambayo mtu yeyote yule mwenye nia ya kujifunza michanganuo ya biashara kwa lengo la kuendesha biashara yake kwa ufanisi basi michanganuo iliyopo katika kitabu hiki inaweza ikawa msaada muhimu sana kwake. Vile vile tuna kakitabu kengine kazuri sana na nafikifi kama hukuwahi kukisoma kitakufaa sana mtu ambaye una nia ya kutengeneza vyanzo mbadala vya mapato, kinaitwa MIFEREJI 7YA PESA.


Mwisho nikutakie shughuli njema na mafanikio katika mradi wako wa kuku na naamini kwa ushauri huu basi hutasita kuanzisha moja kati ya biashara zilizosahaulika kama hii ya kuuza supu ya kuku wa kienyeji, tena kwa bahati njema basi wala hutahangaika kutafuta mtaji, kuku unao mwenyewe, labda utauza hapo wawili au watatu tu upate hela kidogo kwa ajili ya mahitaji mengine kama eneo, vyombo na viungo kama pilipili, ndimu au limao.

0 Response to "BIASHARA HII ILIYOSAHAULIKA NATAMANI KUIFANYA LAKINI SIFAHAMU MCHANGANUO WAKE (USHAURI)"

Post a Comment